Karibu kambi mbili za wanajeshi wa Marekani nchini Iraq zimeshambuliwa kwa makombora kadhaa, kwa mujibu wa idara ya ulinzi ya Marekani.
Runinga ya kitaifa ya Iran imetangaza kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi mauaji ya kamanda mkuu Qasem Soleimani aliyeuawa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani mjini Baghdad, kufuatia agizo la rais wa Marekani Donald Trump.
Pentagon inasema kuwa karibu kambi mbili zilishambuliwa, mjini Irbil na Al Asad.
Bado haijafahamika kama kuna majeruhi wowote kutokana na shambulio hilo.
"Tunafahamu ripoti ya mashambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq. Rais amefahamishwa kuhusu tukio hilo na anafuatilia kwa karibu hali ikoje katika eneo hilo ili kushauriana na kamati ya kitaifa ya usalama," Taarifa ya msemaji wa ikulu ya White House, Stephanie Grisham.
Jeshi la ulinzi la Iran Revolutionary Guard limesema kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi kifo cha Soleimani cha Ijumaa iliyopita .
"Tunaonya washirika wote wa Marekani,ambao wameruhusu vikosi vya Marekani kuwa katika ardhi yao, kwamba wakijaribu uchokozi wa aina yoyote dhidi ya Iran yatalengwa," ilisema kupitia taarifa yake iliyotolewa shirika la habari la Iran, IRNA news agency.
Mashambulio hiyo yalifanyika saa kadha baada ya mazishi ya Soleimani.
Shambulio la pili lilifanyika katika mji wa Irbil muda mfupi baada ya roketi ya kwanza kugonga Al-Asad, kituo cha televisheni cha Al Mayadeen kiliripoti.