Ansbert Ngurumo
NILIWAHI kudokeza mambo mawili kwenye safu hii kuhusu aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), hayati Daudi Ballali.
Kwanza nilihoji kama ugonjwa wake ulitokana na kulishwa sumu. Sikujibiwa. Pili, nilisema kwamba taarifa za watu wanaojua mambo yanayoendelea serikalini zilieleza kuwa Ballali asingerejea Tanzania.
Yote mawili yamekuwa. Ballali hakurejea. Sasa taarifa mpya zinasema kwamba kabla hajafa alimtaja mtu aliyemlisha sumu iliyosababisha ugonjwa wake, hadi akakimbizwa nje ya nchi kutibiwa.
Watu wake wa karibu wamemnukuu hayati Ballali akimtaja mtu aliyemlisha sumu. Yawezekana hii ni kauli mojawapo ambayo wanafamilia walitaka kuiweka hadharani katika mkutano na wanahabari. Tuwape muda.
Kwa sababu zinazoeleweka, hatutamtaja muuaji huyo hapa kwa sasa. Lakini kadiri siku zinavyokwenda, iwapo na sisi hatutalishwa sumu, kama hatajitaja, tutamtaja siku moja, katika kuweka vema historia ya mapambano dhidi ya ufisadi.
Siku mambo yote yatakapokuwa yamewekwa vizuri, Watanzania watakaokuwa hai wakati huo watapata fursa ya kutambua jinsi ufisadi ulivyowahi kuwa sehemu nyeti ya utawala wa nchi hii.
Kitu kimoja hakitawashangaza. Nacho ni sura na majina yanayozungumzwa na kuhusishwa na ufisadi katika serikali za awamu ya tatu na ya nne.
Hata katika hili la sasa, mtu yule yule aliyetajwa na hayati Ballali, kwamba ndiye alinilisha sumu, ni kigogo yule yule ambaye amekuwa anahusishwa katika mazingira na matukio mengi ya ufisadi wa kupindukia.
Yumo katika orodha ya mafisadi 11 walioanikwa hadharani na Dk. Willibrod Slaa, Septemba 15, 2007 katika mkutano wa hadhara wa Temeke Mwembe Yanga, Dar es Salaam.
Yumo miongoni mwa waasisi wa kaulimbiu ya Maisha bora kwa kila Mtanzania. Ni mmoja wa watu ambao kwa sasa wanaangaliwa kwa macho ya chuki, kwa kuwasababishia Watanzania maisha duni.
Ni mmoja wa vinara waliofadhili na kutangaza kwa nguvu zote dhana ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya ambayo imekuwa ikifupishwa kwa kuitwa ANGUKA; na kuwa kiini cha anguko la Tanzania.
Ni muasisi wa dhana iliyoangusha uchumi wa nchi na kudunisha maisha ya Watanzania, huku akiasisi dhana nyingine ya kimya kimya ya Maisha bora kwa kila fisadi. Mtu huyu huyu aliyetajwa na hayati Ballali kwamba ndiye alimlisha sumu, yumo miongoni mwa vigogo wanaotuhumiwa kulihujumu taifa kwa kuunda mitego ya uchotaji wa pesa za wananchi kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu (EPA).
Ndiye anayetajwa kuwa mmoja wa vigogo walionufaika na pesa za Richmond; mtu ambaye inasemekana alikula njama kuchomoa mafaili ya Richmond katika kumbukumbu za msajili wa makampuni ili kuiingiza mjini Kamati ya Bunge iliyokuwa inachunguza tuhuma dhidi ya kampuni hiyo.
Ni kigogo huyo huyo ambaye kwa wakati fulani alidhaniwa kuwa na hisa katika urais wa Jakaya Kikwete, hata ikawalazimu wanahabari kumhoji rais moja kwa moja kuhusu suala hilo.
Ni mtu huyo huyo ambaye miezi michache iliyopita, kabla ya masuala ya ufisadi kupamba moto, alikuwa akidhaniwa kuwa mfadhili na mkombozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM); na ambaye baadhi ya watu wanaojua jinsi awamu hii inavyofanya kazi, waliwahi kudokeza kwamba ndiye rais wa Tanzania asiyeishi Ikulu, anayeendesha nchi atakavyo kupitia kwa rais aliyechaguliwa, anayeishi Ikulu.
Lakini kikubwa kinachomgusa na kumfadhaisha kigogo huyu ni taarifa kwamba ndiye ameshiriki kwa kiasi kikubwa kuchota mabilioni ya EPA kutoka BoT na kuyazungusha kwenye miradi yake, huku akiingiza mengine kwenye kazi za CCM, zikiwamo harakati za kampeni za uchaguzi mkuu.
