Serikali inaficha ukweli – Wanasheria
na Mwandishi Wetu
BAADHI ya wanasheria wameshangazwa na usiri wa serikali kuhusu kuugua hadi kufa kwa aliyekuwa Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Ballali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumapili mwishoni mwa wiki, wanasheria hao walisema lazima serikali inaficha jambo kuhusu Dk. Ballali.
Mmoja wa wanasheria hao, Mabere Marando, alitoa lawama kuhusu ukimya wa serikali, katika kuugua hadi kufariki dunia kwa Dk. Ballali, na kuongeza kwamba kutawafaidisha watuhumiwa wa wizi wa fedha katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA), uliofanyika BoT.
"Nimesikitishwa sana na kifo cha Dk. Ballali, alikuwa Mtanzania mwenzetu. Lakini kinachosikitisha zaidi ni ukweli kwamba kifo chake kitaathiri sana uchunguzi wa wizi wa fedha za EPA.
"Ukimya wa serikali kuhusu kuugua hadi kufa kwa Dk. Ballali, unashangaza, ni wazi kuwa kuna jambo inaficha, kwa sababu haiwezekani isijue mahali alipo gavana wake wakati ilikuwa ikimlipia sehemu ya gharama za matibabu kama tulivyoelezwa na gavana wa sasa," alisema Marando.
Alieleza zaidi kuwa kitendo cha tume iliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuchunguza tuhuma hizo kutomuhoji Dk. Ballali hadi mauti yalipomkuta, nacho kinashangaza, kwa sababu alipaswa kuhojiwa kwanza, kwani alikuwa shahidi muhimu katika kesi hiyo.
Mwanasheria mwingine wa serikali aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alizungumzia suala hilo na kusema ni jambo la ajabu kwa timu inayochunguza kashfa ya EPA kutomuhoji Dk. Ballali hadi anakufa.
"Huyu alikuwa ‘key' katika uchunguzi huu, timu ya rais ilipaswa kumuhoji mapema kabisa, inashangaza kusikia mpaka anakufa hakuwahi kuhojiwa na serikali inasema haimtafuti.
"…Huu uchunguzi unaofanywa ni lazima utiliwe shaka na mjuzi yeyote wa mambo ya kisheria. Uchunguzi unaofanywa ni kama mchezo fulani hivi! "Na hapa wa kushakiwa kwanza ni serikali, haijulikani inaficha nini kuhusu huyu ndugu yetu, kwa sababu tangu alipougua mpaka anakufa, habari zake zimekuwa siri kubwa," alisema na kuongeza kwamba, ni ajabu kwa serikali kutokujua alipo mtuhumiwa wa wizi wa mabilioni ya shilingi. Alisema, hata taarifa zilizotolewa kuwa amefutiwa hati ya kuishi Marekani ziliongeza mashaka, kwa sababu alitakiwa kuondoka nchini humo baada ya kutotambuliwa, lakini hadi anakufa alikuwa huko. Aidha, aliwataka Watanzania kuihoji serikali kwa nini ilifanya siri matatizo ya kuugua hadi kufa kwa Dk. Ballali, na kuongeza kwamba Marekani inatakiwa kutoa taarifa za uchunguzi wa kifo chake ili wananchi wajue, kwa kuwa ni haki yao kufanya hivyo.