Tarehe 07/09/2017 huko Mjini Dodoma Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mh. Tundu Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limeibua hisia na mitazamo tofauti miongoni mwa wanajamii ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Baadhi ya watu wameituhumu serikali moja kwa moja kwamba imehusika na shambulio hilo, lakini swali langu ni “Je Lissu ameikosea serikali kiasi cha kustahili adhabu hiyo?”
Ni kweli kuwa tukio hilo linaweza kuwa limesabashwa na sababu mbalimbali, lakini kwa hatua hizi za mwanzo tukitanguliza sana hisia, tunaweza kumpa ushindi mhalifu aliyetekeleza uhalifu huo, kwa kumtengenezea kichaka cha hisia zetu ambamo ataweza kujificha.
Wachambuzi wengi walioweka hisia zao pembeni wamekuja na mitazamo tofauti. Kwa mfano mchambuzi maarufu wa masuala ya kiintelijensia EVARIST CHAHALI katika makala yake yenye kichwa “
Uchambuzi wa Kiintelijensia Kuhusu Jaribio la Kumuua Lissu: Wahusika Kina Nani?” (
Uchambuzi wa Kiintelijensia Kuhusu Jaribio la Kumuua Lissu: Wahusika Kina Nani ? ~ Kulikoni Ughaibuni) ametoa dhana tatu zinazoweza kuibua wahusika wa shambulio hilo ambazo ni mkono wa dola, mbio za urais 2020, na rogue elements. Na wachambuzi wengine wengi wameegemea katika mlengo huo huo.
Katika bandiko langu hili naipa uzito mdogo sana dhana ya kwanza inayodai kuwa serikali imehusika. Kwa nini? Ni kwamba uzalendo wa Lissu kwa nchi hii hauna mashaka hata kidogo (
His patriotism is indisputable). Ni kati ya watu wachache ambao kwa muda mrefu wamekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi mapana ya nchi yetu katika nyanja mbalimbali ikiwemo ile ya uchumi.
Kuna wachambuzi waliosema kumekuwa na misigano ya mara kwa mara kati serikali na Lissu hivyo serikali yaweza kuwa imehusika. Natofautiana na dhana hii, kwani lazima tukumbuke kuwa serikali inaongozwa na wanasiasa, ambao mbali na kuangalia maslahi ya nchi lakini pia kuna maslahi ya chama chao ambacho kimsingi ni utekelezaji wa ilani yao. Lissu ni mwanasiasa pia ambaye naye anaangalia namna bora ambavyo chama chake kinaweza kujijenga (To get political mileage) na hivyo kushika dola siku za usoni. Ndiyo maana mara zote amekuwa akiangalia udhaifu wa serikali iliyopo madarakani na kuutaja waziwazi. Kwa serikali iliyopo madarakani kupinga hoja za wapinzani ni kitu cha kawaida kwani lengo lake ni kutaka kuendelea kubaki madarakani.
Mara kadhaa tumewasikia wapinzani wakisema “
MAGUFULI ANATEKELEZA HOJA ZETU”. Hiyo inamaanisha kuwa licha ya kuwa Rais hasemi waziwazi kwamba anakubaliana na hoja zao lakini kama anazitekeleza, uadui unatoka wapi kiasi cha kustahili kifo?
Kwa mtazamo wangu, dhana ya pili na ya tatu (According to Chahali) zina uzito mkubwa sana. Lissu ni mwanasiasa aliyejijengea umaarufu mkubwa sana, kiasi cha watu wengine kuonesha hisia zao waziwazi na kumuita Rais wa Tanzania hapo 2020. Tukumbuke kuwa ndani ya chama chake cha CHADEMA kunaweza kuwa na watu ambao wana lengo la kupeperusha bendera katika uchaguzi wa 2020, na hivyo kugeuka kuwa maadui zake wa ndani. Kushushana kisiasa ndani ya chama kimoja kwa maslahi ya mtu au kikundi fulani, na hata kuuana sometimes si kitu kigeni ndani ya ulingo wa siasa. Tukumbuke kuwa ndani ya chama hicho yalishatokea mambo kadhaa hapo awali ambayo yalionekana kuwa na lengo hilo, mfano kifo cha mwanasiasa nguli Marehemu CHACHA WANGWE kiliibua hisia hizo. Aidha mara kadhaa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho enzi hizo ndugu Zitto Kabwe alipoonesha dalili za kupanda kisiasa wote tunajua nini kilitokea, na mara nyingine yeye mwenyewe alinena kwa kinywa chake kwamba anatishiwa maisha. Si hao tu na wengine wengi yamewakuta ya kuwakuta. Je hili la Lissu haliwezi kuwa katika mlengo huo ikizingatiwa kuwa kwa sasa ndiye pekee anayeonekana kukibeba chama hicho?
Tukija kwenye dhana ya tatu nayo ina uzito mkubwa sana kwani Rais kwa sasa ni wazi kuwa anapigana vita vigumu sana, vita dhidi ya wahujumu uchumi. Kwa kuzingatia kuwa “Kisisasa” Lissu ameonekana kuwa anapinga sana hoja na maamuzi ya serikali kumekuwa na mitazamo kwa baadhi ya watu kuwa Lissu ni adui wa serikali. Katika muktadha huo, maadui wa serikali “WAHUJUMU UCHUMI” wanaweza kuja na mbinu za kuhahikisha kwamba serikali iliyopo madarakani inaua wanaoipinga, na hivyo kujenga chuki kwa wananchi dhidi ya serikali yao, na mwaka 2020 wamuweke mgombea ambaye atatimiza matakwa yao, ambayo kimsingi ni kuifilisi nchi na watu wake. Dhana hii si ya kupuuza hata kidogo kwa watu walio na uelewa mzuri wa namna vita hiyo ilivyo. Kuinyooshea kidole serikali, maana yake ni kwamba tumekubali kuwapa ushindi hawa wezi wa mali zetu, ambao wametuingiza kwenye dimbwi la umaskini na kumwangusha Rais ambaye ndiye kiongozi wetu katika mapambano dhidi ya wezi hao.
WITO WANGU
Hima Watanzania tushirikiane na serikali yetu katika hii vita kubwa na ngumu dhidi ya wezi hawa wa maliasili zetu, wasiojali shida za Mtanzania wa chini na kutaka kujinufaisha wao na familia zao huku majority wakitaabika katika dimbwi la umaskini. Tukishikamana kwa pamoja, na kuweka hisia pembeni tutaushidha udhalimu huu.
BenMpo