Uchaguzi 2020 Hotuba ya Tundu Lissu kutangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Juni 08, 2020

Uchaguzi 2020 Hotuba ya Tundu Lissu kutangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - Juni 08, 2020

Kawadanganye mbumbumbu wenzako
Nitajie mwanasiasa mmoja unayemjua aliyewahi kutangaza kugombea urais wa nchi yake akiwa nje ya nchi na akaupata. Kijibu, una chupa kubwa mbili za K Vant hapa hapa Diamond, Kona ya Bwiru. Ahahahahahahah!
 
Huyu ndiye RAIS tusidanganyane watanzania, wakati mwingine tujiongeze wenyewe.
 
Nitajie mwanasiasa mmoja unayemjua aliyewahi kutangaza kugombea urais wa nchi yake akiwa nje ya nchi na akaupata. Kijibu, una chupa kubwa mbili za K Vant hapa hapa Diamond, Kona ya Bwiru. Ahahahahahahah!
Hahaha wazee wa Mbunga za wanyama kule Chatto mumepaniki sana. Tulieni dawa iwaingie vizuri
 
He's untrainable due to his stuborness... eventually they will let him stead his own ship..
Hapana chama chake kinaweza m-shape. Kwa mfano timu ya kampeni sharti imsaidie kuandaa hotuba zake. Inawezekana wakampa semina hiyo na akabadirika kwa maslahi ya emage ya chama. Unajua timu ya kampeni ikiwa organized inaweza kuleta impact mpaka kwa mgombea.
Huwa kuna kuandaa hotuba na mgombea anaweza pewa vimemo kuhusu maswala flani flani akiwa anahutubia.
Public speaking is an art sema Lissu yupo too emotional na ndio anapoharibu.
 


Hotuba ya Tundu Lissu, FULL TEXT:

KWANINI NAGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA?

Wananchi na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania popote walipo, ndani na nje ya nchi yetu;

Wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA);

Marafiki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki, ukanda wa Kusini mwa Afrika, Umoja wa Afrika na katika jumuiya ya kimataifa kwa ujumla;

UTANGULIZI

Kama ambavyo imekuwa jadi ya nchi yetu, siku ya Jumapili ya mwisho ya mwezi Oktoba wa kila mwaka wa tano, sisi raia wa Tanzania hupiga kura ili kuwachagua viongozi wetu wa ngazi mbali mbali. Sasa kipindi hicho kimewadia. Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, na tarehe 25 Oktoba 2020, Jumapili ya mwisho ya mwezi huo, sisi wananchi katika wingi wetu, tutafurika katika vituo vya kupigia kura katika sehemu mbali mbali za nchi yetu kwa lengo la kufanya hiyo sala ya raia walio huru, yaani kuchagua viongozi wetu.

Kama ambavyo nimewahi kugusia siku za nyuma, sasa napenda kuwataarifu kwamba nimetangaza rasmi nia yangu ya kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Tayari nimeshawasilisha taarifa rasmi ya kutangaza nia hiyo kwa Katibu Mkuu wetu wa Chama, kama ilivyoelekezwa kwenye maelekezo yake kwa wanachama wa chama chetu. Nina wajibu wa kutaja kile ambacho kimenisukuma kutaka kugombea nafasi ya juu kabisa ya uongozi katika mfumo wetu wa kikatiba, yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano.

NCHI IKO NJIA PANDA

Kwa kipindi cha miaka mitano itakayoishia Oktoba mwaka huu, nchi yetu imetawaliwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa namna ambayo imeiweka nchi yetu katika mtihani mkubwa kiuchumi, kisiasa na kidiplomasia. Kwa mtihani huo, nchi yetu iko katika njia panda na, kwa vyovyote vile itakavyokuwa, Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa na umuhimu mkubwa katika historia ya nchi yetu.

UCHUMI UMEANGUKA

Badala ya kuzingatia mazingira haya halisi ya kiuchumi ndani na nje ya nchi yetu, Rais Magufuli ameendesha uchumi wetu bila sera au mipango madhubuti ya uchumi, bali kwa kutumia amri za Ikulu na za majukwaa ya kisiasa. Bila sera inayoeleweka au mipango thabiti ya kiuchumi au kibiashara, sasa Serikali yetu imejiingiza kwenye biashara, kuanzia ya kununua na kuuza mazao ya biashara, mabenki, uchimbaji madini hadi biashara ya kuendesha shirika la ndege.

Kwa kutumia njia hizo za amri za kisiasa, vyombo vya ulinzi na usalama, vikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS) pamoja na Mamlaka ya Kodi (TRA) vimetumika kukamata kwa nguvu na kutaifisha mali za wafanya biashara wetu wa ndani na makampuni ya wawekezaji kutoka nje.

Hata wakulima wadogo wa vijijini hawajaachwa salama, kama ilivyotokea kwenye zao la korosho kwenye mikoa ya Kusini mwaka jana ambako wakulima walinyang’anywa mazao yao kwa nguvu za kijeshi na ukatili mkubwa kwa amri ya Rais Magufuli mwenyewe. Badala ya kulipwa bei kubwa kama walivyoahidiwa na Rais, wakulima hao walidhulumiwa fedha zao na wameachwa katika umaskini mkubwa. Hivi ndivyo ilivyotokea pia kwa wafanya biashara wa maduka ya fedha za kigeni ambao walivamiwa na askari wa Jeshi la Wananchi na maafisa wa Benki Kuu na kunyang’anywa fedha na mali zao nyingine.

Ili kupata fedha za kuendeshea miradi yake ya miundo mbinu, Serikali ya Rais Magufuli imekusanya kodi kutoka kwa kila mwananchi na kila mfanya bishara, mkubwa na mdogo, kwa ukatili mkubwa. Wafanya biashara wamebambikiziwa kodi kubwa ambazo hazilingani na mapato yao au hali ya biashara zao. Wasioweza kulipa kodi hizo za kubambikiza sio tu wamefilisiwa, bali wengi wao wameshtakiwa kwa makosa makubwa ya kiuchumi ambayo hayana dhamana. Wengi wanaozea katika magereza mbali mbali ya nchi yetu kwa sababu ya kushindwa kulipa gharama kubwa wanazodaiwa kulipa ili kununua uhuru wao. Wengine hata wamefia magerezani au kutokana na mshtuko wa kunyang’anywa mali zao bila utaratibu.

Matokeo ya sera hizi za kiuchumi za Rais Magufuli yameonekana wazi. Uchumi wetu umeanguka; wafanya biashara wengi na wawekezaji kutoka nje ya nchi wamefunga biashara au kusitisha uwekezaji wao; na wengine wamekimbiza biashara na mitaji yao nchi za nje. Hali hii imesababisha mapato ya serikali kuanguka vibaya; ukosefu mkubwa wa ajira na umaskini wa wananchi wetu, hasa vijana na wanawake, umeongezeka. Hali ya kiuchumi ya wananchi wetu leo ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa wakati Rais Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015 na kabla ya hapo.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utaamua kama Rais Magufuli atapata fursa ya miaka mitano mingine ya kuendelea kuharibu uchumi wetu na kuwafukarisha wananchi wetu, au kama tutaanza na mwanzo mpya wa kiuchumi kwa nchi yetu kwa kumuondoa yeye na chama chake madarakani.

