Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Rais Samia Suluhu Hassan amewahutubia wazee wa Dar es Salaam leo Desemba 2. Kiini cha ujumbe wake kilikuwa ni maandamano yaliyofanyika Oktoba 29, 2025. Kwa kiasi kikubwa hotuba yake ni kama alikuja kutema nyongo iliyomjaa kifuani pake.
Ameeleza chanzo cha maandamano na vurugu zilizoanza Oktoba 29 na kuendelea zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, akisema ni ya kupanga. Kwamba kuna watu walipanga kufanya vurugu kwa lengo la kuvuruga Amani na umoja wa Watanzania.
Kwamba waliopanga na kutekeleza maandamano walilipwa. Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kusema hivyo, amekuwa akirudia mara kwa mara kwamba vijana walioandamana walilipwa
Amewataja waliofanikisha maandamano hayo kuwa pamoja na vyama vya upinzani, akisema baadhi ya wapinzani (hakutaja chama) aliwakuta katika hali mbaya wakiwa wamekimbilia ughaibuni, lakini aliwarejesha na kuwapa misaada ya fedha zake.
Kwa vijana amesema hawakuwa na sababu ya kuandamana kwani ukilinganisha na nchi nyingine, vijana wa Tanzania hawana shida za kuwafanya waandamane.
Amegusia pia dini, akikosoa madhehebu yanayomkosoa, kwamba yana watu wanaopingana wao kwa wao.
Kuhusu nguvu zilizotumiwa na vyombo vya Dola, Rais Samia amesema nguvu iliyotumika ni sawa na vurugu zilizovyokuwa ili kulinda Serikali isije ikapinduliwa na waandamanaji.
Maelezo haya yote, Rais Samia anayatoa wakati tayari ameshaunda Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea Oktoba 29 inayoongozwa na Jaji mstaafu Mohamed Othman Chande. Sasa kama ndivyo anavyoamini hivyo, tume hiyo inakwenda kuchunguza nini?
Kwa sababu tume ile imeundwa na Rais, maana yake aliyeiunda hajui chanzo, sababu na nani waliotekeleza vurugu zile. Lakini anapokuja na maelezo yote haya, maana yake ameshathibitisha chanzo na wahusika wa vurugu zile.
Kwa hiyo Tume ya Jaji Chande inakwenda kufanya kuchunguza kitu gani ambacho hakijulikani? Je, kikileta matokeo tofauti na kile anachoamini Rais Saia, atakubaliana nayo? Atakubaliana na mapendekezo ya tume?
Kwa maana nyingine huu ni upotevu mkubwa wa fedha za umma kwa kuunda tume ambayo inachunguza kile ambacho Rais ana majibu yake. Wazee wale watalipwa posho, watalipwa usafiri, watasumbua watu kuuliza maswali, lakini mwenye tume yake tayari ana majibu.
Ndio maana watu wameshakosoa uhalali wa tume hiyo, kwa kuwa hata Rais Samia mwenyewe anapaswa kuchunguzwa. Hakuna kitu cha maana kitakacholetwa kama matokeo ya maana.
Wakati akiunda tume hiyo, Rais Samia alisema matokeo yake ndiyo yatasaidia mchakato wa maridhiano, lakini kwenye hotuba yake la leo, anasema Serikali yake haipewi masharti ya maridhiano. Sasa hayo yatakuwa maridhiano au maigizo? Utaridhiana vipi na mtu usiyetaka kusikiliza?
Ni lazima kila upande uje na madai yake na katikati awepo msuluhishi. Kama Serikali inaridhiana na wakati huo huo inajifanya kuwa msuluhishi, ni wazi haki haitatendeka.
Vinginevyo Rais atangaze tu kwamba, Serikali yake inaendeshwa kijeshi, haitaki kupata maoni yoyote ya vyama vya upinzani, au asasi za kiraia au wananchi wa kawaida. Ijulikane tu kwamba Tanzania ni nchi ya kidikteta, kwamba wananchi wakitoa maoni yao kwa maandamano au kwa vyombo vya habari watakabiliwa kwa nguvu kali za kijeshi, kwa madai kwamba walitaka kupindua Serikali.
Pia Soma: Rais Samia aunda Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi 2025