lowassa alia na kamati ya mwakyembe
habari zinazoshabihiana
• kamati ya richmond 'yahamia' marekani 14.12.2007 [soma]
• walioipa tenda richmond kuhojiwa 28.11.2007 [soma]
• richmond aibu! *lowassa, karamagi, msabaha, mwanyika, hosea mh! 07.02.2008 [soma]
na mwandishi wetu, dodoma
jana waziri mkuu, bw. Edward lowassa, alikuwa kiongozi wa kwanza kati ya watatu, kutangaza nia yake ya kujiuzulu kutokana na taarifa ya kamati teule ya kuchunguza mkataba wa richmond.
Katika hotuba yake bungeni, bw. Lowassa alionesha kutoridhishwa na taarifa hiyo na yafuatayo ni maneno yake aliyoyasema wakati akitangaza azma yake hiyo:
"mheshimiwa spika, kwanza napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunifanya msemaji wa kwanza katika hoja hii.
Lakini la pili nimpongeze dkt. Harrison mwakyembe, mwenyekiti wa kamati teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli.
Kwa kazi nzuri kwa maoni yao, wamewasilisha vizuri. Lakini nimesimama kuweka kwenye kumbukumbu kutoridhika kwangu na jinsi kazi hiyo ilivyofanywa.
Mheshimiwa dkt. Mwakyembe ni mwanasheria, tena daktari alikuwa anafundisha wanafunzi chuo kikuu. Moja ya vitu alivyokuwa akifundisha ni natural justice.
Mheshimiwa spika, wewe pia ni mwanasheria unafahamu suala la natural justice. Kwamba kamati teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong'ono ya mitaani, wamesafiri mpaka marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja katika watuhumiwa mle, hawakunihoji hata siku moja.
Mheshimiwa spika, nimesimama kueleza masikitiko yangu. Ofisi ya bunge mpaka ofisini kwangu, hata wangeniita ningekwenda kwa miguu kama hamna gari na nilikutwa tayari kufanya hivyo.
Hawa ni watu makini sana, siwezi kuamini kwamba wanaweza wakafanya oversight kama hiyo. Kwa sababu katika kila hoja walizojenga wamesema waziri mkuu ilikuwa hivi.
Kulikuwa na shida gani kuja kuniuliza waziri mkuu, wanasema ulitoa dokezo hili ni sawa sawa ni kweli? Kulikwa na shida gani kwa mfano, kufuata utaratibu wa westminster, kuthibitisha hapo unaposema mwenye richmond ni fulani uka-lay on the table records na ushahidi kuwa ni fulani.
Mheshimiwa spika, taifa letu ni taifa changa, lakini chombo hiki ndiyo mahali pa demokrasia pakubwa katika nchi pote, hapa ndipo penyewe. Kama katika chombo hiki haki haitaonekana kutendeka, nchi yetu haitakwenda vizuri.
Hapa ndipo tunategemea tuwaoneshe umakini wetu, umahiri wetu katika mambo ya demokrasia. Kwa hiyo nilichofanyiwa napenda kuweka kumbukumbu sawa, naona si sahihi, nimefadhaika sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili.
Maana zimechukuliwa tuhuma zikaja zikaelezwa hapa kwamba hivi ndivyo ilivyo. Mimi sijaulizwa. Kulikuwa na shida gani ya kuniuliza, kwa nini muamini minong'ono ya mitaani kuliko maelezo yangu.
Sisi wote hapa ni wanasiasa, tukianza kuamini minong'ono ya mitaani, niambieni mwanasiasa atakayesimama. Huwezi tume imepewa muda wa kutosha lakini inashindwa kumwona mtu ambaye wanamtuhumu na wanamsema kwa kirefu sana.
Mheshimiwa spika, lakini hata pale uliponinong'oneza ukaniambia una ushahidi wowote? Nilikupa ushahidi huo wa maandishi. Katika taarifa yao hakuna hata moja ya ushahidi ambao umetoka kwa waziri mkuu. Kile kitabu cha majedwali kimejaa majedwali mengi pamoja na magazeti mpaka ya udaku, lakini maelezo ya waziri mkuu hakuna hata moja.
Mheshimiwa spika, naamini ingekuwa ni heshima wangeiweka halafu wakasema tunakataa kitambulisho hiki kwa sababu hii na hii na hii, hiyo
ndiyo imejengwa hoja. Lakini kujenga hoja na kuja hapa bungeni tunahutubia nchi nzima na kusema waziri mkuu amefanya hiki, amefanya hiki bila ya kumsikiliza, nachelea kuuliza hivi mtu wa chini itakuwaje?
Mheshimiwa spika, lakini nimetafakari kwa makini sana jambo hili nikajiuliza hivi hasa kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo kulikoni?
Mimi nadhani there is a wish which i am going to grant, ni uwaziri mkuu. Nadhani tatizo ni uwaziri mkuu. Kwamba ionekane waziri mkuu ndiye amefanya haya, tumwondolee heshima au tumwajibishe.
Mheshimiwa spika, nimetafakari sana kwa niaba ya chama changu, kwa niaba ya serikali yangu nimeamua kumwandikia rais barua ya kumwomba niachie ngazi. Nafanya hivyo kwa moyo mweupe kabisa, ili kuonesha dhana ya uwajibikaji, lakini na kutokubaliana na utaratibu uliotumika kusema uongo ndani ya bunge wa kumsingizia mtu.
Mheshimiwa spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana rais kwa heshima aliyonipa ya kutumikia nchi hii kwa uwaziri mkuu kwa miaka miwili. Namshukuru sana mheshimiwa rais.
Nakushukuru wewe, nawashukuru mawaziri na naibu mawaziri, nawashukuru waheshimiwa wabunge na wanachama wa ccm tuliosimamia ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi. Mheshimiwa spika baada ya kusema hayo nakushukuru.
chanzo: majira