Hotuba za Mwalimu Nyerere wakati wa vita vya Kagera

Hotuba za Mwalimu Nyerere wakati wa vita vya Kagera

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
11,884
Reaction score
21,175
Wakati wote wa Vita vya Kagera Mwalimu Nyerere alikuwa anatoa hotuba kila baada ya muda fulani ili kuwajulisha wananchi maendeleo ya vita. Hotuba zote zimewekwa kwenye kakitabu haka. Kitabu unaweza kukisoma ndani ya app ya Maktaba Sauti. Ipo playstore.
Hotuba za Vita vya Kagera.png


Hotuba No 1

2, Novemba, 1978.

Ndugu wananchi,

Nimewaombeni tukusanyike tena hapa niwaelezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua, lakini nadhani si vibaya nikilieleza. Nitajitahidi kulieleza kwa kifupi.
Wakati nilipokuwa katika ziara kule Songea juma la pili la mwezi uliopita, ilitangazwa habari kutoka Uganda kwamba Jeshi la Tanzania limeingia Uganda, limechukua sehemu kubwa ya Uganda, na linaua watu ovyo.

Siku hiyo ulipotangazwa uwongo huo nilikuwa nimealikwa kwenye chakula na vijana wetu wa Jeshi la Wananchi pale Songea. Kwa hiyo nikachukua nafasi hiyo kukanusha uongo huo, na kwa kweli kuwalaumu hao waliozua uwongo, na pia kuvishutumu vile vyombo vya habari duniani ambavyo vinapenda sana kutangaza-tangaza uwongo wa Amin. Amin hutamka la uwongo, na wao huurukia na kulitangaza kana kwamba ni la kweli. Huo ndio ulikuwa uwongo wake wa kwanza, na aliendelea.

Baadaye akabadili sura ya uwongo huo, akaongeza uwongo wa pili:kwamba Watanzania hao bado wapo Uganda wanapiga watu huko, wanaua watu huko na sasa wanasaidiwa na Wanajeshi wa kutoka Cuba. Huo nao ulikuwa uwongo, tuliendelea kuukanusha na kuupuuza. Kwa kweli tulikanusha na kupuuza uwongo mzima.

Lakini Alhamisi iliyopita, saa za asubuhi, ndege za kivita zikaja. Vijana wetu wakazitupia risasi zikarudi. Siku hiyo hiyo zikarudi tena. Vijana wetu wakazitupia risasi zikakimbia, lakini moja ikaangushwa. Ijumaa zikaja ndege za kivita katika eneo la Kyaka. Zikatupa mabomu. Vijana wetu wakazitupia risasi, mbili zikaangushwa.

Wakati huo huo bahati mbaya ndege zetu nyingine nazo zilikuwa zinatoka hapa zinakwenda Mwanza. Kwa bahati mbaya katika hali ya giza, zikakosea katika kutua kwenye kiwanja cha Mwanza. Zikataka kujaribu tena. Lakini ndege hizo zinakwenda kasi sana, na ili ziweze kugeuka na kujaribu kutua tena, ikabidi zigeukie Musoma. Na katika maeneo yale tangu Idi Amin alipoanza kutangaza uwongo, ingawa tulikuwa tunaupuuza ule uwongo, lakini hatuwezi kupuuza yote: Kwa hiyo vijana wetu walikuwa wameshaambiwa ndege za vita zikionekana zipigwe. Kama zile za Bukoba zilivyopigwa, na za Kyaka zilivyopigwa, hizi nazo, kwa bahati mbaya, zilipofika Musoma wakadhani ni za adui. Zikapigwa. Tukapoteza ndege tatu. Lakini katika mambo ya vita ajali zinatokea. Vijana hao walikwisha ambiwa zikionekana ndege wapige. Wangeziacha wanajuaje pengine ni za adui. Kwa hiyo ikatokea bahati mbaya hiyo.
Matukio hayo hatukuyatangaza. Hata kule kupiga ndege za Amin hatukutangaza. Hatukutangaza kwa sababu hatukutaka jambo lenyewe kulipa uzito mno.

Tulisema akiendelea- endelea kuleta hizi ndege zake tutaendelea kuziangusha. Yeye ataendelea kuongopa, lakini hizi ndege tutaziangusha kila zinavyokuja. Uwezo wa kuangusha upo na mwenyewe alijua kwamba uwezo upo na ni vizuri akijua yeye.

Tulikuwa tunaepuka kulipa uzito mno jambo hili kwa sababu mwanzo wake ni uwongo kabisa wa kuzua. Kwa hiyo uwongo wake ukaendelea na tukazidi kuukana, na haya matukio ambayo yalikuwa ni kweli nasema hatukuyatangaza kwa sababu hiyo niliyoisema.

Sasa Jumatatu ndipo akavamianchi yetu. Akaingiza majeshi yake kwa nguvu kubwa yakachukua sehemu kubwa, yakaingia ndani mpaka Kyaka. Hili tulilitangaza, kwa sababu lilikuwa ni jambo la kweli. Yeye, kama kawaida yake, akakana, akasema haikutokea hivyo. Akaendelea kusema tu kwamba Watanzania wao ndio wako Uganda wamechukua sehemu za Uganda. Amin akakana, akasema haikutokea hivyo. Akaendelea kusema tu kwamba Watanzania wao ndio wako Uganda wamechukua sehemu za Uganda. Amin akakana ukweli huo, lakini sisi tukawaeleza Mabalozi walioko Dar es Salaam kwamba huyu mtu amevamia nchi yetu.

Sasa jana ametangaza mwenyewe: kwamba ni kweli majeshi yake yamevamia nchi yetu, na kwamba yamechukua sehemu hiyo ya Tanzania iliyo kaskazini mwa mto Kagera, na kwamba tangu sasa eti sehemu hiyo ni ya Uganda na itatawaliwa kijeshi kama Uganda inavyotawaliwa. Ndivyo alivyotangaza mwenyewe. Sisi ametusaidia katika kutangaza jambo hilo kusudi sasa ubishi uishe, tusiwe tena na tatizo la kuwaambia watu wenye akili duniani ni nini kimetokea. Sasa hiyo ndiyo hali, tufanye nini?Tunayo kazi moja tu, Watanzania sasa. Ni kumpiga. Uwezo wa kumpiga tunao. Sababu ya kumpiga tunayo. Na nia ya kumpiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe hivyo kwamba hatuna kazi nyingine, na tunawaomba marafiki zetu wanaotuambia maneno ya suluhu waache maneno hayo.

Kuchukua nchi ya watu wengine makusudi siyo kwamba majeshi yamekosea njia, na kusema sasa sehemu hiyo mmeichukua, ni kutangaza vita na nchi ile nyingine. Lakini siyo sisi tuliofanya hivyo. Amefanya hivyo mwendawazimu. Amefanya hivyo katika jambo ambalo amewahi kulitangaza zamani. Aliwahi kusema zamani kidogo kwamba mpaka wa haki wa Uganda na Tanzania ni Mto Kagera na siku moja ataichukua. Ametimiza dhamiri hiyo.

Sasa rafiki zetu kama ni marafiki wa kweli, watataka tumwondoe mtu huyu. Hawawezi kutuomba suluhu, au kutuomba jambo la ajabu kabisa la kurudisha majeshi yetu nyuma. Niyarudishe wapi? Kwa hiyo ninasema tunayo kazi moja.

Sisi hatukupenda kufanya hivi: hatukupenda kupigana vita. Maadui wetu ni mabeberu, kwa sasa hivi wako Kusini. Serikali za Afrika hatatunapokuwa hatupendi vitendo vya viongozi wao, hatuwezi kuwahesabu kama ni adui wetu. Na kama Amin angekuwa anasema tu kwamba Tanzania ni adui sisi tungeendelea kumpuuza kama ni maneno tu. Lakini kafanya hasa kitendo cha uadui. Amekuja mwenyewe, ameingia Tanzania mwenyewe. Mtu huyu ni mshenzi, ameua watu wengi sana. Kwa hiyo nasema tunayo kazi moja. Tutampiga.

Vijana wetu wako mpakani sasa hivi, wako kule; na mapambano yanaendelea. Sasa haya si mapambano ya vijana wa T.P.D.F.; ni yetu wote. Kwa hiyo ninachowaombeni wananchi wote kwanza ni hiyo kazi iliyo mbele yetu. Pili, tuwasaidie vijana wetu, kila mtu kwa mahali alipo. Na kila mapambano yatakavyoendelea, tutaeleza nini la kufanya, na nani afanye nini. Tutaelezana wakati wote wakati tunamwondoa huyu nyoka katika nyumba yetu.

Tunawaomba mtulie. Katika mambo haya ya vita, na hasa kama watu mlikuwa na mazoea ya amani, mnaweza kubabaika sana. Msibabaike; tulieni. Fanyeni kazi kama kawaida. Eleweni vitendo tutakavyovifanya; na mtaviona vitendo tutakavyovifanya tangu sasa mpaka hapokazi itakapokuwa imekwisha. Lakini mjue vitendo hivyo kazi yake ni hiyo moja; kumpiga mshenzi huyu aliyekuja katika nchi yetu.
Asanteni sana.
Itaendelea. . . .
 
Ukoloni​

9, Desemba, 1978.

Ndugu Wananchi,

Leo ni siku ambayo Tanzania Bara inatimiza miaka 17 tangu tumejikomboa na ukoloni. Kwa kawaida siku kama ya leo huwa tunafanya sherehe kubwa nchini kote na hapa Dar es Salaam huwa tunafanya Gwaride Rasmi ambalo huwa linakaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Lakini leo hatufanyi hivyo. Hatufanyi sherehe nchini, na wala hatuna hilo Gwaride Rasmi hapa Dar es Salaam, na sababu zake zinajulikana. Tunayo matatizo makubwa. Na hatudhani kwamba katika hali hiyo ya matatizo makubwa ni jambo jema tuwe na sherehe nchini na magwaride ya wanajeshi Dar es Salaam. Kwa kweli hata sina hakika kwamba ni jambo zuri kuwa hivi sisi wengine leo hatufanyi kazi; ni siku ya livu, hatuna kazi. Wenzetu wako kazini; wenzetu wako mpakani, wanafanya kazi, na wanalala ndani ya mahandaki. Nasema sina hakika kwamba hata kule kuacha kufanya kazi leo ni jambo jema.

Lakini nilidhani, kwa sababu ya matatizo haya tuliyonayo, ingawa kwa kawaida katika siku kama ya leo huwa sihutubii Taifa, pengine si vibaya nikazungumza kidogo. Nilidhani, pamoja na matatizo yetu haya tuliyonayo sasa hivi, ni vizuri nikaitumia siku hii ya leo kukumbusha maana ya siku ya leo; nieleze maana ya jeuri ya ukoloni, maana ya fidhuli ya ukoloni.

Jeuri ya ukoloni ni jeuri ambayo inazidi jeuri nyingine yo yote duniani. Ni jeuri ambayo, walio nayo jeuri ile, wanakataa usawa wa watu wote. Maana huwezi ukaamua kwamba utawatawala watu wengine wakipenda wasipende, bila kukana usawa wa binadamu. Lazima kwanza uukane usawa, useme watu sio sawa na wewe. Watawala hawa wa kikoloni, na watawala wa namna yo yote hii ya kijahili, lazima waseme kwamba wao si watu, ni miungu; na wale wanaotawaliwa ndio watu. Na miungu wana wajibu wa kuwatawala watu wakipenda wasipende. Ama wataamua kwamba wao watawala (hawa wa nguvu) wao ndio watu, na wale wanaotawaliwa sio watu, ni wanyama tu.

Mimi nilikuwa bado mwanafunzi shuleni niliposoma filosofia ya mheshimiwa mmoja, kiongozi wa Wajerumani, anaitwa Hitler. Hitler alikuwa anawachukia sana Wayahudi, na katika maisha yake aliua Wayahudi wengi sana. Alikuwa hasa na shabaha ya kuwafuta kabisa duniani, waishe. Alikuwa anawakusanya na anawapeleka katika matanuri makubwa; halafu anafunga milango anafungulia gesi, na Wayahudi wanakufa humo ndani. Na inasemekana katika muda mfupi huo Hitler aliua Wayahudi milioni sita.

Na moja katika madhambi ya Wayahudi, walikuwa na madhambi mengi lakini mojawapo katika madhambi ya Wayahudi, Hitler anasema, ni kwamba walikuwa wanahubiri usawa wa binadamu. Wanasema binadamu ni sawa; na Hitler hakubali kwamba binadamu ni sawa. Anasema, kwa mfano, Wayahudi hawa magazeti yao yanasema kwamba watu weusi na watu weupe ni sawa.

Na mifano yao ni nini? Mfano ni kwamba inawezekana yako mashindano, ya mbio ama ya ngumi. Halafu mtu mweusi anaweza akakimbia akamzidi mtu mweupe, au mtu mweusi anaweza akampiga ngumi mtu mweupe. Basi magazeti haya ya Wayahudi yanasema kwamba, watu weusi hawa ni sawa na watu weupe, au wanazidi; maana unaona wanaweza kuwazidi mbio au wanaweza kuwapiga ngumi.

Hitler anasema ujinga gani huu! Binadamu na mnyama hawawezi wakashindana katika mbio au ngumi, na hawa weusi wamewashinda hawa kwa sababu wao ni wanyama; wanaweza sana mbio zaidi. Badala ya kusema hivyo hawa wanapotosha Taifa letu la wateule, kusema kwamba watu weusi na watu weupe ni sawa.

Ama anasema kwamba magazeti haya ya Kiyahudi yanatoa ushahidi mwingine wa ovyo wa usawa. Wanasema weusi fulani wamekwenda katika Vyuo Vikuu na huko wamesoma, wamehitimu, wamepata shahda sawa sawa na watu weupe, au hata wamezidi. Kwa hiyo Wayahudi hawa wanasema watu weusi ni sawa na weupe. Anasema badala ya kusema kwamba watu weupe ni watu wa ajabu kweli, wanaweza kuwafundisha nusu manyani hawa wakafanya mambo ya kibinadamu, wanapotosha Taifa letu teule kusema kwamba nusu nyani hawa ni sawasawa na binadamu!

Hiyo ndiyo jeuri ya watu kama kina Hitler, kutoamini usawa wa binadamu. Na Hitler hakutaka kuishia hapo. Alikuwa anaamini watu weupe hao wako weupe walio bora zaidi kuliko weupe wengine. Wenzao hawa wa Afrika ya Kusini, hawa akina Voster, hawakupigana vita vile vya Hitler; walikataa kwa sababu imani yao ni ile ile. Walikuwa jela wakati wote wa vita vile vya kumpiga Hitler; wao walikataa kabisa kumpiga Hitler kwa sababu imani yao ni ile ile. Na hawa wanaamini kabisa, kwa Msahafu, kwamba ndivyo Mwenyezi Mungu alivyofanya; ameumba watu weupe kuwa bora zaidi kuliko watu weusi, na kwa hiyo lazima watu weusi watawaliwe na watu weupe.

Nasema jeuri ya ukoloni au ya utumwa, au ya ujahili ni hiyo ama ya kujifanya miungu, ama ya kuwafanya binadamu wengine kuwa ni wanyama. Na jeuri ya namna hiyo, ninasema inazidi jeuri nyingine yo yote duniani. Na inapotokea akili ya binadamu aliyekomaa inakataa: inakataa kabisa kukubali! Kwa hiyo lazima mpambane nayo jeuri hiyo po pote inapotokea.