NCHI YA WAJANE, YATIMA NA VILEMA

Tangu mwaka 1984, nchi yetu imekuwa na Hati ya Haki za Binadamu katika Katiba yetu, ambayo imeweka na kufafanua haki mbali mbali za binadamu na wajibu wa wananchi. Ndani ya miaka mitano ya utawala huu, utaratibu wote wa haki za binadamu na utawala wa sheria umechanwa chanwa vipande na Serikali ya Rais Magufuli na vyombo vyake vya ulinzi na usalama.

Tanzania imekuwa nchi ya vilio na machozi ya wajane, yatima na vilema wa viungo na wa kisaikolojia wa miaka mitano ya utawala wa Rais Magufuli. Upotezaji watu, utekaji nyara, utesaji na ukandamizaji wa wakosoaji wa serikali kwa kuwafungulia kesi za kubambikiza za uchochezi, makosa ya mtandao au utakatishaji fedha. Mauaji ya wananchi wasio na hatia yoyote na wapinzani wa serikali na chama tawala. Haya ni baadhi tu ya matendo mabaya yaliyokithiri sana katika Tanzania ya Magufuli.

Hakuna aliyeachwa salama. Viongozi wa kisiasa, kama marehemu Alfons Mawazo, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita, aliyekatwa katwa mapanga na kutupwa bararabani mchana kweupe. Au Diwani Simon Kanguye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma, aliyechukuliwa na watu wanaosemekana kuwa maafisa usalama wa taifa na kutokomezwa kusikjulikana. Wanaharakati wa mitandaoni na waandishi habari, kama Ben Saanane, msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, aliyenaswa na ‘watu wasiojulikana’ na kupotezwa hadi leo. Au mwandishi habari Azory Gwanda, aliyechukuliwa nyumbani kwake na watu waliojitambulisha kuwa askari polisi na hadi leo hajulikani alipo. Hawa ni baadhi tu ya wahanga wa Tanzania ya Magufuli.

Wapo pia wasanii, kama wanamuziki wa kizazi kipya Roma Mkatoliki na Ney wa Mitego, waliokamatwa na kuteswa katika nyumba za siri za kutesea watu, kabla ya kuachiliwa huru baada ya siku kadhaa. Au wafanyabiashara na matajiri, kama Mo Dewji aliyedakwa nje ya hoteli na kupotezwa kabla ya kutupwa mita mia kadhaa kutoka Ikulu ya Dar es Salaam. Wanafunzi, kama Aquilina Aquiline, aliyepigwa risasi na askari polisi wakati akiwa kwenye dala dala kuelekea chuoni kwake. Orodha ya wahanga wa utawala huu ni ndefu na ya kuhuzunisha.

Matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya wananchi wanaotekeleza haki na wajibu wao kikatiba yamekuwa makubwa. Utamaduni wa kutowawajibisha wale wote wanaohusika na mauaji na mateso haya ya Watanzania umekithiri. Imekuwa ni jambo la kawaida kwa vyombo vya usalama vya nchi yetu kuua au kujeruhi raia wasiokuwa na hatia bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Ukweli kwamba natolea tangazo hili la nia ya kugomea Urais nikiwa uhamishoni barani Ulaya, badala ya kulitolea nikiwa ndani ya nchi nilikozaliwa na kukulia, ni ushahidi tosha wa majanga makubwa ambayo yameikumba nchi yetu katika miaka hii mitano ya utawala wa Rais Magufuli.

Uchaguzi Mkuu huu utaonyesha ni kwa kiasi gani wananchi wa Tanzania hawako tayari tena kuendelea kuonewa, kudhalilishwa na kunyanyaswa na wale waliowapa dhamana ya kuwaongoza, au kama bado wako tayari kuendelea kuwa kwenye minyororo hii. Uchaguzi Mkuu huu utaamua kama vilio hivi vya wajane, yatima na vilema vitapata Mfariji Mkuu wa kuvituliza, atakayefuta machozi ya wanaolia na atakayeponya majeraha na makovu mengi ya Tanzania ya Magufuli, au kama Mtesaji Mkuu atapata miaka mingine mitano ya kuongeza majeraha, vilio na machozi haya.

UTAWALA WA KIIMLA

Tangu nchi yetu ilipoingia katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, mfumo huo wa kidemokrasia umekua na kukomaa kama ushahidi wa chaguzi mbali mbali zilizofanyika tangu wakati huo unavyodhihirisha. Hata hivyo, tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ametangaza vita kubwa dhidi ya mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi vya siasa. Yeye mwenyewe alitangaza hadharani, wakati wa maadhimisho ya miaka 39 ya CCM mwezi Februari 2016, kwamba atahakikisha hakuna tena vyama vya upinzani ifikapo mwaka 2020, yaani mwaka huu.

Wote tumeshuhudia utekelezaji wa ahadi yake hiyo kwa vita kubwa ambayo imeendeshwa dhidi ya viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama halisi vya upinzani, hasa CHADEMA na, kwa upande wa Zanzibar, ACT Wazalendo. Mfumo wa vyama vingi vya siasa umewekwa kwenye hatari kubwa na ya kipekee. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utaamua kama Rais Magufuli anafanikiwa kutekeleza azma yake ya kuua mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi na kuirudisha nchi yetu katika zama za giza za mfumo wa chama kimoja, au kama mfumo huo wa kidemokrasia utadumu na kushamiri katika nchi yetu.

BUNGE DHAIFU

Sambamba na vita dhidi ya mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi, Rais Magufuli ameendesha vita kubwa dhidi ya Bunge na Mahakama. Historia ya Bunge letu la tangu Uhuru sio ya kujivunia sana. Ukiachia miaka michache ya mwanzo ya Uhuru na miaka kumi ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Bunge letu lilikuwa bubu, kiziwi, kipofu na butu. Bunge lilianza kupata nguvu baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 na hasa kuanzia Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995. Baada ya hapo mamlaka, hadhi na heshima ya Bunge letu iliongezeka, hasa katika miaka kumi ya Rais Kikwete iliyoishia mwaka 2015.

Ni heshima kubwa kwa marais wa nchi yetu wa wakati wa vyama vingi, hasa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwamba wakati wa utawala wao, Bunge letu lilipata nguvu na heshima kubwa mbele ya wananchi na katika jamii ya kimataifa. Ni heshima kubwa kwa Maspika wa Bunge letu wa kipindi hicho, hasa marehemu Samuel John Sitta na Mheshimiwa Anna Semamba Makinda, kwamba katika uongozi wao wa Bunge letu, Bunge lilipata sauti ya kusemea, masikio ya kusikia, macho ya kuona na meno ya kuuma katika kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali.

Bunge la Tanzania ya Magufuli, chini ya uongozi dhaifu wa Spika Job Yustino Ndugai, limeingiliwa, kuvurugwa na kutekwa nyara na Serikali ya Magufuli kwa namna ambayo halina tofauti tena na Bunge la Tanzania ya zama ya chama kushika hatamu, hasa la kati ya miaka ya 1965 na 1985. Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 utaamua kama tutarudi kwenye Bunge linalojitambua, kama la marehemu Spika Sitta na la Mama Makinda, au kama tutaongezewa miaka mingine mitano ya Bunge lililopoteza mwelekeo kama hili la Spika Ndugai.

