Biswalo Mganga, mzaliwa wa kijiji cha Igala Wilayani Ukerewe, msomi wa sheria na miongoni mwa Watanzania wenye bahati sana katika teuzi, aliteuliwa kuwa DPP na Rais wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014. Alimrithi Elieza Feleshi ambaye mara moja aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.
Nafasi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa Taifa ni nafasi kubwa, nyeti na ambayo ikitumiwa vibaya inaweza kuathiri Uhuru wa mtu kimakosa, uchumi au hata maisha.
Tangu nafasi hii ianzishwe nchini, Biswalo Mganga anaweza kuwa DPP aliyefanya mabaya mengi kwa Watanzania wenzake kuliko mazuri waliyotarajia. "Biswalo" jina lenye asili ya Kikerewe likiwa na maana ya "Aibu" ni jina linalotumiwa na mtu aliye kinyume kabisa na maana halisi ya jina lake. Biswalo Mganga hana aibu, hana kabisa soni wala simile pale anapotekeleza kile alichoelekezwa na mkubwa wake kiwe kibaya au kizuri.
Ni katika uongozi wa Biswalo ulipoanzishwa utaratibu wa ovyo ambao awali haukuwepo kisheria lakini yeye bila AIBU aliuanzisha na alipoona anapigiwa kelele yeye na Mteuzi wake wakapeleka mswada wa dharura Bungeni. Huu ni utaratibu eti wa Ku Bargain kati ya mtuhumiwa wa uhujumu uchumi ambaye yuko Mahabusu na serikali kama mshitaki mkuu ikiwakilishwa na Biswalo Mganga. Wengi wameumia na kufilisika kwa utaratibu huu hasa pale ulipotumiwa vibaya.
Mtu anakamatwa anapewa kesi ya Uhujumu uchumi ambayo imewekewa sheria ya kutokuwa na dhamana kisha anapewa nafasi ya kuandika barua kuomba kuelewana na mshitaki wake na kwamba yuko tayari kulipa kiasi chochote cha fedha atakachotajiwa. Hivyo anatajiwa na akifikiria kuendelea kukaa Mahabusu na mateso yote yale anaona bora akubali.
NIJE KWENYE SABABU YENYEWE!
Baada ya utangulizi huo utaona jinsi ambavyo mtu huyu Biswalo asiye na Swalo (aibu) alivyojitengenezea maadui wasio na sababu ya kuwa maadui maana wengi hawakukosa kwa kiwango cha kutozwa kiasi kikubwa vile cha fedha. Wengine walioona fedha zao zinapotezwa bila kosa waliamua kubali mahabusu kuliko kuuza Uhuru wao kwa kukiri wasichotenda kama alivyofanya Rugemarila na Seth.
Ukichukua orodha ya waliofanyiwa hayo na wengine ambao bado wako ndani lakini ndugu zao wanahangaika bila mafanikio, utaona wigo wa maadui halali na wa bandia ulivyo mkubwa. Hivyo Mama Samia ambaye alikuwa anayaona madudu yote ya Biswalo na asingependa Serikali yake iendelee kuchafuliwa na kashifa za uonezi kama hii ya kuchukua fedha za watuhumiwa kwa kisingizio cha watuhumiwa kukiri kosa.
Hivyo ili kusafisha kashifa hiyo akaona ni muda sahihi kumweka pembeni, lakini kumweka pembeni mtu huyu na kumwacha akae bila kumwangalia huku akiwa na siri nyingi za serikali ya kikatili iliyopita ni kujivua nguo kwa serikali na chama chao. Hivyo amepelekwa kwenye nafasi ambayo ataendelea kulindwa muda wote ili kuhakikisha usalama wake na usalama wa siri za ukatili uliopita.