Wangwe kuishitaki CHADEMA
na Mwandishi Wetu, Dodoma
ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chacha Wangwe, ambaye alisimamishwa uongozi juzi, amesema atakifikisha chama hicho mahakamani iwapo kitamzushia kashfa ambazo si za kweli.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, baada ya CHADEMA kutoa taarifa rasmi kuelezea kusimamishwa kwake katika nafasi ya makamu mwenyekiti, Wangwe aliwataka viongozi wa chama hicho wanaomtuhumu kwa mambo mbalimbali, kuyathibitisha madai yao, huku akionya na kusisitiza kuwa, iwapo watamzulia jambo lolote, atakwenda mahakamani.
"Hawawezi kunituhumu kwa masuala ya uongo. Inabidi wa-prove (wathibitishe) tuhuma wanazotoa dhidi yangu… kama wanasema nimevujisha nyaraka wathibitishe hivyo, kama wanasema nakihujumu chama wathibitishe pia," alisema Wangwe.
Hata hivyo, alikiri kusimamishwa uongozi, lakini akasema kusimamishwa kwake kumetokana na hila za Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambaye juzi katika mkutano wa Kamati Kuu alieleza kuwa hawezi na hataki kufanya kazi na yeye.
Alisema kuwa ni kweli uamuzi wa kusimamishwa kwake ulifikiwa kwa mujibu wa katiba ya chama hicho baada ya wajumbe wa Kamati Kuu kupiga kura ya kuafiki uamuzi huo, lakini alidai kuwa maamuzi hayo yalichagizwa na msimamo wa Mbowe.
"Tuhuma zote walizotoa walishawahi kuzitoa awali na nikazijibu… huu ni mwaka wa uchaguzi ndani ya CHADEMA, na nadhani wanafanya hivi kama sehemu ya kampeni dhidi yangu," alisema.
Aliliambia gazeti hili kuwa hivi sasa anataka kukata rufaa katika Baraza Kuu la chama hicho kwa sababu Kamati Kuu si chombo cha mwisho kufikia maamuzi kuhusu suala hilo.
Aidha, alisema anakusudia kuipeleka ajenda hiyo kwa wanachama, ili waweze kujua ukweli halisi kuhusu jambo hilo.
"(Viongozi wa CHADEMA) Wanajua kuwa kuna kundi kubwa la wanachama mikoani wananiunga mkono, kitendo chao kinalenga kuninyima jukwaa la kuzungumzia, lakini wanachama wananiamini na ndiyo maana waliamua kunipa jimbo Tarime na umakamu mwenyekiti mwaka jana," alisema.
Awali, viongozi kadhaa wa CHADEMA waliorodhesha tuhuma takriban nne, dhidi ya Wangwe, zilizosabisha asimamishwe kushika wadhifa huo.
Aidha, licha ya kufafanua tuhuma hizo akisaidiwa na viongozi wengine waandamizi, Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari mlolongo wa hatua zilizochukuliwa ili kumrejesha kiongozi huyo katika mstari.
Mbowe alisema Kamati Kuu ya chama hicho, iliyokutana mjini hapa juzi hadi usiku wa manane, ilifikia hatua ya kumsimamisha Wangwe baada ya wajumbe wa kamati hiyo kupiga kura za siri, kama ambavyo inaeleza sehemu ya katiba ya CHADEMA.
Ilielezwa katika mkutano huo wa waandishi wa habari kuwa, tangu Wangwe achaguliwe kukaimu nafasi hiyo, amekuwa akikisababishia chama matatizo kwani hana ushirikiano na viongozi wenzake na ameshiriki katika kufanya mambo kadhaa ambayo yanakihujumu chama hicho, akishirikiana na watu wengine wa nje wasioitakia CHADEMA mema.
Mbowe alisema kuwa chama hicho kinaongozwa na katiba, kanuni, maadili na itifaki, na inapotokea kiongozi akakiuka hayo, kama ambavyo Wangwe anatuhumiwa kufanya, chama hakiwezi kuulea udhaifu huo.
Orodha ya tuhuma zilizosababisha Kamati Kuu ya CHADEMA imsimamishe Wangwe katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, ilitolewa na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu Lissu.
Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Wangwe anajihusisha na makundi au kufanya vitendo vya uchochezi akishirikiana na mtu (jina tunalihifadhi) ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa CHADEMA kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliitaja tuhuma nyingine dhidi ya Wangwe kuwa ni kutoa tuhuma nzito, lakini zisizo na msingi wala ukweli dhidi ya viongozi wa juu na watendaji wa chama hicho bila kupitia taratibu mahsusi.
"Wangwe amesambaza vipeperushi na maandiko ya mkono wake, akikituhumu chama kwa ufujaji wa fedha na rasilimali, uzushi kuhusu kutotoa ruzuku mikoani na mahesabu ya chama wakati anajua kabisa kuwa Kamati Kuu inapokea na kupitia mahesabu yote ya chama," alisema Lissu.
Aliitaja tuhuma nyingine dhidi ya Wangwe kuwa ni kukikashifu chama, viongozi na watendaji wa chama wa ngazi za juu kwa kutumia njia zinazokiuka taratibu za chama na ukosoaji wa kisiasa.
Akiifafanua tuhuma hiyo, Lissu alisema kuwa Wangwe amekuwa akisambaza taarifa ya maandishi kuwa kuna ukabila ndani ya chama hicho, akielezea mgawanyo wa nafasi za ubunge wa viti maalum kuwa ni kigezo.
Hata hivyo, baadaye, Mkurugenzi wa Vijana wa chama hicho, John Mnyika alitoa ufafanuzi kuhusu taratibu zilizofanyika kuwapata wabunge hao na kueleza kuwa iwapo CHADEMA ingepata nafasi nyingi, ingekuwa na wabunge kutoka katika kila mkoa kwa mujibu wa orodha waliyoiwasilisha katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Lissu aliitaja tuhuma nyingine dhidi ya Wangwe kuwa ni kuvujisha taarifa za siri za vikao vya chama kwa lengo la kutaka kuonyesha kuwa anaonewa na kudhulumiwa ndani ya chama na baadhi ya viongozi na sekretarieti.
Akifafanua kuhusu tuhuma na hatua zilizochukuliwa dhidi ya Wangwe, Mbowe alisema kuwa kiongozi huyo amekosa ushirikiano mzuri na karibu viongozi wengine wote wa juu wa CHADEMA, wakiwamo wazee wa chama hicho na watendaji.
Alisema hali hiyo inakiathiri chama hicho na kudumaza demokrasia kwa jumla na kimeona ni bora kichukue hatua hizo pamoja na kuwa inafahamika kuwa zitakitikisa chama hicho, kwani ‘chama ni zaidi ya mtu'.
Akielezea hatua za kumrejesha Wangwe katika mstari, Mbowe alisema kuwa tayari wameshafanya vikao kadhaa, vikiwamo vya sekretarieti, yeye na katibu na Wangwe na vikao vya wazee, na amekuwa akikubali makosa na kuahidi kushirikiana, lakini hugeuka muda mfupi baada ya kutoka katika vikao hivyo.
Baadaye, Katibu Mkuu wa CHADEMA, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, Makamu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa wabunge wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alisema Wangwe, ambaye pia ni Mbunge wa Tarime, amekosa ushirikiano na wabunge wenzake na kambi nzima ya upinzani bungeni.