MAHAKAMA MATEKA

Rais Magufuli ameingilia na kuvuruga uhuru wa Mahakama ya Tanzania kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia yetu yote. Amewatisha na kuwadhalilisha hadharani majaji wa mahakama zetu za juu. Ameondoa baadhi ya majaji kinyume na utaratibu uliowekwa na Katiba ya nchi yetu. Ameingilia utendaji wao wa kazi kwa kuwaelekeza namna ya kufanya kazi zao wakati yeye sio mwanasheria. Ametoa ahadi za kuizawadia Mahakama endapo itawatia hatiani watuhumiwa wa kesi za kubambikiza za serikali yake. Ameahidi hadharani kuwapandisha vyeo mahakimu waliowafunga wapinzani wa CCM na kuwafanya Majaji wa Mahakama Kuu.

Matokeo ya vitendo hivi vya Rais Magufuli ni kwamba, Mahakama imekuwa sehemu kubwa ya kukandamizia haki za binadamu za wananchi wetu. Badala ya kuwa chombo cha kulinda Katiba yetu, haki za binadamu na utawala wa sheria, Mahakama imegeuzwa na utawala huu kuwa chombo cha kukandamizia haki kwa kunyima watuhumiwa wa kesi za kubambikizia dhamana ; kuwarubuni majaji na mahakimu wetu ili watoe adhabu kali kwa wapinzani wa serikali, au watumie visingizio vya kiufundi vya kisheria ili kukwepa kutenda haki ya msingi kwa mujibu wa sheria.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utaamua kama tutaendelea kuwa na Mahakama inayotumika kukanyaga haki za wananchi, au tutakuwa na Mahakama itakayolinda misingi muhimu ya kikatiba na haki za binadamu za wananchi wetu.

‘FUNGO WA KIMATAIFA’

Ndugu wananchi,

Rais wa nchi yoyote ile ni Mwanadiplomasia Mkuu wa nchi yake. Kwa takriban robo karne ya uongozi wake, Baba wa Taifa aliiweka Tanzania yetu katika ramani ya kidiplomasia ya kimataifa. Tulitengeneza marafiki na washirika wa maendeleo katika pande zote mbili za Vita Baridi. Tulitengeneza mshikamano na mahusiano ya karibu na nchi za Afrika Mashariki. Tulikuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika; na tulikuwa kinara katika harakati za kuunganisha nguvu za Bara la Afrika na Ulimwengu wa Tatu.

Nchi yetu na viongozi wake waliheshimika kila mahali duniani. Tuliielewa na kuiheshimu dunia, na dunia ilituelewa na kutuheshimu. Kwa sababu ya kuwa na mahusiano hayo mema na jumuiya ya kimataifa, nchi yetu ilifaidika sana na fursa na misaada mbali mbali ya jumuiya ya kimataifa. Tulijengewa reli ya TAZARA na Wachina; na tulijengewa Kitivo cha Uhandisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo kadhaa vya ufundi na Wajerumani Magharibi. Tuliletewa chakula cha njaa cha mahindi ya yanga na unga wa dona na Wamarekani na tulijengewa shule za sekondari za kilimo na Wakuba. Msingi wa diplomasia ya kimataifa uliowekwa na Baba wa Taifa uliendelezwa na warithi wake katika Ikulu yetu.

Hata hivyo, tangu aingie madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli ameharibu mahusiano yetu na jumuiya ya kimataifa. Ametutenganisha na kila rafiki tuliyekuwa naye miaka ya nyuma. Ametutenganisha na majirani zetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; na ndugu zetu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambao tuliwatolea damu yetu ili wajikomboe, na katika Umoja wa Afrika. Ametufarakanisha hata na mashirika muhimu ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa na taasisi zake kama WHO. Ametugombanisha na Umoja wa Ulaya na marafiki zetu wa kihistoria kuanzia China iliyoko mashariki hadi Marekani iliyoko magharibi.

Sasa nchi yetu inasemwa vibaya katika mabaraza ya kimataifa na inatengwa au kuwekewa vikwazo katika misaada, fursa na manufaa mengi yatokanayo na diplomasia yenye busara na akili. Leo kila chombo cha habari cha kimataifa kinachoandika habari za Tanzania kinaanza kwa kutaja jinsi Rais wetu asivyoendana na taratibu zinaoeleweka na kukubalika kimataifa. Kama nilivyosema miaka miwili na nusu iliyopita, nchi yetu imekuwa ‘fungo wa kimataifa.’ Fungo ni mnyama wa jamii ya nguchiro ambaye akifukuzwa anatoa harufu mbaya inayowafukuza wale wote wanaomkimbiza.

Badala ya kujirudi na kujirekebisha, viongozi wa serikali yetu, wamekuwa wanawatukana marafiki zetu wa tangu Uhuru kwa kuwaita ‘mabeberu’ na kufukuza au kuwasumbua mabalozi na wawakilishi wao hapa kwetu. Uchaguzi Mkuu wa mwaka utaamua kama sisi tutaendelea kujifanya kisiwa katika bahari pana ya mahusiano ya kidiplomasia ya kimataifa, au tutajirudi na kutambua kwamba sisi ndio tunaoihitaji dunia kuliko dunia inavyotuhitaji sisi.

KATIBA MPYA

Mwaka 1978 Rais wetu wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitamka, katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza (BBC), kwamba alikuwa na mamlaka, kwa mujibu wa Katiba na sheria za yetu, ya kuwa dikteta. Katiba aliyokuwa anaizungumzia Baba wa Taifa wakati huo ni hii hii tuliyonayo leo. Na sheria alizokuwa anazizungumzia bado zipo na nyingine nyingi zimeongezwa katika kipindi hiki cha Tanzania ya Magufuli.

Katika miaka mitano ya utawala wake, Rais Magufuli ametufundisha somo kubwa na lisilosahaulika la umuhimu wa Katiba Mpya na kuwa na mfumo wa kisheria ulio wa haki na unaozingatia haki na utu wa binadamu. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utaamua kama tumelielewa somo hili kubwa na tuko tayari kuendelea kuwa na katiba na sheria zinazotengeneza watawala wenye mamlaka ya kidikteta, au kama tutarudi kwenye mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya uliovurugwa na wanaCCM mwaka 2014.

SASA, BAADA YA YOTE HAYA NILIYOYALALAMIKIA, JE, NI KITU GANI NITAKIFANYA TOFAUTI ENDAPO NITAPATA HESHIMA, IMANI NA DHAMANA YA KUWAONGOZA WANANCHI KAMA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO?

