Asili ya wanadamu kwa mujibu wa vibao vya kale vya Sumeria.
Sumeria, au ardhi ya ’wafalme waliostaarabika’ ilistawi huko Mesopotamia, kwa sasa panaitwa Iraq, kwenye miaka 4500BC. Wasumeria walifanikiwa kutengeneza himaya za kiutawala zenye mifumo yao wenyewe ya ujenzi , sanaa, unajimu wa nyota na hisabati. Mfumo wao wa kidini ulikuwa mtambuka sana na ulihusisha mamia ya miungu. Kwa mujibu wa maandiko ya kale, kila mji wa Sumeria ulilindwa na mungu wake; na japo binadamu waliishi sambamba na miungu, binadamu walikuwa ni watumishi wa miungu.
Hadithi ya uumbaji kutoka kwa waSumeria inapatikana katika kibao cha udongo kilichovumbuliwa huko Nippur, katika Mesopotamianya kale, mji ulioundwa takriban miaka 5000 kabla ya kuzaliwa kristu.
Uumbaji wa Dunia (Enuma Elish) kwa maelezo ya vibao vya Sumeria ulikuwa hivi:
“Wakati katika anga za juu mbingu haikuwa na jina,
Na ambapo dunia chini yake haikuwa na jina, Na ambapo Apsu wa kale, aliezifanya kuwa,
Na vurugu, Tiamut, mama wa wote wawili
Maji yao yalikorogwa pamoja,
Na hakuna ardhi iliyotengenezwa, hakuna kinamasi kilichoundwa; kipindi ambacho katika miungu, hakuna aliyeitwa kuwa, Na hakuna kati yao aliekuwa na jina, na hakuna hatma zilizokuwa zimekwisha kugawiwa; Basi hapo wakaumbwa ‘miungu’ katikati ya mbingu, Lahmu na Lahamu wakaitwa kuwa...”
Hadithi za waSumeria zinadai kwamba, hapo mwanzo, ‘Miungu’ wenye mfanano na binadamu walitawala Dunia. Walipokuja Duniani, kulikuwa na kazi nyingi sana za kufanya, na waliifanyia kazi ardhi, waliichimba kuifanya iwe sehemu inayoweza kubeba uhai huku wakichimba madini yake .
Maandiko hayo yanasema kwamba, baada ya muda ‘Miungu’ hao walifanya mgomo kutokana na kazi hiyo kuwa ngumu sana.
Miungu hao walipoifanya kazi hiyo ngumu
Waliona ni mateso makali sana, maumivu ya uvujaji jasho wao ulikuwa mkubwa sana
Kazi ilikuwa nzito, mateso yalikuwa makali.
ANU, mungu wa miungu, alikiri kwamba kweli kazi hiyo ilikuwa ni nzito sana. Mtoto wake wa kiume ENKI, akatoa wazo kwamba aumbwe binadamu ili abebe mzigo huo mzito wa kuvuja jasho na kufanya kazi hiyo nzito, na hivyo basi, kwa msaada wa dada yake nusu aitwae NINKI, wakafanya ikawa .
mungu mmoja wapo akauwawa, na mwili wake na damu yake vikachanganywa na udongo wa mfinyanzi. Na kutokana na mchanganyiko huo binadamu wa kwanza akaumbwa, kwa mfano wa miungu hao.
“Mmemuua mmoja wa miungu pamoja na haiba yake
Hivyo basi nimewaondolea mateso ya kazi yenu nzito
Kazi hiyo nzito nimeihamishia Kwa binadamu.
...”
Katika udongo (mfinyanzi), mungu na bindamu wataunganishwa,
Kwa umoja utakaoletwa pamoja;
Ili katika siku za mwisho
Mwili na roho
Ambavyo katika mungu vimeiva –
Kiasi roho katika udugu wa damu viunganishwe.
Binadamu wa kwanza aliumbwa ‘Eden’, Eden ni neno la kiSumeria linalomaanisha ardhi isiyo na mabonde. Katika maandiko ya Gilgamesh, Eden ipo Mesopotamia kati ya mito ya Tigris na Euphrates.
Hapo chini, ni moja wapo ya vibao vya Sumeria, vikimuonyesha ENKI katika hadithi ya uumbaji
View attachment 2247194
Hapo awali binadamu hawakuweza kuzaliana wenyewe, ila baadae walifanyiwa maboresho kwa msaada wa Enki na Ninki.
Hivyo, Adapa akaumbwa kama binadamu kamili anayejitegemea na aliyejitosheleza katika ukamilifu wake. Maboresho haya yalifanyika bila ruhusa ya kaka yake ENKI, aliyeitwa ENLIL, na ugomvi mkubwa baina ya miungu ukaanza. ENLIL akawa adui mkubwa wa binadamu, na kibao hicho cha Sumeria kinasema kwamba binadamu waliwatumikia miungu na walipitia nyakati ngumu na mateso makali sana katika utumishi wao kwa miungu.
Adapa, kwa msaada wa ENKI, alipalizwa hadi juu kwa Anu ambapo alishindwa kujibu swali kuhusu ‘mkate na maji ya uzima’.
Hadithi za waSumeria
Uumbaji wa wanadamu
Shairi hili linaanza kwa kuelezea jinsi ilivyowabidi miungu kufanya kazi kwa ajili ya mkate wao wa kila siku kwa kuchimba mifereji mikubwa ya umwagiliaji:
Miungu walikuwa wakichimba mito na kuweka mchanga pembeni
na miungu waliokuwa wanachimba mfinyanzi wakaanza kulalamika.
