CHIFU ALIYEZUNGUKA NA HOT POT SAFARINI
Alexander (Aliki) Bandekile Mwamakula (1914 - 1996), alizaliwa Kijiji cha Iponjola, Kajunjumele ambapo sasa huitwa Isyeto (Makaburi ya Chifu Mwamakula). Alikuwa mtoto wa pili wa kiume wa Malafyale (Chifu) Bandekile Mwamakula wa Itunge, Kyela. Mwaka 1940 alikwenda Kambofi (Zambia) kufanya kazi za ukarani katika migodi ya Shaba. Taarifa zinasema kuwa aliishi miji ya Kitwe, Ndola, Shesheke, Lusaka, nk.
Mwaka 1945, akiwa Kabofi (Zambian) alipata taarifa kuwa baba yake mzazi, Chifu Bandekile Mwamakula alikuwa amefariki dunia. Alirejea nchini kumuombolezea baba yake na akarudi tena Zambia. Taratibu zilitaka kuwa mdogo wa Chifu Bandekile aliyeitwa Chifu Lasili Mwaihojo Mwamakula wa Lugombo, Mwaya ndiye arithi na achukue wake wote wa kaka yake. Mtoto wa kwanza wa kiume wa Chifu Bandekil, aliyeitwa Andalwisye, alikataa mama yake kurithiwa, kwa hiyo, Chifu Lasili akachukua wote wa Bandekile akaenda nao Mwaya isipokuwa mke mkubwa wa Chifu Bandekile, aliyeitwa Basikile Lubanga.
Chifu Andalwisye alimjengea nyumba mama yake katika mji wa mumewe kule Itunge, Kululu ambapo aliishi pale hadi pale alipofariki dunia mwaka 1963. Ndipo Chifu Andalwisye akawa ni mrithi wa mahali pa baba yake hadi alipofariki dunia mwaka 1966. Wakati hayo yakijiri, Chifu Aliki alikuwa nchini Kambofi ila alirejea nchini kumuombolezea mama yake mwaka 1963.
Chifu Aliki, alirejea nchini mwaka 1970 kabla ya kustaafu baba ya kaka yake kufariki dunia. Kwa hiyo, ilikuwa lazima Chifu Aliki arejee kwa ajili ya kurithi mamlaka ya Chifu Bandekile. Wakati hayo yote yakijiri, Chifu Korosso Mwamakula ambaye ndiye alikuwa undagili (chifu mtawala) wa nNkirwa alikuwa hai. Na alisimamia vizuri sana utaratibu wa kupeana madaraka katika ile Nyumba ya Chifu Bandekile ambaye alikuwa ni baba mdogo wa Chifu Korosso Mwamakula.
Katika kipindi chote cha miaka 4 baada ya kifo cha Chifu Andalwisye, mamlaka ilikuwa chini ya Chifu Timoti Bandekile Mwamakula ambaye alikuwa mdogo wa Chifu Aliki. Lakini utaratibu haukuruhusu yeye kuendelea kukalia Kiti cha Chifu Bandekile wakati kaka yake yungali hai. Hii ndiyo sababu iliyomfanya Chifu Aliki arejee nchini mwaka 1970.
Waliomfahamu Chifu Aliki, wanamkumbuka kwa mambo yafuatayo: Alikuwa mtu mwenye utani mwingi, hakupenda watu wavivu ingawa hakuwa mchoyo kwa wavivu. Aliwapa chakula lakini baadaye ni lazima awaseme. Alikuwa ni mtu mtanashati sana. Mahali popote alipokuwa akisafiri alikwenda na 'hot pot' zake zikiwa na chakula. Alitembea na 'hot pot' zenye ngazi alizotoka nazo Zambia. Alipenda kun'gata ulimi wake kila akifanya kazi. Wanyakyusa huitwa ni 'ukuluma ing'asi'!
Chifu Aliki alikuwa baba yangu mkubwa. Baada ya yeye walizaliwa shangazi wawili na ndipo akazaliwa baba yangu Chifu Timoti Bandekile Mwamakula (1924 - 2014). Mamlaka ya Serikali ya Mtaa imetambua Nyumba ya Bandekile kwa kutoa jina la Barabara ya Timoti, aliyekuwa ni mmoja wa watoto wake.
Picha hii chini ilipigwa Kambofi (Zambia) kati ya mwaka 1964. Chifu Aliki alinipatia picha hii mwaka 1987 kama kumbukumbu na hii ndiyo picha pekee ambayo iliyobakia katika sehemu ya kumbukumbu muhimu. Mwaka 1987 ndio mwaka ambao niliishi na Chifu kwa mara ya mwisho. Nilipokwenda nyumbani kwa likizo ya masomo niliamua kutumia muda ule kuishi na yeye kupata historia zaidi ya ukoo. Hata hivyo, Chifu Aliki hakuwa anasimulia sana habari za ukoo wake zaidi kupenda sana kusimulia zile habari za Zambia na habari za mama yake.
Mwaka 1987, Chifu Elukaga (Mzaramo), mtoto wa mwisho wa Chifu Bandekile kwa mke wake mkubwa aliyeitwa Basikakile Lubanga alifariki dunia. Habari za Chifu Elukaga Mwamakula ambaye alikuwa ni afisa katika Jeshi la Polisi Hadi Mwanzoni mwa miaka ya 1960s tutakuja kusimulia baadaye kama Mungu atatupa kibari na neema ya kuendelea kuishi.
Simulizi hii inaweza kuwa na thamani ndogo kwa ukoo wa Chifu Mwamakula na matawi yake ingawa inaweza isiwavutie wasomaji wengine. Hata hivyo, yale tusiyoyapenda na kuyathamini yanaweza kuwa na manufaa zaidi kwetu kuliko yale tunayoyapenda. Prof. Janabi anasema kuwa nyama choma, ice cream hata perfume zinaweza ziwe na manufaa kidogo kwa afya zetu kuliko kisamvu na dagaa kauzu!
Je, nini kimekushangaza? Je, nini maoni yako?
Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!
Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula
Dar es Salaam, 10 Machi 2024; 7:00 mchana