Sasa ilitokea kwetu. Rafiki zetu Waingereza hawa, ingawa wao hawakupenda kutawaliwa na kina Hitler, wao walidhani wana haki kutawala sana duniani. Watu wachache Waingereza wakajidai wanakwenda kutawala Wahindi. Wahindi ni wengi sana. Lakini jeuri hii ya kwamba wao ni bora zaidi kuliko watu wengine ikawafanya Waingereza hawa wathubutu hata kwenda kuwatawala Wahindi na sisi pia; na wote tukawa chini ya himaya hiyo ya Kiingereza. Lakini hatukukubali. Afrika haikukubali, Asia haikukubali; na mahali po pote walipokuwa wanatawaliwa, watu hawakukubali. Wakafanya jitihada mpaka wakajitawala. Jeuri ya namna hiyo inapotokea, nasema, akili ya binadamu aliyekomaa inakataa, na lazima uipinge mpaka ujitawale.

Sasa tumeipinga na tukajitawala. Hivi leo tunaadhimisha huko kukataa kwetu kutawaliwa na watu wengine ambao wanajidai kwamba labda wao ni bora zaidi kuliko binadamu wenzao. Basi tumepata uhuru wetu. Na baada ya kupata uhuru wetu tumetangaza: tumesema nini shabaha yetu tukiwa nchi huru. Na shabaha zetu tumesema ni mbili.

Moja ni kuutumia uhuru wetu katika jitihada ya kuwaendeleza wananchi; kuvunja yale makovu yaliyofanywa na ukoloni, kujenga heshima ya wananchi wetu, kuleta maendeleo. Na tukasema maana ya maendeleo kwetu ni kila litakalosaidia kuleta heshima ya Mtanzania. Kila kitendo kitakachoweza kumrudishia ubinadamu wake Mwafrika, ubinadamu uliokuwa umevurugwa-vurugwa na matope ya ukoloni, sisi tutakiheshimu kukifanya kwamba ni kitendo cha maendeleo. Hiyo ndiyo jitihada yetu ya kwanza. Lakini shabaha yetu ya pili ilikuwa ni kuwasaidia wenzetu nao katika Afrika ambao hawajajikomboa, hawajafikia hatua hii ambayo sisi tumeifikia, na wao wajikomboe.

Kwa hiyo tumekuwa tunazo shabaha hizi mbili, ya maendeleo ya nchi yetu, kuendeleza uhuru wetu na maana ya uhuru, na kuwasaidia wenzetu nao katika Afrika wajipatie uhuru wao. Hatuna uwezo mkubwa sisi, uwezo wetu ni mdogo. Uwezo wa kuleta maendeleo ndani ya nchi yetu ni mdogo; na uwezo wa kuwasaidia ndugu zetu wajikomboe nao ni mdogo.

Lakini dunia inajua, na Afrika inajua, kwamba pamoja na udogo wa uwezo wetu, tumefanya jitihada za dhati kuzitekeleza shabaha hizo mbili: kuleta maendeleo kwa wananchi wetu, na kuwasaidia wenzetu katika Afrika kujikomboa. Nasema dunia inajua, na Afrika inajua, kwamba pamoja na udogo wetu na unyonge wetu, lakini shabaha hizo tumejitahidi kuzitekeleza kwa dhati.

Na uhusiano wetu na nchi za nje unategemea sana msimamo wao katika shabaha zetu hizo mbili. Hatukupata kugombana na nchi yo yote kwa sababu haitusaidii kuleta maendeleo katika nchi yetu; hata mara moja. Kuleta maendeleo katika nchi yetu, tumesema, ni jukumu letu, na hatuwezi kugombana na mtu mwingine kwa sababu eti hatusaidii; hata kidogo. Hatujapata kugombana na nchi yo yote kwa sababu haitusaidii sisi au haiwasaidii wenzetu katika jitihada ya kuleta ukombozi katika Bara la Afrika; hata kidogo. Kwa sababu tumesema jukumu la ukombozi wetu, ni letu sisi Waafrika wenyewe.

Lakini tumegombana. Tumegombana na nchi ambazo tumeamini zinatuingilia sisi katika kuleta maendeleo yetu katika nchi yetu. Zinatuwekea vipingamizi, zinatuvurugia mipango yetu, ama ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, ama ya kuwasaidia wenzetu katika ukombozi wao. Tumegombana nazo, nyingine nchi kubwa kubwa tumegombana nazo. Tuliwahi kuvunja uhusiano na Waingereza, tuliwahi kugombana na Wajerumani, tulitaka kugombana na Marekani kwa sababu ya msimamo wao katika shabaha zetu mbili hizo; moja, maendeleo ya nchi yetu wenyewe hapa, na pili, ukombozi wa Bara la Afrika.

Lakini hata mara moja hatukuwahi kugombana na nchi ya Kiafrika; hata mara moja. Katika miaka yetu hii 17 ya kujitawala kwa Tanzania Bara, hatujawahi kugombana na nchi ya Kiafrika, kwamba imetuingilia katika shabaha hizi mbili: hizo za maendeleo ya nchi yetu au za ukombozi wa Afrika. Tumenung'unika-nung'unika, kwa mfano, tulipokuwa bado Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo, tumenung'unika-nung'unika kwamba mipango ya maendeleo haiendi vizuri; nchi nyingine zinafanya mambo ambayo yanaweza kuvuruga maendeleo ya wenzao. Lakini sisi tulipokuwa tunanung'unika, na wenzetu vile vile walikuwa wakinung'unika. Lakini hatukufika mahali pa uhasama, tunaiona nchi moja kwamba inafanya jambo la uhasama hasa kwa sababu inatuingilia katika maendeleo ya nchi yetu.

Tumenung'unika juu ya msimamo wa baadhi ya nchi za Kiafrika katika jambo la ukombozi. Viongozi wa nchi nyingi za Kiafrika, katika suala hili la ukombozi, wanafikiri ni suala la kupitisha maazimio. Basi kila kikao watakapokutana watapitisha azimio juu ya Zimbabwe, Namibia na Apartheid watapitisha maazimio kila kikao. Tena wanaweza kuandika vitabu virefu sana vya maazimio. Lakini baada ya hapo wanasahau; jitihada ni ndogo zaidi kuliko maneno.

Kwa hiyo, mara nyingi tumenung'unika nung'unika kidogo. Jamani, tupunguze maneno, na tuzidishe vitendo kidogo katika jitihada yetu hii ya kuleta ukombozi katika Afrika. Lakini tumenung'unika tu, hatujapata kugombana na nchi yo yote ya Kiafrika kwamba inavuruga shabaha za ukombozi.

Rafiki yetu Amin wa Kwanza; ndiye wa kwanza kutugombanisha na nchi ya Kiafrika katika jambo kubwa kama hili la kutuvurugia hasa mipango yetu ya maendeleo katika nchi yetu wenyewe, na kutuvurugia hasa jitihada zetu za kusaidia wenzetu wa Afrika ya Kusini na wao wajikomboe. Ndio nchi ya kwanza kutufikisha katika hali ya uhasama na nchi ya Kiafrika.

Ni kisa cha kwanza kutufikisha katika hali ya uhasama na nchi ya ki-Afrika. Hatuna majeshi mipakani mwa majirani zetu. Uganda ndiyo peke yake tulikuwa tunacho kikosi kimoja mpakani. Na batalioni hiyo imekuwapo tangu mwaka 1972. Na baada ya ugomvi wa mwaka 1972, na mapatanisho tuliyopatanishwa na Somali kwamba askari wa Uganda warudi nyuma kilometa kumi kutoka mpakani na Watanzania warudi nyuma kilometa kumi kutoka mpakani, sisi kwa kweli askari wetu walikuwa mbali zaidi ya kilometa kumi, walikuwa kilometa 30 kutoka mpakani. Nasema tulikuwa na kikosi kimoja na kikosi chenyewe wala hakikuwa kamili.

Kwa nini. Mimi simpendi Amin. Tangu Amin ashike nchi hiyo watu wananishawishi kweli kweli nimpende, na sina sababu ya kumpenda hata kidogo. Amin ni mwuaji. Kuna jambo la ajabu sana katika Afrika na kama hatukuangalia tutavuruga sana heshima ya bara letu. Amin ni mwuaji. Tangu Amin ameshika uongozi wa nchi hiyo, sijui unaitwa uongozi wa uonezi wa nchi hiyo, ameua watu wengi zaidi kuliko Smith alivyoua Rhodesia; ndiyo, ameua watu wengi zaidi kuliko Voster alivyoua South Afrika. Lakini kuna tabia ya ajabu Afrika, kwamba kiongozi wa Afrika madhali ni Mwafrika anaweza kuua Waafrika anavyopenda na huwezi kusema kitu! Amin yule angekuwa ni mweupe, tungekuwa tumempitishia maazimio mengi ajabu. Lakini mweusi, na weusi wake ni shahada ya kuua Waafrika. Kwa hiyo kimya kabisa; hasemwi! Nilishangaa wenzangu walivyoamua kwamba watakwenda Uganda kwenda kufanya mkutano wa O.A.U. Nikapiga kelele, lakini mwuaji huyu mnampelekea heshima hiyo kwa nini? Akapelekewa heshima ile. Na kwa muda wa mwaka mzima akawa ndiyo Mwenyekiti wetu. Jambo la aibu kubwa!

Mambo haya mengine afadhali tuwe tunayasema wazi wazi, kwani baadhi yetu na baadhi yenu wengine hapa, kuna kumpenda- penda kidogo Amin. Amin aliwafukuza Wahindi na kwa sababu hiyo kuna Waafrika walifurahi kidogo. Waliposikia Amin amewafukuza Wahindi walifurahi, waliona huyu ndiyo Bwana barabara; huyu ndiyo mwafrika. Amin aliwahi kuwaambia Wazungu wampigie magoti kidogo; wakampigia magoti. Waafrika walifurahi wakasema huyu ndiye Mwafrika, maana wazungu hawa lazima kuwafanyia namna hiyo.

Lakini kwa nini jambo hili latufurahisha? Kwamba Amin amewafukuza Wazungu, amewafukuza Wahindi, liwe jambo la furaha rohoni; kwa nini? Niliwauliza mimi wakati anawafukuza, kwa nini hasa linafurahisha jambo hili? Wahindi ni watu, ni binadamu; unafurahi kuona binadamu wanaonewa, kwa nini? Kwa sababu, unasema, siyo rangi yangu. Lakini ukisha sema hivyo, wewe ni sawa sawa kabisa na Mkoloni mwingine ye yote yule anayeonea watu kwa sababu ya rangi yao. Wamekosa nini? Tena Wahindi wale wanapigwa, hawana cho chote, kwa sababu hawana mtetezi wao; hata Waingereza wakati huo wameogopa kuwatetea. Wanapigwa, wanafukuzwa, bila mali; na watu wengine wanafurahi rohoni! Wanyonge hawa wanapigwa mateke; wewe unafurahi nini, kinakufurahisha nini? Hawa ni binadamu wenzako sawa sawa kabisa na wewe. Wamekosa nini? Wana rangi tofauti tu, basi.

Rangi ni dhambi? Nani aliomba rangi yake duniani. Mimi sikumwomba Mungu kunipa rangi hii, mimi nimeshtukia tu ninayo rangi hii. Mimi rangi yangu siyo kitu cha kujivunia, wala siyo kitu cha kuonea fedheha; mimi sikuiomba. Kitu ninachoweza kuonea fedheha ni kumtukana binadamu mwenzangu, kumtemea mate, kumnyanyasa, kwa sababu hiki ni kitendo changu mimi. Lakini rangi yangu siyo ya kujivunia, wala siyo ya kuonea fedheha. Nywele zangu nimeshtukia tu mimi nina nywele za kipilipili, wenzangu wanazo nywele za singa; mimi sikuziomba zangu za kipilipili. Kwa nini tunafurahia mambo ambayo ni ovyo kabisa wala hayana maana.

Namsema huyu Amin hivyo kwa sababu amewahi kuwaonea Wahindi pale; na amewahi kuwadhalilisha Wazungu wawili watatu pale, basi, amejipatia heshima kubwa. Lakini hakumwua Mhindi. Mnamjua Mhindi aliyemwua? Safari moja alimpiga Mwiingereza mmoja pale anaitwa Denis Hill. Akatishwa kweli kweli! Alitishwa sana pale alipojaribu kumpiga mwiingereza Denis Hill, kwamba anaweza akamwua. Kwa hiyo wale walio na haki ya kutetewa walitetewa. Lakini Waafrika wamechinjwa wengi sana; hakuna hata sauti! Kimya kabisa, kama anaua mbuzi.

Nasema, mimi sina sababu ya kumpenda mshenzi huyu hata kidogo. Nitampenda kwa sababu ya rangi tu? Ni mwuaji tu; kwa hiyo mtu huyu simpendi mimi tangu zamani. Lakini pamoja na kutokumpenda, nawaambieni Watanzania, sijajaribu kumng'oa hata mara moja.

Mwaka 1972 alituudhi tu. Maana 1971 alipoingia, mara alipomng'oa Obote, akatangaza mwaka ule ule kwamba atataka kuichukua sehemu ile ya Kagera. Alitangaza mwaka ule ule wa 1971, mliosahau nataka kuwakumbusheni. Mwaka ule ule mara baada ya kumtoa Obote ndipo alipotangaza kwamba ataichukua sehemu ile ya Kagera. Nchi mbili zilizomkumbatia mapema kabisa ilikuwa ni Israel, na Waingereza. Aliambatana na Israel kwa sababu wakati huyu rafiki yangu Amin alipokuwa kiongozi wa jeshi la Uganda, alikuwa anasaidiana na Anyanya wale waliokuwa wanajaribu kulimega jimbo la kusini la Sudan lisitawaliwe na Sudan. Na kwa hiyo Serikali ya Sudan ilikuwa inapambana nao. Sasa Amin alikuwa anawasaidia hawa Anyanya. Na Wayahudi walikuwa wanapenda mpango huo, maana walitaka vita vile vya Kusini mwa Sudan viendelee na jeshi la Sudan likae kule Kusini, lisije likaenda kusaidia mapigano ya Middle-east. Kwa hiyo walimkumbatia huyu mara.

Waingereza nao rafiki zangu walimkumbatia kwa mambo yao ya ajabu ajabu. Serikali ya Conservative ilipoingia ikageuza makubaliano tuliyokwisha kukubaliana na Serikali iliyopita ya Uingereza kwamba Serikali ya Uingereza na nchi nyingine zisiuzie silaha

Serikali ya Afrika kusini. Serikali hiyo ya Con- servative ilipoingia wakaamua kwamba wataiuzia silaha serkali ya Afrika Kusini. Tukagombana. Nikaenda Uingereza mimi, nikakaribishwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Edward Heath. Naukumbuka ugomvi huo, siwezi kuusahau, Rais Kaunda wakati ule alikuwa ndiyo mwenyekiti wa O.A.U., naye akaenda. Wakati ule nikawaonya rafiki zangu Waingereza, nikasema, Jamani mwambieni Heath jeuri hii aliyonifanyia mimi asije akamfanyia Kaunda. Kaunda ni mpole zaidi kuliko mimi; lakini hapendi jeuri ya namna hii. Mimi naweza nikavumilia vumilia kidogo, lakini Kaunda havumilii jeuri ya namna hiyo. Sasa mwambieni Heath asije akamfanyia jeuri ya namna hii. Sijui kama salamu hizo zilifika au hazikufika. Lakini akaifanya, Kaunda alimwacha kwenye chakula chake. Alikuwa amemkaribisha kwenye chakula, akasema, Chakula chako sasa kula mwenyewe, mimi sikubali. Mimi nilikila.

