Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa ufafanuzi kuhusu sanduku kubwa la mbao lililotelekezwa na kuzua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi katika eneo la Mwenge, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa leo Agosti 6, 2026 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam inaeleza kuwa sanduku hilo lilionekana majira ya saa 3:00 asubuhi katika kituo cha daladala cha mabasi yaendayo Tegeta, likiwa limefungwa kwa kufuli na kuzungushiwa kitambaa kwa mtindo wa alama ya jumlisha.
Baada ya kupokea taarifa hizo, timu ya wachunguzi kutoka Jeshi la Polisi ilifika eneo la tukio na kulifungua sanduku hilo, ambapo walikuta vipande vya mbao vilivyotengenezwa kwa muundo usio wa kawaida.
"Baada ya kufanya uchunguzi wa awali na kulifungua sanduku hilo, wataalamu wetu walikuta ndani yake kipande cha mbao kilichochongwa kwa mithili ya mguu wa kiti au kitanda cha mtindo wa kizamani. Kitendo hiki kinaweza kuhusishwa na imani za kishirikina au nia ya kutengeneza taharuki kwa umma," imeeleza taarifa hiyo ya Polisi.
Jeshi la Polisi limewatoa hofu wananchi na kuwataka kuendelea na shughuli zao za kila siku huku likiendelea na uchunguzi kubaini mtu au watu waliohusika kutelekeza sanduku hilo kituoni hapo.
#PolisiDarEsSalaam #Mwenge Kinondoni #TaharukiMwenge #JeshiLaPolisi #DarEsSalaam SasaLive
View attachment 3644524