Wenzetu Watanganyika washalitumbua jipu, sasa ni zamu yetu Wazanzibari kuukamua usaha mpaka tuufikie moyo wake na kuliponya moja kwa moja jeraha.
Ingefaa tuwaulize wenzetu, kama wao wameumia mno kwa kuona uhuru na rasilimali zao zimeingia hatarini kwa mkataba mmoja TU wa bandari, wanadhani wametuumiza kwa kiasi gani sisi wenzao kwa miaka 60 yote hii tangu walipoupora uhuru na mamlaka yetu YOTE na kutudumaza kiustawi kwa kutufungia njia kuu za kiuchumi.
Wanaumia kuona Mzanzibari anakuwa rais wa Tanzania hata kama ni kisheria na kikatiba, wakati wao wamejipa mamlaka ya kimabavu, kwa miaka yote hii ya kutupangia nani atuongoze Wazanzibari na kwa mipaka gani ya mamlaka!
Tuwathibitishie kwamba iwe iwavyo, sasa tumeshabaini bila chembe ya shaka, kwa yaliyotoka kwenye ndimi zao, kwamba wana chuki kubwa dhidi ya Uarabu na Uislamu na kwamba chuki hizo ndizo zilizochangia pia kutubana tusifurukute ndani ya 'muungano'; na ndio maana kina Lukuvi na Sitta hawakuulizwa chochote na yeyote waliponena waliyoyanena dhidi ya Uarabu na Uislamu, kwa sababu waliwasilisha na kuwakilisha mtazamo rasmi wa Tanganyika kuhusiana na Wazanzibari katika muungano.
Na kwa hapa tulipofika tukubaliane kwamba, kama ni kuuendeleza muungano, basi hakuna mbadala mwingine wa mahusiano yetu ya kisiasa na Watanganyika isipokuwa kufuta kwanza jina Tanzania na kurudi kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuamua ama kuwa na muungano wa mkataba au wa serikali tatu. Ghairi ya hivyo ni kila nchi kurudi kwenye asili yake ya taifa na nchi kamili