Loftins,
AHADI YA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE KWA WAISLAM 1962
Haiwezekani kuielewa ahadi ya Nyerere katika haki na usawa kwa raia wote kama alivyoahidi wakati wa kudai uhuru, hadi usome hotuba yake aliyoitoa tarehe 10 Desemba, 1962 katika Bunge wakati Tanganyika inakua jamhuri.
Hotuba ya Nyerere ilijikita kwenye matatizo ya upogo kati ya Waislam na Wakristo.
Nyerere alikuwa na haya ya kusema:
‘’Hakuna njia nyepesi ya kuondoa tafauti baina ya raia wetu Waafrika na wasio Waafrika; hakuna njia nyepesi ya kuondoa tofauti za elimu kati ya Wakristo na Waislam, au baina ya wachache wenye elimu na wengi wa watu wetu wasio kuwa na elimu; hakuna njia nyepesi ambayo Wamasai na Wagogo wanaweza wakalingana na Wahaya na Wachagga na Wanyakyusa.’’
Hii ilikuwa kauli ya serikali ya kudhihirisha nia yake njema kwa Waislam.
Kauli hii ilikuwa ya kuwapa matumaini na kuwahakikishia Waislam na wale wote walioathirika na dhulma ya wakoloni, kuwa serikali ilikuwa inatambua shida zao na itachukua hatua zifaazo kurekebisha hali hiyo.
Bila shaka Nyerere alisema maneno haya akitambua mchango mkubwa wa Waislam wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Nyerere alisema maneno haya akijua kuwa ingawa yeye alikuwa Rais Mkatoliki lakini Waislam kwa nia ya kuleta umoja wa Watanganyika chini ya TANU na kupigania uhuru hawakusita kumuunga mkono kwa dhati.
Na siku alipoacha uongozi baada ya kutawala kwa robo karne Mwalimu Nyerere katika hotuba yake maarufu ya kuaga aliyotoa Diamond Jubilee Hall alikuwa na haya ya kusema:
''Waislam wametupa nafasi kupitia sera yetu ya elimu, kurekebisha upogo.
Sasa nipo katika hali ya kufurahisha kwa kuwa wakati mwingine sielewi kama Mbunge mpya, Waziri, au Katibu Mkuu katika wizara zetu za serikali, ni Muislam au Mkristo au hana dini labda pale jina lake la kwanza linapotoa utambulisho.
Na hata hivyo hiyo siyo njia ya kuaminika kutoa utambulisho wa dini kwa kuwa tuna Wakristo wenye majina ya Kiislam, na Waislam wenye majina ya Kikristo.
Kuvumiliana huku nyie ndiyo sababu; nilichofanya mimi ni kuzungumzia maadili haya kwa niaba yenu.''
Huyu ndiye Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyoeleza tatizo la Waislam na jinsi alivyolitatua.
Yapo mengi ambayo yangewezwa kuelezwa kuhusu ukweli wa kauli hii lakini tutosheke na haya.
Leo Waislam wanatatazika na idadi yao katika Baraza la Mawaziri lililo na Waislam 3 dhidi ya Wakristo 20.
Picha ya kwanza kulia ni Mshume Kiyate, Julius Nyerere, Max Mbwana na Mwinjuma Mwinyikambi mwaka wa 1962.
Picha ya pili ni Mshume Kiyate na Julius Nyerere 1964 na picha ya tatu ni kulia Haruna Taratibu, Saadan Abdu Kandoro, Julius Nyerere, Sheikh Mohamed Ramia na Iddi Faiz Mafungo wakiwa Dodoma 1956.