Kutokana na ukaribu wake na walio madarakani, serikali imeshindwa hata kuchukua hatua madhubuti dhidi ya walioiba pesa za EPA; ikasema haiwajui, lakini ikakiri kwamba wanarudisha pesa taratibu! Serikali hii hii ikashindwa kuiweka hadharani ripoti kamili ya uchunguzi wa wizi wa EPA kama ilivyoandaliwa na wataalamu wa Ernst & Young.
Serikali ikamficha mtu wake kwa jinsi ile ile ilivyokuwa inaficha ugonjwa wa Ballali, nchi aliko na hospitali alikolazwa, huku baadhi ya maofisa wa serikali wakisemekana kumtembelea mgonjwa wao kushuhudia kama bado yuko hai.
Usiri wa serikali katika suala la Ballali umeiaibisha yenyewe, na umeondoa kabisa imani ya wananchi kwa serikali hii. Umeonyesha unyonge na udhaifu mkubwa wa watawala wa sasa, na kudhihirisha wasiwasi ambao tumekuwa nao siku zote, kwamba nchi hii sasa inaendeshwa na mafisadi.
Lakini huu umekuwa usiri uliokithiri, kiasi cha serikali kudiriki kuficha hata kifo chake, hadi gazeti hili lilipoibua taarifa hizo, na kulazimisha serikali kukiri.
Nawaonea huruma watumishi wa serikali hii wasio mafisadi, lakini wanaofunzwa kutunza siri za mafisadi.
Tabia hii ya serikali ndiyo imewafanya wananchi wengine kudhani kwamba hata Ballali mwenyewe hajafa; kwamba ni njama za mafisadi kumficha kabisa ili kuua ushahidi katika suala la EPA.
Lakini hata wale wanaoamini kwamba amefariki dunia, wanajenga hoja hiyo hiyo; kwamba wamemuua ili kuficha siri yao.
Kwa kifo cha Ballali lipo jambo ambalo hatutalijua kamwe kuhusu wizi wa EPA. Maana kabla hajafa, Ballali mwenyewe alisema hakula hela za EPA, bali anawajua waliozichota, na kwamba asingekufa peke yake.
Sasa wamemtanguliza wakidhani atakufa peke yake. Lakini sisi wengine tunasema kwamba hao hao waliomtanguliza, watamfuata.
Hatuwezi kujua mapenzi ya Mungu, na si vema kumsingizia Mungu. Lakini akili timamu inatueleza kuwa kama tungekuwa na serikali makini, kifo cha Ballali kingeahirishwa.
Huyu ndiye alipaswa kulindwa na serikali ili aweze kutoa ushahidi ambao ungeiwezesha serikali kuchukua hatua za kujisafisha, na kudhibiti ufisadi mwingine.
Lakini kwa kuwa si serikali makini, na kwa kuwa haina nia ya kujisafisha; na kwa kuwa inawajua na kuwalinda waliohusika na wizi wa EPA; na kwa kuwa wanaohusishwa na kifo cha Ballali ni wale wale walioshiriki kuiumba serikali hii; Watanzania hawatakuwa na makosa wakiibeza na hata kuituhumu kwa kumuua Ballali.
Ndiyo maana, ingawa kwenye misiba hatutarajii watu wamkejeli marehemu, Watanzania wameshindwa kuzuia hisia zao. Kwa kujitahidi sana, wamezielekeza zaidi kwa serikali badala ya marehemu.
Mojawapo ya kauli zilizozagaa mitaani sasa ni kwamba kafa Ballali, bado wengine kumi. Hawa wanaosema hivi wanarejea orodha ya mafisadi iliyotajwa na Dk. Slaa, ambayo huko nyuma niliwahi kuiita JK Eleven. Lakini kikubwa ni kwamba huyo anayesemekana kumlisha sumu Ballali ni mmojawapo wa hao kumi waliobaki.
Hili linakomaza dhana nyingine kwamba watu hawa sasa wameamua kumalizana wakigombea maisha bora walioyowanyima wananchi.
Tunachojua tulio wengi ni kwamba Ballali si wa kwanza. Na hawezi kuwa wa mwisho. Lakini mwisho wao wote ni mmoja.
Yawezekana bado kumi au zaidi ya kumi. Lakini ukweli ni kwamba Ballali ametangulia, ushahidi wa EPA umekufa, na imani ya watu kwa serikali imekufa!
+447853850425
ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
source:
http://www.freemedia.co.tz/daima/2008/5/25/makala2.php
Kama RA vile