KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII imebaini matumizi mabaya ya fedha kiasi cha Bilioni 375 zilizopangwa kutumika kupima ardhi badala yake asilimia kubwa zimetumika kufanyia semina na kulipana posho za uratibu.
(b) Semina kuhusu Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.
Mheshimiwa Spika, semina hii ilitolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi kwa lengo la kuwajengea wajumbe uwezo juu ya mradi huu ambapo Kamati ilielezwa kuwa Serikali imepata mkopo kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Kimarekani Milioni 150 sawa na Shilingi Bilion 375 utakaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano (2022/2023 hadi Juni, 2027). Aidha, Kamati ilielezwa kuwa mradi huu unalenga kuimarisha usalama wa taarifa za ardhi, kuimarisha miundombinu ya upimaji na kujenga majengo ya Ofisi
Mheshimiwa Spika, matarajio ya Wajumbe wa Kamati ni kwamba sehemu kubwa ya fedha ingeelekezwa kwenye mipango ya matumizi ya ardhi ambayo imeonekana kuwa ni suluhisho la migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya watumiaji mbalimbali nchini hasa wakulima na wafugaji lakin hali halisi inaonyesha kwamba ni Asilimia 1 tu ya fedha zote ndiyo itaelekezwa kwenye zoezi hilo. Lakini kinyume chake fedha nyingi zimeelekezwa katika kutekeleza mambo mengine kama vile uratibu wa mradi.
Mheshimiwa Spika, Kamati haioni tija katika mradi huu kwa kuwa haugusi kwa kiwango cha kutosha maeneo yanayolenga kutatua migogoro ya ardhi nchini. Aidha, utekelezaji wa mradi huu ungeweza kutekelezwa kwa ufanisi endapo wangeiwezesha Tume ya Mipango ya Ardhi ambayo imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya upangaji kwa ufanisi; hata hivyo ufinyu wa bajeti umefanya ishindwe kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Mathalani hadi kufikia Desemba 2022 ni vijiji 2,678 kati ya vijiji 12,319 vilivyopo nchini ndio vimepangiwa matumizi ya ardhi.