Ufunuo mpya:Ballali aliungama ukweli kashfa ya EPA
Habari Zinazoshabihiana
Kikwete ashtushwa kifo cha Ballali 24.05.2008 [Soma]
...Mdogo wake afichua wosia mwingine 25.05.2008 [Soma]
...Watanzania washtushwa usiri wa kifo chake 22.05.2008 [Soma]
*Majira Jumapili lanasa alichokisema
*Serikali ya Kikwete yasubiri kuumbuka
Na Hassan Abbas
ALIYEKUWA Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Daud Ballali, kabla ya kufikwa na mauti yake nchini Marekani, aliungama 'dhambi' yake kuu ya kuhusishwa na kashfa ya ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), gazeti hili linawathibitishia Watanzania.
Katika ungamo hilo, Ballali (65), aliyekuwa akichukuliwa kuwa mmoja wa watuhumiwa na mashahidi wakuu wanaoweza kueleza nani hasa walikuwa nyuma ya ufisadi huo, imebainika alitaja moja kwa moja mhusika, ungamo ambalo sasa baada ya kifo chake, linaiacha Serikali ya CCM kuwa ndiye mtuhumiwa mkuu.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili limezipata kutoka vyanzo vya kuaminika na maelezo ya siri yaliyotolewa na baadhi ya ndugu zake, Ballali amekufa akiwa ameinyooshea kidole Serikali kuwa ndiyo inayohusika na fedha za EPA zilizochotwa BoT, kauli inayoonesha kuwa yeye alikuwa akipokea tu maagizo ya kuziidhinisha.
Ungamo la kwanza la Ballali katika fumbo kuu la ufisadi huo, uchunguzi wetu umebaini, alilifanya katika mahojiano yake na wakaguzi wa Deloitte & Touche, ambao ndio wa kwanza kuibua kashfa ya EPA kabla ya wakaguzi wengine wa Ernst&Young kuhitimisha.
Katika mahojiano yake na Ballali ya Septemba 8 na 9, 2006, Mkurugenzi Mwandamizi wa Ukaguzi wa Kampuni ya Deloitte, Bw. Samuole Sithole kutoka Afrika Kusini, aliyesafiri rasmi kuja nchini kumbana Ballali, ndiye aliyefanikiwa kupata ungamo la Gavana huyo.
Nyaraka zinaonesha kuwa siku ya kwanza ya mahojiano hayo, Ballali alifanikiwa, hata baada ya kubanwa sana, kuificha siri kuu iliyojificha juu ya wahusika halisi wa ufisadi wa EPA ambapo kampuni zipatazo nane zilipitishiwa kijanja kiasi cha sh. bilioni 133.
Hata hivyo, akitumia utaalamu na umahiri wake wa kuhoji watuhumiwa ambao ni wataalamu wa masuala ya fedha na uchumi waliokumbwa na kashfa mbalimbali, Jumamosi ya Septemba 9, Bw. Sithole aliweza kupata kile alichokitaka kutoka kwa Ballali ambaye alifanya ungamo ambalo hadi anakufa, alikuwa anaangalia uwezekano wa kulifafanua zaidi, ili jamii iujue ukweli.
Ballali katika mahojiano hayo, aliitaka Serikali moja kwa moja, kupitia Wizara ya Fedha kuwa ndiyo inayojua kuhusu suala la malipo ya EPA.
Katika ungamo hilo pia Ballali alikwenda mbali zaidi kwa kuwafahamisha wachunguzi hao kuwa ni Serikali pia ambayo inaweza na inapaswa kutoa risiti za kuthibitisha matumizi ya pesa hizo.
Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji iliwahi kuuma maneno kwa kuzikana fedha hizo lakini baadaye ilieleza kuwa zilitumika kwa matumizi 'mahsusi yenye maslahi ya taifa.'
Duru za siasa zinazihusisha fedha hizo na kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ingawa karibu viongozi wote waandamizi wa chama hicho akiwemo Katibu Mkuu mstaafu, Bw. Phillip Mangulla waliwahi kukanusha walipoulizwa na gazeti hili wakidai kuwa chama hicho kina miradi, wafadhili na wanachama wanaokifanya kijitosheleze.
Hata hivyo wiki hii tena, siku chache baada ya kufariki dunia, ungamo hilo la Ballali limepata nguvu baada ya mmoja wa wanafamilia wake wa karibu aliyezungumza na Majira Jumapili Dar es Salaam kwa sharti la kutotajwa jina, kufichua kuwa katika siku zote alizopata kumsikia marehemu akizungumza na watu wake wa karibu enzi za uhai wake, alikuwa akisononeka sana kuhusishwa na ufisadi huo na alipanga kuyasema yote.
"Alikuwa akiufuatilia mjadala wote, alikuwa mvumilivu sana, lakini alishajipanga kusema ukweli wote," kilidokeza chanzo hicho.
Akaongeza: "Alikuwa akitaka kusikia kauli ya mtu mmoja muhimu sana, ninyi pia mtakuwa mnamjua, kama mtu huyo angekuwa akitoa kauli za kuonekana kumkandamiza, basi naye alikuwa tayari kusema ukweli wote kwamba kuna waliohusika kuchukua fedha za EPA.
Lakini alisita baada ya mtu huyo kila ninyi (waandishi wa habari) mlipokuwa mkimbana, akawa haongei mengi kuhusu hilo. " Hakutaka kufafanua mtu huyo ni nani.
Source:
http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=6753