  • Endapo nitachaguliwa kuwa Rais, Serikali yangu itaandaa sera thabiti za kiuchumi zitakazohakikisha kwamba Serikali inabakia kama mwangalizi wa shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na sekta binfasi. Aidha, Serikali itakuwa msimamizi wa maslahi ya jumla ya wananchi ili kuhakikisha usalama wa bidhaa na udhibiti wa bei za bidhaa na huduma muhimu kwa ustawi wa wananchi.
  • Vile vile, Serikali yangu itafanya mageuzi makubwa ya mfumo wa utozaji kodi ili kuondoa utitiri wa kodi na hali ya sasa ambapo TRA inatumika kuangamiza biashara na mitaji ya wafanya biashara na wajasiri amali, badala ya kuhakikisha biashara zao zinashamiri na kuendelea kukua, kutengeneza ajira zaidi kwa wananchi wetu na kuongeza mapato ya kikodi ya Serikali.
  • Endapo nitapata dhamana ya kuiongoza nchi yetu, nitamaliza kabisa vitendo hivi kikandamizaji kwa kufutilia mbali sheria zote za kikandamizaji ambazo zimetumika kuumiza wananchi wetu na wakosoaji wa Serikali.
  • Aidha, Serikali yangu itafanya mageuzi makubwa ya mfumo mzima wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuvifanya kuwa walinzi wa Katiba, haki za binadamu na uhuru wa wananchi kufanya shughuli zao kwa mujibu wa Katiba.
  • Serikali yangu haitatumia vyombo vya ulinzi na usalama dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa na wakosoaji wake au vyombo huru vya habari. Serikali itaendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala wa sheria zinazoendana na matakwa ya Katiba na ya mikataba ya kimataifa ambayo nchi yetu imeikubali kwa kuiridhia.
  • Endapo nitapata dhamana ya kuwa Rais wa nchi yetu, nitakuwa Mfariji Mkuu. Sitakimbilia mafichoni kijijini kwetu Mahambe endapo nchi yetu na wananchi wetu watakabiliwa na majanga, yawe ya asili kama matetemeko ya ardhi, au yawe ya maradhi kama COVID-19. Kama Rais, nitakuwa mstari wa mbele kuwapa waliofikwa na majanga hayo faraja na misaada na afueni za kibinadamu watakazohitaji. Tofauti na sasa kamwe sitawasimanga, kuwakejeli au kuwatweza waliofikwa na maafa.
  • Tofauti na Rais Magufuli, endapo nitachaguliwa katika nafasi hii ya juu kabisa katika nchi yetu, nitatii, kulinda na kuhifadhi mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa kuondoa vikwazo na vizingiti vyote vya kikatiba, kisheria na kiutendaji vinavyozuia wananchi kufurahia haki zao zote za kidemokrasia. Katika uongozi wangu, mazuio ya mikutano ya hadhara na maandamano ya kisiasa ya wananchi, wawe kwenye vyama vya siasa au katika taasisi zao nyingine, yataondolewa. Kazi ya vyombo vya usalama itakuwa kulinda mikutano na maandamano hayo, badala ya kuwa vyombo vya kudhibiti wapinzani wa kisiasa wa chama na serikali iliyoko madarakani.
  • Endapo nitapata ridhaa ya wananchi wa Tanzania kuwaongoza kama Rais, nitarudisha hadhi, heshima na madaraka ya Bunge kama mhimili huru wa dola wenye mamlaka yanayolingana na ya Serikali ndani ya mipaka yake iliyowekwa na Katiba. Nitaondoa vikwazo na vizuizi vyote vya kikatiba, kisheria na kiutendaji ambavyo vimelizuia Bunge letu kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia na kuiwajibisha Serikali na kuwawakilisha wananchi.
  • Endapo nikuwa Rais nitaifungulia Mahakama kutoka katika kifungo chake cha sasa kwa kuondoa kivuli cha Urais wa Kifalme na vizuizi na vizingiti vingine vyote vya kikatiba, kisheria na kitaasisi ambavyo vimeikabili kwa muda mrefu.
HAJA YA MARIDHIANO YA KITAIFA

Ndugu wananchi,

Mahatma Gandhi, mwasisi wa Taifa la India, aliwahi kusema : ‘Jicho kwa jicho itatufanya wote kuwa vipofu.’ Makosa mawili hayatengenezi jambo moja la haki; kama ambavyo waongo wawili hawatengenezi mkweli mmoja. Ninaamini kwamba matatizo makubwa na ya msingi ya matumizi mabaya ya madaraka na uonevu waliofanyiwa wananchi hayawezi kutatuliwa kwa kulipiza kisasi dhidi ya wale waliotutesa na kutukandamiza. Visasi ni upanga wa walio waoga na dhaifu, sio ngao ya walio jasiri. Kwa hiyo, kama Rais, Serikali yangu haitalipiza visasi vya mabaya mengi ambayo wananchi wetu, mimi mwenyewe na viongozi na wanachama wenzangu wamefanyiwa na utawala huu na hata na serikali za nyuma.

Badala ya kulipiza visasi, Serikali yangu itarudisha, kujenga na kuimarisha mapatano na maridhiano ya kitaifa yatakayojengwa katika misingi ya ukweli juu ya makosa yaliyofanyika; msamaha kwa wanaotubu makosa yao, na fidia kwa wahanga wa makosa hayo.

NIMEJIANDAA KWA MAJUKUMU

Nitaendelea kufafanua masuala haya na mengine mengi katika siku, wiki na miezi inayofuatia; na wakati wa kampeni ya Uchauzi Mkuu endapo nitapata ridhaa ya Chama changu ya kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano. Itoshe tu kusema, kwa sasa, kwamba ninaamini ninazo sifa zote stahiki za kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Kwa zaidi ya miaka 20 nimetetea haki na maslahi ya wananchi wa Tanzania katika maeneo mbali mbali ya nchi yetu. Nilikuwa wa kwanza kupigia kelele ukandamizaji mkubwa na dhuluma walizofanyiwa wananchi wa maeneo mbali mbali ya nchi yetu yenye utajiri wa madini. Nilikuwa wa kwanza kuonyesha matatizo makubwa yaliyoko kwenye sekta ya madini na maeneo mengine ya rasilmali asili za nchi yetu.

Kwa miaka saba, kabla ya risasi 16 za ‘watu wasiojulikana’ wa utawala wa Magufuli hazijaniondoa Bungeni na Tanzania, niliongoza mapambano ya haki, utawala wa sheria na demokrasia kama Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Niliongoza na kuratibu harakati za kupigania Katiba Mpya Bungeni na katika Bunge Maalum la Katiba kati ya 2011 na 2014. Nimekuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kabla ya uongozi wangu kukatishwa kikatili na waitwao ‘watu wasiojulikana’ Septemba 7, 2017. Msimamo wangu katika masuala yote muhimu ya nchi yetu na ya watu wetu unajulikana wazi na wote na haujawahi kutetereka.

Katika utumishi wa kitaaluma na kisiasa wa zaidi ya miaka ishirini, nimetembelea kila mkoa na karibu kila wilaya ya nchi yetu. Kwa sababu hiyo, ninaifahamu Tanzania kwa undani na ninawafahamu Watanzania. Ninaelewa hofu zao, na ninaelewa matumaini yao. Muhimu zaidi, ninafahamu hifadhi kubwa ya nguvu, akili na ubunifu wa Watanzania ambao umejificha kwa sababu ya watu wetu kulazimishwa kuishi katika mazingira ya kikandamizaji na yaliyojaa hofu na kutojiamini.

Katika kipindi hicho hicho, nimetembelea, kusoma na kufanya kazi katika nchi mbali mbali za dunia. Nimeishi, kusoma na kufanya kazi katika Afrika yetu, Ulaya na Marekani ya Kaskazini. Katika mabara yote ya dunia hii, ni Bara la Australia peke yake ndiyo sijalitembelea bado. Ninaelewa masuala ya kimataifa kwa upana. Kwa sababu hizo, nitaleta katika Urais wa nchi yetu sio tu ufahamu wa Tanzania na Watanzania, bali pia uelewa wa mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya kimataifa na nafasi yetu katika mifumo hiyo.

Kwa sababu nimekuwa mmojawapo wa wahanga wakubwa wa Tanzania ya Magufuli, ninafahamu maana ya kuishi chini ya utawala wa aina hii ambao tumekuwa nao kwa miaka mitano sasa. Nina uwezo wa kuwafuta machozi wale waliofanywa wajane na yatima na vilema wa utawala huu. Nina uwezo wa kutibu majeraha na makovu mengi ambayo wamesababishiwa watu wetu wengi.