Nammu, ambae ni mungu wa bahari na mito, akaenda kwa mtoto wake aitwae ENKI, ambae alikuwa amelala na akamuamsha kutoka usingizini na kumuamrisha kwa kusema "waumbe watumishi wa miungu". Enki, ambae ndiye mungu wa hekima, akawaza kuhusu nguvu ya urutubishaji ya mfinyanzi na maji ya kinamasi, kisha akamwambia Nammu awaamrishe miungu wa ‘tumbo la uzazi’ waufinye huu mfinyanzi na kisha wafinyanzi waufanye uwe mzito ili aweze kuufinyanga na kuzaa.
“Changanya moyo wa mfinyanzi uliopo kwenye kinamasi,
Kisha wafinyanzi wataufanya uwe mzito,
Wewe, [Nammu] fanya mikono na miguu iwe;
Ninmah [mama wa dunia au mungu wa uzazi] atafanya kazi juu yako, mungu wa uzazi atakuwa pembeni yako wakati wa uumbaji wa kijusi; O mama yangu, toa hatma yake (kijusi tumboni),
Ninmah atahuisha sura ya uso wa miungu kwenye kijusi hicho,
ni mwanaume . . . .
Hivyo mwanadamu aliumbwa ili kuwapunguzia miungu mzigo wa kazi nzito na ngumu.
Miungu wakaamua kufanya karamu kubwa sana ili kusheherekea uumbaji huu mpya wa binadamu ambao wangebeba mzigo wa kazi zao, Kisha Enki na Ninmah wakaanza kunywa bia / pombe na kisha ‘wakaanza kujisikia vizuri ndani yao’
Ninmah akaanza kujisifia kwamba yeye, akiwa kama mungu wa uzazi na tumbo la uzazi, ndiye anaeamua kama uumbaji wa kijusi tumboni uende vizuri au uende mrama. Enki akajibu kwamba yeye, akiwa kama mungu wa hekima na mwerevu, anaweza akamtafutia nafasi ya utumishi katika jamii hata kwa wale watakaozaliwa na vilema vya aina mbalimbali. Ninmah akaumba kutoka katika udongo mwanaume mwenye mikono inayotetemeka, lakini Enki akampa kazi ya utumishi wa mfalme. Baada ya hapo Ninmah akaumba mwanaume kipofu, lakini ENKI akamfanya mwimbaji wa hadithi. NINMAH akaamuma kuumba mwanaume mwenye miguu iliyopinda, lakini ENKI akamfanya kuwa mtumishi wa wafua vyuma. NINMAH akaendelea kuumba binadamu wenye vilema: "akaumba mtu asiyeweza kuzuia mkoja wake, akaumba mwanamke tasa, akamumba binadamu asiyekua na jinsia ya kiume wa ya kike, na vilema vingine vya aina mbali mbali, lakini mara zote hizo ENKI aliweza kumtafutia kilema huyo nafasi katika jamii na kiweza kuendesha maisha yake". Mwanamke ambae hakuweza kuzaa kwa mfano, alipewa nafasi ya kuwasimamia wasusi katika nyumba ya malkia,
, na yule mtu aliyezaliwa bila jinsia alipewa nafasi ya kusimama pembeni ya mfalme.
NINMAH baada ya kuona amezidiwa ujanja na ENKI, akautupa chini ule
Mfinyanzi wa uumbaji kwa hasira. Sasa ENKI akaamua yeye kuumba binadamu mwenye kilema, na akamzodoa NINMAH ajaribu kama ataweza kuamua aina ya kilema atakachozaliwa nacho mtu huyo. Sasa ENKI, katika namna ambayo haijaelezwa vizuri sana kwenye kibao hiki, akafanya mtu azaliwe njiti (kabla ya siku zake)" . Kiumbe kilichozaliwa kilikuwa na ulemavu wa hali ya juu sana : Mikono yake ilitetemeka, / hakuweza kuweka chakula mdomoni, / uti wake wa mgongo ulikuwa umepinda vibaya, / njia yake ya haja kubwa ilikuwa imeziba/ mifupa ya mapaja ilikuwa laini, / miguu na ngozi yake ilikuwa inavunjika vunjika / hakuweza kutembea kwenye kinamasi. NINMAH akajaribu kumlisha kipande cha mkate kiumbe huyo, lakini alikuwa dhaifu sana na hakuweza kula mkate aliopewa. Hakuweza kusimama, wala kukaa wala kukunja magoti yake. NINMAH alipata mshangao wa uwoga pamoja na huzuni kwa kile alichokiumba ENKI na akamlaani kwa kitendo hicho, maana NINMAH aliona kwamba endapo watu wenye vilema vikali aina hii watazaliwa mara kwa mara basi watu wataacha kumuabudu. ENKI akaamua kupooza hasira za ninmah kwa kukiri kwamba kiumbe kile chenye ulemavu hakikuwa kazi ya mikono ya NINMAH bali kazi ya mikono yake.
Shairi linaisha kwa wimbo wa kutukuza nguvu na uwezo wa uumbaji wa kiume wa ENKI pamoja na werevu wake, lakini hadithi yenyewe pia inajaribu kuonyesha kwamba ENKI haweza kufanya uumbaji bila msaada wa mungu wa uzazi NINMAH.
Pia hadithi inavuta zaidi umakini kwa kuanza na miungu wanaofanya kazi ngumu kwa ajili ya mkate wao wa kila siku, halafu inaisha kwa kiumbe kisichoweza kupewa mkate na mungu wa uzazi.
Sehemu ya chini ya kibao hiki kimekatika na hakuna anaejua kilichoandikwa kwenye kipande hicho cha chini, hivyo hadithi imebidi iishie hapa. Kwa anaetaka kukiona anaweza kutembele kwenye jumba la makumbusho huko Uingereza, unalipia kiingilio kidogo tu.
Tujiandae kwa hadithi ya kibao kingine kinachofauta, vibao vipo maelfu kwa maelfu.