Mwaka uliofuata tukafanya mkutano Singapore, mkutano wa nchi hizi zinazoitwa za Commonwealth. Tukawabana sana Waingereza, na kubanwa huko kuliongozwa na kikundi chetu kilichokua kinaitwa Mulungushi Club, yaani Kaunda, Obote na mimi. Tukawabana sana Waingereza. Ndiko Obote alikotoka akapitia Nairobi akaja hapa. Hakurudi tena Uganda.

Waingereza rafiki zangu wakamfurahia sana Amin, siku hizi Waingereza wanapolialia juu ya Amin mimi hucheka. Wakamkumbatia, wakanicheka, sasa mimi nasema marafiki zake wawili walikuwa ni hao: Wayahudi kwa sababu zao hizo na Waingereza kwa sababu zao hizo. Wakamkumbatia Amin, Amin akatangaza kwamba anataka kuichukua sehemu hiyo ya Kagera, akatangaza mara moja kwamba ataichukua sehemu hiyo ya Kagera. Akaondoka kwenda Uyahudi kwenda Israel, kwenda kuomba silaha kwa sababu hiyo hiyo. Akawaomba Wayahudi silaha, wakamnyima, Sasa yameandikwa mambo yale. Siku hizi wanasema wanaulizana kikwao, wanasema huyu mtu ana akili au mjinga huyu?

Akatoka hapo akaenda kwa Waingereza kuomba silaha, Waingereza Walimpokea vizuri wakampeleka hata kwa Malkia. Malkia wa Uingereza huyu anasumbuliwa sana siku nyingine. Sasa sijui walizungumza nini, lakini rafiki yangu Amin akarudi silaha hana. Lakini akapata askari, Ofisa mmoja wa jeshi wa Kiingereza, sijui alimpataje, amshauri jinsi ya kutimiza shabaha yake.

Amin ndiyo shabaha yake sasa ikapanuka, ikawa siyo kuchukua Kagera peke yake, lakini sasa kuchukua sehemu yote ya Ziwa, ya Mikoa ile ya Ziwa, afike mpaka Tanga. Maana alisema kwa nini nchi yangu mimi isiwe na bandari. Kenya wanayo Mombasa, Tanzania wanayo Dar es Salaam na Tanga, na mimi sina bandari. Na mipango kweli akaitengeneza, ndipo mwaka huu wa 1972 aliponichosha na watu wa Obote nilijua hawajafurahi sana naye. Nikafumba macho. Mwaka 1972 nikafumba macho. Hatukuwasaidia wale; tulifumba macho tu. Tukafumba macho kwa sababu ya jeuri yake hiyo, wakamtikisa tikisa kulee.

Lakini nasema pamoja na kutokumpenda, na sina sababu ya kumpenda, sijajaribu hata mara moja kumpindua au kuhujumu serikali yake. Amin amekwishakuja Tanzania. Alikuja Mwanza safari ile, Amin tumempelekea ujumbe mara nyingi sana. Aboud Jumbe amefika Uganda mara tatu, mara ya mwisho ilikuwa ni ya ajabu kweli. Nilijaribu kumshawishi asiende, alisema Bwana acha niende. Sasa mtu huyu. amesema niende, na lazima niende nimalize mambo haya. Akaenda Uganda. Na huyu Amin ni mtu wa tabia ambayo Waingereza wanaita buffoon sijui Kiswahili wanasema nini. Unapokuwa naye atajidai wema wa ajabu kabisa, utaridhika kweli na maneno yake. Anasema, mimi moyo wangu wote uko Tanzania, sina ugomvi na ninyi. Mazuri yote atayasema. Basi akampokea Makamu, akasema vizuri, akamkaribisha vizuri. Makamu akaja, niko Butiama napumzika kidogo. Makamu akapita pale Butiama, akaniambia Bwana we, nadhani mambo yamekwisha. Huyu mtu bwana tumezungumza vizuri sana, sana. Nikamwambia, Ee unadhani yamekwisha! Akasema, Nadhani yamekwisha. Nikasema, Kama mwujiza huo umeufanya, nitakushukuru kweli.

Na Makamu alikuwa siku ya pili au ya tatu yake anaondoka kwenda kutembelea nchi za Uarabuni. Basi amekuja Butiama amenieleza hivyo, halafu ameondoka kwenda Zanzibar kujiandaa kwenda Uarabuni. Asubuhi yake au siku inayofuata Amin amepeleka simu katika nchi zote za Uarabu, anasema, Mwangalieni huyu anayekuja, mtu mbaya kweli huyu anayekuja. Huyu nikibaraka wa Wayahudi, huyu ni kibaraka wa Imperialism. Anapeleka barua kwa nchi zote za Kiarabu, maana ndiko sasa Amin alikokuwa amegeukia, baada ya kunyimwa silaha na Wayahudi, na kunyimwa na Waingereza, sasa akageukia Uarabuni kuzipata zile silaha..

Basi nasema mtu huyu ndiyo namna yake ilivyo. Lakini, nasema, pamoja na kumjua namna hiyo, hatukupata hata mara moja kujaribu kumng'oa au kumhujumu. Lakini sasa yeye ameahidi na amekwisha tekeleza, sasa sisi tufanye nini. Maana jeuri yenyewe ndiyo jeuri Waswahili wanayosema "kuvuka mpaka". Maana kutenda alivyotenda ni kuvuka mpaka: kuvuka mpaka kwa maana zote mbili. Amin akavuka mpaka, akavuka mpaka pamoja na kutuongezea jeuri ile ile tunayoikataa, na ametamka kwamba atachukua sehemu ya Tanzania na kuwatawala Watanzania wale waliomo katika sehemu hiyo, wakipenda wasipende.

Sasa mtu akishasema hivyo tunajua kazi yetu moja tu. Ni kumchapa. Sasa na hiyo wananchi ndiyo kazi ambayo vijana wetu tumewapa, kazi ya kumchapa. Nilidhani nilipotangaza habari hii kwamba nitajitahidi kuwaelezeeni kila inapowezekana, lakini mambo haya magumu kueleza. Kwa hiyo nawaombeni mniwie radhi kama tumeshindwa siku nyingine kueleza eleza mambo yalivyo.

Kwanza ilikuwa tunalo tatizo, tatizo kubwa. Wale waliomshauri Amin walikuwa wamemshauri vizuri kweli, walimshauri vizuri, Mto ule Kagera ni mgumu sana, na daraja moja hilo la Kyaka, daraja letu zuri sana. Alikuwa ameshafika pale penye daraja na amelivunja. Amepata tabu kulivunja. Walijitahidi sana kulivunja, ingawa askari wake walipigwa, lakini askari walishindwa. Halafu akaenda, akamchukua engineer wa mgodi mmoja wa shaba: huyu akaja akalipua kwa baruti. Alitumia baruti za mgodi na akalikata vibaya daraja lile. Akakata kipande cha mita kama 100 hivi, kikatolewa chote.

Sasa ni dhahiri ikishakuwa umefanya hivyo, wale Watanzania watapata matatizo makubwa hawataweza kuvuka mto kabisa. Walikuwa wanavuka watu, wananchi raia waliokuwa upande wa Kaskazini, walikuwa wanavuka kuja Kusini, lakini walikuwa wanavuka namna ya kukimbia. Kuvuka kwenda kupigana vita maana yake lazima uvuke na silaha, na silaha zenyewe sio rungu. Hivyo aliyemwambia Amin, Vunja daraja, ukivunja daraja uko salama, hakuwa anaogopa marungu anajua silaha anazoziogopa zikivuka pale.

Kwa hiyo siku za mwanzo, vijana wetu. walikuwa wanayo matatizo makubwa kabisa wakati ambapo daraja lile lilikuwa limevurugwa kabisa; hakuna. Kwa hiyo, mwanzo kilichokuwa kinaweza kufanyika ni kwamba kama askari wa Amin wakifanya makosa, kwa sababu wanasema wamechukua dakika 25 kufika pale basi mambo ni rahisi, wakawa katika masafa ambayo wanaweza kupigwa na mizinga mikubwa kutoka kusini, watapigwa. Na ndivyo walivyofanya tarehe 15 Novemba. Wakapigwa vizuri sana, wakakimbia. Lakini huwezi kufukuza watu kwa mizinga tu unapiga mizinga watarudi nyuma. Kwa hiyo baada ya kupigwa katika eneo la masafa yale, wakarudi nyuma, akapiga kelele, Watu hawa wana mizinga ya ajabu sana, inapiga kwa mbali sana! Ndipo pale tulipoanza kumtania kwamba anaanza kutapatapa, tukasema, Hizi ni mvua za rasha rasha tu, za masika bado!

Hayo tulisema na alipopigwa vile vile tulisema. Sasa baada ya hapo tungesema nini: tungeongopa tu? Baada ya hayo tungewaambia, Anapigwa, tungekuwa tunaongopa tu. Kwa nini tuongope? Kwa hiyo tukanyamza, mwenyewe akawa anapiga kelele zake, sisi tukajua hatuwezi kumpiga mtu huyu mpaka kwanza daraja lile limejengeka. Yeye aliambiwa huko kwamba Tanzania ukishalivunja hili hawalijengi tena. Lakini vijana wakalijenga. Daraja lile wakalijenga kwa muda mfupi kabisa likesha. Wakavuka, Walipovuka Amin akapiga kelele, Jama wameniingilia!

Niliwahi kuona mchezo mmoja, watu wawili wanapigana, Sasa mmoja huyu maneno yake mengi sana. Sasa anawaambia hawa waliopo hapo, Jamani mshikeni huyo nitamwumiza mimi! Amin, tulipovuka mpaka, akapeleka matangazo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika, anasema, Jamani, huyo mtu amevuka; angalieni sana, ama sivyo nitampiga tena mara ya pili. Anasema hivyo Idi Amin, na huku anajitapa sana.

Akanikumbusha hadithi nyingine, huenda mliwahi kuisikia. Yuko askari mmoja, aliyekuwa anajitapa sana kwa kiongozi wake. Anasema, "Mimi, Afande, mimi shujaa kweli kweli". Akawa anajitapa sana. Sasa siku moja yule kiongozi wake akamwita, "Wewe, askari, wewe siku zote unajitapa tapa, ushujaa. Lakini mimi nimekuwa ninakutazama siku nyingi: kila ikilia risasi unakimbia! Huu ushujaa wako hasa uko wapi?" Akasema, "Tazama, Afande, mimi shujaa kweli kweli; nina moyo kama wa simba. Taabu yangu mini ni miguu. Kila ikipigwa risasi miguu inakimbia pamoja na moyo wake". Amin hodari sana kwa kupiga makelele. Lakini vijana walipokwisha vuka mto si kelele hizo. Na mbio hazikuwa ndogo.

Lakini akapigwa tena tangu kuanzia tarehe 24, 25, 26, 27 hadi 28 mwezi uliopita. Alipigwa, rafiki yangu, na akapiga kelele nyingi sana. Na sisi tukanyamaza, tuseme nini? Ndipo waongo wenzake walipoanza kumsaidia, wanasema "Watanzania wameingia mpaka Mbarara wako maili 20 katika Mbarara!" Uongo mtupu, wananchi, hatukuingia Mbarara. Wanasema, "Wamekwenda maili 20 kuelekea Masaka". Hata kidogo, wananchi, hatukuingia Masaka. Lakini kuchapwa alichapwa!

Hali ya sasa ilivyo. Hali ya sasa ni kwamba Amin na watu wake wamefukuzwa kabisa katika eneo letu. Hawamo kabisa! Vijana wetu wameishakalia sehemu zote zile ambazo ni muhimu Kaskazini ya mto. Hiyo ndiyo hali yenyewe. Lakini ninaposema hivyo, sisemi kwamba sasa mashambulizi yamekwisha, sitaki mnielewe vibaya. Nasema sasa hivi askari wa uvamizi wamefukuzwa kabisa kutoka eneo la Kagera. Vijana wetu wameshashika sehemu zote muhimu Kaskazini ya mto na wanaimarisha ulinzi wa eneo hilo. Lakini nataka mnielewe vizuri, hiyo sio kwamba maana yake sasa mashambulizi hakuna; si kweli hata kidogo.

Si kweli kwa sababu mbili. Kwanza bado Amin anapenyeza penyeza watu, wanaingia katika eneo hilo na kufanya jeuri kidogo. Nadhani vile vile vijana wetu wanaendelea kufagia-fagia watu mmoja mmoja ndani ya msitu. Hiyo ndiyo sababu ya kwanza, sababu ndogo zaidi. Lakini sababu ya pili, kubwa, kwa nini matatizo yetu hayajaisha, ni kwamba analeta askari mpakani, anazidi kuleta askari kwa wingi mpakani.

Sasa sababu za kuleta askari mpakani zinaweza zikawa mbili. Kwanza inaweza ikawa ni hofu; anaogopa. Anaweza akawaza, "Watanzania baada ya kututoa katika eneo lao sasa wanaweza wakaingia kushika eneo letu; kwa hiyo lazima tukae tukijihami". Inawezekana hiyo hofu ya kudhani kwamba Watanzania watashambulia, wataingia Uganda, ikawa sababu moja. Sababu ya pili, inawezekana, ni kutaka kutushambulia tena. Maana hata katika kelele zake zile alizotawanya dunia nzima, "Mshikeni huyo ama sivyo nitampiga", alisema, "Watanzania wananishambulia, wakiendelea namna hiyo mimi nitatekeleza hatua yangu ya pili ya uvamizi wa Tanzania". Alitamka hiyo, hatua yake ya pili ya uvamizi wa Tanzania.

Nasema ni vigumu sasa sisi Watanzania, katika hali hii ya leo, tupuuze kitisho chake hiki, kwamba anakusudia kutekeleza "hatua yake ya pili" ya uvamizi wa Tanzania. Huko nyuma nimepuuza. Huko nyuma amekuwa akisema, "Nitafanya hivi", tukampuuza, tukamwita mwenda wazimu. Hata tarehe 9 Oktoba alipotamka, mkasema, "Mzee, tuendelee na shughuli zetu". Kumbe anajiandaa kuivamia nchi yetu!

Sasa hawezi tena atamke kwamba anajiandaa kutekeleza hatua yake ya pili" ya uvamizi ya Tanzania, halafu sisi Watanzania tupuuze, tuseme, "Mwongo huyu, ni mwenda wazimu". Hatuwezi kumhesabu kwamba ni mwenda wazimu. Tukimhesabu kwamba ni mwenda wazimu, dunia itaamini kwamba sisi sasa ni wenda wazimu. Kwa hiyo, nasema, ingawa tumekwisha kumtoa katika eneo letu, hatuwezi kusema kwamba mambo yamekwisha. Hayawezi kwisha madhali anao watu wake pale mpakani na bado anayo shabaha hiyo. Hajakanusha kuitaka sehemu ile ya Kagera, Sisi tumemtoa; lakini hajasema kwamba haitaki sehemu ile ya Kagera.

