Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, ametoa angalizo la kiuchumi kuhusu mipaka na uwezo wa kifedha wa serikali, akisisitiza kuwa nchi haiwezi kuendelea kubeba mzigo wa kujenga kila mradi wa kibiashara huku ikikabiliwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu linalohitaji uwekezaji wa haraka katika elimu ya ufundi na maarifa.
Akiongoza mhadhara, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, alieleza kwa mantiki kuwa mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi si anasa, bali ni dharura ya kiutawala inayosaidia kuondoa urasimu na kuelekeza rasilimali kwenye maeneo yenye tija zaidi kwa jamii.
“Serikali haiwezi kuwa na bajeti ya kutosha kujenga barabara kuu, masoko na vituo vya mabasi, kisha ikagharamia hadi ujenzi wa vyoo ndani ya stendi hizo na kubakiwa na uwezo wa kuwapatia elimu bora watoto wa familia masikini,” alisema Kafulila.
Alibainisha kuwa njia mbadala ya kimkakati ni kuziachia kampuni na sekta binafsi kujenga na kuendesha miradi yote ya kibiashara, ili fedha zinazookolewa zielekezwe kwenye ujenzi wa hospitali, ununuzi wa dawa na utoaji wa elimu bora.Mkurugenzi mtendaji huyo alianika takwimu zinazoonyesha kuwa kasi ya ongezeko la watu nchini imefikia asilimia 3.4, kiwango ambacho ni cha juu ukilinganisha na wastani wa bara la Afrika ambayo ni asilimia mbili.
“Ongezeko la idadi ya watu duniani limefikia asilimia moja huku India ikifikia asilimia 0.8, na kwamba China ambako idadi ya watu inaendelea kupungua,” alibainisha. Alionya kuwa iwapo kasi hii ya ongezeko la watu ambao wengi wao wanatoka katika kaya masikini haitadhibitiwa kupitia elimu ya uzazi wa mpango, itaendelea kuwa mzigo mzito wa kibajeti ya Taifa katika utoaji wa huduma za msingi.