SIFA ZA KUGOMBEA URAIS

Ninafahamu kwamba baadhi yenu mna hofu kubwa na ya halali kabisa juu ya mimi kuwa na sifa za kikatiba na kisheria za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano. Hii ni kufuatia uamuzi wa Spika Ndugai wa kunifutia Ubunge mwezi Juni ya mwaka jana. Nitalitolea suala hili ufafanuzi wa kina wa kikatiba na kisheria endapo utahitajika. Itoshe tu kusema kwamba mtu anayekosa sifa za kugombea Urais (au Ubunge) kwa kukiuka masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni yule tu ambaye amepatikana na hatia ya kukiuka Sheria hiyo na chombo pekee kilichoanzishwa kwa mujibu wa Sheria hiyo, yaani Baraza la Maadili.

Katika utumishi wangu wote kama kiongozi wa umma, mimi sijawahi kutuhumiwa, kushtakiwa, kuitwa kwenye shauri, kutolewa ushahidi wowote dhidi au kwa niaba yangu, na kuhukumiwa na Baraza hilo la Maadili kwa kosa lolote lile chini ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Aidha, sijawahi kutuhumiwa, kushtakiwa, kuitwa kwenye kesi, kutolewa ushahidi dhidi ya au kwa niaba yangu, kuhukumiwa na kuadhibiwa kwa kosa lolote linaloweza kunifutia sifa za kugombea nafasi yoyote ile ya uchaguzi wa umma kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu za Uchaguzi.

Spika Ndugai ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, licha ya dhamana hiyo kubwa ya uongozi aliyonayo kitaifa, yeye sio Baraza la Maadili, na wala sio Mwenyekiti au mjumbe wake. Kwa sababu hiyo, uamuzi wa Spika Ndugai wa kunifutia ubunge haujaniondolea sifa za kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au nafasi nyingine yoyote ya uongozi.

Kwa hiyo, wananchi wenzangu, nawaombeni wote mniunge mkono katika safari hii ngumu iliyopo mbele yetu ya kuhakikisha kwamba:


  • Tunatibu majeraha na makovu mengi na makubwa ya Taifa letu;
  • Tunawatunza wajane, yatima na vilema wengi wa miaka hii mitano;
  • Tunafuta machozi na kutupilia mbali hofu tulizojazwa katika miaka hii ya adha kubwa;
  • Tunawaweka huru wafungwa na mateka wa utawala huu, tunaleta haki, amani ya moyo na nafuu ya Maisha kwa watu wote na kulirudisha Taifa letu katika misingi ya utu, haki na ubinadamu;
  • Tunaziba nyufa ambazo zimeligawa Taifa letu ; na
  • Tunajenga Taifa letu na kuwatoa wakulima, wafanyakazi, watumishi wa umma, wafanya biashara, wamachinga, mama lishe, vijana wasiokuwa na ajira, wake kwa waume wa Jamhuri ya Muungano kutoka kwenye lindi la umaskini, ukandamizaji, hofu na kukosa matumaini walilogubikwa na Tanzania ya Magufuli.
Nelson Rolihlahla Mandela, Rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru na ya kidemokrasia alisema yafuatayo siku alipoapishwa Rais wa nchi hiyo tarehe 10 Mei 1994 : ‘Isijetokea kamwe, kamwe na kamwe kwamba nchi hii nzuri itashuhudia tena ukandamizaji wa mtu mmoja dhidi ya mwenzake na kubebeshwa dharau ya kuwa fungo wa kimataifa.’ Maneno haya yanaihusu nchi yetu kwa sasa.

Nawashukuruni sana kwa uvumilivu wenu na Mwenyezi Mungu awape baraka zote.

Tundu A.M. Lissu (MB)

Tienen, Ubelgiji

8 Juni 2020


Huyo akagombee huko huko Ubelgiji. Hatutaki vibaraka wa Mabberu, at
 
Mumepaniki sana, Mwacheni JPM ajitetee.

Utetezi wa JPM ni tathmini ya utekelezaji wa ahadi zake kwenye hotuba ya kufungua Bunge la kwanza alipoingia madarakani. Atahukumiwa kwa kile alichoahidi mithili ya mpandaji kuchuma alichopanda.


Kwa wale wenye bando kidogo au wavivu wa kusikiliza, naweka hotuba hiyo kwa maandishi.

"HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,
20 NOVEMBA 2015


Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema, na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo.

Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi huu.

Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11. Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia imani na matumaini yangu makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya uongozi wako Bunge letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.

Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la 11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika nafasi za udiwani katika kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu mbili:

Kwanza, ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.


Pili, nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki.

Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.

Mheshimiwa Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka Wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani pia watafanya hivyo hivyo kama tutakavyofanya sisi.

Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watanzania wote. Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia kwa karibu sana kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. Kinyume na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na utulivu mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga kura. Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa, na hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.

Wale waliotarajia kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu Watanzania, kwa mara nyingine tena tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa cha Amani katika bahari iliyochafuka. Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali hii na kuilinda amani ya nchi yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa wa vyama vyote na viongozi wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya nchi yetu.

Aidha, napenda niungane na ninyi pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa pamoja na mgambo) kwa jinsi walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama katika kipindi chote cha uchaguzi.

Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima la uchaguzi toka hatua za awali za kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi. Hongereni, hongereni sana!

Mheshimiwa Spika;
Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu wa nchi yetu walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi yetu. Natambua mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga misingi imara wa umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na kuijenga misingi yake.

Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua na kuimarisha misingi ya uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao. Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.

Mhishimiwa Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja, tumeshindana katika kampeni tukiwa wamoja, na tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi za Umoja na Amani. Hatutakuwa na simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga umoja na amani yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila, vyama au ukanda.

Mheshimiwa Spika;
Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza kwa kulalamikiwa sana na wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni pamoja na:

• Rushwa - Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa wananchi.

• TAMISEMI - Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi, uzembe, n.k.;

• Ardhi - Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;

• Bandari - Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;

• Maji - Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji kupatikana mbali na makazi, n.k.;

• TRA - Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara wakubwa;

• TANESCO - Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;

• Maliasili na Utalii - Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya mipaka kati ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;

• Huduma za Afya (Hospitali) - Huduma kuwa mbali na wahitaji, Ukosefu wa madawa, hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo, vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato yanayowahusu, n.k.;

• Uhamiaji na Ajira - Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi nchini kwa wageni, Kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa na wazawa, n.k.;

• Elimu - Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni pamoja na majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;

• Polisi - Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari, Ukosefu wa nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;

• Zimamoto - Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea kazi kama maji, n.k.;

• Mizani - kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;

• Mahakama - Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa kesi. Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji wa kesi.

• Madini - Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa fidia, n.k;

• Kilimo na Mifugo ? Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la masoko, Kukopwa mazao ya wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa Maghala, Mabwawa, Malambo, Majosho, n.k.;

• Uvuvi - Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi hususan viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa bahari;

• Reli - Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa reli, upungufu wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara, n.k.;

• ATC - Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa mishahara ila ndege ni moja (1);

• Makundi Maalum - Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa;

• Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo ? Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, Haki na maslahi yao, n.k.;


Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi na Taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue na mshirikiane na Serikali na wadau wengine tuzitatue haraka.

Pamoja na kero hizo tutashughulikia pia mambo yafuatayo.

Kuimarisha Muungano

Mheshimiwa Spika;
Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani.

Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu.

Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.

Serikali nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuendelea kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake ya awali ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na pia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein tutahakikisha tunasimamia na kuimarisha Muungano wetu.

