Amani ni tunda la haki.
Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa nchi yenye utulivu bila amani ya kweli. Utulivu umetokana na uvumilivu wa wananchi. Lakini ukweli ni kuwa uvumilivu una mwisho.
HAKI ndiyo hakikisho la kudumu la Utulivu na amani ya kudumu.
Mwalimu Nyerere alitamka kuwa kuwa tuna katiba ya hovyo ambayo Rais akikosa hekima na huruma anakuwa dikteta, na katiba isimzuie.
RAIS Mkapa, katika kitabu chake alitamka kuwa aliiba hela ya Serikali kuipatia CCM. Katiba kwa kuwa ni ya hovyo, haikumzuia wala kumwadhibu yeye na CCM yake. Mkapa akakiri kuwa nchi hii haina uchaguzi huru, wa wazi, na wa haki. Akasema kuwa angetamani Tanzania iwe nchi yenye chaguzi huru na za haki.
Licha ya wakuu hawa wa nchi kukiri ushetani wa katiba yetu, sheria mbaya za uchaguzi, na Taifa kutokuwa na Tume huru inayoweza kusimamia uchaguzi huru na wa haki, CCM ya sasa, Rais wa sasa na Serikali yake, wamegoma kabisa kuiondoa nchi kutoka kwenye udhulumaji wa haki za wananchi.
Siku zote, mtu anayegandamiza haki za watu, anaanzisha na kupalilia kuondoka kwa amani na utulivu, kwa sababu uvumilivu wa mwanadamu una kikomo.
Ni vema sasa, tukawatangaza kwa uwazi maadui wa amani na utulivu wa nchi yetu:
1. RAIS SAMIA
Huyu ndiye kiongozi wa nchi ambaye kama angekuwa na upendo na uzalendo kwa Taifa hili, alitakiwa kufanyia kazi maneno ya Mwalimu Nyerere na Mkapa, lakini ameungana na waovu maadui wa Taifa hili, kuhakikisha tunaendelea kuwa na katiba ya hovyo, tunakosa Tume huru ya uchaguzi, na kuhakikisha tunaendelea kuwa na sheria na kanuni za hovyo za uchaguzi.
2. CCM
Hiki chama ndicho kilichoandaa katiba ya hovyo na sheria na kanuni mbaya za uchaguzi. Hiki chama ndicho huwa kinashinikiza polisi, TISS na wasimamizi wa uchaguzi kufanya uovu.
3. BUNGE BANDIA LA CCM
WAkati wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, wananchi na taasisi mbalimbali zilitoa mapendekezo mazuri sana ambayo yangezifanya chaguzi zetu kuwa huru na za haki. Lakini wabunge wale bandia, waliungana kuyakataa mapendekezo yote ya wananchi na taasisi mbalimbali, wakatengeneza sheria za kishetani, na Rais Samia akazikubalia, ikiwa ni pamoja na yeye Rais Samia kung'ang'ania kuunda Tume ya uchaguzi inayowajibika kwake.
4. BARAZA LA MAWAZIRI
Baraza la mawaziri, kikatiba ndiyo baraza la ushauri la Rais. Hivyo Rais kusaini sheria ile ya kishetani ya uchaguzi, maana yake Baraza la mawaziri liliridhia.
Licha ya uovu huu mkubwa wa Rais Samia, Wabunge, CCM na Mawaziri, kwa upande mwingine, kuna watu au taasisi ambazo majina yao yanastahili kuandikwa kwa wino wa dhahabu kwa sababu wakati wote wamepinga uovu na kutoa ushauri ili nchi iwe na haki, na hivyo kuwa na amani ya kudumu:
1. CHADEMA
Licha ya vitendo viovu kabisa vya CCM vya kuhatarisha amani na utulivu, CHADEMA na viongozi wake, wakati wote imesimama na kukemea uovu kwenye demokrasia na kwenye masuala yote ya kupora haki za wananchi. Wameyatenda hayo yote bila ya kubeba rungu, panga au bunduki. Wakati wote wamehamasisha majadiliano ya kitaifa, lakini Rais Samia na CCM wameziba masikio na kutumia nguvu ya polisi. Dhamira njema ya CHADEMA inajibiwa kwa utekaji, uuaji na hata kesi za kubambikiziwa
2. TEC na Shura ya Maimam
Hizi taasisi mbili za kidini, hakuna hata wakati mmoja zilipokosa kukemea uovu wakati wa uchaguzi. Pia wakati wote ilipotokea nafasi ya kutoa maoni na ushauri namna ya kuifanya Tanzania ya haki na demokrasia ya kweli, walifanya hivyo bila ya unafiki wala woga.
3. TLS
Hii taasis ya wasomi wa sheria, wakati wote wameonesha ubovu wa katiba na sheria zetu katika kulinda mamlaka ya wananchi, katika kuwapata viongozi wanaowataka. Hata kwenye mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, walipeleka maoni yao, lakini lile bunge la waovu lilitatupilia mbali maoni mazuri yote toka kwawadau wote.
4. Jaji Warioba, Prof. Shivji, Joseph Butiku
Hawa wote ni wanaCCM, lakini ni wanaCCM wanaoipenda Tanzania. Hawa wakati wote wameweka bayana misimamo yao dhidi ya ugandamizaji wa haki za wananchi katika kuwapata viongozi wanaowataka.
5. Jaji Nyalali
Huyu kwenye report yake kuhusu katiba na sheria mbalimbali, aliweka bayana ubovu wote wa katiba na alitoa mapendekezo ya kufutwa sheria zote mbaya na zilizo kinyume cha haki za binadamu, lakini CCM aliyatupilia mbali hayo mapendekezo, na kuendelea kukumbatia uovu.
7. Mwalimu NYERERE RIP
Huyu licha ya kuiongoza Tanzania ya chama kimoja, angalo mwishoni aliweza kutamka wazi kuwa katiba ya nchi yetu ni mbaya, na hivyo inahitaji mabadiliko.
8. BENJAMIN MKAPA
Licha ya yeye kufanya uovu kama ule wa kuiba pesa na kuipatia CCM, licha ya yeye kuwa tunda la uovu wa CCM, lakini mwishowe alikiri wazi kuwa katiba yetu ni ya hovyo, sheria zetu za uchaguzi ni mbaya, na Tume yetu ya Uchaguzi siyo huru. Kwa kuyakiri tu hayo, anastahili kukumbukwa kwa wema.
9. Nape NNAUYE
Nape na January ni miongoni mwa waliwahi kudhulumu haki za Watanzania kwa kiwango kikubwa sana. Lakini sijui kama ni kwa dhamira njema au kwa bahati mbaya iliyo njema, alitamka wazi kuwa Watanzania huwa hawawachagui wabunge, madiwani, wala Rais, bali wale ambao huwa wamepachikwa kuhesabu kura.
Hawa watawala wa sasa wote, kuanzia Rais, mawaziri, wabunge na viongozi wa CCM, majina yao yatunzwe vizuri sana ili hata vizazi vingi vijavyo waje wasome na kuwatambua watu hawa waliowahi kuwa maadui wakuu wa Taifa, waliotumia nguvu zao zote kuulinda ugandamizaji wa haki za Watanzania katika kuwapata viongozi wanaowataka.
Ikiwezekana hata watu wa dini wangeendesha ibada maalum ya kuomba mkono wa Mungu uwafikie watu hawa ili waujutie uovu wao, na kisha wabadilike, ili wasibakie kwenye utawala wa shetani maisha yao yote ya kuwepo kwao hapa Duniani.