View: https://www.youtube.com/watch?v=wxK-HnLPxTA&t=18s
Kundi la maafisa wa kijeshi wamesema wametwaa udhibiti wa Guinea-Bissau huku kukiwa na ripoti kwamba rais, Umaro Sissoco Embaló, amekamatwa.
Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embaló amekamatwa na watu wenye silaha siku chache tu baada ya uchaguzi wenye utata ambapo upinzani ulizuiliwa kushiriki.
Milio ya risasi ilisikika katika mji mkuu huku Embaló na mpinzani wake Fernando Dias wakidai ameshindi.
Vilevile, milio ya risasi imezuka karibu na makao makuu ya tume ya uchaguzi ya Guinea-Bissau Jumatano, siku moja kabla ya matokeo ya urais yenye mvutano yalitarajiwa kutangazwa.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi yenye historia ya mapinduzi ilifanya uchaguzi wa rais na wabunge Jumapili.
Kinyang'anyiro hicho kilimkutanisha Rais aliye madarakani Umaro Sissoco Embalo na mpinzani wake mkuu Fernando Dias, na pande zote mbili zinadai ushindi katika raundi ya kwanza mapema wiki hii.
Haikuwa wazi mara moja ni nani aliyehusika katika ufyatuaji risasi, ambao ulishuhudiwa na mwandishi wa habari wa Reuters na wakazi wengine wawili.
Msemaji wa Embalo, Antonio Yaya Seidy, aliambia Reuters kwamba watu wenye silaha wasiojulikana walishambulia tume ya uchaguzi ili kuzuia kutangazwa kwa matokeo ya kura.
Alisema watu hao walikuwa na uhusiano na Dias, bila kutoa ushahidi. Msemaji wa Dias hakujibu ombi la kutoa maoni.
Mmoja wa mashahidi alisema wakazi walikuwa wakikimbia kutoka eneo la tukio huku milio ya risasi ikiendelea karibu na jengo la tume ya uchaguzi.
Dereva mmoja huko Bissau ambaye aliomba asitajwe jina alisema pia kulikuwa na milio ya risasi katika wizara ya mambo ya ndani na ikulu ya rais.
Taifa hilo dogo la pwani kati ya Senegal na Guinea lilishuhudia angalau mapinduzi tisa kati ya 1974, lilipopata uhuru kutoka kwa Ureno, na 2020, wakati Embalo alipochukua madaraka.
Embalo anasema amenusurika majaribio mengine matatu ya mapinduzi tangu wakati huo, ingawa wapinzani wake wamemtuhumu kwa kutengeneza migogoro kama kisingizio cha ukandamizaji - madai ambayo anayapuuza.
Embalo alikuwa akitafuta kuwa rais wa kwanza katika miongo mitatu kushinda muhula wa pili mfululizo nchini Guinea-Bissau.
Uchaguzi huo ulikuwa wa kwanza kufanyika bila Chama kikuu cha upinzani PAIGC, chama kilichoongoza mapambano ya uhuru kutoka kwa Ureno katika miaka ya 1960 na 1970.
PAIGC ilizuiwa kuwasilisha wagombea baada ya mamlaka kusema iliwasilisha hati kwa kuchelewa.