JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema hadi kufika hapa siku ya leo, napenda kuwashukuru nyote kwa kuja, tunapoungana kwa ajili ya kuadhimisha siku ya mtoto njiti Duniani leo tarehe 17 Novemba 2020. Aidha ninayo furaha kuwa sehemu ya maadhimisho haya, jambo muhimu kwa taifa na kwa afya ya watoto njiti wote Tanzania.
Kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wadau wa maendeleo na wadau binafsi kama “Doris Mollel Foundation, ambao wanafanya kazi ya kunusuru maisha ya watoto njiti nchini. Kwa mara nyingine leo hii, sote tunaalikwa kutathimini na kuangalia namna bora tunayoweza kutatua changamoto ya maisha ya watoto njiti nchini.
Mabibi na Mabwana, Watoto njiti huhitaji uangalifu wa karibu na huduma ya kipekee kutoka kwa, wazazi/walezi na watoa huduma za afya hususuni wauguzi ili waweze kuendelea kuishi, hivyo huwapasa wazazi (hususani mama) kutokuwa na majukumu mengine kwa kipindi kirefu. Kuzaliwa kabla ya muda ni mojawapo ya sababu za vifo kwa watoto wa chini ya miaka mitano, na hii ndiyo sababu iliyotukusanya sote hapa leo kuendeleza juhudi zetu kwa kuhakikisha kwamba, kila mtoto anayezaliwa, anaendelea kuishi huku wazazi wote wakichukua jukumu la kumtunza.
Mabibi na Mabwana, Vifo vya watoto wachanga bado ni tatizo kubwa hapa nchini. Kwa mujibu wa takwimu za TDHS 2015/16, vifo hivi vinachangia kwa takribani asilimia 40 ya vifo vyote vya watoto chini ya miaka mitano, vinavyotokea hapa nchni, saw ana jumla ya vifo 39,500 kwa mwaka. Aidha, taarifa ya Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto inaonesha jumla ya vifo vya Watoto wachanga 11,524 na 9,681 vilitolewa taarifa kwa mwaka 2018 na 2019. Aidha, Takwimu zinaonesha Watoto wachanga 25 kati ya 100 hufa kutokana na matatizo yanayoambatana na kuzaliwa na uzito pungufu, ambapo wengi wao ni wale wanaozaliwa kabla ya wakati.
Mabibi na Mabwana, Mtoto kuzaliwa kabla ya wakati (premature), ni pale ambapo mtoto huzaliza kabla ya mimba kukamilisha wiki 37 za ujauzito, yaani mimba kukomaa. Hapa nchini tatizo hili ni kubwa, Taarifa ya “World Population Prospects” ya mwaka 2013 inaonesha Tanzania ni kati ya nchi 20 Duniani zinazoongoza kwa kuzaliwa watoto njiti, ambapo takribani Watoto njiti 236,000 huzaliwa, na 10,800 hufa kila mwaka (January 2016, EveryPreemie.org).
Mabibi na Mabwana, Watoto njiti huwa katika hatari zaidi ya kupoteza maisha ukilinganisha na watoto wanaozaliwa baada kukamilisha wiki 37 ya umri wa mimba. Inakadiriwa watoto njiti wako kwenye hatari hiyo mara 6 hadi 26 zaidi, ukilinganisha na waliozaliwa baada ya kukomaa. Siyo tu hatari ya kufa lakini pia watoto njiti wako kwenye hatari ya kupatwa na vilema mbalimbali maishani kama vile matatizo ya kuona na kusikia, matatizo ya mapafu na moyo, n.k.
Mabibi na Mabwana, Kuna sababu tofautitofauti zinazopelekea mtoto kuzaliwa njiti; sababu za upande wa mama inawezakuwa ni historia ya kuzaa mtoto njiti, umri wa mama mjamzito, mimba za karibu karibu, kutokupata muda wa kupumzika wakati wa ujauzito, lishe duni, magonjwa mbalimbali/uambukizo wakati wa ujauzito, upungufu wa damu, shinikizo la damu, hali ya kondo la uzazi na mtoto mchanga tumboni. Hivyo ni muhimu kwa mjamzito yeyote kunaza Kliniki mapema mara tu anapojigundua kuwa mjamzito na kuhudhuria Kliniki ipasavyo katika kipindi chote cha ujauzito. Hii itamsaidia kuchunguzwa na kufaham maendeleo ya mama na mtoto wakati wote wa ujauzito, kupewa matibabu yanayohitajika na kupewa ushauri nasaha ikiwemo lishe ya mama mjamzito na mtoto mchanga.
Mabibi na Mabwana, Ili kutatua changamoto hizi, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha huduma za afya ya Uzazi na Mtoto katika kuboresha huduma za Kliniki kwa mama mjamzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, na huduma kwa watoto wachanga waliozaliwa njiti, kama ifuatavyo;
Kuwapatia wajawazito dawa (corticosteroids) ya kusaidia mapafu ya mtoto kukomaa haraka iwapo mama ana dalili/hatari ya kujifungua kabla ya wakati/mtoto njiti. Watoto njiti wanakabiliwa na hatari ya kushindwa kupumua mara wanapozaliwa kutokana na kutokomaa kwa mapafu, hivyo afua hii inalenga kuwawezesha kupumua.
Huduma ya Mama Kangaruu katika ngazi ya hospitali na Vituo vya afya ili watoto njiti watunzwe ngozi kwa ngozi na mzazi au mlezi ili watunze joto. Watoto njiti wanaweza kufa kutokana na
- Kupoteza joto, na miili yao haiwezi kuzalisha na kutunza joto kwa kiasi cha kutosha, kama ilivyo kwa Watoto wengine.
- Uanzishaji wa vyumba maalum kwa ajili ya matibabu ya Watoto wachanga wagonjwa kwenye baadhi ngazi ya hospitali , na kuwajengea uwezo Watoa huduma wa afya.
- Ununuzi wa dawa na vifaa tiba muhimu kwa ajili ya matibabu ya watoto wachanga wagonjwa.
- Kutayarisha miongozo mbalimbali inayolenga kuboresha Afya ya Uzazi na Mtoto nchini
- Wajawazito wote wahudhurie Kliniki ipasavyo, wajifungulie kwenye vituo vya kutolea huduma na wahudhurie Kliniki baada ya kujifungua ili mama na mtoto mchanga wapatiwe huduma ya afya stahiki.
- Halmshauri na wadau kusaidia zoezi la uanzishaji wa vyumba maalum vya matibabu ya Watoto wachanga wagonjwa (NCU),ikihusisha chumba cha mama Kangaruu, kujenga uwezo wa watoa huduma na vituo vya kutolea huduma ili vitoe huduma bora kwa Watoto wachanga wote ikiwemo Watoto njiti.
- Jamii kwa ujumla ihamasike na kufahamu kuwa lishe bora, kumpunguzia kazi mama mjamzito, kumsindikiza Kliniki kwa ajili ya ujunguzi na matibabu ni miongoni mwa mambo muhimu katika kuepusha mama mjamzito kuzaa mtoto njiti. Aidha mama aliyejifungua mtoto njiti anapaswa kusaidiwa kumhudumia mtoto njiti nyumbani.
ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA
Dkt. LEONARD SUBI
MKURUGENZI WAKINGA
17 NOV 2020
Dkt. LEONARD SUBI
MKURUGENZI WAKINGA
17 NOV 2020
Upvote
1