Mbowe atoa kauli nzito kifo cha Ballali
na Lucy Ngowi
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Ballali kina mkono wa baadhi ya vigogo wa serikali, kwa sababu alikuwa shahidi muhimu katika vita ya ufisadi.
Mbowe ambaye anakuwa kiongozi wa kwanza kutoa kauli hiyo nzito, alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa Mtaa wa Ufipa, pamoja na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Alisema kuna kitendawili kinachotegwa sasa na baadhi ya vigogo wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuwa Ballali alikuwa shahidi muhimu sana katika vita ya ufisadi aliyodai kufanywa na chama tawala.
Mbowe alisema, tangu Ballali alipoondoka nchini Agosti, mwaka jana, vyombo vyote vya habari viliandika vikidai gavana huyo wa zamani ana ushahidi wa kina kuhusu ubadhirifu wa pesa za BoT, matokeo yake Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wake na kuunda kamati ya kuchunguza ufisadi huo.
Mwenyekiti huyo wa CHADEMA alisisitiza kuwa, Ballali hakula peke yake, bali alikula na baadhi ya viongozi waandamizi wa serikali ya awamu ya tatu na ya nne na kuongeza kuwa, hata baadhi ya fedha zilizotumika wakati wa kampeni ya mgombea wa CCM, zilitokana na fedha za EPA.
Kuteketea kwa Ballali, tutaamini kuna mkono mchafu wa baadhi ya viongozi wa serikali, kwa sababu ni shahidi muhimu katika vita ya ufisadi. Wasifikiri kufa kwa Ballali, ndiyo mwisho wa mapambano, lakini nawaambia ndiyo kwanza vita ya ufisadi itapamba moto.
Ufisadi na mchezo mchafu wa CCM, umewatesa watoto wetu, wazazi wetu na sasa basi, tutapambana hadi watakapouana wote waishe. Wamemuua Ballali, Amina Chifupa wataendelea kuuana, alisema mwenyekiti huyo.
Amina alikuwa Mbunge wa Viti Maalum (UVCCM), aliyefariki mwaka jana baada ya kuugua ghafla, na kifo chake kuzua gumzo nchini kutokana na msimamo wake wa kutaka kutaja majina ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa Mbowe, katika pesa zilizoibwa BoT, pesa pekee zinazochunguzwa ni fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), lakini tuhuma za ubadhirifu na wizi wa BoT hazikuwa za akaunti hiyo peke yake.
EPA ni sehemu tu, pesa nyingine hazijaundiwa tume. Tunamwambia Rais Kikwete, utawala wake kwa miaka miwili iliyobakia utakuwa ni wa kuunda tume tu. Wamemwondoa Ballali kwa sababu ndani ya Ballali, kuna mambo mengi yaliyofichika, alisisitiza.
Alisema BoT ni benki ya serikali, hivyo pesa zinazohifadhiwa ni kodi za Watanzania na ili ziweze kuchukuliwa, lazima mamlaka itoke serikalini.
Mwenyekiti huyo alisema, aliyekuwa Waziri wa Fedha awamu ya tatu, Basil Mramba na Katibu Mkuu, Grey Mgonja, wanahusika katika wizi huo wa BoT kwa kuwa walimwidhinisha Ballali, alipe pesa mbalimbali zilizokuwa zinatoka bila mpangilio, lakini mpaka sasa hawajaguswa.
Tunataka Mramba, Mgonja watueleze ukweli kuhusiana na ubadhirifu uliokuwa unafanywa BoT, alisema mwenyekiti huyo.
Alisema anamshangaa Rais Kikwete kuunda tume nyingine iliyomhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea ilhali serikali imeficha ripoti ya awali.
Awali, mwenyekiti huyo alizindua tawi la CHADEMA Mtaa wa Ufipa, Kinondoni na kusema kuwa, huo ni mkakati wa uzinduaji wa matawi ya chama chake katika Jiji la Dar es Salaam.
Alionya kuwa, kamwe tawi hilo lisiwe la CHADEMA tu, bali liwe kwa nia ya kuwatetea wananchi wote katika eneo hilo. Pia lisiwabague wanachama wa vyama vingine vya siasa.
Viongozi wa CHADEMA na tawi la Ufipa, msiwe wa kwanza kuhujumu wanachama wa vyama vingine vya siasa, bali muwe kimbilio la wote wenye matatizo katika mtaa huo, alisema Mbowe.
Ballali alifariki dunia Mei 16 nchini Marekani na kuzikwa juzi katika makaburi ya Wakatoliki ya Gate of Heaven, Silver Spring, nchini humo, ambako watu maarufu walihudhuria mazishi yake, akiwemo Balozi wa Tanzania nchini humo, Ombeni Sefue.
Ballali amekuwa akiripotiwa kuugua kwa muda mrefu, lakini muda wote serikali haijawahi kutaja ugonjwa uliokuwa ukimsumbua na hospitali aliyokuwa akipata matibabu.
Hata alipofariki, serikali haikuwahi kutangaza kifo chake hadi gazeti hili lilipoibua taarifa hiyo siku tano baadaye.