Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatoa taarifa kwa Vyombo vya Habari na Umma wa Watanzania kuhusu ratiba ya vikao vya ndani ambavyo vitahitimisha uteuzi wa Mgombea wa Urais na Mgombea Mwenza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea wa Urais wa Zanzibar.
Vikao hivyo vya kitaifa ambavyo ni, Kamati Kuu ya Chama, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, vitaketi kwa siku tatu mfululizo na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya Mwaka 2006, Toleo la Mwaka 2019.
Kikao cha kwanza kitakuwa ni Kamati Kuu ya Chama itakayokutana Jumapili, Agosti 2, mwaka huu, itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba unaoelekezwa kwenye ibara ya 7.7.16(a) “Kufanya utafiti wa wagombea wa Urais na Mgombea Mwenza na kuwasilisha ripoti zake kwa Baraza Kuu.”
Tarehe 3, Agosti 2020, Baraza Kuu la Chama litakutana katika kikao chake, ambapo litajadili masuala mbalimbali ikiwemo “kufanya mapendekezo ya wagombea wa Urais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na kuyawasilisha katika Mkutano Mkuu kwa uamuzi,” inavyoelekezwa kwenye ibara ya 7.7.12(a).
Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 7.7.12 (n) Baraza Kuu litajadili rasimu ya Ilani (manifesto) ya Uchaguzi Mkuu na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mkutano Mkuu kwa maamuzi.
Tarehe 4, Agosti 2020, Mkutano Mkuu wa Chama utaketi na kutekeleza kazi zake, ikiwemo “kuteua mgombea wa Urais na mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa Zanzibar,” inavyoelekezwa kwenye ibara ya 7.7.10 (c). Halikadhalika, Mkutano Mkuu wa Chama utainidhinisha Ilani (manifesto) ya Chama kwa Uchaguzi Mkuu, kwa mujibu wa ibara ya 7.7.10 (h).
Vikao vyote kuanzia Agosti 2 hadi 4, 2020, vitafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa leo Jumamosi, Agosti 1, 2020 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano