Kwenu,
Katika muda wote ambao nchi inaomboleza kimya kimya kifo cha mwanafunzi wa NIT, Akwilina, Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako ameonekana kuwa mstari wa mbele katika kufariji, kuhakikisha maziko yanafanyika kama Serikali ilivyoahidi na kuhimiza uchunguzi unaharakishwe ili muuaji afikishwe mbele ya sheria.Sijamsikia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Mwigulu.
Inatia uchungu na kusikitisha binti mdogo kuuawa bila hatia. Mauaji kabla, wakati na baada ya chaguzi ndogo ni kitu kilichozoeleka. Imezoeleka si kwa kuwa ni kawaida, la hasha, ni kwa sababu dola haijawahi kuhangaika kutafuta au kushughulikia muuaji/wauaji.
Ni jambo la kusikitisha pia, kwamba mauaji haya huwalenga viongozi na wanachama wa CHADEMA. Baada ya mauaji ya Akwilina, polisi walitangaza kumsaka Mwenyekiti wa CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe ingawa hakuwa amejificha. Polisi pamoja na mashabiki wengi wa CCM wanamnyooshea kidole Mh. Mbowe kama mhusika mkuu ingawa hakufyatua risasi. Ni sahihi kufyatua risasi za moto kwa kulenga ili kutawanya waandamanaji?
Inaelekea kuna mtu alilengwa lakini risasi haikumpata. Ingempata kusingekuwa na kauli za kukanganya toka kwa polisi. Kufyatua risasi kwa kulenga raia hakuna maana ya kutawanya, kuna makusudi ya kuua. Ukikusudia kuua unashindwaje kumjua muuaji?
Waliomuua Alfonce Mawazo,waliowachinja viongozi wa CDM Kata ya Usa River Arumeru Mashariki wakati wa uchaguzi mdogo,waliomteka kisha kumuua katibu wa CHADEMA kata ya Hananasif Kinondoni ni watu wa aina moja na lengo moja, kupata faida za kisiasa kwa gharama ya uhai wa watu wengine(ambao hawastahili kupewa uongozi japo wa kata).
Kugharamia mazishi kwa milioni 80 kwa mtu aliyeuwawa kwenye maandamano(ingawa alikuwa mpita njia)ni huruma ya ajabu sana ambayo haijapata kutokea. Serikali itawajibu nini ndugu wa raia watakaodai gharama za mazishi kwa kuuawa wapendwa wao katika mazingira yaleyale ya Akwilina?
Ni vema kufanya uchunguzi na kuwabaini wauaji wote waliohusika kwenye mauaji kabla, wakati na baada ya chaguzi ndogo/chaguzi za marudio. Kila mtu ana haki ya kuishi, hata kama humpendi.
RIP Akwilina.