Inside10,
Sikutegemea hata kidogo kama post hii yangu itagusa watu wengi kiasi hiki.
Nimeamua In Shaa Allah kukuelezeni historia yote vipi TANU iliingia Lindi na Southern Province yote kama nilivyoandika katika kitabu cha Abdul Sykes (1998):
TAA mjini Lindi ilikuwa chini ya uongozi wa Suleiman Masudi Mnonji aliyekuwa Rais na Katibu wake alikuwa Mohamed Waziri. Mnonji alikuwa fundi cherahani na Waziri alikuwa mchoraji wa ramani za nyumba. TAA ilichelewa kuanza mjini Lindi. TAA ilianzishwa Lindi mwaka 1953 wakati uongozi wa TAA mjini Dar es Salaam si tu ulikuwa unaigeuza TAA kuwa chama cha siasa bali ulikuwa ukifanya mipango kumpeleka mjumbe wake Umoja wa Mataifa kudai uhuru.
Masudi Mnonji alikuwa na uzoefu wa kutosha katika siasa. Baada ya Vita Kuu ya Pili alikuwa amejaribu kuanzisha vyama vya wafanyakazi katika mashamba mbalimbali ya mkonge kusini mwa Tanganyika. Vilevile aliwakusanya wapishi na madobi mjini Lindi waanzishe umoja wao. Ilikuwa kupitia juhudi zake binafsi TAA ijapokuwa ilichelewa, ilikuja kuanzishwa mjini Lindi na Mnonji alijitolea nyumba yake katika mtaa wa Makonde kama ofisi ya chama.
Mnonji kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uongozi ulioelimika vizuri, alimleta Nangwanda Sijaona kutoka Nachingwea aje aishauri TAA jinsi ya kufanya mambo kwa utaalamu. Wakati huo mjini Lindi kulikuwa na chama cha wafanyakazi bandarini Dockworkersí Union chini ya uongozi wa Mussa Athumani Lukundu, chama ambacho kwa kiasi chake kilianzisha vuguvugu la siasa za vyama vya wafanyakazi. Ingawa vyama hivi viwili, yaani TAA na Dockworkersí Union vilikuwepo katika mji mmoja, siasa za hiki chama cha pili cha wafanyakazi bandarini hazikupitia TAA kama ilivyokuwa mjini Dar es Salaam. Hii kidogo ilidhoofisha mwamamko wa siasa kwa wananchi.
Jimbo la Kusini lilikuwa katika usingizi mzito wakati sehemu nyingine Tanganyika zilikuwa zikipiga hatua kwenda mbele zikiandaa vita dhidi ya utawala wa kikoloni. Chanzo cha usingizi huu mzito huko kusini ulikuwa na asili yake katika historia ya Tanganyika.
Vita vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya kuwafukuza Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi zilikataa kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya Wajerumani na kupigana bega kwa bega na dhidi ya wazalendo.
Hii ilitokana na sababu ya kuwa uasi dhidi ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo yenye Waislam wengi na vita vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya Wazungu ambao dini yao ni Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika wa wakoloni, walichukuliwa kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji Maji.
Kutokana mashambulizi haya, Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama vita dhidi ya Ukristo. Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani walifanya ufisadi kubwa dhidi ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha kovu kubwa katika fikra za wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao walinusurika na ghadhabu ya Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina yoyote ya kupinga ukoloni.
Kufuatia historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa chini ya utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari walipumbazwa kiasi kiasi kwamba waliogopa siasa. Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali za Wazungu sasa Kanisa likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo kwa kutoa vishawishi kama vile shule na hospitali.
Kwa hiyo Wamishionari na Waingereza walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na serikali katili na ya kidhalimu ya Wajerumani. Vuguvugu la siasa kama ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo ya Waislam kufuatia mfumo ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni wa Wajerumani. Wakristo katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama harakati nyingine za Waislam zilizokuwa zinakuja tena kwa mara ya pili kuvuruga amani na utulivu.
TANU ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa wamemua kuanzisha vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na Wajerumani.
Tafsiri hii ya Kiswahili ya kwanza imechapwa na Phoenix Publishers, Nairobi 2002.
(Itaendelea...)