Miaka kadhaa nyuma nilikuwa mwenyekiti wa kamati ya harusi ya kijana mmoja kwenye kanisa nililokuwa ninasali hapa Dar.
Upekee wa hii ndoa ni misuguano na mabishano yaliyokuwepo kati ya kijana na familia yake hasa mama yake na dada zake. Sababu ya mabishano ni dada anayetaka kuolewa na kijana alikuwa ana mtoto.
Bahati nzuri au mbaya, huyu dada alipata ujauzito akiwa kidato cha tatu, wakati ule ilikuwa kuna ruhusa ya binti kwenda kujifungua na kisha kurudi shule na kumaliza. Jamaa aliyempa binti mimba baada ya misukosuko kadhaa polisi na vyombo vya dola, akafikia muafaka na familia(uswahilini tunasema kutumia busara),jamaa akaendelea na maisha yake lakini akihudumia mimba huku binti akiwa kwao.
Dada alijifungua na hatimaye alirudi shule japo alipoteza mwaka mmoja na kufanikiwa kumaliza kidato cha nne. Huyu alisoma mpaka akapata shahada (Bachelor degree.)
Kwahiyo hii ilikuwa ndoa ya watu wawili wote wakiwa na Bachelor degree; huku dada akiwa na mtoto wa miaka 6+ Hili suala lilifika mpaka kwa mchungaji na kwa kweli familia ikaambiwa iache vijana waoane, kuzaa sio jambo baya.
Wasiwasi wa familia ulikuwa wapi? Kwa namna ambavyo nilikuwa nafuatilia, nikaambiwa na dada wa kijana anayetaka kuoa kuwa wao hawana tatizo na binti kuwa na mtoto lakini tatizo lao ni kuwa mahusiano ya dada na mzazi mwenzie hayajaisha. Nikatafakari kisha nikamwambia mahusiano ya wao kama wazazi hayawezi kwisha ila dada anaweza kuheshimu na kushika kiapo cha ndoa vizuri kabisa.
Familia ya kijana ikanyoosha mikono kwa shingo upande na maandalizi ya harusi yakafanyika mimi nikiwa mwenyekiti. Baba wa kijana alikuwa hana tatizo kabisa na suala la kijana wake kuoa binti mwenye mtoto.
Ndoa ya kanisani ikafungwa na tafrija ikafanyika pale NSSF Waterfront House, watu wakafurahi na wanandoa wakaenda honeymoon Zanzibar.
Miaka ikapita na mimi nikiwa kwenye harakati zangu, nikakutana nao siku moja pale JNIA - terminal 1; walikuwa wenye furaha wakiwa na watoto watatu (Yule wa kwanza kabla ya ndoa na watoto wengine wawili wa kwenye ndoa).
Tukasalimia pale na kila mtu akaendela na safari yake. Sasa, mwaka jana nikapishana na jamaa pale Kivukoni katika harakati za kupanda Azam Sea Tax, alikuwa wa kwanza kuniona akaja akanisalimu na tukaongea mambo machache. Aliuliza kuhusu familia yangu, nami nikamuuliza vipi familia yake. Nikaona uso wa jamaa unabadilika ghafla kisha akasema ''kaka ndoa ilivunjika''.
Nikampa pole na tukafika upande wa pili kila mtu akaendelea na safari yake. Nikabaki natafakari. Nikawa sijaridhika maana ndoa imevunjika sababu ni nini? Siku mbili baadaye nikatumiwa picha whatsapp na mmoja wa washiriki wenzangu wa kanisa.
Picha ilikuwa ya la yule dada akiwa na jamaa wakiwa wanaonyesha pete ya ndoa. Harusi ya Bomani kwenye ofisi za mkuu wa wilaya. Nikiangalia naona kabisa yule jamaa kwenye picha umri umesogea, nikauliza huyu jamaa ni nani? Msharika akasema ''huyu ndio mzazi mwenzake'' jamaa aliyempa mimba akiwa sekondari.
Nikapigwa na butwaa!!!! Whaaaaat. Baada ya hapo nikapewa lawama nikiwa miongoni kwa watu ambao nilikuwa naunga mkono ndoa hii licha ya mashaka ya ndugu wa mwanaume.
Nikamjibu na kumwambia, mwanamke amefanya uchaguzi wake mwenyewe, angeweza kufanya hivyo hata kama angekuwa hajazaa na jamaa. Jambo moja nimejifunza kuwa binadamu hawatabiriki.
Natumai jamaa aliyeachwa na mkewe atapata ushauri mzuri wa kuendelea na maisha, i hope ndugu zake hawatatumia kilichotokea kama fimbo ya kuthibitisha mashaka yao miaka 15 iliyopita.
Muwe na siku njema.
Disclaimer: Sina tatizo na wanawake wenye watoto nje ya ndoa; wala sina tatizo na wanaooa wanawake wenye mtoto/watoto.
Siamini kwamba wanawake wote wenye mtoto/watoto basi wana tabia zinazofanana.