Kuimarisha Mihimili ya Serikali

Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaheshimu na kuendeleza utamaduni mzuri uliojengeka nchini wa kuheshimu mihimili ya dola. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata fedha za kutosha kuendesha shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Kwa upande wa Bunge, tutahakikisha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinapatikana kwa wakati ili Waheshimiwa Wabunge mkashirikiane na wananchi wenu kusukuma maendeleo. Kwa upande wa Mahakama, tutalipa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa Mahakama kwa kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, kuongeza kasi ya utoaji haki na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama zetu.

Mchakato wa Katiba

Mheshimiwa Spika;
Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.

Uchumi na Matarajio ya Wananchi

Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kukiwa na msingi imara wa kiuchumi uliojengwa katika Awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu umekuwa ukiimarika na kukua wastani wa asilimia 7. Katika kipindi hicho fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa. Hii ni kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali za Awamu zilizopita za kujenga miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, uimarishaji wa bandari, uimarishaji wa reli, na ukuzaji wa sekta za mawasiliano ya simu na mitandao, ukuzaji na uongezaji wa uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme.

Napenda kuwahakikishia kuwa tutaendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu mipya na kuiimarisha iliyopo ili kuvutia na kushawishi wawekezaji wa ndani na wa nje.

Mheshimiwa Spika;
Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa ahadi tulizowaahidi Watanzania ni kuendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya mikoa na wilaya; barabara ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na kiuchumi; na upanuaji wa barabara za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga flyovers, barabara za pete (ring roads), n.k. Uboreshaji wa barabara na njia nyingine za uchukuzi na usafirishaji kuingia na kutoka Dar es Salaam ni muhimu sana kwa sababu bandari ya Dar es salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu na nchi jirani.

Mheshimiwa Spika;
Katika jitihada hizo hizo za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi Serikali ya Awamu ya Tano, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza nguvu zake katika ujenzi wa reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani standard gauge). Reli ambazo tunakusudia zianze kujengwa ni:

Dar es Salaam - Tabora - Kigoma/Mwanza

Uvinza - Msongati (Burundi) na Isaka - Kigali (Rwanda)

Mtwara - Songea - Mbamba Bay na matawi ya kwenda Mchuchuma na Liganga;

Tanga - Arusha - Musoma

Kaliua - Mpanda - Karema


Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu pia imejaliwa kuwa na madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi asilia umeongeza matumaini ya watu wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi katika miaka ijayo. Serikali itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo.

Aidha, napenda kuipongeza kwa dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Bunge la 10 kwa kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi yaani The Oil and Gas Revenues Management Act, 2015. Serikali yangu itasimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini mkubwa.

Ujenzi wa Viwanda

Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda. Natambua kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Hatuna njia nyingine kama kweli tunataka kujenga msingi wa uchumi endelevu katika nchi yetu utakaopaisha uchumi na maisha ya watu wetu. Dira ya Maendeleo ya 2025 inatutaka tuwe nchi ya watu wenye kipato cha kati.

Tunaweza tukafika huko, na dalili zipo, lakini pia tunaweza tukafika huko kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia wa mambo ni tofauti. Utofauti ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha kwamba sisi ni nchi ya kipato cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha ya watu wengi hazifanani na takwimu hizo.

Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda.

Mheshimiwa Spika;
Tutahakikisha suala la viwanda linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa. Matarajio yangu ni kuwa Bunge lako Tukufu litatuunga mkono mimi na Serikali nitakayoiunda katika kufikia lengo hili.

Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema wakati wa Kampeni, na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda vilivyopo na kuhakikisha vinafanya kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa viwanda vilivyokuwa vya umma kwa makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka wafanye hivyo mapema. Na hapa nataka nisisitize wito wangu huo kwao. Najua huko nyuma ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya aina hiyo umekuwa ukilegalega na watu wamejifanyia mambo watakavyo.

Wapo walioacha kabisa uzalishaji na kufumua hata mitambo ya uzalishaji. Mimi niliahidi, na nataka niseme hapa kwa wazi kabisa, kwamba wale waliobinafsishiwa viwanda hivyo waanze kazi, waanze kazi mara moja. Wakishindwa basi tutavitwaa viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na kuwapa watu wengine wenye nia ya kuviendeleza.

Hatuwezi kuwa na watu wanajiita wawekezaji tunawapa viwanda vyetu halafu wanaviatamia tu. Mimi hilo sitalikubali na wala sitalivumilia. Nimeielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanza kushughulikia suala hili mara moja. Naomba Bunge lako lituunge mkono.

Mheshimiwa Spika;
Njia ya pili ya kuendeleza viwanda ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu ya kufanya hivyo tayari ipo na baada ya muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo watu wanaotaka kuwekeza Tanzania sasa, katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka ya nyuma kidogo, lakini wakati mwingine sisi humu humu ? tukiwemo sisi viongozi kwa kushirikiana na wafanyabiashara matapeli na laghai ? tumehujumu mipango na shauku ya wawekezaji wa nanma hiyo.

Pamoja na shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea vikwazo na kuwapiga vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi jirani. Sisi katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa usumbufu na urasimu wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji wa Serikali watakaokwamisha jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda hapa nchini hatutawavumilia.

Mheshimiwa Spika;
Ni viwanda vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura ya kwanza ya viwanda tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani, hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini ? na maliasili nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa uzalishaji ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana.

Viwanda vya aina hii vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa sekta nilizozitaja, na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la uhakika humu humu ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha bidhaa ambazo zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) ? yaani bidhaa kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi vitakuwa na uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. Viwanda hivi vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje.

Yote mawili yakitokea, yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje, itatuongezea akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na kuendeleza mipango mingine kwa ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura ya tatu ya viwanda tunavyovikusudia ni kuzalisha ajira nyingi. Shabaha yetu ni kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40 ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.

Mheshimiwa Spika;
Nimeamua kulisema hili kwa kirefu sana kwa sababu ili tufanikiwe lazima tuelewane na tusaidiane kulisukuma kwa pamoja jambo hili.

Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Mheshimiwa Spika;
Sekta nyingine ambazo lazima tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza ni kilimo, mifugo na uvuvi. Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani mazao yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi kikubwa ni nchi ya kilimo, ufugaji na uvuvi.

Hii inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia 75 wanaishi vijijini na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao na wanazalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula chote kinacholiwa hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25 kwenye pato la taifa yaani GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu ya fedha za kigeni.

Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu na maisha yetu ni mkubwa sana. Nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi wote wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika maisha yetu na uchumi wa nchi yetu. Nataka kuahidi kwao sitawaangusha.

Mheshimiwa Spika;
Pamoja na umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu wakulima, wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni watu maskini. Mapato yao yako chini na wanaishi maisha duni. Lengo letu ni kuuimarisha sekta hizi ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi lakini pia ziweze kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadili maisha yao.

Tukiweza kuboresha sekta hizi vijana wengi zaidi watavutiwa kujiunga nazo na hivyo kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira. Nataka niwahakikishie wakulima, wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao tutahakikisha zinatekelezwa. Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia kwa dhati ahadi hizo ili kuhakikisha kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa zaidi na wenye tija.

