Uchunguzi wa awali wa jeshi la polisi kuhusu tukio la Mgombea Udiwani kata ya Ngarenaro (CCM) Abdulaziz Abubakari Chande "Dogo Janja" kumshambulia kwa risasi Bakari Halifa Daudi (18) huko sombetini jijini Arusha umebaini kuwa mtuhumiwa alikuwa akijihami.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo zimesema kuwa tukio hilo lililotokea Agosti 23 majira ya saa 5:30 usiku lilihusisha bakari kujeruhiwa kwa risasi mguuni.
"Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, wakati Abdulaziz, mkazi wa Levolosi, alipokuwa akishuka kwenye gari, alidai kutaka kuvamiwa na Bakari akiwa na mwenzake wakiwa na silaha ya jadi. Hali hiyo ilisababisha mtuhumiwa huyo kutumia silaha aliyokuwa nayo na kumpiga risasi Bakari," imesema taarifa ya polisi.
Hata hivyo, polisi mkoani Arusha wamewakamata watu wawili kuhusiana na tukio hilo na wamesema uchunguzi zaidi unaendelea.