Heri ya pasaka kwa wote waamini na wasioamini.
Moja ya kauli ambayo inaendelea kumuweka mwananchi katika box la ujinga, utumwa, utegemezi na umasikini ni kauli ya kuitwa wanyonge. Mara nyingi tunawasikia viongozi wakijinasibu kuwa wao ni viongozi wa wanyonge, kiukweli huwa nashindwa kuelewa wanachomaanisha! Je huwa wanamaanisha kuwa wao ni imara hivyo wanawaongoza wanyonge au wenyewe ni wanyonge wanaowaongoza wanyonge?
Kwa maana kiongozi wa jamii fulani au kundi flani ni lazima awe na sifa zinazofanana na anaowaongoza. Kwa mfano kapteni wa timu ya mpira ni lazima na yeye awe mchezaji wa mpira. Hivyo basi kama viongozi wetu ni viongozi wa wanyonge je ina maana na wenyewe wana sifa ya unyonge au ni wanyonge zaidi yetu kwa kuwa kiongozi ni lazima awe na uwezo mkubwa kuliko anaowaongoza katika sifa inayotengeneza kundi hilo.
Na kama viongozi sio wanyonge bali ni imara ina maana watakuwa hawana sifa za kuongoza kwa sababu hawafanani na kundi hilo. Ni kama paka awe kiongozi wa panya, ni kitu ambacho hakiwezekani kwa kuwa panya na paka wana uadui wa kiasilia kulingana na utaratibu wa 'life cycle'
Paka siku zote anamwinda panya ili ajipatie kitoweo ili maisha yaendelee na ndivyo ilivyo hata kwa simba na swala.
Ukiangalia makundi ya Wanyama yana viongozi wao ambao wanatoka ndani ya ndani ya hilo hilo kundi na wala hawatawaliwi na Wanyama kutoka kwenye kundi linguine lenye sifa tofauti.
Kiukweli unyonge ni udhaifu, kutokuweza, kutawaliwa, kutokujitetea, kutokujikwamua na unyonge unaonesha kila aina ya shida na matatizo na ndio sifa inayowakilisha kundi hilo.
Ukiitwa mnyonge utaamini siku zote hauwezi kufanya mpaka ufanyiwe, hauwezi kuamua mpaka uamuliwe, hauwezi kutawala mpaka utawaliwe na hauwezi kuhoji ila we ndio unahojiwa.
Kama viongozi wetu nao ni wanyonge ina maana na wao wanatawaliwa,kuamuliwa,kuhojiwa na kuamrishwa? na kama sio kwa nini watuite sisi wanyonge ilihali tunajua unyonge ni udhaifu wa kujitetea, kutawala nk.
Au wanafanya hivyo ili kutudumaza kiakili na kihisia tujione na tuhisi hatuwezi kuwa imara na kujitawala katika kila nyanja hasa nyanja ya kufanya maamuzi ya kisiasa.
Kwa nini viongozi wasitumie kauli ya kuwaongoza watu imara ili tukiunganisha nguvu tulete matokeo chanya kwenye jamii zetu kwa kuwa wanyonge hawawezi kuwa na nguvu moja kwa kuwa ni dhaifu mbele ya mabwana zao ni Zaidi ya mtumwa kabisa.
Nawashauri wananchi wakatae kuitwa wanyonge na viongozi wasituite wanyonge kwa kuwa mnyonge hawezi kukuweka madarakani au kukupa mamlaka ya kutawala. Bali watuite imara ili inapofikia hatua ya kumpa madaraka mtu mwingine isiwe tabu kama ambavyo mnyonge ANGEPATA TABU SANA.
Be blessed.