Baadhi ya mambo tuliyowaahidi kuyatekeleza ni pamoja na haya yafuatayo:
1. Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa ikiwa pamoja na ufugaji wa samaki,

2. Kuwapatia pembejeo,

3. Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,

4. Kuwapatia wataalamu wa ugani,

5. Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,

6. Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana kufikia lengo hili,

7. Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa, kule Kagera ina kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda ambako bei iko juu, tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili wakulima wapate bei nzuri. Tutafanya hivyo pia kwa mazao mengine kama mahindi, chai, pamba, korosho, mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki, n.k.),

8. Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa wao kuondolewa kwenye ardhi zao kupisha wawekezaji,

9. Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya migogoro hiyo tunaviondosha haraka,

10. Kuhakikisha kwamba tatizo la wavuvi kuvamiwa na majambazi na uvuvi haramu linashughulikiwa kikamilifu.

Tatizo la Umaskini na Ajira

Mheshimiwa Spika;
Nimezungumzia umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu ya matatizo makubwa mawili yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo la UMASIKINI na pili ni tatizo la AJIRA. Ni kweli uchumi wetu umekuwa ukikua kwa kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana na kasi ya kuondoa umasikini na uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana wetu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.

Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 28.2 ya Watanzania ni maskini. Na kwamba kwa namna na kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo baina ya matajiri (walionacho) na maskini (wasionacho) linazidi kukua. Tukiendelea hivi tunavyoendelea sasa hatutakuwa tunaitakia mema nchi yetu kwa sababu mgawanyiko mkubwa wa kimapato na tofauti kubwa za kimaisha baina ya matajiri na maskini ukiachiwa uendelee na kuzidi kukua utachochea chuki na uhasama baina ya walionacho na wasionacho.

Lazima tujizatiti na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na kuibadilisha hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa watu wetu. Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni uendelezaji wa sekta ya viwanda na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA. Kama nilivyokwisha kugusia, ukuaji wa uchumi wetu haujaenda sambamba na kasi ya watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka. Tatizo la ajira ni kwa vijana wote waliosoma viwango mbalimbali vya elimu na wasio na ujuzi. Hii inamaana kwamba sekta zinazochangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu sizo zinazozalisha ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka msisitizo kwenye sekta ya viwanda hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo ambavyo ndio mwajiri mkubwa hivi sasa.

Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuweka msisitizo katika Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi kuwawezesha vijana wetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango mbalimbali. Ili hili liwezekane, na sisi tutalifanya, linahitaji mambo mawili makubwa.

Kwanza, kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi. Hatuna budi kuweka mkazo katika viwango vya ubora vya elimu na stadi za kazi wanazopata vijana wetu. Nalisema hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia uendelezaji wa viwanda ikiwa hatujaandaa vijana wenye uwezo, ujuzi, na stadi za kufanya kazi hizo kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu; hatuwezi kutaka kuwekeza katika viwanda vya nguo au samani ikiwa hatuna wahandisi wa mitambo wazuri, wabunifu wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa na kukubalika.

Aidha hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha shughuli za uzalishaji kama hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi na kuiendeleza. Kwa hivyo tutaelekeza nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa shule na vyuo vyetu katika ngazi mbalimbali vinafundisha na kutoa vijana wenye viwango vya hali ya juu vya elimu, maarifa, ujuzi na ufundi.

Mheshimiwa Spika;
Pili, ni suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka kujiajiri. Katika kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua na kutekeleza hatua mbalimbali ikiwemo:

Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na fani walizosomea;

Kuwawezesha vijana kuanzisha SACCOS zao na kupitia SACCOS hizo kuwawezesha kupata mikopo;

Kuwawezesha vijana wajasiriamali kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na mafao mengine katika mifuko hiyo.


Mheshimiwa Spika;
Tatu, ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha shughuli za kina Mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda na Maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k. Shughuli za makundi haya zinatusaidia sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa tu na kuzurura zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo wetu wa kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha.

Niliahidi, na nataka nirudie hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri zetu, pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na rafiki kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao na shughuli nilizozitaja tutauondoa.

Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato, na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali mabilioni ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana mitaani. Viongozi na watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.

Afya

Mheshimiwa Spika;
Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kufanya baadhi ya mambo yafuatayo:

Kwanza, kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo. Lengo ni kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa unakuwa na hospitali ya Rufaa.

Pili, tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika Nyanja za afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi; kwa kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma mahsusi hapa hapa nchini na hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa nchi za nje.

Tatu, tutaongeza bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha, tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.

Elimu

Mheshimiwa Spika;
Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya sayansi. Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.

Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa wakati. Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze kuwanufaisha zaidi.

Maji

Mheshimiwa Spika;
Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi sana ya ukosefu wa maji. Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanzisha miradi mipya mikubwa na midogo ya maji kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya uhakika vya maji ikiwa pamoja na kuvuna maji ya mvua. Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.

Umeme

Mheshimiwa Spika;
Suala la upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo katika nchi yetu pamoja na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita. Hatuwezi kuzungumzia suala la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi. Serikali yangu itahakikisha kwamba umeme unapatikana wa kutosha na wa uhakika. Tutakamilisha miradi ya umeme iliyopo na kujenga mingine mingi mipya ili wananchi wengi zaidi wanufaike na nishati ya umeme na viwanda vingi zaidi vidogo vidogo, vya kati na vikubwa vianzishwe.

Madawa ya Kulevya

Mheshimiwa Spika;
Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike. Familia nyingi zimeathirika na nguvu kazi ya taifa imepotea. Tutaushughulikia mtandao huo hususan wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila ajizi.

Mheshimiwa Spika;
Masuala mengine tutakayoyawekea mkazo katika utawala wa Awamu ya Tano ambayo ninaamini yatasaidia katika kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya Utalii, Mawasiliano, Madini, Ardhi na Makazi, Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara, Ulinzi na Usalama, utunzaji wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu na Ualbino, Wazee, Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari, wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa masuala haya umefafanuliwa vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015. Tutayatekeleza ipasavyo.

Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ufisadi

Mheshimiwa Spika;
Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa nilichokikusudia.

Mheshimiwa Spika;
Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo. Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya watu wetu.

Mheshimiwa Spika;
Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa na ufisadi. Ndio maana moja ya Imani kuu za CCM ni ile isemayo: ?Rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa?
Kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na ufisadi.

Mheshimiwa Spika;
Mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kuifananisha rushwa na ufisadi ?Kama Adui Mkubwa wa Watu?. Akiongea Bungeni Mei 1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
?Rushwa [na ufisadi] havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.?

Mheshimiwa Spika;
Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi aliyeichukia na kuikemea rushwa katika maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha tu nini kinaweza kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri, wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako tayari kuvumilia upuuzi wa serikali itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.

Mheshimiwa Spika;
Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine. Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.

Mheshimiwa Spika;
Ninafahamu ugumu wa vita niliyoamua kuipigana. Nasema nafahamu ugumu na changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha na rushwa sio watu wadogo wadogo. Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi yetu hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi na utumishi ambazo wamezipata kutokana na ridhaa ya watu. Kwa hivyo ili niweze kufanikiwa lazima nipate ushirikiano mkubwa toka kwa Bunge lako tukufu na vyombo vingine vilivyopo na vyenye majukumu ya kupambana na vitendo hivi.

Aidha, tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina mashaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya dhidi ya rushwa na ufisadi.

Mheshimiwa Spika;
Katika kushugulikia tatizo hili nimeahidi kuunda mahakama ya Rushwa na Ufisadi. Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili havitanikwamisha.

