Hili ni jibu nilimwandikia mtu mahali fulani:
"...kadri utakavyojua na kujua huwezi ukaifahamu historia ya African Association kama alivyoijua Kleist Sykes na wanae au walivyoijua wajukuu zake Daisy Abdul Sykes na mdogo wake Kleist Abdul Sykes...au nilivyoijua mimi kufikia kuisahihisha historia iloyoandikwa na Chuo cha Kivukoni mwaka wa 1981 au kufikia mimi kuwa mmoja wa waandishi 500 kutoka kila pembe ya dunia walioandika Dictionary of African Biography (DAB), mradi wa Harvard na Oxford University Press, New York (2011).
Hizi ni volume sita.
Huwezi kuijua historia ya Tanganyika kwa kiasi cha kufanya mhadhara wa somo hilo kama nilivyofanya vyuo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania pamoja na Northwestern University, Evanston, Chicago chuo kinachoongoza duniani katika African History...bado hujafanyiwa review ya kazi yako yoyote katika Cambridge Journal of African History...kote huko nimepita "in flesh and blood."
Leo kwa taarifa yako limeundwa jopo likiongozwa na Prof. Shivji linaandika historia ya Mwalimu Nyerere na nimefanyanao mahojiano nyumbani kwangu mara mbili na nimewapa nyaraka na picha.
Wao wameamua kufanya hilo katika kuiweka sawa historia ya uhuru wa Tanganyika na kitabu cha Abdul Sykes ndicho chanzo.
Sidhani kama wewe una lolote la kumstaajabisha yeyote.
Lakini eleza unachojua tutakusikiliza.
Nimetaabika kusema haya lakini imebidi ili tufahamiane vizuri.''
MRADI WA DICTIONARY OF AFRICAN BIOGRAPHY (DAB) MWAKA WA 2008
Baada ya matatizo yaliyoniandama katika vitabu hivyo viwili nilivyoandika siku moja mwaka wa 2008 nikapokea email kutoka kwa Prof. Emmanuel Akyeampong kutoka Harvard akaniomba niwe mmoja wa waandishi karibu 500 kutoka kila pembe ya dunia watakaoandika kamusi ya watu mashuhuri Afrika.
Mradi huu ulikuwa unajulikana kama Dictionary of African Biography.
Huu ulikuwa mradi wa Harvard na Oxford University Press New York.
Prof. Akyeampong akaniomba pia niwe mshauri wake kwa majina ya Watanzania ambao mimi naona wamefanya makubwa kwa hiyo wanastahili maisha yao kuandikwa katika hii kamusi.
Prof. Akyeampong akaniomba mimi niandike maisha ya Kleist Sykes yeye akimkusudia Kleist Abdulwahid Sykes.
Mimi hapo hapo nikaanza kazi yangu ya ushauri.
Nikalikata jina la Mayor wa Jiji la Dar es Salaam rafiki na ndugu yangu Kleist, nikamshauri kuwa anaestahili kuingia katika DAB ni babu yake, Kleist Sykes Mbuwane (1894 - 1949) na si huyu Kleist mtoto wa Abdul Sykes.
Prof. Akyeampong alivutiwa sana na kile alichosoma kuhusu babu yake Kleist Abdulwahid na kamusi ilipochapwa mwaka wa 2011 maisha ya Kleist Sykes Mbuwane babu yake Kleist Abdulwahid yakawa ndani ya DAB.
Abdul na Ally na wao pia wametajwa pamoja na baba yao katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.
DAB ina volume sita na ni maarufu hivi sasa duniani kama kitabu vya rejea kwa watu mashuhuri na mashujaa wa Bara la Afrika.
