Habari ya muda huu Wakuu,
Mnamo mapema wiki iliyopita niliandika uzi nikihoji nafasi ya sanaa ya Tanzania (Muziki) katika kuelezea na kuonesha uhalisia wa jamii yetu (Tanzania yetu). Nilipata wazo la kuandika uzi ule kutokana na kukithiri kwa nyimbo mbalimbali zenye mlengo wa kusifia pekee (kusifia awamu ya tano).
Unaweza kujikumbushia kidogo hapa chini:
Je, ni ipi nafasi ya wasanii wa kizazi kipya kumulika uhalisia wa jamii yetu?
Nikirudi kwenye mada, nimeridhishwa sana kuona jambo lililokuwa linaniumiza katika sanaa ya Tanzania limefanyiwa kazi. Naona kama sanaa imerudisha uhai wake kwa kuwa na maudhui yanayogusa pande zote. Leo katika pitapita zangu Mjini, nimepata bahati ya kuusikia wimbo mpya wa msanii Roma unaoitwa
“Anaitwa Roma”. Aidha, katika wimbo huo Roma ameonesha mtazamo tofauti na wasanii wengine (wasanii wanaosifia pekee) kwa kujaribu kugusia na kukosoa matukio mbalimbali yanayotokea Tanzania. Aidha, uzi huu hautazama sana kuchambua maudhui ya wimbo huo, isipokuwa uzi huu utaeleza kwa ufupi namna ambavyo nimefurahishwa kuona sanaa ya Tanzania inasawazishwa (imebalance) kwa kuwa na wasanii wanaosifia na wengine wanaokosoa.
Wakuu, kuwa na sanaa ya aina hii ni muhimu sana katika ustawi wa Nchi yetu kwa sababu, wasanii wanaposifia wanawapa nafasi wananchi (wanajamii) kuona mema yanayofanywa na viongozi. Ama pale wanapokosoa, wanaipa nafasi jamii kuona udhaifu na maovu yanayofanywa na viongozi. Kimsingi, mimi ni muumini wa dhima ya ukosoaji katika sanaa kwa sababu naamini dhima hiyo husaidia kumulika mabaya ya viongozi na kuwafanya wawe na uoga wa kufanya maouvu na kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao. Kwa upande wa dhima ya kusifia sio mbaya, lakini kwa mtazamo wangu naona sehemu kubwa ya masuala yanayosifiwa ni sehemu ya majukumu ya viongozi kwahiyo si lazima sana kuyasifia na kuyatangaza (mtazamo wangu).
Kongole Roma Mkatoliki kwa kuonesha mfano, sanaa ili iwe hai lazima iwe hivyo. Wakuu kazi ya sanaa sio kusifia peke yake, sanaa inatakiwa ikosoe pia. Hakika nitasikitika sana kama ikatokea wimbo huu wa Roma ukafungiwa. Viongozi watakuwa wameonesha udhaifu wa hali ya juu. Unapokubali kusifiwa lazima ukubali kukosolewa pia. Naamini Roma atakuwa amewasaidia watu wengi wenye mtazamo wake kuyasema yale ambayo hawawezi kuyasema
Naomba kuwasilisha.