Zimenijia nchi za Kiafrika hapa na kuniambia, "Mwalimu sasa acheni mapigano haya hizi ni nchi mbili za Kiafrika kwa nini mnapigana". Sasa mimi nimewaambia wenzangu, "Tazameni, wenzangu, mimi ugomvi sikuuanza, kauanza huyu mwenda wazimu. Sasa huyu mwenda wazimu. Sasa kama kweli mnataka ugomvi huu uishe, tusaidieni; wasaidieni Watanzania ugomvi huu uishe. La kwanza, lazima mlaani kitendo hiki alichofanya huyu mtu; mkilaani mkisema, "Wewe mtu mbaya: kwenda kuvamia nyumba ya mwenzako na namna hii ni vibaya". Lazima kwanza mseme hivyo. Pili, mnamwambia mtu huyu yale madai yako kwamba sehemu ile ni yenu sharti uyafute hadharani. Tatu, madhara ambayo mmeingia Tanzania, mkayafanya, lazima kabisa myafidie madhara yale.

Sasa mkisha kumlaani kwanza; mkamlazimisha aseme kwamba hataki tena. sehemu yoyote ya Tanzania, mkamfanya angalau aseme atafidia madhara aliyofanya, nasema ingawa mtu mwenyewe ni Amin, ahadi yake haina maana, sasa mtakuwa mmepata sauti ya kuniambia jambo lo lote. Tunajua ahadi yake ya kusema "Kagera hiyo siitaki tena haina maana kwetu. Tunajua sisi haina maana, mtu huyu ni mwenda wazimu, neno lake halina maana. Hata hii ya pili ya kuahidi kulipa, tunajua vile vile haina maana. Ahadi inayoaminika ni ahadi ya mwungwana; huyu si mwuungwana.

Kwa hiyo, ingawa kusema "Hatuitaki Kagera tena", au, "Tutalipa", ni kauli ambazo haziaminiki, kwa sababu ni kauli zinazotoka kwa Amin, lakini wakati huo huo mmekwisha kulaani kitendo chake alichokifanya, sasa mkaigeukia Tanzania. Hapo sasa mnaweza kuniambia, Tazama, Mwalimu. Mtu huyu tumeshamlaani kwamba kitendo chake hiki kibaya. Pili, tumemwambia aseme, dunia nzima isikie, kwamba hadai tena sehemu yo yote ya Tanzania. Tumemwambia aseme, dunia nzima isikie, kwamba kama amefanya madhara, atalipa. Sasa tufanye nini zaidi? Na nyinyi kwa nini mnataka kuendelea zaidi?" Nasema angalau hapo mtakuwa mmepata sauti ya kuniambia jambo lo lote. Lakini bila hivyo hamna sauti ya kuniambia.

Nchi yenye kauli ya kuniambia cho chote ni nchi ambayo imekwisha laani kitendo chake. Nchi ambayo haijalaani kitendo cha Amin haina kauli ya kuniambia kitu, itaniambia nini?

Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali iliyopo. Mtu anachosema tu ni kwamba atatekeleza "hatua yangu ya pili" ya uvamizi wa Tanzania. Sasa mtu wa namna hii utamfanya nini? Mtu wa namna hii la kumfanyia ni kujiandaa zaidi na kumpiga vizuri sana. Na hiyo ndiyo hali yetu; hali yetu ya sasa ni kama hivyo nilivyowaelezeeni. Lakini tunajua mtu huyu shabaha zake hazijesha bado. Kwa hiyo tutajiandaa na kama hapana budi tutamchapa zaidi.

Asanteni sana, wananchi.
 
3 Kumkemea Mwizi ​

iliyotolewa tarehe 28, Februari, 1979

Ndugu Wananchi,

Nawataka radhi kuwasumbueni tena. Nilidhani ni vema niitumie nafasi hii kueleza hali ya mgogoro wetu huu unaoendelea na jirani yetu. Na hasa nilitaka kuwatoeni wasiwasi, kutokana na maneno mengi mengi yanayosemwa-semwa sasa hivi. Nilidhani nitumie nafasi hii, ili hata kama siwezi kuwatoa wasiwasi kabisa, angalau niwapunguzieni wasiwasi.

Kwanza nataka kueleza msimamo wetu juu ya jambo la usuluhishi. Sasa hivi ziko jitihada za usuluhishi; na jitihada hizi zimekuwapo wakati wote. Tangu mgogoro huu uanze, zimekuwako jitihada za usuluhishi, na mimi nimekuwa nikieleza-eleza matatizo yetu juu ya usuluhishi. Sasa uko uwezekano wa kutoeleweka, na mimi nahofu uwezekano huo uko, na kwa hiyo ningependa kueleza ili isiaminike hivyo. Maana inaweza ikadhaniwa kuwa Tanzania haitaki suluhu; uko uwezekano wa kudhaniwa kwamba Watanzania ni wagomvi, hawataki suluhu. Watu wanaweza kudhani kwamba Mwalimu ni mkorofi, hataki suluhu; anayetaka suluhu ni Amin..

Sasa nataka niwaeleze kwamba hivyo si kweli hata kidogo. Si kweli kwamba hatutaki suluhu. Tulichosema tangu mwanzo, na ambacho tunakisema hadi sasa, ni maelezo ya msimamo wetu juu ya suluhu. Tumeeleza msimamo wetu kwanza kwa wasuluhishi, hasa wa OAU, juu ya kitendo chenyewe kilichoanzisha mgogoro. Nasema wasiwasi wetu si juu ya suluhu yenyewe, la; ni juu ya msimamo wa wasuluhishi wenyewe, na hasa OAU, juu ya chanzo cha mgogoro huu ambao wangependa kuusuluhisha. Pili ni msimamo wa mwenzetu huyo ambaye tunataka kusuluhishwa naye. Hayo ndiyo niliyokuwa nayasema, kwa niaba yenu, na nitaeleza sasa hivi kwa nini tumekuwa na msimamo huo na kwa nini tutaendelea kuwa na msimamo huo, ikiwa hali yenyewe haitabadilika.

Kwanza juu ya OAU, nasema hivi. Kama jirani yako amekuibia, ameingia katika nyumba yako akaiba, kwa desturi mwizi huyu akipata nafasi atakimbia, kwa sababu amekwisha pata lile analolitaka. Wewe utajitahidi kumkimbiza. Sasa mtu asiyejua chanzo cha kumkimbiza huku, akija akaingilia tu hapo katikati, akasema, "Huyu unamkimbiza kwa nia ya ugomvi; simama!" Akakusimamisha. Kitendo chake cha kutomkimbiza mwizi kinamsaidia yule mwizi. Ijapokuwa anaweza kusema kweli kwamba kitendo hicho ni cha suluhu, lakini suluhu hiyo ni kumsaidia yule mwizi, kumpa nafasi akimbie na mali yako. Ama kama msuluhishi huyo anawakuta mmeshikana hasa, wakati mnapigana ngumi, mali yako anayo mwizi mfukoni. Lakini yeye msuluhishi, anasema, "Mimi kazi yangu ni usuluhishi tu, jingine sijui", basi atakuwa anamsaidia mwizi. Kwa kujitahidi kupita katikati yenu, kuwaachanisha ninyi mnaogombana; kwa kufanya hivyo mwizi ataondoka, na ile mali yako atakwenda nayo. Ukimwuliza msuluhishi huyo, "Bwana we, vipi mali yangu?" Atakujibu, "Mimi msuluhishi!" Lakini ukimwambia msuluhishi, "Ugomvi huu unaujua hasa mwanzo wake? Huyu ana mali yangu, bwana!" Msuluhishi anasema, "Katika jambo hili la mali mimi simo". Wewe mwenye mali itakulazimu kumwambia, "Kama wewe humo, bwana, niachie, maana namweza huyu".

Kwa hiyo katika jambo hilo la ugomvi wetu na Amin, nasema tunachokisema ni msimamo wa OAU, siyo ule usuluhishi; usuluhishi nitakataaje?

Ninapokea wajumbe hapa, nimepokea wajumbe wengi kabisa, wajumbe wa nchi mbali mbali za Umoja wetu. Wamekuja nimekaa nao, nimezungumza nao. Na nimewaeleza namna ya kuweza kusuluhisha, kuleta suluhu ya kweli. Kwa hiyo kwanza kwa jambo hilo la msimamo wa OAU, nimesema, Tusaidieni na sisi kulimaliza jambo hili. Katika kusaidia jambo hili watambue kwamba kuna kosa limefanyika hapa: kwamba katika nchi mbili hizi, Uganda na Tanzania, nchi moja imekosa na nchi nyingine imekosewa. Watambue hivyo, waseme hivyo; na iwe waziwazi kabisa. Na hasa kwa suluhu, hapana sababu hata ya kutafuta ushahidi kwa sababu huyu aliyeiba kasema, "Nimeiba". Amesema, "Nimekwenda, nimeingia katika nyumba hii; nimeivunja na mali nimechukua, na tangu leo mali hii ni yangu". Hakuna ubishi. Nimeiambia OAU, Tunachowaombeni mkemeeni huyu, mseme wizi ni jambo baya.

Nilitaka waeleze kwamba Amin kwa kuivamia Tanzania umeikosea kwanza Tanzania, pili umeikosea OAU yenyewe; kwa hiyo tunakukemea hivyo kwa sababu umevunja misingi ya Katiba ya OAU. Nimewasihi OAU waseme hivyo lakini hawasemi. Huu ni mwezi wa nne sasa. Wananiambia, "Lakini unajua OAU ina matatizo sasa ya kuita mikutano; siyo rahisi kuita mikutano ya OAU". Nimesema, "Vema," na kuwauliza kwamba kwa kitendo hiki cha nchi moja kuvamia nchi nyingine ya Afrika kweli hatuwezi kuita mkutano wa OAU? Nimesema tuite mkutano, kikao cha harakaharaka, si lazima kuita kikao cha Wakuu wa Nchi, bali tunaweza kuita kikao cha Mawaziri. Haijafanyika hivyo.

Mpaka mgogoro ulipoendelea, na zikaanza mvua za rasharasha. Mwenzetu akaanza kulia, na akakipeleka kilio chake OAU. Ukaitwa mkutano wa Kamati ya Usuluhishi. Sisi tulipoomba mkutano, tukaambiwa kuna ugumu. Sisi tulipotaka mkutano, haukufanyika; lakini mwizi huyu anataka mkutano, unaitwa. Tulijiuliza tufanyeje? Tusiende au twende? Tukasema kwa nini tusiende? Maana tulitumaini kwamba haidhuru nani kauita mkutano huo, bado utasuluhisha. Tunachotaka sisi ni kauli; tunataka mahala ambapo inaweza ikatoka kauli hii ya OAU. Kwa hiyo sasa hivi Waziri wetu wa Mambo ya Nchi za Nje yuko huko Nairobi. Kiko kikao; tumekwenda huko. Na bado tunaomba kwamba, madhali sasa Kikao kipo, kinakaa, tunaamini kwamba OAU itatusaidia. Iseme kwa Uganda kwamba ugomvi huu usingekuwepo ila kwa sababu ya ninyi kuivamia Tanzania; mkajaribu kuchukua Tanzania na kuikalia, kuifanya sehemu ya Uganda; na kitendo hicho ni kinyume kabisa cha Sheria za Dunia na Katiba ya OAU. Tulitaka OAU waseme hivyo; watoe kauli ya haki kabisa kusema hivyo.

Baada ya kusema hivyo, tulitaka waiombe Uganda kwanza ikane madai yake, waseme, "Sisi hatudai tena sehemu ya Tanzania." Waseme hivyo. Mwizi huyo lazima aseme, "Siibi tena!" Na hawa wanaosuluhisha lazima wamwulize mwizi, "Je utaiba tena, au huibi?" Hamwezi mkasuluhisha kwa maana ya kwamba kesho na kesho kutwa anaweza akaiba tena.

Hata kama akiiba, lakini kwa leo hii mnataka aseme, "Siibi tena." Uganda ituambie, "Sina madai ya nyumba hiyo; nyumba hiyo si yangu, sina madai, hakuna kitu ndani ya nyumba hiyo ambacho ni changu." Maana madhali ulikwisha sema katika nyumba hiyo. "Nyumba ya jirani kuna mali yangu," ulikwisha sema hivyo, sasa ni lazima uikanushe kauli hiyo. Useme, "Ndani ya nyumba hiyo ya jirani sina ninachodai." Uganda lazima iseme hivyo, haidai Tanzania kitu cho chote. Lazima waseme hivyo.

Pili madhali Uganda waliingia, wakavuruga-vuruga ndani ya nyumba yetu, wamevunja vitu, na vingine wamekimbia navyo, lazima angalau waseme, "Tumevunja vitu humo, vingine tumekimbia navyo; tutalipa." Kusema lazima waseme; sasa kama watalipa kweli, au hawatalipa hilo ni shauri jingine. Maana inataka uwezo wenyewe wa kulipa. Umevunja mali ya watu, halafu unasema nitalipa, kiasi ulichovunja huko ndani unajua thamani yake? Lakini kusema lazima useme kwamba utalipa; lakini uwezo wa kulipa ni shauri jingine. Ndiyo tuliyoyaomba hayo.

OAU haiwezi kusema tumeiomba jambo lililo haramu. Mimi nasema ni halali. Kunyamaza ni haramu. OAU kunyamaza ni haramu; kusema ni lazima, na ni halali kabisa. Katika kitendo cha nchi moja kuivamia nchi nyigine, kinyume cha Katiba ya OAU, kinyume cha sheria za Dunia, OAU kuiambia nchi

46

iliyofanya hivyo kwamba kitendo hicho ni haramu ni jambo la halali kabisa..

Ingekuwa jambo hili la nchi moja kuvamia nchi nyingine tumelipeleka katika Umoja wa Mataifa, hivi sasa wangekuwa wanazungumza habari za uvamizi huu. Umoja wa Mataifa hauwezi kusema, "Sisi katika jambo hili hatuna la kusema." Nchi mbili zinaposhitakiana, moja inasema nchi hii imetuvamia, kinachotafutwa na Umoja wa Mataifa ni ushahidi wa kuvamia. Hamwezi kusema, "Hatuhusiki." Umoja wa Mataifa hauwezi kusema hivyo. Sheria za dunia ni kwamba kama nchi moja inaivamia nchi nyingine, United Nations haiwezi kusema hatuna neno la kusema, labda kama ugomvi huo haukupelekwa mbele yake. Lakini ukishafika, lazima waseme neno.

OAU, kwa kukataa kulaani uvamizi, anatiwa moyo mwizi. Kunyamaza kwa OAU kunamtia moyo mwizi; kunamsaidia mwizi. OAU haina jeshi; OAU ina kauli tu. OAU ingekuwa ina jeshi, tungetazamia kwamba nchi moja inapovamiwa hivi, nchi iliyovamiwa itakuwa na haki kudai mbele ya OAU kwamba imevamiwa kinyume cha kanuni za OAU. Na nchi hiyo iliyovamiwa itakuwa na haki kusema, "Tusaidieni, tumtoe mvamizi huyu."

