Saturday, 22 November 2014
SAKATA LA ESCROW BUNGE KULIPUKA
SAKATA la akaunti ya Escrow limezidi kuchukua sura mpya, baada ya kuibuka mambo mazito ikiwemo taarifa za baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kudaiwa kuchukua rushwa kwa kampuni ya Independet Power Limited (IPTL).
Taarifa hiyo imekuja wakati ripoti ya uchunguzi wa akaunti hiyo ikitarajia kusomwa ndani ya bunge, ambapo imeelezwa kuwepo kwa makelele mengi ndani ya bunge kunatokana na baadhi ya wabunge kukosa mgawo wa fedha na wengine na wao kuchukua rushwa.
Nyaraka za malipo, ambazo gazeti hili ilizipata ambazo zinamuhusisha mtumishi wa bunge ambaye ni mmoja wa makatibu wa kamati ya PAC, Beatus Malima na wakili wa Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe aitwaye Alberto Msando, ambao walichukua milioni 10 kila mmoja kwa nyakati tofauti na kuzipeleka kwa wajumbe PAC ili waandae Ripoti itakayoonyesha kwamba kwenye IPTL haina Tatizo.
Katika vocha ya malipo iliyotoka PAP inamuonyesha April 8, 2014 Wakili Msando alipokea sh. milioni 10 kwa ajili PAC na Zitto kuandaa majibu ya malalamiko ya kampuni ya MECHMAR dhidi ya IPTL/PAP kazi ambayo inasemekana zitto aliifanya Machi 28, mwaka huu.
Taarifa zaidi zinaonyesha kwamba tarehe hiyo, mtumishi wa bunge anayefanya kazi na Kamati ya PAC, Beatus Malima naye alichukua kiasi kama hicho cha fedha kwa kazi hiyo hiyo
Msando alitambulishwa na Zitto kwa uongozi wa IPTL/PAP kama mshauri wake wa kisheria na mwanasheria hivyo chochote atakachowaambia ni maagizo kutoka kwake, ambapo Zitto alimtambulisha kwa Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, Harbinder Sethi baada ya kikao kirefu walichokifanya yeye na zitto kabla ya Mwenyekiti huyo wa PAC hajasafiri kwenda India kwenye matibabu ya marehemu mama yake, siku chache kabla ya malipo haya hayajafanyika.
Mmoja wa wabunge, ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema hili suala lina makandomakando mengi na wala si hayo yanayozungumzwa kwa kuwa PAP waliipata IPTL kwa kufuata taratibu zote kisheria pamoja na malipo waliyopewa katika akaunti ya Escrow yalikuwa halali kwao.
Taarifa hizo zilionyesha kuwa wakili huyo na mtumishi huyo waliendelea na utaratibu wa kuwa wanachukua pesa IPTL kwa sababu mbalimbali na mwishowe kuwapa maagizo kwamba itabidi PAC walipwe kiasi cha billioni 1.5 ili wazuie mjadala uliotarajia kuibuliwa kipindi hicho kuhusu sakata hilo.
"Hawa jamaa wanaonewa kwa kuwa kuna kundi kubwa la wafanyabiashara nyumba ya IPTL, ambao waliitaka kampuni hii lakini wameshindwa. Hawa hawana makosa yeyote na kinachofanyika ni kuwaonea na mvutano uliopo kwa wale waliokosa mshiko wao ndio wanatumiwa,''alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo, alisema "hebu fikiria, kama wangepewa hizo pesa walizoomba, je IPTL ingekuwa halali leo machoni mwao?, kwanini wawatese watu wasio na hatia kwa uroho na njaa zao binafsi?, ninakuhakikishia safari hii hatutakubali bunge kutumiwa kama kichaka cha watu kutimiza matakwa yao ya kisiasa baada ya kukosa hongo walizoomba" alisema.
Hivyo, alisema wabunge wengi wamejiandaa kueleza ukweli ndani ya bunge pamoja na kutoa mawasiliano ya simu kati ya wajumbe wa PAC na baadhi ya wabunge kuwaomba wawape nguvu katika suala hilo, pamoja na mawasiliano ya fedha kwa viongozi wa PAP yalivyokuwa yakifanyika.
HABARI MOTO: SAKATA LA ESCROW BUNGE KULIPUKA
SOURCE GAZETI UHURU, JAMII FORUMS