Kwa nini deni la taifa linaendelea kuongezeka nchini Tanzania?
CHANZO CHA PICHA,IKULU TANZANIA
Maelezo ya picha,
Rais wa Tanzania Samia Suluhu akizungumza na waziri wa fedha wa taifa hilo wakiwa Makao Makuu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), jijini Washington DC.
Maelezo kuhusu taarifa
- Author,Damas Kanyabwoya
- Nafasi,Mchambuzi
- 13 Disemba 2022
Kuongezeka kwa deni la taifa kwa kiasi cha Shilingi 21 trilioni ndani ya miezi 6 kumezua tafrani na mijadala mikali kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari nchini Tanzania.
Taarifa ya uchumi ya mwezi Novemba 2022 iliyotolewa hivi karibuni na Benki Kuu ya Tanzania inaonyesha kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba 2022 deni la taifa lilikuwa limefikia Shilingi 90.35 trilioni.
Alipokuwa akisoma Bajeti ya Serikali mwezi Juni, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba alisema hadi mwezi Aprili 2022 deni la taifa lilikuwa limefikia Shilingi 69.4 trilioni.
Hii inaonyesha wazi kuwa deni la taifa limeongezeka kwa kiasi cha Shilingi 20.91 trilioni kati ya Mwezi Aprili na Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za miongo miwili iliyopita za taarifa za deni la taifa kutoka Benki Kuu ya Tanzania, ongezeko la Shilingi 20 trilioni kwa muda mfupi kiasi hicho halijawahi kutokea.
Haishangazi kuwa wadau wengi wanaona ongezeko la deni hili ni kubwa sana. Suala wanalouliza katika mijadala na ambalo halijapata ufafanuzi wa kutosha ni kwa nini deni limepanda kwa kasi hiki?
Kuna wanoauliza pia kuwa pesa zilizokopwa zimeenda wapi ikiwa gharama za maisha zinazidi kupaa siku hadi siku na huduma za jamii zinadorora.
Wapo pia wanaoonyesha hofu zao kuwa kasi hii ya kupanda kwa deni la taifa inaweza kuiingiza nchi kwenye matatizo ya makubwa ya kiuchumi na kuifanya ishindwe kukopesheka.
Alipoingia madarakani hayati Rais John Magufuli, deni la taifa lilikuwa ni Shilingi 35 trilioni, kwa mujibu wa taarifa rasmi za Bunge la Tanzania.
Mwezi Aprili 2018 deni lilifikia Shilingi 49.9 trilioni, kwa mujibu wa Bajeti ya serikali iliyosomwa Bungeni. Mwaka mmoja baadae (Aprili 2019) deni la taifa likafika Shilingi 51.03 trilioni. Deni halikupungua. Likaendelea kukua na kufikia Shilingi 60.7 trilioni mwezi Aprili 2021.
Maelezo ya viongozi serikali
Viongozi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wamejitokeza kujibu baadhi ya hoja zinazoibuliwa na wadau katika mijadala kuhusu ongezeko kubwa la deni la taifa. Lakini hakuna hata mmoja wa viongozi hao aliyetoa majibu ya kina kwa nini deni limepanda na pesa zimeenda wapi.
Akiongea na gazeti la The Citizen mwishoni mwa juma Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Emmanuel Tutuba alidai kuwa deni la taifa ni himilivu na kuwataka watanzania waondoe hofu.
“Hakuna haja ya kuwa na wasiwasi. Deni la taifa lina uhimilivu wa kutosha kwa sasa, kwa baade na kwa muda mrefu,” Bwana Tutuba alisema.
CHANZO CHA PICHA,AFRICA-PRESS.NET
Maelezo ya picha,
Waziri wa fedha na mipango Tanzania, Mwigulu Nchemba
Waziri Nchemba yeye aliingia kwenye mtandao wa Twitter na kudai kuwa ongezeko kubwa la deni la taifa limechangiwa na sekta binafsi ambayo hivi majuzi ilikopa Shilingi 20 trilioni.
