ANAANDIKA BABA ASKOFU BAGONZA (PhD)
BANDARI: Tumefikaje? Tutatokaje?
Mjadala wa “kuuzwa”, “Kubinafsishwa”, “Kukodishwa” au vyovyote ilivyofanywa, umeonyesha nyufa za hatari katika nyumba yetu TANZANIA. Nitaje kadhaa:
1. Rushwa
Rushwa bandarini ndiyo imesababisha bandari ifanywe inachofanyiwa. Wakiishapeana rushwa, serikali inakosa mapato, mizigo inachelewa, inapotea, na bandari limekuwa pango la majizi.
Swali ni je, kila penye rushwa tuuze? Tubinafsishe? Tukabidhi sekta binafsi? Je rushwa ikishika kichwani na moyoni? Tujadili ufa huu bila jazba. Rushwa itavuruga wawekezaji wapya.
2. Umoja na Utaifa
Mjadala umeonyesha, wanaodai wanaujenga/kuutetea umoja na utaifa, ndio wanaubomoa. Wanaoonekana kuubomoa, ndio wanaujenga. Bandari imeujeruhi umoja na utaifa wetu. Hii ina gharama mbeleni. Tumejuana, tuishi kwa tahadhari.
3. Udini na Siasa Zetu
Viongozi wetu wana dini zao. Sitamani kuchagua kiongozi asiye na dini. Tatizo tunalo viongozi wa dini. Tunawakosoa viongozi wa dini ileee na kupongeza wa dini zetu. Au tunanyamaza mpaka tupigwe sindano ya kupongeza badala ya kushauri. Inapendeza kumkosoa na kumshauri kiongozi wa dini yako japo haizuiwi kumkosoa wa dini isiyo yako.
4. Ujuzi wa Sheria na Uchumi.
AJABU: Wanasheria walioongea tukaelewa ni wachache sana. Walio wengi ujanja wao unaishia Kisutu.
Wanauchumi wetu ujanja wao unaishia Kariakoo. Mkataba huu hawauelewi na wakiuelewa hawatuelezi tukaelewa. Huu ni ufa wa hatari.
5. Bunge
Hili lingebinafsishwa kabla ya bandari. Walichoongea bungeni sicho wanachoongea mitaani na kwenye baa. Wanamdanganya rais kuwa wanamuunga mkono wakati wamebeba mishale ya kumwangamiza. Mjadala wa Bandari umefanywa mgumu na bunge letu.
6. Serikali
Mjadala na tabia za watu vimeonyesha serikali hii si ya rais Samia hata kama kaiteua yeye. Hii ni mchanganyiko wa serikali zilizopita. Ina utii uliogawanyika - kiapo kimoja Chamwino na vingine huko makaburini, Msufini, na Butiama. Serikali bila “Uwajibikaji wa pamoja” ni sawa na genge la wasela. Ufa huu unadai tuanze upya.
7. Rushwa part 2.
Katika Mjadala wa Bandari tumesikia malalamiko ya rushwa za aina tatu: Wanaonufaika na uzembe wa bandari wakikazana kukwamisha mkataba; DP World wakikazana mkataba upite; na wanaoitwa wazalendo wasio wa taka DP World wala wazembe wa bandari LAKINI bila kutoa suluhisho. Ufa huu ni mgumu kuushughulikia bila kuchelewesha mkataba na kusikilizana kwanza.
8. Rais Wetu
Rais SSH ni wetu sote. Ni muhimu kama taifa kumkinga na mipasuko inayotokana na mjadala huu. Kuna maisha baada ya mjadala wa bandari. Yeye analo jukumu la kutuongoza sote na makundi yote mpaka tuvuke. Subira itatufundisha kuliko haraka. Ufa huu unazibwa kwa kusikiliza na kuchukua hatua.
9. Miafaka yetu
Mjadala huu umejeruhi miafaka yetu na kufukua baadhi ya makaburi. Baadhi ya makaburi tumekuta marehemu hawajaoza.
Katiba, maridhiano, Muungano, maelewano ya kidini, uhuru wa maoni na mamlaka ya wananchi bila bunge ni mambo muhimu sana katika kuziba nyufa zilizojitokeza.
10. Upinzani wetu
Mjadala unaonyesha aina mpya ya upinzani. Ndani ya chama tawala na serikali kuna upinzani mkali dhidi ya suala la bandari. Hii ni afya kwa nchi lakini hatari kwa utawala. Vyombo vyetu vijifunze kutotumia nguvu kupambana na maoni. Bora upinzani wa hadharani kuliko wa moyoni.
Nawashukuru wooote wanaochangia kwa hoja na kutuelimisha tulio wajinga wa sheria, uchumi, mikataba ya kimataifa na katiba yetu.