86.-(1) Siku ambayo Muswada wa Sheria uliokwisha kujadiliwa na Kamati umepangwa kwenye Orodha ya Shughuli, Waziri,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Kamati au Mbunge mwenye Muswada husika atawasilisha hoja kwamba Muswada wa Sheria ambao atautaja kwa jina Kusomwa Mara ya Pili.
(2) Hoja ya Muswada wa Sheria Kusomwa Mara ya Pili itakuwa
kama ifuatavyo:-
Kwamba, Muswada wa Sheria uitwao
.. sasa usomwe mara ya pili. Au kadri itakavyokuwa; Kwamba, Muswada uitwao
kama ulivyorekebishwa kwa mujibu wa jedwali la marekebisho au kama ulivyochapishwa upya sasa usomwe mara ya Pili.
(3) Haitakuwa halali katika hatua hii kuleta hoja ya kufanya mabadiliko katika hoja isipokuwa tu kwamba:-
(a) mabadiliko bila kutoa sababu yanaweza kutolewa kwa kusema: Kwamba, Muswada huu usisomwe mara ya Pili sasa na badala yake usomwe baada ya
.. kuanzia
.., na hapo muda ambao Muswada huo unaokusudiwa kusomwa utatajwa.
(b) mabadiliko yenye kutoa sababu yanaweza kutolewa kwa kusema: Kwamba, Bunge hili likatae Muswada huu Kusomwa
Mara ya Pili kwa sababu zifuatazo
., na hapo sababu za kupinga Muswada Kusomwa Mara ya Pili zitatajwa kwa ukamilifu.
(4) Iwapo hoja itatolewa chini ya fasili ya 3(a) na (b) ya Kanuni hii, Spika atalihoji Bunge ili kufikia uamuzi.
(5) Mwenyekiti wa Kamati iliyopelekewa Muswada wa Sheria au Mjumbe mwingine wa Kamati aliyeteuliwa kwa ajili hiyo, atatoa
maoni ya Kamati kuhusu Muswada husika.
(6) Ikiwa Muswada wa Sheria unaohusika ni Muswada wa Serikali, basi Msemaji wa Kambi ya Upinzani atatoa maoni yake juu ya
Muswada husika na endapo ni Muswada Binafsi au Muswada wa Kamati, basi msemaji wa Serikali atatoa maoni yake.
(7) Mjadala wakati wa Muswada wa Sheria Kusomwa Mara ya Pili utahusu ubora na misingi ya Muswada huo tu.
(8) Majadiliano juu ya hoja kuhusu Muswada kama yapo yatahusu maneno yanayohusiana na hoja tu.
(9) Mbunge yeyote au Waziri anaweza, wakati wa mjadala huo, kumshauri Mtoa hoja afanye mabadiliko katika Muswada, ama
mabadiliko ya jumla au yale atakayoyataja Mbunge.
(10) Katika hatua hii iwapo mtoa hoja anataka kufanya marekebisho au mabadiliko katika Muswada wa Sheria kutokana
na ushauri uliotolewa ama katika Kamati au wakati wa Muswada wa Sheria Kusomwa Mara ya Pili au kwa sababu nyingine yoyote,
iwapo Muswada huo ni wa Serikali atamjulisha Mwandishi Mkuu wa Sheria na iwapo Muswada husika ni wa Kamati au Binafsi
atamjulisha Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria ili atayarishe na kumkabidhi Katibu ambaye atagawa kwa kila
Mbunge nakala ya:-
(a) Muswada wa Sheria uliochapishwa upya ukiwa na marekebisho au mabadiliko yanayokusudiwa kufanyika; au
(b) Jedwali la Marekebisho au mabadiliko yanayokusudiwa kufanyika.
(11) Kamati au Mbunge anaweza kuwasilisha kwa Katibu, kwa maandishi, mabadiliko anayokusudia kuyafanya katika Muswada
huo wakati wa Kamati ya Bunge Zima akionesha bayana mabadiliko yanayokusudiwa kufanyika katika kila Ibara inayohusika.