Kuna siku polisi walinikamata, wakawa wanataka kunibabatiza na kesi zao za kipuuzi.
Wakawa wanataka kunipeleka kituoni.
Nikasema sawa, si tatizo. Ngoja nimpigie simu mshua nimtaarifu mmenikamata watu nyumbani wapate habari nimekamatwa na polisi. Halafu mtawaeleza kosa langu ni lipi.
Wakaniuliza kwani mshua wako nani?
Nikawaambia mshua tu.Msijali.
Nikaona wanaanza kuogopa.
Wakang'ang'ania kumjua.
Nikawatajia.
Haraka sana wakaanza kujibaraguza basi nenda tu.
Nikasema hapa kama mtu hajulikani angelala polisi.
Siku nyingine tumekaa maskani Upanga.
Tunaona polisi kama 20 wametanda mtaani wanakuja.
Mimi nikawaambia madogo fulani tumekaa nao, nikasema hapa kama mtu hawezi kuongea nao hawa ajikate kabisa, hapa tunabaki wabishi tu.
Basi wakafika mpaka pale tulipokuwa.
Mmoja akaanza kusema "hapa mnafanya nini nyie?".
Dah, kosa. Jamaa mmoja akamjibu "Hivyo ndivyo mlivyofundishwa kusalimia watu?"
Ikawa kama mzozo. Watu wakasema hapa tupo nyumbani.Polisi wakaanza kuuliza mmoja mmoja, wewe unakaa wapi? Watu wanaonesha nyumbani hapo, nyumbani hapo.
Wakamfikia jamaa mmoja tuko naye maskani.
Wewe unakaa wapi?
Jamaa akajibu "Kwa Ben".
Polisi wakawa wanashangaa, wakauliza, kwa Ben? Ben gani?
Jamaa akajibu, Ben Mkapa huyo huyo wa Jamhuri ya Muungano, kwani wewe unamjua Ben gani?
Hapo rais ni Ben Mkapa.
Askari wakastuka. Ikawa kama hawaamini.
Mmoja wao akawa kama anawanong'oneza, nikamsikia anasema "huyu namjua, nilikuwa namuona nyumbani kwa Mkapa pale Sea View kwenye lindo". Presumably wakati Mkapa akiwa Waziri.
Basi hapo hapo tukaona askari polisi walioanza kutuingia kwa inda wanabadilika mara moja.
Wakaanza kusema "mnajua wazee ni katika kufahamiana tu, hatukuwa na lengo baya, ni kufahamiana tu".
Nikasema hawa huko mitaa ya watu wasio na majina wanawakamata watu na kuwatoa upepo vizuri sana, bila kosa.
Bahati yao mbaya leo wamekutana na kisiki.
Ile maskani waliipigia alama kituoni kwao, waliambizana maskani hii msiguse, kuna mtoto wa rais anakaa hapo.
Haki ya kikatiba ya kila mtu ya kutosumbuliwa na kuchukuliwa hana hatia mpaka atakapopatikana na hatia inavurugwa na inakuwa privilege ya watu wenye majina.