Aidha, nataka niahidi mbele ya Bunge lako tukufu kwamba, kiongozi yeyote wa kuteuliwa, ambaye mimi nitakuwa nimemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na ninayo mamlaka ya kumwajibisha, pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya mimi kuchukua hatua hizo hatua na taratibu zingine za kisheria zitafuata.

Mheshimiwa Spika;
Ninachotaka kusema ni kuwa Serikali yangu itafuatilia kwa karibu mienendo ya viongozi na watendaji wake ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi. Na tukishajiridhisha hatutasubiri, tutachukua hatua. Ni imani yangu wengine pia katika ngazi mbalimbali mtafanya hivyo. Kwa sababu bila kufanya hivyo rushwa na ufisadi vitazoeleka na kuwa wimbo unaoburudisha badala ya kuudhi na kukera.

Muundo wa Serikali na Utumishi

Mheshimiwa Spika;
Nilipokuwa nazunguka na kuzungumza na wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi, niliahidi kuwa nitaunda serikali ndogo ya wachapa kazi.

Aidha, niliahidi pia kuunda serikali ambayo itawatumikia watu na hasa wananchi wa kawaida. Serikali nitakayounda, nataka iwe inawahudumia wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa watumishi wa serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu watumishi wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali nitakayoiongoza.

Lugha za ?hiyo ni changamoto tutaishughulikia?, au ?Mchakato unaendeela? hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi Tu. Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza ofisi za umma kuwa ni mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuwataka watumishi wa Serikali kufanya kazi hatuna budi kuyaangalia na kuboresha mishahara na maslahi yao na mazingira yao ya kufanyia kazi kwa kuwapatia vitendea kazi bora na vya kisasa. Na jambo moja tutakalolitekeleza ni kuangalia namna ya kupunguza kodi ya mapato katika mishahara ya wafanyakazi yaani PAYE. Pia tutajitahidi kuwatambua na kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.

Kuongeza Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali

Mheshimiwa Spika;
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio kwa sababu mbalimbali. Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma.

Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika;
Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo tutayasimamia kwa lengo la kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza, safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.

Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:7

Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;

Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;

Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;

Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT), Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.

Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za walimu ngapi?, madawati mangapi? n.k. Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.

Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje ya nchi zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.

Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha ambayo kwa kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na wala hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya Serikali.

Nne, tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu tunaiziba. Ni matarajio yangu kutakapoleta Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono.

Tano, tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu ununuzi wa bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Samani zote kwa ajili ya matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa hapa hapa nchini.

Sita, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu na kuthibiti ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi waandamizi wa Serikali; na

Saba, tutaendelea kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na Taasisi zake zote yasiyo na tija kwa uchumi wa taifa letu.

Mheshimiwa Spika;
Kwa ajili hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia kuiunda vitakuwa ni: kupunguza urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali; kubana matumizi kwa kupunguza yale ambayo kutokana na hali yetu ya uchumi kwa sasa yanaweza kuepukika; na kurejesha nidhamu ya Serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Tutatekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja na mambo mengine kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri; kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na maduhuli ya Serikali kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha kwamba wale wote wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu ya matumizi ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na waajiri wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kubainisha maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaigharimu Serikali fedha nyingi na kuyadhibiti.

Aidha, nitoe wito kwa Watanzania wote kila mmoja wetu afanye kazi iwe shambani, ofisini, kiwandani, sokoni, n.k. Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka kwa Watanzania kutokupenda kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi vijiweni, muda ambao ungetumika kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu yangu ni HAPA KAZI TU!

Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa

Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja ya diplomasia na ushirikiano wa kimataifa katika awamu zilizotangulia za uongozi. Serikali yangu itaendeleza sifa hiyo kwa kujenga juu ya msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa waumini na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu.

Tutaendelea kuwa waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na daima tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi wanachama. Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano wetu hatua kwa hatua.

Mheshimiwa Spika;
Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama ambao tunauhusiano wa kihistoria na kidugu. Tutaendelea kuamini katika Umoja wa Afrika (AU) na azma ya ndoto ya waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika. Tutaendelea pia kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) na kushirikiana na nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu ya amani, usalama na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.

Tutaendeleza na kustawisha mahusiano na marafiki zetu wote Magharibi, Mashariki ya Mbali na Mashariki ya Kati kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi zetu na watu wetu. Tutapenda kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri kisiasa kukuza mahusiano yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi. Tutafanya hivyo pia kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu na Umoja wa Mataifa (UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), n.k.

Aidha, tutazitaka Balozi zetu zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya fedha tunazowapelekea hususan katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na mchango wao katika ukuzaji wa sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia yetu na Sera yetu ya nje ikijibu changamoto zetu za ndani za ajira, miundombinu, masoko ya mazao ya wakulima, viwanda n.k.

Hitimisho

Mheshimiwa Spika;
Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Bunge hili linalo nafasi ya kuweka historia ya kuwa kitu kimoja na kuweka masilahi ya Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha za vijembe, mipasho, na ushabiki wa vyama bungeni. Kwanza, tukumbuke wote bila kujali itikadi za vyama vyetu sisi ni kitu kimoja; na pili tumechaguliwa kuwawakilisha wenzetu. Baada ya miaka mitano kila mmoja atarudi kwenye jimbo lake kuomba kura na huko atapimwa kwa maendeleo aliyopeleka.

Tusimame pamoja, Tanzania ni yetu sote tutangulize masilahi ya nchi mbele, na kwa mara ya kwanza Watanzania waone Bunge tofauti na sio Bunge la kuzomea, kutoka nje, kutukanana, mipasho, n.k. Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya dhamana tuliyopewa na Bunge hili Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi kuheshimiwa.

Aidha, napenda kusisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa. Matarajio na matumaini ya Watanzania waliotuchagua na kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni makubwa. Wanachotaka kuona ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na mimi, baada ya miaka mitano toka sasa, tutapimwa kwa namna tutakavyokuwa tumetekeleza mambo ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu.

Mimi nina amini kabisa kwa ushirikiano wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu tutaweza kuzitimiza ndoto za Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Spika;
Sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!

Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza."
 
Nitajie mwanasiasa mmoja unayemjua aliyewahi kutangaza kugombea urais wa nchi yake akiwa nje ya nchi na akaupata. Kijibu, una chupa kubwa mbili za K Vant hapa hapa Diamond, Kona ya Bwiru. Ahahahahahahah!

Hill la kutangaza nia nje ya nchi lazima liwaume sana maana awamu ya tano kimataifa imekuwa sawa na uyawala was Nduli Amini na Mabuto.
 
Angalia usinyang'anywe uanachama wako wa lumumba
TL ametoa hotuba nzuri sana inaleta matumaini mapya katika nyanja zote kiuchumi na kijamii inaponya majeraha,inaonyesha matumaini ya uhuru wa wananchi ambao unazidi kupotezwa.
Inaleta matumaini ya mahusiano mazuri ya kimataifa na kuondokana na dhana ya "ubeberu"

Inaleta matumaini ya sekta binafsi kuongoza uchumi wa nchi badala ya serikali kufanya biashara jambo ambalo linaleta mgongano wa kimaslahi.
Imeleta matumaini mapya ya kuleta katiba mpya ya wananchi, ambayo itaondoa ukiritimba wa kiimla kutoka kwa watawala.
Inaleta matumaini ya maridhiano kataifa kuondoa uhasama unao zidi kukua kati ya wanavyama wa vyama tofauti Tz

Ni hotuba inayo ponya inayotibu inayotia matumaini.

Hongera TL kwa kuonyesha nia
 
Back
Top Bottom