OAU haina jeshi la namna hiyo. Lakini bado ina Katiba yake, ambayo inataka ilindwe. OAU inailindaje Katiba hiyo? Inailinda kwa kauli tu. Huyu anayevamia anakemewa; anakemewa na OAU. OAU inamwambia, "Umefanya vibaya wewe". Kwa hiyo kesho na kesho kutwa kila atakayeamua kufanya kitendo cha kuvamia nchi nyingine, anajua atakemewa. Ukiogopa hata kule kukemea, umejivua silaha ya pekee uliyo nayo. Kama huna la kufanya, basi afadhali sema huna.

Sasa kama nchi iliyovamiwa yenyewe ina uwezo wa kumkemea huyu mvamizi basi afadhali iachwe imkemee. Siyo ninyi mshindwe kumkemea huyu, halafu mumzuie huyu mwenye kuibiwa kumkemea mwizi wake. Au akianza tu kumkemea mwizi wake, ninyi muwe mmepata kauli kumkemea yeye! Mwizi hamkumkemea, huyu anamfukuza mwizi wake, anamshika anampiga kakofi kamoja tu, ninyi mnamkemea huyu mwenye kuibiwa.

Basi hayo ndiyo mazungumzo yetu na OAU. Matumaini yangu ni kwamba yatakubalika. Matumaini yangu ni kwamba kwa kweli OAU itakielewa kilio chetu hiki, watusaidie kwa kauli tu ya kumkemea Amin. Nani atasema, jamani, "Tanzania wanaomba jambo la ajabu sana la kumkemea mvamizi". Nani atasema, "Tanzania hawa wanadai jambo gumu kweli eti wanatudai tumkemee Amin kwa kuvamia nchi yao na kuchukua kipande kile na kusema sasa ni mali yake.

Kwa Sheria ya OAU kumkemea mvamizi wa namna hii ni haramu, ni jambo gumu!" Ugumu wake nini hasa? Bila kukemewa, mwizi anatiwa moyo, na anaweza akasema kumbe na kesho nikipata nguvu, naweza nikarudia, kwani hata kule kukemewa sitakemewa.

Kwa hiyo nasema wenzetu wanakaa na hilo tu, ndilo tunalowaomba. Wamkemee huyu waziwazi kabisa, dunia nzima ijue kwamba wavamizi katika Afrika hukemewa. Ingekuwa ni nchi nyingine ya nje imeivamia nchi yangu, sasa OAU kumbe wangenyamaza. Tuache Uganda; ingekuwa nchi moja ya Makaburu imenivamia hapa, hivi OAU ingenyamaza kimya kabisa! Ama hiyo wangeikemea? Kwa msingi gani? Makaburu wakinivamia, wanaweza kukemewa; ila nchi ya Kiafrika ikinivamia haikemewi. Kwa msingi gani? Uvamizi ni uvamizi tu. Hakuna kusema huyu aliyevamia ni wa rangi yangu. Mwizi ni mwizi tu; hakuna mwizi mmoja wa rangi yako, na mwizi mwingine wa rangi nyingine. Vipi iwe mvamizi huyu hawezi kukemewa? Hilo ndilo tunaloomba, hatuombi zaidi ya hapo.

Baada ya hapo tunataka huyu mtu atoe ahadi, na tunasema hata kama ahadi hizo akizitoa pengine hazitakuwa na maana, lakini zitakuwa na uzito. Akisha kuzitamka zina uzito. Amin atamke wazi, aseme, "Mimi sitaki tena nchi hiyo, sidai sehemu yoyote ya Tanzania tena! Na niko tayari kulipa". Akiisha tamka hivyo OAU wanaweza kutuambia, "Mwalimu, wewe unataka nini zaidi; unachotaka hasa zaidi ni nini?" Sisi tumemkemea mwizi wako, unajua hatuna zaidi ya kufanya isipokuwa kumkemea. Ameahidi hadai tena sehemu ya Tanzania na ameahidi kulipa. Wewe unasema hawezi, tena mwongo, lakini hata waongo hugeuka wakishapata funzo. Sasa si basi!"

Na sisi itakuwa vigumu kweli kusema isiwe basi. Kama mtasema, "Lakini Bwana unajua, mtu huyu haaminiki, mtaulizwa na OAU, Watanzania tutaulizwa "Sasa mnataka kufanya nini zaidi?" Mtajibu vipi? Mtasema kwamba tunataka kumfuata? Mumfuate wapi?

Hivi sasa Amin anasambaza uwongo, na ninawaonya marafiki zangu wasije wakakubali uwongo huo mwingine. Amin anaeneza uwongo huu, anasema, "Watanzania wanataka kuning'oa." Sasa nasema hivi. Amin huyu Serikali yake siipendi. Lakini sasa nimeishi naye miaka minane, nimekaa na Serikali ya Amin, na kusema nimemsema hivi hivi. "Serikali hii mbaya, Serikali ya mwuaji hii, imeua watu wengi zaidi kuliko ya Makaburu." Nimesema wakati wote, sijaacha kusema. Sasa kumbe kama nilikuwa na nia ya kuing'oa, hii miaka minane nilikuwa nangojea nini? Basi nilikwenda mwezi wa Oktoba nikamnong'oneza Amin, nikamwambia, "Amin we, unajua nataka kukung'oa mimi, lakini kisingizio sina. Kwa nini usivamie kwetu? Ukituvamia tu basi sasa nitakuchapa nitakung'oa." Nani anasema kama nilikuwa ninatafuta kisingizio ndio nimng'oe. Hili ni la uwongo, la kusema kwamba sisi tunataka kumng'oa.

Sisi tulikuwa na shabaha hii moja. Shabaha yetu ilikuwa ni kumtoa Tanzania. Ameivamia nchi yetu, shabaha yetu ni kumtoa. Mimi nilianza kuwa Mshauri wa Amin. Nilikuwa nawatuma watu nawaambia, "Nendeni, mwambieni Amin aseme kuwa hataki sehemu ya Tanzania tena; na atalipa". Mwambieni aseme, "Hizo hasara nilizofanya naiomba OAU mwende huko mzitazame-tazame hasara hizo ni kiasi gani, baada ya hapo nitalipa". Aseme hivyo. Akisha sema hivyo mnigeukie mniambie: "Sasa Mwalimu unataka nini?" Itakuwa sina jibu kabisa. Na hasa tutakapokuwa tumekwisha kumtoa katika mipaka yetu sisi. Watasema, "Sasa mtu huyu hayuko katika mipaka yenu na, mmekwisha mtoa. Amekwisha sema hataki tena sehemu ya Tanzania; anasema yuko tayari kuwalipa. Hivi mnataka nini zaidi ya hapo?" Ningekuwa sina la kufanya.

Ila ninajua ninyi Watanzania mngekuwa bado hamjaridhika na mimi ningejua ninyi Watanzania hamjaridhika. Lakini ingekuwa lazima niwafuate, niseme, "Jamani, mimi najua hamjaridhika, lakini kumbe tufanyeje?" Ningekuja tu ningewaambia hapa hapa, "Jamani mtu huyu tumemtoa ndani ya mipaka yetu. Sasa amekwisha laumiwa; amekwisha kemewa na OAU. Amekwisha tamka, anasema hataki tena sehemu ya Tanzania; na pamoja na uwongo wake anasema atalipa. Lakini sasa tunabanwa na wenzetu, tuache; kumbe tusipoacha tunatafuta nini?" Ningewageukia; ningewajieni nikasema hivyo hivyo.

Lakini ninajua Watanzania wasingeridhika. Kwa nini? Kwa sababu mshenzi huyu ameingia katika nchi yetu. Amevuruga- vuruga nchi, amepigapiga, na ameua watu. Amevunja nyumba, na mali, na nyingine amekwenda nazo. Mwizi hatoki nje tu, halafu anasema yuko nje. Kuwa nje inatosha? Uingie ndani ya nyumba yangu, uvuruge vuruge, halafu baada ya hapo unasema, "Jamani, lakini nimeshatoka!" Lakini mimi nasema tungefikishwa hapo ningekuwa sina la kufanya. Mimi ninajua matatizo yote haya, lakini nikatoa mashauri haya.

Amin, badala ya kufanya hivyo, anatutisha. Anaendelea kututisha, kututisha, kututisha. Ndio maana nikawaambia vijana wetu mchapeni kidogo. Ndipo nikaruhusu zinyeshe kidogo zaidi. Sasa zimenyesha. Waswahili wanasema mvua unayoisifia imekunyeshea.

Kwa hiyo kabisa narudi pale pale. Huyu mtu tumemtoa katika nchi yetu. Alipoendelea uchokozi wake tumeruhusu zinyeshe. Aseme tu, aseme hilo analosema. Ugomvi wetu hakuna, ila hayo ninayoona. Kumng'oa si kazi yetu; sisi hatuna shabaha ya kumng'oa, ingawa nitafurahi kabisa aking'olewa. Maana dunia nzima itajua Mwalimu sasa ameanza kuongopa nikisema eti nikisikia kuangushwa huko mimi nitalia! Nikisikia ameangushwa nitafurahi tu.

Lakini kazi ya kumwangusha si yangu wala si ya Jeshi la Tanzania, ni kazi ya wananchi wa Uganda. Kazi yangu ilikuwa ni kumtoa nje ya mipaka yetu na hasa akifanya ukorofi zaidi ni kumpa adhabu kidogo. Kazi ya kumng'oa ni ya Waganda wenyewe.

Kwa hiyo narudia. Tumetoa masharti matatu. OAU wamkemee huyu. Halafu yeye aseme hadai sehemu ya Tanzania. Na tatu aahidi kulipa. Ndivyo nilivyokuwa ninasema siku zote. Lakini juzi nimewaambia ndugu zangu wa OAU, nikasema hivi. Huwezi kuwa una jirani yako na ukaahidi kwamba tangu leo tutaishi kwa amani kabisa, lakini inapokuwa huyo jirani yako akigombana na mkewe anakusingizia wewe! Wewe ulikuwa hupo, huna habari; umekuja unakuta kumbe jana usiku aligombana na mkewe. Sababu ya kugombana hata hujui. Anakuambia, "Ni Abdallah tu, ndiye anayeleta ugomvi huo nyumbani kwangu!" Siku nyingine anagombana na watoto wake au kwa ulevi wake mwenyewe, au kama mtu ye yote anavyogombana na watoto. Akiisha gombana tu, anajua mwenyewe sababu za kugombana na watoto hao, anasema mimi nisingegombana na watoto hawa isipokuwa ni Abdallah tu. Sasa jirani wa namna hii, kuna mawili: ama aache kukusingizia, ama uhame.

Kwa sababu kwa kweli ikiwa ataendelea namna hiyo, wewe uahidi nini? Wakufuate watu kwako na kuja kusema huu ugomvi baina yako na Abdallah lazima uishe. Utasema, "Mnakuja kwangu kwa nini; nendeni kwake msije kwangu. Yeye kila akigombana na mke wake anasema ni mimi. Sasa mimi mnanifuata nije nifanye nini! Akiwa na ugomvi wa nyumbani mwake anasema ni mimi tu siku zote, mimi nifanye nini?" Ninasema afadhali mtu jirani, unaweza ukahama. Unaweza kusema, "Jamani mimi nahama hapa, mtu mwenyewe mlevi". Lakini nchi itahama kwenda wapi? Tanzania tuhame tumwache Amin hapa, twende wapi? Ningekuwa na uwezo kumhama ningemhama mtu huyu, maana najua ana ugomvi nyumbani; na sababu za ugomvi wake anazijua vizuri wala haziishi. Kwa hiyo tunamwomba, wala hatutanii, na tunawaomba wenzetu wasema hivyo: Ugomvi wa nyumbani kwake asitusingizie.

Kwa hiyo nataka kumalizia kwa hilo. Amin sasa hivi amekabiliwa na magomvi haya mawili. Mimi nasema kuwa ugomvi wa kwetu akipenda utakwisha kesho. Amin amekabiliwa na magomvi mawili. Moja analo wakati wote. Anachinja wananchi wa Uganda pamoja na askari wake mwenyewe. Tangu ameingia katika nchi anachinja watu pamoja na askari: wanajeshi wake mwenyewe. Akiamua tu, anawachinja, na dunia inajua, siyo kwamba ninamsingizia. Na wanajeshi wake wanajua hivyo, maana ndio wanaochinjwa. Akibaki anajua amebaki tu, lakini zamu yake haijui itakuja lini. Anao ugomvi wake mwenyewe na huo tulikuwa tunaujua siku zote. Kama asingetuingilia, ugomvi huu wa pili usingetokea. Alituingilia, ndipo akazua huo wa pili. Wa kwake upo, amekuwa nao wakati wote, bila sisi na ataendelea nao wakati wote bila sisi. Huo ni ugomvi wake yeye, baina yake na watu wa Uganda.

Ninalopenda kulisema, na napenda kulisema wenzangu wanielewe, ni hili. Mimi sina haki, Tanzania haina haki hata kidogo kujaribu kumng'oa Amin, au kung'oa serikali yo yote. Hatuna haki hiyo. Maana nikikubali tuna haki hiyo sasa nasema nchi nyingine nazo zina haki ya kuja kung'oa yetu. Mimi sina haki ya kung'oa serikali ya Amin; na serikali nyingine yo yote ya Afrika au duniani haina haki ya kwenda kuing'oa serikali ya Amin. Hili ni jambo la msingi. Pamoja na kutokumpenda Amin (na simpendi kweli) lakini sina haki hiyo. Serikali ya Tanzania haina haki kuingia Uganda kwa sababu ya kwenda kumtoa Amin, hatuna haki hiyo. Serikali ya Amin ni serikali ya kishenzi. Watu wa Uganda wana haki, ambayo watu wengine mahali pengine duniani wanayo, kujaribu kumng'oa Amin. Narudia wakati wote maneno hayo, na wala si mara yangu ya kwanza kusema hivyo.

Wafaransa kama hawaridhiki na Serikali yao wanaweza wakavumilia. Wakavumilia, wakavumilia, lakini utafika wakati kwa Wafaransa watasema: "Potelea mbali. tutaing'oa". Wakaing'oa. Waingereza nao wanavumilia Serikali yao mbovu wee, mpaka wanasema: "Hapana jamani, tumechoka sasa, hatuwezi kuvumilia zaidi, tuing'oe." Wakaing'oa. Dunia inashangilia, inaandika vitabu, inatueleza jinsi walivyojikomboa Waingereza hao na jinsi Wafaransa walivyojikomboa. Nimesoma yote hayo katika shule. Marekani walichoshwa, wakashika silaha wakaitoa serikali yao Warusi wamefanya, Wachina wamefanya. Juzi Iran wamefanya. Iran wamevumilia, wamevumilia, wamevumilia wakachoka, wakasema, "potelea mbali". Wamemng'oa yule Shah. Mimi ninawapa pongezi wananchi wa Iran; ni haki yao. Kila nchi ina haki, kila mwananchi ana haki ya namna hiyo.

Hawana haki ile kwa nini? Serikali ni ya watu walioko pale. Kama inawaridhisha, vyema; lakini kama haiwaridhishi, mpaka wanakaa watu kama vinyama ndani ya nchi yao, unafika wakati binadamu wanasema: "Sasa kama hatukushika silaha hatuwi watu tena, wala hatuwezi kujihesabu tena katika nchi yetu. Sasa shika silaha, tunatoa." Nasema haki hiyo wanayo, siyo wa-Iran tu, nasema wananchi wa Uganda wanayo; na Watanzania wanayo.

