Wanajamvi hebu tujikumbushe kidogo tulitokea wapi na tunaelekea wapi;
1.Tarehe 20 Desemba mwaka 2010 wakati Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika alipowasilisha bungeni hoja binafsi ya mabadiliko ya katiba mpya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alisema kuwa haiwezekani kuandikwa upya na badala yake kinachowezekana ni kuifanyia marekebisho iliyopo. Jaji Werema ambaye ndiye mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya kisheria aliweka msimamo wake huo katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam katika hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande.
2. Aliyekuwa Waziri wa Sheria wakati huo, Celina Kombaine, akimuunga mkono mwanasheria mkuu, naye alidai kutokuwepo na umuhimu wa kuwepo katiba mpya na kwamba Serikali inaridhika na utaratibu uliopo wa kuifanyia katiba hiyo marekebisho ya mara kwa mara pindi umuhimu wa kufanya hivyo unapokuwapo. Alisema hayo mara baada ya kuhudhuria kikao cha baraza jipya la mawaziri kilichofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete na kuongeza kwamba wale wanaodai katiba mpya ni watu wa barabarani wasiokuwa na uelewa juu ya masuala hayo.
Nimetoa mifano hii miwili kwa lengo moja tu kuonesha kwamba kabla ya mswada binafsi wa Mbunge wa Ubungo kuwasilishwa bungeni, hakuna ushahidi wowote unaoonesha kwamba upatikanaji wa katiba mpya uliwahi kuwa sera, ilani au ajenda ya chama tawala wala serikali yake. Kwa ufupi ni kwamba madai yoyote kuhusu katiba mpya kama kawaida yalipuuzwa na kubezwa kila yalipotolewa na wananchi wema walioweza kuona dira ya wapi tunakotoka na wapi tunataka kufika.
Kama mlivyoshuhudia hapo juu kauli hizo mbili zilitolewa kwenye
viwanja vya Ikulu na vilitolewa baada ya ama shughuli au vikao rasmi vilivyosimamiwa na Raisi Jakaya Kikwete. Si hayo tu, miongoni wa ama waliohudhuria au waliotoa kauli hizo ni pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Sheria na Jaji Mkuu wa Mahakama nchini. Pamoja na hayo, matamko haya yalitolewa wakati ambapo msimamo wa chama tawala, CCM, ulijulikana kuhusu swala zima la katiba mpya.
Swali linalojitokeza hapa kama anavyodokeza Mwanakijiji ni je, Kikwete alipata wapi madaraka ya kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba mpya ya JMT? Kama aliamua kama Raisi, kipengele gani cha katiba ya nchi kilimruhusu? Kama aliamua kama Mwenyekiti wa CCM, maamuzi ya kikao gani yalimruhusu? Kama aliamua kama Mkuu wa serikali, je Baraza la Mawaziri lilishirikishwa? Okay, wapo watakaodai kama Raisi hahitaji ruhusa, kama ni hivyo huu mchakato ni haramu!
Hii nchi haiendeshwi kidikteta, ni nchi ya kidemokrasia inayoendeshwa kulingana na matakwa ya katiba iliyopo ambayo yeye kama Raisi aliapa kuilinda na kuitetea. Katiba ya nchi si jambo dogo, katiba ni sheria mama na ni katiba hiyo hiyo ndiyo inampa mamlaka Raisi pamoja na serikali anayoisimamia. Kuuacha mchakato wa katiba mikononi mwa mtu ambaye kwa kiwango chochote kile ameonesha udhaifu mkubwa katika kusimamia mambo ya msingi bila kuyumba ni kujitafutia balaa.
Mfano wa udhaifu ninaouongelea ni kama huu wa sintofahamu uliojitokeza sasa wa kutoweza kutoa maamuzi mara moja kuhusu mswada uliopitishwa na Bunge uliogubikwa na utata. Raisi alitakiwa awe anafuatilia kwa makini sana huu mjadala mzito ndani na nje ya Bunge hata kama angekuwa hayupo nchini. Wakati mwingine msimamo wa Raisi hutakiwa kutolewa mapema hata kabla ya mswada kumfikia kama ataukubali au la kulingana na hoja zinavyotolewa bungeni.
Hapana, kwa mtindo huu hatufiki na kama hatukujifunza kwa majirani zetu Kenya nguvu ya Umma ulipokataa rasimu iliyofikishwa kwao kwa njia ya kura ya maoni, basi hatuna tofauti na mbuni. Katiba ni ya wananchi na wao ndio watakuwa waamuzi wa mwisho kama wataafiki kitakacholetwa mbele yao au wataikataa...naomba kunukuu sehemu ya utangulizikatika misingi ya katiba yetu ya sasa inavyotamka;
KWA HIYO, BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BUNGE MAALUM LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, kwa niaba ya Wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.
Mungu ibariki Tanzania.