Bezecky
JF-Expert Member
- Apr 28, 2024
- 494
- 897
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ametoa maoni yake kuhusu hali ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akisisitiza kuwa chama hicho kilikumbwa na majeraha makubwa wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita na sasa kinahitaji kujenga umoja na mwelekeo mpya wa kisera.
"Siku moja nilisema wakati mnafanya kampeni zenu za uchaguzi CHADEMA, mlijeruhiana sana na sisi tunajua kazi yetu ni kama fundi nyundo, ukiwa unaezeka bati huangalii kwamba ni saa sita mchana huwezi kupanda juu kugonga msumari. Kufikisha ujumbe ndilo jukumu letu la msingi," amesema Balile.
"Mpaka ikafika hatua nikasema ama Tundu Lissu ama Mbowe atakayeshinda baada ya uchaguzi huu ninaamini ataanza kuzungumza kama Mwenyekiti. Wakati ule mlikuwa hamzungumzi kama Mwenyekiti bali kama wagombea."
"Nimeona CHADEMA ya Wenyeviti wote waliotangulia na sasa Tundu Lissu, mlikuwa na sera yenu ya majimbo, lakini haizungumzwi sana siku hizi," amesema Balile, akitaka kufahamu ikiwa sera hiyo bado ni nguzo muhimu kwa chama hicho.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa Tundu Lissu akizungumza wakati wa mkutano kati ya CHADEMA na Jukwaa la Wahariri (TEF)
"Hapa hatutazungumza sera zingine tutazungumza habari ya uchaguzi kwasababu tunatekeleza maamuzi ya chama chetu (CHADEMA), tunataka (Wahariri) mtuelewe, tunataka mkituelewa kama mnakubaliana na sisi na nyinyi muwe sehemu ya mapambano haya,"
"Vyombo vya habari ni sehemu muhimu sana ya mapambano haya na ni sehemu muhimu vilevile ya ukandamizaji, kwasababu wanaokandamiza si tu wanakandamiza vyombo vya habari lakini vilevile wanataka kuweka vyombo vya habari viwasaidie katika ukandamizaji wao. Vyombo vya habari vinaweza kutumika kama daraja la ukombozi na vinaweza kutumika na vimetumika katika historia kama vyombo vya ukandamizaji. Tunataka vyombo vya habari vya Tanzania vichague upande wa kuwa vyombo vya ukombozi, vyombo vya kuleta demokrasia katika nchi ya Tanzania."
"Sasa shida iko wapi? Kwanini kila tume inayoteuliwa (Ikiwamo Tume ya Jaji Warioba) inasema tufanye mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi? Huu mfumo wa uchaguzi una shida gani hasa? Na hii shida hii ndiyo inayoelezea sababu ya bila mabadiliko hakuna uchaguzi."
"Hiyo shida ndiyo tunayosema isipotatuliwa hakutakuwa na uchaguzi. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, lugha yangu ilikuwa bayana kabisa, tumesema siyo hatutasusia uchaguzi, tutazuia uchaguzi, lugha siyo kususia uchaguzi lugha ni kuzuia uchaguzi, na tumesema tutazuia uchaguzi kwa nguvu ya umma, tutawaalika Watanzania wahakikishe uchaguzi huu haufanyiki."
"Bila mabadiliko hakuna uchaguzi na siyo bila mabadiliko hatutashiriki uchaguzi, hiyo siyo lugha yetu, lugha yetu ni bila mabadiliko uchaguzi hautafanyika, ndiyo lengo letu. Sasa ni kwanini, hii lugha mbona kali sana, ni kwanini? Mfumo wetu wa uchaguzi una shida gani? na kwanini wazee waliopendekeza ubadilishwe kwanini walipendekeza hivyo? Una shida gani? Shida ya kwanza kabisa, mfumo wetu wa uchaguzi ni mfumo wa Rais, ambao unadhibitiwa kutoka juu mpaka chini ya Rais na mnafahamu Rais wa nchi hii ni Mwenyekiti wa CCM, na Marais wa CCM wametumia udhibiti wao wa mfumo wa uchaguzi kuhakikisha kwamba CCM inabaki madarakani kwa njia zozote, nyingi haramu"
"Majimbo haya yametengenezwa kwa upendeleo mkubwa sana – upendeleo kati ya Tanganyika na Zanzibar, kati ya miji na vijijini, na kati ya mikoa na mikoa. Matokeo yake, dhana ya usawa wa uwakilishi wa umma imevurugwa kabisa,"
"Jiulize, haya majimbo ni kwa ajili ya uchaguzi wa binadamu au kwa ajili ya kuangalia wapi tutaweka barabara na umeme? Kwa nini idadi ya watu haizingatiwi?"
"Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Jimbo la Temeke lilikuwa na wapiga kura 478,000 waliomsimamisha mbunge mmoja. Lakini kwa upande wa Zanzibar, majimbo yote 50 yalikuwa na wapiga kura 566,000 tu, ambao waliwachagua wabunge 50. Hii ina maana kwamba mbunge mmoja wa Temeke anawakilisha watu wengi zaidi kuliko wabunge wote wa Zanzibar kwa pamoja, lakini bado wote wanalipwa mshahara sawa na posho sawa."
"Utaratibu mzima wa kupiga kura umevurugwa na namna ya kuutengeneza kwanza ni kubadilisha Katiba ili kuwe na Haki ya Kikatiba ya kupiga kura, na pili Katiba iseme wapigakura na raia wa nchi hii na vyama vyao vya siasa wana haki ya kuthibitisha chochote inachokifanya Tume ya Uchaguzi, na ikikosea ishitakiwe mahakamani, sasa hivi haiwezekani."
"Utaratibu huu ndiyo uliokuwepo katika Katiba tuliyopewa na Waingereza mwaka 1961, katiba ya Waingereza ilikuwa bora kwenye masuala haya kuliko katiba ya Nyerere kuanzia mwaka 1962 mpaka hapa tulipo. Tumevuruga mambo muhimu kama haki ya kupiga kura"
Kupata taarifa na matukio yanayojiri kuelekea uchaguzi mkuu kwa kila mkoa ingia hapa: Special Thread: Mijadala na Matukio ya Uchaguzi Mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025