Ndugu wanabodi,
Leo nawarudisha nyuma ambako siku zote za mijadala hapa JF tumejaribu sana kuepuka swali hili. Pengine zipo mada zinazofanana na swali hili lakini bado kabisa tumekuwa tukiepa sana kutoa majibu kwa sababu linatugusa moja kwa moja na wakosa ni sisi wenyewe japokuwa kwa mila na desturi za Mtanzania tunaamini kwamba matokeo mabaya ya matarajio yetu lazima kuna mkono wa mtu sii bure.
Hivi kweli tumewahi jiuliza kwa nini sisi maskini? na kama sisi maskini tumewahi tafakari kwa undani zaidi tumefika fikaje hapa tulipo ili tupate ufumbuzi wa matatizo yetu maana tumeimba sana nyimbo, hadithi na ngonjela zinazohusiana na maadui zetu wakubwa Ujnga , Umaskini na Maradhi lakini ukweli ni kwamba jitihada ndogo sana zimetumika kuelekeza mapambano yetu ktk maadui hao. Tunatumia mabillioni ya fedha ktk miradi ambayo hailengi kutuondoa hapo tulipokwama bali tunatarajia kuongeza kasi ya mwendo wakati tumekwama na gari letu la maendeleo haliendi popote..
Baada ya kuwa mwanajanvi wa JF kwa muda mrefu sana, kusoma mabandiko mbalimbali na kusoma makala za magazeti, mawazo ya wasomi wetu na kadhalika nimegundua kitu kimoja ya kwamba sisi Watanzania - We are into denial..Ni maskini lakini hatudhani kama sisi ni maskini kweli na tumejenga fikra za kwamba MTU akifanya kazi kwa bidiii kubwa bila shaka ataweza kufanikiwa kutokana na umaskini. Lakini tunasahau kwamba Umaskini ni stage ya mtu kukwama ktk hali na mali na mbinu zinazotumika hapa ni tofauti kabisa na zile za kuendelea mbele. Sasa unapoweka nguvu kubwa ktk uzalishaji kweli unaweza kujiondoa ktk umaskini hali umaskini unatokana na sababu zake kama vile gari lililokwama tunatakiwa kutazama limekwamba wapi Je, ktk tope, mchanga au shimo na ndipo tutafahamu jinsi ya kujikwamua na sii kukanyaga mafuta kuongeza kasi. Magurudumu yatazunguka tu hatutatoka hapo tulipokwama.
MTU, hili neno pekee linajenga Ubinafsi na kubomoa nguvu ya jumla, inavunja Utaifa na kuelekeza mapambano haya kwa fikra za kila mmoja wetu atachunga mzigo wake kama abiria walikosa matumaini ya usafiri baada ya gari lao kukwama na hivyo kila mmoja wao atafute usafiri wake..Fikra hizi za kila mmoja atafute usafiri wake, ndicho kinachofanyika nchini na ndio sababu tumeshindwa kutoka ktk umaskini maana sote tumeliacha gari la Taifa lilipokwama na kila mmoja wetu anatazama usafiri wake hali tuko katikati ya msitu na pasipo dira..na maskini ya Mungu hatufahamu tunaelekea wapi. Ni kweli kabisa kwamba uongozi mbaya ndio ulotupeleka ktk korongo hili la umaskini na tumekwama lakini sio uongozi mbaya unaotufanya tuchukue maamuzi ya kila mtu abebe msalaba wake..
Je, tunafikiri fikra za kwamba tukipata kiongozi au uongozi mzuri tutaweza kujinasua ktk umaskini tulipokwama? na huyu kiongozi au viongozi wanatakiwa wawe na moyo gani, wananchi wenyewe wanaweka matumaini yapio ikiwa leo kila mmoja wetu anadai maisha magumu aongezewe mshahara na posho ili hali wanajua fika kwamba tumekwama sote. Hivi kweli ikiwa wabunge kujiongezea posho ni makosa basi yatulazimu sisi wote tuombe raha hizo sawa na wao japokuwa tunajua fika kwamba wanayodai viongozi wetu ni makosa makubwa na ndizo sababu zinazotuweka ktk umaskini?..Ndizo sababu zinazotufanya tuwatake waondoke ktk madaraka na mageuzi ya kweli lazima yazingatie kwanza kwamba tumekwama na uzalendo unatakiwa kwanza.
Watanzania wenzangu ifike mahala tufikirie tumetoka wapi na tumekwama wapi, badala ya kuendelea kufikiria tunakwenda wapi.. Tanzania tumekwama ktk umaskini na tumeshindwa kutoka ktk umaskini. Na kibaya zaidi ni kwamba - WE CAN"T HANDLE THE TRUTH!.. bado tupo ktk kuamini kutoamini kwamba tuna watu wachache sana WAZURI (A few good men) ktk ngazi zote za uongozi na uwajibikaji kuweka Uzalendo mbele ya kila kitu. Hivi kweli Utawala wa leo toka Azimio la Zanzibar wamekosa aibu kabisa ya kufikiria Ufisadi mkubwa wanaoufanya kwa wananchi wao huku wakiendesha siasa za chuki baina ya watanzania kwa kutumia mapungufu ya Mtanzania huyo (ujinga, umaskini na maradhi) kama nyenzo ya kumuumiza zaidi.