Kama Watanzania wanafika mahali wanasema: "tumechoka sana, maneno mengi, tunaishi katika nchi yetu wenyewe, tunaishi kama vinyama-nyama hivi, tumechoka. Tukifanywa hivi vinyama katika nchi yetu, anatufanyia nani mnyama katika nchi yetu? Tumechoka". Wanasema: "Potelea mbali". Watanzania wana haki ya kusema, "Potelea mbali", na ninasema ninasema wanaposema, "Potelea mbali," hakuna mtu wa kuweza kuwazuia, hakuna mtu mwenye haki ya kuwazuia. Hakuna mtu ana haki kutoka nje kwenda kuwazuia. Kweli hakuna nchi ina haki ya kwenda kuing'oa serikali ya Amin; lakini pia hakuna nchi ina haki ya kuwazuia wananchi wa Uganda kuing'oa Serikali ya Amin. Hii ni haki ya kila watu katika nchi yao.

Litakuwa jambo la ajabu sana kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika utawazuia wananchi wa Uganda wasiing'oe serikali wasiyoipenda. Sasa hivi hizi serikali za Kusini ni za Wazungu, na Makaburu. Kwa hiyo Waafrika wa Namibia na wa Rhodesia na Waafrika ya Kusini wanaweza kuitumainia OAU. Wanaweza wakalia, "Jamani tunaumia," na OAU inaweza ikawasikiliza. Kama ina jambo la kuweza kufanya itaweza kufanya; kama haina angalau itapitisha azimio tu la kuikemea serikali ya Makaburu.

Waafrika wa serikali ya nchi inayojitawala hawana. Wanaweza wakachinjwa kama nguruwe, hakuna sauti itakayotoka mahali po pote kuwasemea. Hakuna. Haya yanafanyika katika Afrika na tunaona wanachinjwa

Waafrika. Lakini hakuna sauti, labda Umoja wa Mataifa unaweza kuchukua jukumu hilo. Labda waende United Nations. Lakini OAU hapana. Hawawezi watu kwenda katika OAU, na kusema, "Jamani, nchi inaumia," au kwamba wenyewe viongozi wa OAU waseme, "Jamani lakini mwenzetu mbona anachinja watu kule!" Hata kidogo, hawafanyi. Wanasema ni mwiko kabisa kabisa wa OAU. Mimi nashangaa mwiko huu unatoka wapi? Smith akichinja watu tunampitishia Azimio, lakini Amin yeye anaweza akachinja watu, hatufanyi kitu. Kwa nini?

Vema basi. Mimi naiona ni dhambi kubwa kutomkemea mtu anayechinja Waafrika; serikali inachinja Waafrika hatuikemei! Ni dhambi ya kutosha hii. Sasa wenyewe wakiisha sema, "Potelea mbali", waacheni basi. Hapana tena kufanya vitendo vya kumpa heshima, na kumpa nguvu mchinjaji wa watu. Heshima hiyo mnapompa, na heshima yake mwenyewe mnaona inakwenda, mnamtafutia heshima kwa nguvu kufanyaje, na ninyi mnajua akipata heshima ile na nguvu ile atawachinja watu wale zaidi?

Kwa hiyo mimi nasema, sisi tunadai hayo. Kesho unakuja Ujumbe wa OAU. Mimi ninayotaka kuona ni kwamba Amin anakemewa na OAU kwa kutuvamia sisi na kuvunja misingi ya OAU, na pili anatamka wazi wazi hadai tena sehemu ya Tanzania; na tatu, anaahidi kulipa. Mimi nasema nikiyapata hayo nitarudi kwenu wananchi na kusema, "Jamani, masharti yale yameshatimizwa." Hata mngenuna namna gani nitasema masharti yale yameishatimizwa; ningesema wazi wazi maana sidai jambo la ajabu.

Kwa hiyo matumaini yangu ni kwamba tutayapata hayo. Tukiyapata hayo jamaa wakishaelewa hivyo, halafu wakiondoka, tutasema, "Lakini nendeni, mwambieni. Mimi nina hakika ugomvi wake utaendelea; nisije tena nikasingiziwa kwa ugomvi wa nyumbani". Sasa baada ya kusema yote hayo, yaliyobaki nitayasema kwa kifupi.

Mmesikia maneno mengi ya vita. Mmesikia kwamba Masaka imeshikwa, na hiyo Masaka imeshikwa na Watanzania na Marekani na Wayahudi na "mercenaries" wanaoongozwa na askari wa Uganda. Mmesikia pia kuwa Mbarara imo katika matatizo.

Halafu baadaye ikatokea kauli kwa jirani yetu kwamba Masaka tumeishika. Kulitolewa kauli kwamba tumeshika sisi, tukisaidiwa na Marekani na mataifa mengine tukaishika Masaka. Mara, nadhani ni jana, akaanza kulia, anapiga kelele akisema, "Mimi nimekwisha, watu hawa wamekuja kwa wingi sana, mvua ilikuwa kali, nimeshindwa kabisa nguvu. Kwa hiyo tunaomba marafiki po pote mlipo tuletewe misaada, wala siyo ya silaha tu, nafikiri na watu vile vile". Nataka mlielewe hilo la kusema na watu vile vile. "Tunaomba misaada siyo ya silaha tu, lakini na askari vile vile." Amin anaomba askari kutoka nje. Nataka hilo tulielewe maana yake.

Halafu jana ikatoka habari. Askari wake wa Masaka wanasema, "Tumechoka kuuana. Huyu mtu tangu ashike nchi yetu ameivuruga mno, halafu anatufanya sisi tunauana wenyewe kwa wenyewe. Sasa tumeacha, na kiapo kile tulichoapa kumtii, sasa tunakikana. Sasa tunamtafuta po pote alipo." Nataka hilo nalo lieleweke.

Huyu mtu ameshasema Masaka imechukuliwa, Mbarara imechukuliwa, watu hawa wanakuja kwa wingi sana; na anaomba sio silaha tu, anaomba na askari. Askari wake wamekwenda wapi? Unaweza kuomba silaha, lakini yeye anaomba na askari kutoka nje; askari wake wamekwenda wapi? Halafu tukasikia kauli hiyo ya askari wake wanasema, "Tumeasi." Wengine tukaanza kusema, "Ala, kumbe hana askari!"

Maana mambo hayo lazima tutafute njia ya kuyaelewa. Huyu mtu anasema, "Jamani, mimi nimeelemewa huku; naomba silaha na naomba na askari vile vile." Tukashangaa huyu mtu anaomba na askari; askari wake wamek- wenda wapi? Tukasikia kauli inatoka Masaka, "Mtu huyu ametuchosha, kiapo tulichokuwa tumeapa, sasa tunakikana. Sasa tunamtafuta; na askari wenzetu po pote mlipo tunaomba na ninyi vile vile mwungane na sisi katika kumsaka." Tukaona labda ndio maana mwenzetu anasema haombi silaha tu: anaomba na askari vile vile. Pengine hiyo ndiyo maana yake.

Sasa jana akatangaza. Anasema Masaka tumekwisha ishika. Tumeishika tena. Kumbe anao askari. Sasa kama anao, tunaomba aseme; asiombe askari kutoka nje.

Pili, tuna mashaka; tunadhani jana kaongopa. Tunadhani kauli yake ya kwanza ya kuomba silaha na askari ilikuwa kweli. Ingawa amesema uongo mwingi mtu huyu, lakini kauli ya mwanzo ilikuwa ya kweli. Tunadhani kauli ya askari wale ilikuwa ya kweli. Tunadhani kauli yake ya kuomba silaha na askari kutoka nje ina maana hiyo. La sivyo, Masaka kesha ishika, sasa na apeleke watu Masaka. Maana mambo haya ya uwongo niliwahi kuyaeleza. Safari moja tumesingiziwa hapa, wakasema askari wa Tanzania wako maili ngapi ndani ya Uganda. Nikauliza, "Lakini ushahidi huu uko wapi?" Nikaambiwa, "Mwalimu, ushahidi uko. Vinapita hivi vianga vinavyozunguka-zunguka dunia, vimepiga picha". Nikawaambia wazitoe basi hizi picha, ya ni tuendelee kubishana watu wazima kama watoto wadogo; wazitoe hizo picha, waseme, "Hawa ni askari wa Tanzania", tena waonyeshe. Unaona uniform ya Tanzania iko hivi, na ya Uganda iko hivi; kwa picha inaonekana namna hii kama ni kweli".

Sasa lakini kwa nini tunataka kuihangaisha dunia kama wenda wazimu. Amin askari wake wanasema wameasi; wamechoka, wanamtafuta. Na mimi nasema tusije tukasingiziwa ugomvi wa Uganda; sitaki nikasingiziwa mimi hata kidogo. Ugomvi wa Uganda sitaki tukasingiziwa sisi. Mimi nasema ugomvi wetu unaweza kwisha kesho. Mimi nangojea Ujumbe wa OAU; matumaini yangu ni kwamba ugomvi wetu wa Uganda unakwisha kesho. Lakini ugomvi wa ndani ya Uganda sitaki tukasingiziwa sisi. Sasa askari wake wamesema wanamsaka; wanamtafuta.

Sasa kama hawamtafuti, basi anao. Anatafuta askari wa kutoka nje kuja kutafuta nini, na askari wake anao! Wamesema wanamtafuta. Sasa kama si kweli, Masaka ni yake, ameishika Masaka; kama ni waongo hao waliosema kwamba imeshikwa, basi kesho na apeleke watu, waende kwa ushahidi, awapeleke pale Masaka, aseme, "Si mlisikia wajinga hawa, walisema askari wangu wameniasi miye." Ama awapeleke wakawaone hao Watanzania. Amin huyu mpaka sasa hajamshika hata Mtanzania mmoja? Hivi kweli tunaweza kuingia ndani mle, asionekane Mtanzania hata mmoja? Basi na awapeleke watu wawatafute hao Watanzania. Kusema kweli Watanzania labda tutamzuia, maana kama tupo sisi tunaweza tukamzuia kuja Masaka. Lakini walioko Masaka kumbe waongo, hao wanaosema kwamba wameshika Masaka, kumbe kesha watoa; ama kawatoa wao, ama kama ni sisi tulikuwepo Masaka basi kesha tutoa. Sasa kesho apeleke mashahidi, kuthibitisha hayo yanayosemwa eti "watu wangu wameasi wananisaka". Maana inawezekana huyu Mwalimu Nyerere hivi sasa anatafuta kisingizio cha kusema nasakwa na watu wangu, kumbe yeye ndiye ananisaka. Mimi simsaki. Sasa apeleke watu kesho, awapeleke kesho kwamba ni hawa. "Hao anaosema kwamba wamefika Masaka, Masaka si hii? Tuko sisi, na kikosi changu kile kilichokuwa kinasemwa kimeasi: si hiki! Kamanda wake si huyu na Kikosi chake kingine si hiki, na Kampuni si ile! Kampuni zote si hizi hapa mnaziona".

Ya nini mbishane? Watu wazima mbishane kama watoto wadogo. Amin aliwahi kuleta watu mpaka Mtukula. Tena wakawa wananikejeli. Wanakuja hapa hasa kuja kunikejeli, wanasema; "Mwalimu tumefika Mtukula". Sisi wakati huo hatuna uwezo wa kufika Mtukula. "Tumefika Mtukula, tumekuta upande wa Amin kule nyumba zote imara, upande wa kwenu huku hakuna hata kibanda, vyote vimepigwa chini". Nikawaambia, "Waambieni kwamba sisi ndio tumepiga kwetu, na kule kwake tukaacha". Wakasema, "Naam". Na kukubali mnakubali. Baada ya wakati huo anasema sisi tumeingia Uganda, tumepiga Uganda, tumevuruga-vuruga Uganda, halafu ndio akaanza kutufukuza. Nikawaambia, Amelikubali hilo, kwamba tumeingia Uganda, tumepiga, halafu tukarudi tukaanza kupiga kwetu huku? Mnalikubali hilo?"

Sasa nikawaomba, mpaka sasa kusema kweli nawaomba, kama hivyo ni kweli, kama tuliingia Uganda tukapiga, iteni mkutano: muiseme Tanzania, muilaani Tanzania. "Tanzania washenzi wakubwa ninyi mnaingia ndani ya nchi nyingine, mnakwenda mnavamia, mnapiga watu". Mtulaani sisi.

Kama kitendo hicho hatukufanya, kafanya yeye, mumlaani yeye. Mkemeeni. Kama hamwezi kumkemea; acheni sisi tumkemee.

Asanteni sana.



4 Masharti Matatu​

Hotuba iliyotolewa tarehe 5, Februari, 1979.

Ndugu Chairman


Kwanza ningependa kuwashukuruni viongozi wa Dar es Salaam kwa kunipatia nafasi hii tena kueleza hali ya matatizo yetu ilivyo. Kwa desturi yetu siku kama ya leo, tungekuwa tunaadhimisha mwaka wetu wa pili wa kuzaliwa kwa CCM, na kuanza kwa mwaka wa tatu. Kwa bahati mbaya, kwa sababu zinazojulikana, hatukufanya hivyo. Tulikuwa tumeisha amua hasa tusifanye hivyo. Wenzetu wa Mwanza walikuwa wanajiandaa vizuri. Hivi leo wangekuwa katika shamra shamra; nchi nzima tungekuwa katika shamra shamra; baadhi yetu sasa hivi tungekuwa hatuko hapa, tungekuwa tuko Mwanza kwa sababu ya kuadhimisha kutimiza mwaka wa pili wa CCM.

Nasema kwa bahati mbaya, kwa sababu tunazozijua hatukufanya hivyo. Kwa hiyo nilidhani niitumie siku hii ya leo kueleza tena hali yetu ya mapambano haya au matatizo yetu haya na jirani yetu ilivyo. Hali yetu hivi sasa ikoje.

Nilieleza mara ya mwisho tarehe 9 Desemba. Wakati ule nilisema kwamba baada ya matatizo ya mwanzo yaliyokabiliwa na vijana wetu, baada ya vijana kumaliza matatizo yale ya kwanza, hasa ya kutengeneza daraja pale mtoni, basi vijana walivuka. Baada ya kuvuka wakaweza kuwatoa maadui kutoka katika sehemu yetu ya Kaskazini ya Kagera, ambayo ilikuwa imekaliwa na jamaa hao. Nilieleza wakati ule kwamba vijana wetu wamevuka mto, wamewatoa maadui kutoka katika maeneo yetu, na wao wameyashika maeneo hayo.

Lakini nikasema matatizo yetu bado hayajaisha. Nilitoa tahadhari- tusidhani kwamba kule kuvuka mto, na kuwatoa maadui, basi ilikuwa ndio matatizo yetu yamekwisha. Bado yalikuwa hayajaisha, na nikaeleza sababu zake. Nikasema sababu moja mi kwamba ingawa maadui katika wingi wao tumewatoa katika eneo la Kaskazini, lakini bado inaelekea vimo vikundi vidogo vidogo vinawasumbua sumbua vijana wetu. Na kwa hio kazi kuwatoa hao lazima iendelee. Pili ya acha hao ambao wakati huo walikuwa bado wako kaskazini ya mto wetu, nilisema bado vikundi vya adui vidogo vidogo vinatokea Uganda vinaingia tena kuja katika eneo hilo kuwasumbua-sumbua vijana wetu. Kwa hiyo wanasumbuliwa na vikundi vya aina mbili. Kikundi cha kwanza ni vile vikorofi vilivyomo mle hatujaving'oa; na kikundi cha pili ni hawa wanaoingia-ingia ndani ya eneo lile kutoka Uganda. Hizo zilikuwa sababu ndogo zilizofanya nikasema kwamba bado matatizo yetu hayajaisha.

