Kuna tetesi kuwa kikao kinachoendelea kati ya Kamati Kuu ya Chadema na Tume ya uchaguzi, Chadema wamepewa nafasi 22 za viti maalumu.
Kitendo cha Chadema kukubali kupeleka hayo majina kimsingi ni kukubaliana na mchakato mzima wa Tume, na itakuwa hadaa kwa wanachama na jumuiya za kimataifa kuwa wameibiwa kura.
Chadema ijue huo ni mtego wa fisi kuonyeshwa kipande cha mfupa, mkikubali mjue mmekwisha, dhihaka mtakazopata hamtaweza kuzijibu, ile hoja ya kuwa chama cha ruzuku itathibitika wazi.
Kutoa hayo majina ni kuwadhulumu wagombea waliojitoa kwa damu kupigania haki majimboni ambao baadhi yao wamepoteza viungo wengine wamepoteza uhai na baadhi hadi leo bado wapo magerezani.
Kamati kuu haitamtendea haki mgombea urais Tundu Lissu ambaye hadi sasa amekimbilia ubalozi wa Ujerumani kunusuru maisha yake.
Vile vile haitawatendea haki wapenzi, wanaharakati na wafuasi wa mitandaoni wanaohatarisha maisha yao kuitetea CHADEMA.
Kwa hadhi ya Chama kilipofikia na kwa gharama mliyopoteza kukijenga haiwezi kulipwa kwa kupewa ruzuku ya viti maalumu 22 tena na watu waliowadhulumu ushindi wenu.