Kwenye shirikisho la afrika mashariki Rais wa Tanzania hatakuwa tena Amiri-Jeshi Mkuu ana jeshi la kuliamrisha ndani ya shirikisho? -- itamlazimu afanane na Rais wa serikali ya wanafunzi au Rais wa TFF asiye na majeshi. Urais ni jina tu au ni yale 'yatokanayo' na jina hilo? Hata kwa hili jamani midomo inakuwa mizito kuSEMA "NO!"?
Kwenye shirikisho la afrika mashariki, bunge la Tanzania litakuwa halina tofauti sana na bunge la watoto ambalo maamuzi yake hayana nguvu yoyote. Spika na wabunge wa Bunge la Mkoa wa Tanzania wakati huo watakuwa sawa tu na wachezao mchezo wa kuigiza. Maneno yote ya kibunge yatakuwa EAC, ndani ya shirikisho. Kwa sasa waheshimiwa Wabunge wetu 'wanapozwa' na maneno laini kwamba Bunge la Tanzania 'litabakia tu vilevile' kwenye shirikisho ili wasithubutu kuSEMA 'No" kwa EAC.
Walioko kwenye chama tawala CCM, wanashindwa kuSEMA "NO" kwa EAC kwa kudhani shirikisho litakapokuja, CCM itabakia kuwa CCM, chama tawala Jamhuri ya Tanzania. Wanasahau kwamba kwa kuanzisha "Jamhuri ya Muungano wa Shirikisho la Afrika Mashariki" maana yake hakutakuwepo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama hamna Jamhuri ya Tanzania, basi maana yake hakutakuwepo na chama tawala, chama cha upinzani, wala cha mageuzi. Siasa litakuwa suala la muungano wa shirikisho. Kama ambavyo si ruksa kuanzisha chama cha siasa upande mmoja tu wa Jamhuri ya Tanzania hivi sasa, ndivyo itakavyokuwa wakati huo. EAC itakuwa ni nchi moja pasipoti moja, vitambulivyo vya raia vimoja, Rais mmoja ambaye kwa kuanzia ni Yoweri Museveni. Kwa vile wote tutakuwa raia wa nchi moja, haitawezekana kumzuia raia mwenzio kufanya shughuli za siasa popote kwenye Jamhuri ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Hii ina maana Watutsi wa kutoka Rwanda wataruhusiwa kugombea ubunge Dar es Salaam, wakati ambapo Wazaramo wa Dar es Salaam wataweza kwenda kugombea ubunge Rwanda au Uganda. Je, Hayo ni mambo ambayo hatujui iwapo tunatakiwa kuSEMA 'No'?
Kodi inayokusanywa Tanzania, inaweza na bila shaka itatumiwa nje ya Tanzania, lakini ndani ya Jamhuri ya Shirikisho la Afrika Mashariki kwa kuwa Tanzania itakuwa ni kijimkoa tu cha EAC. TRA itakuwa imefutwa na badala yake kuanzishwa mamlaka ya mapato ya EAC. Kodi za wengine nazo huenda zikatumika Tanzania, iwapo wabunge kwenye EAC ya wakati huo watakuwemo wale ambao zamani walikuwa Watanzania, na wakaweza 'kasi mpya' ya kutwangana mingumi bungeni, kama wenzao walivyozoea. Hili nalo ni la kuvuta pumzi kusita kuSEMA 'No'?
Sasa ni wakati wa kuSEMA 'NO! HATUTAKI! hilo halina manufaa kwa nchi yetu na kwa hiyo hatutaki! Tuwe na msamiati wa hapana! Tusikubali kila kitu, mradi tu wameSEMA Wazungu au wamegawa posho za kushiriki mijadala.
Shirikisho ya afrika mashariki ni jaribio kwenye maisha ya Watanzania ambalo wazi matokeo yake yatakuwa mabaya mno kwa Tanzania na Watanzania.
EAC itamsaidia vipi mwananchi wa Tanzania kupata maisha bora? Tumchukulie huyu mwanakijiji aliyeko Nanjilinji, Kilwa.
*
Yeye maisha yake yataboreshwa vipi na shirikisho?