Lakini ilikuwepo sababu kubwa zaidi, nayo nadhani niliieleza kwamba ndio msingi wenyewe wa ugomvi ule. Nilisema ugomvi ulipoanza, wasuluhishi wakaanza, ndugu zetu, kuja na kusema, "Jamani, haifai kuendeleza vita, afadhali kuleta amani." Hatima yake niliwaomba jamaa hao, nikasema, "Jamani, kama kweli mnataka tufikie amani mapema, basi lazima mjitahidi kuisaidia Tanzania nayo ikubali amani. Kwa sababu bila kutusaidia tutapata taabu sana kukubali amani. Mtu huyu ameshambulia nchi yetu; amechukua eneo letu, ametamka kwa jeuri kabisa kwamba eneo hili amelichukua atalikalia na litakuwa ni sehemu ya Uganda. Sasa wenzetu mnatujia na kutuambia tutake amani, (amani tangia hapo tulikuwa tunataka; mwenzetu ndiyo kaivuruga); sasa tusaidieni basi tufike hapo ambapo hata sisi tunaweza tukakubali amani. Na mnavyoweza kufanya ni kwamba angalau na nyinyi mngetusaidia, kwa kuwa upande wetu katika kulaani kitendo hiki. Kitendo hiki ni kitendo kibaya! Basi Tanzania tutawashukuruni. Tutawashukuruni wenzetu kwamba angalau mmekuwa pamoja nasi katika kukubali kwamba kitendo hiki ni kibaya.

Lakini pili, mkamshawishi huyu jirani yetu afanye mambo mawili. La kwanza atamke kwamba huku kudai sehemu ya kaskazini ya Kagera kuwa ni sehemu ya Uganda ni kosa! Aseme, "Nilifanya kosa, Uganda haina sehemu yo yote ya Tanzania." Aseme, "Tulifanya makosa, na haturudii tena kuyafanya makosa hayo, kwa maana Uganda haina haki na sehemu yo yote ya Tanzania; na sehemu ile ya Kaskazini ya mto wa Kagera ni sehemu ya Tanzania. Uganda hatuna madai nayo, na tulifanya makosa kuidai." Basi kwanza atamke hilo, kwamba amefanya kosa hilo.

Tatu, amekwisha fanya kitendo chenyewe; amevuka, amefanya madhara; ameua watu na kuharibu mali. Hawezi kuturudishia watu, lakini kajuta na amekwisha kuonyesha kwamba amejuta, kwa hiyo angalau mumuwezeshe kusema tu kwamba amefanya makosa. Aseme, "Nimeingia Tanzania, nimeua nimeharibu mali; naahidi kwamba nitaifidia Tanzania kwa madhara hayo niliyoyafanya na yanayoweza kufidiwa." Kwa maana hawezi kufidia roho za watu! Basi angalau huyu jamaa mwezesheni aseme atafidia kinachoweza kufidiwa.

Kwa kweli hata akisema hivyo, kwa sababu sisi Watanzania tunamjua jirani yetu, ni mtu asiyeaminika, bado maneno yake yatakuwa hayana maana sana. Amin leo kusema, "Mimi nilifanya kosa kudai sehemu hii, siku nyingine siidai tena," ni maneno tu; kwa sababu anaweza akasema leo na kesho akafanya tena yale yale. Lakini atakuwa amesema; atakuwa ametamka hivyo. Amin kusema, "Ndio, nimeingia Tanzania, nimeua watu, na nimeharibu mali; naahidi kulipa," si kauli ya kuaminika. Kauli ya kuaminika ni ahadi ya mwungwana; huyu si mwungwana. Lakini atakuwa ametamka.

Kwa hiyo nyinyi mnaotaka suluhu mtatwambia hivi. Tazameni, nyinyi Tanzania; mtu huyu amefanya makosa. Kesha tamka kwamba ile nia yake ya kudai Tanzania sasa hana tena. Ninyi mnasema ni mwongo; lakini kumbe angekuwa mkweli angesemaje! Na kama sasa amejuta hasa, tunajuaje; maana hata waongo hujuta. Sasa kama amejuta angesemaje; si atasema vivyo hivyo? Akisema, "Nilifanya makosa kudai sehemu ya Tanzania, sasa nasema sirudii tena," ingawa mnasema kauli hii ni kauli ya mwongo, lakini inaweza ikawa kauli ya mkweli: na sasa kaisema. Lazima nyinyi muichukue kwamba ni kauli ya mkweli, mpaka hapo atakapoivunja.

Kadhalika malipo. Anaweza akasema leo, "Nitalipa," lakini asilipe. Lakini kaahidi: kaahidi kwamba atalipa. Sasa si mtataka muda? Mnataka muda watu waje wathamini hiyo hasara iliyofanywa, waweze kusema hasara iliyofanywa hesabu yake ni kadha, sasa huyo mtu mwone kama atalipa ama halipi. Lakini kesha tamka hivi. Kumbe mtaendelea na vita? Mnatafuta nini, naye kisha tamka? Si mpaka hapo mtakapoona kwamba halipi? Nikasema angeyatamka haya, japo hayana maana, lakini yangekuwa yana uzito kwenu nyinyi wasuluhishi kuibana Tanzania, Amin kwa kutamka hayo angekuwa amewapeni sababu za kufanya muibane Tanzania!

Lakini pamoja na kwamba kauli hiyo haiaminiki, na kwamba yeye, mwongo huyu, angeitamka ingemsaidia, ingewasaidia ninyi kutubana sisi, pamoja na hayo hajatamka! Amegoma kabisa kutamka! Ni kauli ambayo ingeweza ikawa ya manufaa kwake kuitamka, tena naisema mimi; ni kama mimi namtafutia mkorofi huyu namna ya kusema ili ajinasue katika mtego huo alikojinasa. Mimi nawaambieni, "Nendeni mkamwambie basi, angalau aseme hivyo!" Hataki! Hasemi! Hasemi! kwamba hataidai tena sehemu ya Tanzania hiyo. Hasemi kwamba atatulipa kwa madhara aliyopata. Sio hilo tu. Sasa anayoyasema si ya suluhu; ni kinyume kabisa. Anasema: "Hawa Watanzania wakiendelea kufanya mambo yao haya wanayoyafanya, mimi sasa nitatekeleza hatua yangu ya pili ya kuivamia Tanzania." Hivyo ndivyo anavyosema!

Nilieleza safari ile kwamba madhali mtu huyu bado hivyo ndivyo anavyosema. Mosi, anakataa kutoa kauli ya bure kabisa ambayo ingawa haina maana kwetu lakini ingeweza ikatumiwa na wasuluhishi kutubana Tanzania. Hataki kuisema. Pili, maneno yake ni ya vitisho tu. "Watanzania hawa wakiendelea na mambo yao (na mambo yetu yenyewe ni ya kumtoa katika maeneo yetu aliyeyachukua), sisi tutatekeleza mpango wetu wa pili wa kuivamia Tanzania. Na safari hii tutawapiga sana; tutawapiga mpaka mbali sana." Hayo ndiyo maneno anayosema.

Kwa hiyo basi, ingawa tumewatoa, vijana wetu wamekwisha watoa maadui kutoka katika maeneo hayo, nasema bado matatizo yetu yako pale pale. Kwanza kwa sababu ndogo zile mbili: bado viko vikundi vidogo vinawasumbua- sumbua vijana wetu, na vile vile viko vikundi vidogo vidogo vinavyoingia kutoka Uganda kuja kutusumbua. Lakini kubwa linalosababisha niseme mgogoro wetu uko pale zaidi pale ni kwamba sababu ya kuanzisha ugomvi huu haijaondoka: iko pale pale. Mtu huyu nia yake inaelekea ni ile ile. Hivyo ndivyo nilivyoeleza tarehe 9 mwezi Desemba.

Sasa ninaweza nikasema sasa hivi kwa kweli katika haya niliyoyaeleza hali haijabadilika, iko vile vile, isipokuwa katika madogo tu. Katika madogo ni kwamba vikundi vile tulivyoamini vilikuwa ndani ya eneo letu sasa havimo tena. Vijana wetu baada ya kujiimarisha vizuri, wenyewe wanasema walifagia eneo zima: wakafagia kabisa, na sasa hamna tena. Pili, hawa wanaotumwa kujaribu kuingiaingia ndani ya sehemu zetu ingawa hawajaacha lakini kuingia kwao sasa si jambo rahisi tena: wanapata taabu kidogo. Wanajaribu, mimi sisemi wanaacha kujaribu; wanajaribu kuingia. Lakini kila wanapojaribu kuingia wanapata matatizo zaidi. Kwa hiyo hali imebadilika kwa maana hiyo. Yale matatizo yetu niliyosema kuwa ni madogo, sasa yamekwisha. Kubwa bado liko pale pale, na linatutia wasiwasi ule ule.

Karibuni hapa mtakumbuka jirani yetu alianza tena. Mtakumbuka alivyoanza mwezi wa Oktoba. Mwezi Oktoba alianza kwa kusema, "Watanzania wameingia Uganda; wameingiza batalioni nzima: imepiga watu, imechoma majumba!" Wakati huo mimi nilikuwa Songea, nikayasikia maneno hayo na nikayapuuzilia mbali: nikasema mtu mwongo huyu jamani! Lakini kumbe mwenzetu anayo sababu ya kuongopa namna hiyo. Tangu nimesema nanyi tena, ameendelea na uwongo huo, "Watanzania wameingia ndani." Wakati mmoja alianza kwa sauti kubwa sana: "Watanzania wameingia ndani, wanatupiga; wameingia kilometa thelathini." Sisi tunajua ni uwongo! Hata waongo wengine wakaanza kumsaidia nao, "Naam, Watanzania wako ndani, wengine tumewaona kwa vyombo hivi vinavyoruka vya angani!" Sasa kama mmewaona jamani ya nini tubishane watu wazima! Tubishane kwa nini watu wazima kwa maana vyombo hivi vinapiga picha! Vyombo hivi havina ubishi. Mmepiga picha mnawaona askari wale, na mnajua; sijui mnawajuaje askari wa Tanzania tofauti yao nini na askari wa Uganda! Lakini kama mnaweza kupiga picha namna ile basi wapigeni picha, halafu mseme, "Mnaona askari wa Tanzania hawa." Ingawa Tanzania wanakataa, askari wao ni hawa! Hamwoni wanavyofanana Kitanzania?"

Lakini hakuna, ni uwongo mtupu! Hatuna askari. Hakuna askari wetu Uganda, hata kidogo; tunajua anaongopa. Na mwongo huyu kila akiongopa ana jambo ama ana matatizo ya ndani makubwa anayatafutia dirisha, ama anapanga vurugu. Tukatulia.

Halafu tukaona anaazma kuleta askari mpakani. Sasa nchi mbili mnapokuwa katika hali ya vita, kuleta askari mpakani ni hali ya mgogoro. Sisi tumepeleka askari mpakani na Amin anayo haki ya kuleta askari mpakani. Anayo haki: kwa nini asilete askari na hali tuko katika hali ya vita? Sisi tunapeleka askari mpakani, naye lazima ataleta askari mpakani. Ulikuwapo wakati tulipokubaliana tuwatoe askari mpakani; sisi tukawatoa, na yeye akawatoa. Halafu baadaye yeye akaleta askari wake. Lakini katika hali hii, hali ya vita, sisi tumekuwa tukipeleka askari mpakani, na yeye anawaleta askari wake. Lakini mwenzetu anawaleta na vitisho!

Sisi tunaweza tukawaza na kuamua kwamba tumekwisha peleka askari mpakani, na kwamba sababu ya kuwapeleka mpakani inajulikana. Ilikuwa ni ya kumtoa mtu huyu, aliyekuwa ndani ya ardhi yetu. Kitendo hiki kimemalizika, tumemtoa. Sasa na yeye analeta askari mpakani. Anaweza kuleta askari wake kwa sababu mbili.

Moja, anaweza kuwa anatuwazia sisi kwamba tutamshambulia. Akawaza kwamba hawa baada ya kuwatoa askari wetu katika ardhi yao, hatua yao ya pili itakuwa kutushambulia sisi Uganda. Kwa hiyo tukae vizuri vizuri mpakani tukiwasubiri. Ana haki kabisa ya kufanya hivyo. Ingawa kafanya madhambi, sasa afanyeje? Huwezi ukafanya madhambi, halafu uache mlango wazi. Unaweza ukafanya madhambi, na bado ukafunga mlango. Na hasa kwa sababu umefanya madhambi, si jambo la ajabu kufunga mlango? Kwa hiyo Amin anaweza akaleta askari wake kwa sababu hiyo. Upande mmoja ni halali. Hawa Watanzania tumewafanyia madhambi, sasa wanakuja. Wamekwisha jiandaa; watu wetu wamekwisha watoa, watakalia hapo hapo? Huenda wakavuka mpaka. Kwa hiyo anaweza akajiandaa kwa sababu hiyo ya kujihami endapo Watanzania watavuka mpaka.

Au inaweza kuwa ni sababu ya kutuvamia tena mara ya pili. Na wanaweza kutuvamia mara ya pili kwa sababu mbili. Sababu ya kwanza ni hiyo hiyo ya kujilinda. Wakafikiria Bwana wee, hawa Watanzania wanajiandaa. Safari ile tuliwavamia wamelala usingizi, sasa wanazidi kujiandaa, tukisubiri wakamilishe maandalizi yao, tunaweza tukapata taabu. Kwa hiyo tuwawahi." Amin anaweza akaamua kufanya hivyo: kuwawahi watu wetu. Lakini bado sababu yake itakuwa ni ya kujilinda.

Sababu ya pili inaweza kuwa anajiandaa kutuvamia hasa mara ya pili, huo anaoueleza kuwa "Mpango wake wa pili". Anaweza kuwa hasa anajiandaa, akasema, "Watanzania hawa ngoja tu, ngoja safari hii." Sasa wanakuja wanadhani safari hii watatushinda, ngoja tujitengeneze vizuri." Anaweza kuwa anajitengeneza vizuri kwa sababu hiyo.

Sasa Watanzania ni hiyari yetu sisi kuamua, huyu analeta askari wake mpakani kwa kujilinda tu, kwa hofu ya kwamba tutamvamia? Maana kama hivyo ndivyo tunaweza tukampuuza, kwa sababu hatuna nia sisi kumvamia jirani yetu Uganda. Tunaivamia Uganda ya nini? Tusiivamie siku zote hizi, tunakwenda kuivamia leo! Kwa hivyo tunaweza tukaamua hivyo. Lakini si rahisi Tanzania kuamua hivyo, kwa sababu mtu huyu mliwahi kumpuuza safari moja. Mliona analeta watu mpakani, akasema, "Watanzania hawa wamenivamia." Huku na huku anasema, analeta askari wake.