Hata hivyo alitoa mchanganuo wa deni ambao umeongeza sintofahamu badala ya kufafanua. Mchanganuo wake pia una kasoro za waziwazi za kimahesabu.
Mchanganuo wa Waziri Nchemba ulikuwa hivi; deni la serikali kuu na mashirika yake ni Shilingi 46.6 trilioni; deni la sekta binafsi ni kati ya Shilingi 17 trilioni hadi 20 trilioni; hati fungani za serikali ni Shilingi 26,600 bilioni (ambayo ni 26.6 trilioni).
Halafu Dk Nchemba akatoa jumla yote ya mchanganuo huu kuwa ni Shilingi 71.2 trilioni wakati hesabu rahisi zinaonyesha kuwa jumla ya mchanganuo wake ni Shilingi 90.2 trilioni inayoendana na taarifa ya Benki Kuu ya Oktoba ya jumla ya deni lote.
Dk Nchemba akaongeza kuwa sekta binafsi ilikopa tena hivi karibuni kiasi cha takribani Shilingi 20 trilioni, ambazo kadiri ya mahesabu yake Waziri Nchemba ndizo zimefanya deni la taifa kufikia Shilingi 91 trilioni.
Ufafanuzi wa Dk Nchemba unachangaza kwa sababu unaongeza deni badala ya kulipunguza. Mchanganuo wake unaonyesha deni limefikia Shilingi 112 trilioni badala ya Shilingi 91 trilioni inayoonyeshwa na Benki Kuu ya Tanzania. Kama ni hivyo kuna tatizo la kimahesabu na la ki-taarifa.
Yote kwa yote mchanganuo na ufafanuzi wa Dk Mwigulu bado hauelezi kwa nini deni la taifa limeongezeka kwa Shilingi 20 trilioni kati ya Aprili 2022 na Oktoba 2022.
Ni wazi kuwa hii sio mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na mijadala mikali kuhusu deni la taifa. Wakati wa utawala wa Rais Magufuli kuongezeka kwa deni la taifa kulizua mijadala.
Wakati huo serikali ilidai kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ilikuwa ndio sababu ya kuongezeka kwa deni hilo. Hata hivyo ongezeko la deni la taifa halikuwahi kufikia kiasi kikubwa kama cha mwaka huu.
CHANZO CHA PICHA,TRC
Maelezo ya picha,
Serikali ya Tanzania ina miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli za kisasa na vituo vya umeme
Uhakiki wa deni la taifa ufanyike
Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ya reli ya kisasa ya SGR, ujenzi wa bwawa la umeme la Nyerere na barabara za mwendokasi kutoka katikati ya mji wa Dar es Salaam kwenda Mbagala.
Hata hivyo serekali ya Rais Samia imeweza kupata mikopo mingi yenye riba nafuu kutoka Benki ya Dunia na Shirila la Fedha Duniani (IMF) ambayo mtangulizi wake. Mikopo hii inazidi kiasi cha dola za kimarekani 2 bilioni (zaidi ya Shilingi 4 trilioni) tangu Rais Samia aingie madarakani mwezi Machi 2021. Mikopo hii ambayo ilielekezwa kwenye shughuli za kukuza uchumi na kuboresha huduma za jamii ingetosha kabisa kuleta ahueni kwenye deni la taifa badala ya kuliongeza kwa kasi kubwa hivyo.
Kwa namna yoyote ile maelezo ya kina kutoka serikalini yanahitajika. Serikali ya Tanzania ni lazima ieleze ni kwa nini deni la taifa limeongezeka kwa kiasi cha Shilingi 20 trilioni ndani ya miezi sita. Hakuna mtu nje ya serikali, hata angekuwa na utaalam kiasi gani, ambaye angeweza kuelezea ongezeko kubwa kiasi hicho.
Dk Nchemba ni mwanasiasa. Inawezekana kuna baadhi ya taarifa ambazo hajazipata kuhusu ongezeko kubwa hilo la deni la taifa. Ni wakati sasa kwa Gavana wa Benki Kuu na wataalam wake kujitokeza kutoa ufafanuzi wa kina. chanzo.BBC