*
Ni kipi ambacho hakipati sasa hivi, nje ya Jamhuri ya Muungano wa Shirikisho la Afrika Mashariki, ambacho atakipata pindi Tanzania ikisitishwa kuwa Jamhuri na kugeuzwa mkoa mmoja wapo wa mikoa / majimbo ya Jamhuri ya Muungano wa Shirikisho la Afrika Mashariki?
*
Pana ulazima gani wa kufanya MAJARIBIO kwenye MAISHA ya mwanakijiji huyu kuona iwapo ataweza KUISHI Maisha Bora au Bora Maisha baada ya kumletea "ushindani" kutoka nje ya nchi kupitia shirikisho la afrika mashariki?
Watu ambao maisha yao hutumiwa kwenye majaribio ni wale ambao huonekana hawana thamani yoyote machoni pa wanaobuni jaribio. Yaani majaribio hufanyika kwa wale wanaotazamwa sawa tu na wanyama ambao wanaweza kutumiwa kwenye majaribio husika. Ni kweli Watanzania tumeshuka thamani kiasi cha kufanya majaribio kwenye nchi yetu na maisha yetu?
Wanaounga mkono jaribio la EAC kwenye maisha ya Watanzania wanatoa hoja kwamba "msiwe waoga" kufanyiwa majaribio haya. Wengine wamefikia hatua ya kuSEMA kwamba Watanzania ni watu wanaojali sana mambo ya nje kuliko ya kwao. Kwa hiyo Watanzania hawajui kuSEMA 'NO'. Ndivyo wadhanivyo. Na kuthibitisha hivyo wamekuja na wazo la kuSEMA "Watanzania hamuwezi, tena hamfai kujitawala wenyewe lazima mjiunge na EAC." "Hivi kweli Watanzania ninyi mnajua KuSEMA 'No'?" Ndiyo maana Wabunge walipokataa muswada wa Shirikisho, bado Tanzania ilibakia tu kwenye mchakato huo, kwa vile majirani zetu hawaamini iwapo "No!" inayosemwa na Watanzania inamaanisha kweli "NO!". Hoja ikarudi tena kinyemela, na zile sauti za "NO" hazisikiki tena.
Sasa hivi ule mkataba wa EAC uliopo umerudishwa uandikwe upya. Watawala wetu wameridhia uandikwe upya. Chochote kitakachoandikwa humo nani ana uhakika itasemwa "NO" na watawala wa Tanzania utakapofika wakati wa kusaini? Moja ya mageuzi makubwa kwenye kuandika upya mkataba huo ni kutoa uwezo wa kufikia maamuzi ya mwisho EAC kwa watu walioko kwenye ngazi ya uafisa mawizarani na siyo mawaziri kama ilivyo sasa, au marais kama ilivyokuwa EAC iliyokufa. Umefika wakati wa kuSEMA 'NO' kwa EAC.
Tanzania ijitoe EAC.
EAC ina tofauti ipi na COMESA? Kwa nini tusifanye kweli ya kuSEMA 'NO' kwa EAC, kama tulivyofanya COMESA?
Wale Watanzania wanajipatia rizki zao kwa sasa EAC, pamoja na wale wanaoishi kwa matumaini ya kunufaika binafsi EAC, serikali ya Tanzania iwafidie pesa zote ambazo wanatumainia kuzipata EAC.
Serikali, na hasa Bunge la Tanzania, lianzishe mchakato wa kuitoa Tanzania EAC. Ni wakati wa kuSEMA 'No' kwa EAC. Vyama vya mageuzi vipo nchi hii? Au vinangojea uchaguzi tu? Yaani hata vyama vya upinzani navyo havina msamiati wa kuSEMA 'NO' kwa EAC? Jambo la kutia moyo ni kwamba tayari wameshaanza kujitokeza viongozi wa vyama vya mageuzi kufanya kazi ya KuSEMA 'NO!' kwa EAC.
Burundi, Rwanda, Kenya, Sudan na Uganda, zinaweza kuendelea na shirikisho lao ndani ya EAC au IGAD kwa kushirikiana na Somalia, Ethiopia, Eritrea na Jibuti wakipenda. Tanzania tutaendelea na SADC. Hapa Tanzania wanaweza kuja kupiga stori tu. Mengineyo yote kwao. Kapu la mjanja, mjinga hatii mkono!
Email:
mlenge@yahoo.com
Simu: +255 75 4372902
Blogu:
http://mlenge.blog.com