Lakini si rahisi Tanzania kuamua hivyo, kwa sababu mtu huyu mliwahi kumpuuza safari moja. Mliona analeta watu mpakani, akasema, "Watanzania hawa wamenivamia." Huku analeta askari wake na huku anasema, "Watanzania hawa wamenivamia." Na ninyi mmesema, "Mjinga huyu bwana, si anasema tunamvamia. Atagundua kwamba hatumvamii, halafu hafanyi kitu." Akagundua kwamba hatumvamii. Akafanya kitu.

Sasa Watanzania mnaweza kuamua kufanya kosa la pili hilo. Mnaweza tena mkamwona hivi hivi analeta askari wake mpakani. Anawaleta, anawajaza, anawaongoza, anawafundisha. Anawaambia raia, "Ondokeni hapa, ondokeni hapa, Watanzania washenzi sana hawa, watavamia." Mnaona raia wanatoka na yeye analeta askari wake, vikosi vyake hivi anavizidishia nguvu. Na ninyi mnaendelea kusema, "Mwenda wazimu huyu. Huyu anadhani tutamvamia bwana, si atagundua, zitapita wiki tatu, wiki nne, wiki tano ataona hatumvamii halafu basi tena ataondoa watu wake." Mnaweza mkaamua kufanya hivyo. Lakini alikwisha fanya hivyo. Alikwisha leta watu wake mpakani namna hiyo hiyo, mkapuuza, mkasema. "Anadhani tunamvamia. Anasema tuna watu wa Obote, mwongo mkubwa; anasema watu wetu wamemvamia, mwongo mkubwa. Hayo ni matatizo yake ya kelele za ndani, yapuuzeni kabisa." Mkampuuza, halafu akavamia. Sasa mnaweza kuamua mara ya pili tena; mkampuuza halafu akafanya hivyo.

Kwa hiyo, nasema kwamba, tangu nimesema na ninyi mara ya mwisho ameongeza tena askari wake. Na anafanya vitendo vyote viwili: analeta askari wake mpakani, na anasema. Anapeleka mabarua kwa Umoja wa Mataifa anatusingizia kwamba tumevuka mpaka. "Tanzania wamevuka mpaka, ngoja watanitambua!" Na anaandaa watu wake. Na kauli ni ile ile, inafanana na ile ile ya Oktoba. "Tanzania wamevuka," analeta watu wake. Na tukajua mwisho wake alituvamia.

Kwa hiyo safari hii niliwaambia vijana mpakani, niliwapa ruhusa vijana mpakani, nikasema, "Vijana, mtakapokwisha kuona kwamba analeta askari, kweli analeta askari wake wengi, na kauli yake haiondoki, inabaki ile ile, dalili hizi zinafanana sana na zile zile za mwezi Oktoba, safari hii vukeni mpaka."

Kwa hiyo mwisho wa juma la tatu la mwezi uliopita, na jambo hili nalieleza mwenyewe makusudi kabisa, niliwaruhusu vijana wavuke mpaka, wasiwapige kwa mizinga tu hivi. Niliwaruhusu vijana wavuke mpaka, kumwambia Amin kwamba hatuwezi kuendelea kupuuza kauli yake hata kama anaongopa, maana hatujui. Sasa si rahisi kwetu kujua lini anaongopa na lini ananuia kutekeleza anayosema; vigumu sana sisi kujua. Akitaka tumwamini, asitende wala asiseme kitendo kinachoelekea kututisha. Akitenda, au akisema, na yote mawili haya yakalingana, maneno na vitendo vinaonekana kweli nia yake ni kutufanyia hasara, msimpuuze. Vukeni mpaka, mpigieni kwa ndani

Haya nayasema makusudi kabisa, nasema makusudi kabisa, hasa haya nitakayoyasema ya mwisho haya.

Tunataka watuamini marafiki zetu, na adui yetu Amin. Sisi hatuna maadui wengi, na hao wako Kusini; Amin kaja kujiletea mwenyewe. Tunataka tuaminike. Tukisema hatukusudii kuvuka mpaka, dunia ikubali, iseme, "Kauli hii ni ya Watanzania, wakisema hawavuki mpaka basi hawavuki mpaka. Tunasema vile vile, tukipewa sababu ya kuvuka mpaka tutavuka, tuaminiwe vile vile, kwamba tutavuka.

Sasa nataka kusema hivi. Nataka kusema mawili. Moja. Hatudai sehemu yo yote ya Uganda, hata robo nchi ya Uganda, hata kidogo. Hatuna madai kwa Uganda. Nchi ya jirani tumekaa vizuri sana na Uganda na Tanzania na Kenya. Tulikuwa mfano mmoja mzuri katika Afrika. Na katika dunia nzima ilikuwa hakuna mfano wa nchi tatu ambazo zimekaribiana na kushirikiana kiasi hicho; ilikuwa hakuna. Na kusema kweli mtu anaweza kusema chanzo cha kutuvurugia Afrika Mashariki ni balaa hili kwa Uganda. Kama si yeye pengine Afrika Mashariki ingekuwa bado vile vile kama ilivyokuwa zamani; isingevurugika.

Uganda ni jirani yetu, Kenya ni jirani yetu. Tumekaa vizuri pamoja, na bado tunayo nia ya kukaa pamoja, hata kama hatukurudia hali ile ile ya zamani. Lakini nchi za Afrika Mashariki raia wake wanajuana sana, viongozi wake wanajuana sana, tulikuwa ni kama nchi moja. Hatuna ugomvi na Uganda, hatuna madai na Uganda; tuna huruma tu na Uganda. Kwa hiyo nasema la kwanza ni hilo. Kwa hiyo ninaposema hatuna sababu ya kuvusha majeshi yetu kwenda Uganda tunasema hivyo, tuvushe majeshi yetu kwenda Uganda kwenda kutafuta nini? Kwa sababu hatuna madai na Uganda.

La pili ninalotaka kulisema ni kwamba wananchi wa Uganda wana sababu zao nzuri za kumchukia Amin. Amechinja sana watu wake; amewaua sana. Na mimi bado narudia yale yale kwamba, mimi sikubali kweli kwamba Wafaransa wakiwa na Serikali mbaya ya Wafaransa wenzao, wana haki ya kuing'oa; Waingereza wakiwa na Serikali mbaya ya Waingereza wenzao, wana haki ya kuing'oa; Warusi wakiwa na Serikali mbaya ya Warusi wenzao, wana haki ya kuing'oa; Waajemi wakiwa na Serikali mbaya ya Waajemi wenzao, wana haki ya kuing'oa; lakini Waafrika hapana. Waafrika wao wakiwa na Serikali mbaya ya Wafrika wenzao, ni mwiko kuing'oa: maana ni ya Waafrika wenzao. Mimi filosofia hii ya serikali siielewi hata kidogo; sijui msingi wake. Serikali inayoua inaua tu, huwezi kuisamehe kwa sababu ya rangi ya mwuaji. Serikali kidhalimu ni ya ya kidhalimu tu, watu wanaweza wakaogopa, wasifanye kitu; wanaweza wakashindwa kuamua kufanya kitendo juu ya serikali hiyo. Wanaweza wakaogopa, ingawa wanakufa. Unaweza ukawauliza, "Mbona hamfanyi kitu?" Wakasema, "Bwana, tutaanzia wapi: tunachinjwa: Hata ukinong'ona tu, unachinjwa." Wanaweza wakasema hivyo. Wanaweza wakaacha kutenda kitendo kwa sababu ya hofu kwamba hawana pa kuanzia.

Wananchi wa Uganda wamechinjwa ; wamechinjwa sana. Wanaweza wakaamua kukaa na serikali hiyo, maana hawana la kufanya. Na mimi pia sina la kufanya. Wakiamua kukaa naye, wakae naye; si juu yangu mimi kwenda kumtoa Amin, na kusema Watanzania wamekuja kuwasaidieni kumtoa Amin, ili Wananchi wa Uganda sasa mkae katika hali ya amani. Hata kidogo. Hiyo ni kazi yao Wananchi wa Uganda. Lakini Wananchi wa Uganda wakiamua kumtoa Amin, si kazi yangu mimi kwenda kumtetea. Siwatetei wengine, itakuwa Amin! Watu watashangaa kweli, wakisikia Mwalimu anapeleka majeshi Uganda kwenda kumlinda Amin. Watashangaa kweli.

Majeshi ya Tanzania, nasema, hayana sababu ya Kitanzania ya kuingia Uganda, maana hatuna madai Uganda; hatuna hata kidogo. Wananchi wa Uganda hata kama wana sababu wao ya kumtoa Amin, si sababu yetu.

Si yetu; si kazi yetu. Hatuingizi majeshi yetu sisi ndani ya Uganda kwenda kumtoa Amin; si kazi yetu sisi. Maana kama ingekuwa hivyo, tulikuwa tunangoja nini miaka yote minane hii? Na uwezo wa kumng'oa tunao. Ni kazi ya Wananchi wa Uganda wenyewe. Naweza nikawaombea dua wananchi wa Uganda hawa "Yarabi, huwezi ukawasadia?" Lakini sala tupu; sipeleki jeshi la Tanzania ndani ya Uganda kumng'oa Amin. Kwa hiyo hayo nayo nataka tuaminike; nataka na Amin atuamini.

Mwenyewe amekuwa anapiga kelele, "Mwalimu Nyerere anamweka Obote huko; yeye anataka kuning'oa mimi, na kumleta Obote." Nilikuwa ninangoja nini miaka yote hii? Si kweli hata kidogo. Nataka Amin aniamini hivyo. Mwenyewe amekataa kuniamini; lakini hilo ni shauri lake.

Lakini tunasema, lazima aache vitisho vyake. Mambo mawili aache. Aache madai yake ya mwanzo kabisa. Madai haya aliyaanza mapema, mara aliposhika madaraka ya Uganda, mwanzo kabisa mwaka 1971, akasema, "Nadai sehemu ya Kaskazini ya Kagera". Ana wazimu yule. Sasa matumaini yangu ni kwamba wazimu huo umemtoka, hana tena. Lakini nimeomba aseme kwamba hana tena. Hajasema. Na madhali hajasema nitaamini kwamba bado haja hiyo anayo. Nimeombwa na watu wakubwa kabisa, watu waliokuwa wana nia ya suluhu, wamwambie aseme kwamba hadai sehemu ile ya Tanzania. Hajasema. Mimi, lazima niamini kwamba Amin bado anaitaka sehemu hii, anaona kosa sasa tumemharibia mpango wake tu. Akipata nafasi atapanga upya. Jambo la pili ambalo lazima aache ni kutusingizia. Kila akipata matatizo ndani ya nchi yake, askari wake mle wanapigana wenyewe kwa wenyewe, anachinja chinja watu, husingizia kuwa Tanzania inafanya migogoro. Si kweli hata kidogo. Na, ili ajaribu kuufanya ulimwengu uamini kwamba Tanzania inafanya ukorofi, basi atafanya kitendo cha uchokozi kwa Tanzania kusudi Tanzania tufanye tendo halafu aseme ni Tanzania.

Kama safari iliyopita, amefanya mambo ya ajabu sana. Ameua askari wake wengi, amewaleta wamebebwa maiti, wamekuja kutupwa ndani ya Tanzania! Tutakumbuka vijana wetu baada ya kuvuka mpaka walikwenda wakagundua maiti nyingi katika kilima kimoja. Vijana wetu wakasema wazi wazi, hawaongopi vijana wetu, hawataki kuongopa. Wakasema, "Ziko maiti ambazo tunadhani zimetokana na vipigo vyetu, mapigo yetu sisi; lakini maiti hizi hazikutokana na mapigo yetu hata kidogo. Hizi maiti zimeletwa tu, zimepachikwa hapa. Aliwaua mwenyewe, askari wake, halafu akaja kuwaficha Tanzania, ili aseme wameuawa na Tanzania." Na vijana wetu hawasemi uwongo. Hawakudai safari ile kwamba tumewaua. Wangeweza kudai; watu wengine huongopa, wanadhani uwongo unasaidia katika vita. Wangeongopa tu. Lakini vijana wetu hawafanyi hivyo.

Hata safari nyingine mtakumbuka, mtakumbuka kwamba, yalitokea tena mapigano. Sijui kama haya niliyaeleza au sikuyaeleza. Yalitokea tena mapigano. Ikaja ndege kutoka Uganda, ikaingia katika eneo letu. Halafu vijana wetu, ingawa walikuwa wameitupia risasi, baadaye wakaona inaanguka Uganda. Wakasema wenyewe, vijana wetu, ingawa ndege ile tumeona inaanguka, hatudhani kwamba ni sisi tulioipiga. Wangeweza wakadai, vijana, hawa madhali imeanguka, risasi wameitupia, na kuanguka imeanguka, wangeweza vijana hawa wakadai kuwa wameiangusha. Wakasema, "Tumeitupia risasi sisi tumeipiga." Hawakusema hivyo. Walisema, "Tumeitupia risasi, lakini hatudhani kama tumeiangusha sisi, Lakini imeanguka." Hawaongopi vijana hawa.

Sasa huyu mtu anapokuwa na matatizo ndani ya nchi yake mwenyewe, anaweza akatafuta sababu ya uchokozi kwetu sisi, ili hayo madhara yake yatakapotokea, idhaniwe kwamba wakorofi ni Tanzania. Na hila hizo alifanya tangu zamani. Hata mwaka 1972 alifanya hivyo. Alikwenda Mutukula, akaua askari wake wengi sana ndani ya jela. Halafu akazua uwongo, kwamba Tanzania imempiga vita, kusudi aweze kueleza hawa wafu wametoka wapi. Akasema hivyo. Sasa hivi anayo matatizo, na matatizo yake haya. yanapanda kama homa. Hivi sasa "temperature" yake iko juu sana ndani ya Uganda. Juzi juzi kulikuwa na mapigano mjini Kampala, na uko ushahidi kwamba matatizo yake hayo yanaongezeka; "temperature" yake inapanda.

Haya ninayosema sasa hivi nayasema makusudi kabisa. Asije tena akajaribu kutafuta njia ya kuepukana na matatizo yake haya kwa kutuletea sisi matatizo. Tutafanya vile vile. Tutampiga sana ndani ya Uganda. Haya maonyo nayatoa makusudi, nayatoa katika hadhara makusudi kabisa ili Amin ajue hivyo, na marafiki zetu wajue hivyo, kwamba hatuna sababu ya kwenda ndani ya Uganda isipokuwa kwa kulinda ardhi yetu wenyewe.

Na jamaa huyu amekwisha kufanya vitendo vya kutusumbua. Siwezi kumpuuza tena. Tumempuuza miaka minane. Tumempuuza mpaka juzi juzi, hapo mwezi wa Oktoba bado tukampuuza; halafu akatufanyia hasara kubwa sana. Akiendelea na namna ile ile, hatutampuuza tena. Na sasa anayo matatizo haya ya ndani, kelele zake bado ni zile zile. Tutaomba tu kwamba vitendo vyake hivi vinavyofuata tangu sasa, visije vikafanana na matisho yake aliyotutisha mwezi wa Oktoba. Vikifanana na matisho yake ya Mwezi Oktoba tunayo sababu nzuri sana ya kusema, "Mshenzi huyu anataka tena kufanya ukorofi wa mwezi Oktoba." Tutampiga.

Asanteni sana.

Itaendelea. . .
 
Back
Top Bottom