Tuna msemo wa kwamba TAIFA MBELE? hivi tunaposema Taifa kwanza huwa tuna maana gani? Ni vitu gani vinatangulia ktk kulinda maslahi ya Taifa hadi tuseme TAIFA kwanza hali nafsi zetu zimegawanyika ktk makundi ya Ukabila, dini, rangi wanawake na wanaume, vyama na kadhalika. Hivi tunaposema Utaifa kwanza huwa tunatazama sifa zipi za uzalendo ikiwa kila mmoja wetu anatafuta riziki yake, anapanga malengo yake kwa manufaa ya maslahi yake ikiwa ni haki yake ya kuzaliwa na kama mtu huru?. Nini maana na kipimo cha UTU wa kila mmoja wetu ktk Utaifa wetu na huu utaifa unatokana na mipaka gani?.
Wanabodi lazima tukubali ukweli uliosimama ya kwamba tumeshindwa!...TUMESHINDWA!... na hakuna njia bora zaidi ya kufikiria - Ikiwa kweli tumeshindwa, je tulikosea wapi?... Mada nyingi sana hapa JF zinazungumzia sana matumizi mabaya ya mamlaka kwa viongozi wetu lakini katu tumeshindwa kujitazama sisi wenyewe sote kama ni MASIKINI na tumekwama ktk umaskini kama Taifa na sii mtu au kundi la watu pekee.. Vita ya kujikomboa kutokana na umaskini, ujinga na maradhi imekuwa sii vita ya kitaifa japokuwa tunasema na kulalama siku zote kwamba sisi ni Maskini.
Ebu tufikirie mfano mmoja mdogo sana ktk kutazama mbinu za kidunia ktk ubunifu. Leo hii Somalia wako ktk matatizo makubwa ya Ukame (drought and famine) na wamekwama... Hivi kweli itakuwa busara kwao leo kufikiria kupambana na matatizo haya ya ukame inatakiwa regime change?.. au kila mmoja wao atie nguvu ktk uzalishaji. Kama ndivyo tumewahi jiuliza kwa nini Somalia imeshindwa kuondokana na vita kwa zaidi ya miaka 20 sasa hivi hadi wamefikia hapo walipo!...
- Je, kumpata kiongozi bora inaweza kuwaondolea njaa na ukame ili hali regime change na nguvu ya kumtafuta kiongozi bora zaidi ndio chanzo cha mtafaruku baina yao toka aondolewe Siad Barre na leo wamefikia hapo walipo?..
- Je, sii kweli kwamba ukame ni matokeo ya vita ambayo imetokana na kupoteza UZALENDO unaomfanya kila mmoja wao kuto heshimu na kuwajibika kwa taifa lake kwanza. Somalia wamekwama na hawataweza kujikwamua hata siku moja kama hawatarudi nyuma na kutazama jinsi gani walipoteza Utaifa wao.
Kwa hiyo, wanabodi tuumize vichwa vyetu kutazama tumekwama wapi na sababu zipi zilizotukwamisha na sii wapi tunakwenda ama tunataka kwenda. Ni imani yangu kwamba siku tuloomba Uhuru tulijua fika tunataka kwenda wapi na nadhani hakuna shida ya leo kujua tunataka kwenda wap bvali kuondoka ktk shimo hili la umaskini tulipokwama. Ni lazima tukubali vichwani mwetu kwamba tumekwama ili tupate kufikiria na kutunga mbinu zote za ujasiri, mhanga na uzalendo zilenge ktk kujinasua ktk shimo hili.
Hao Somalia leo hawawezi kufikiria kutafuta chakula kilichopikwa na chef toka hotel za nyota tano kama suluhisho la ukame. Itakuwa ujinga na ulimbukeni mkubwa sana lna bahati mbaya sisi Watanzania tunajaribu sana kutafuta suluhisho la umaskini wetu kwa kutafuta vitu kutoka nyota tano, kutafuta ushauri wa ki nyota tano bila kujali kwamba tumekwama. Huu ni ulimbukenii wa kuficha uchafu wetu wenyewe, ni ulimbukeni wa kujisitir aibu na kamwe hatuwezi kupambana na imaskini kwa majigambo na usanii wa kuweka viraka ktk nguo iliyochakaa. Watanzania wenzangu hatuwezi ondokana na Ujinga umaskini na maradhi ikiwa vita hii ni ya mtu mmoja mmoja kwa fikra kwamba umaskini wetu ni wakujitakia, kila mmoja wetu atabeba msalaba wake wa matatizo.
Sio Ufisadi wala uongozi mbaya ndizo sababu kubwa, bali haya yote ni matokeo ya upungufu ktk imani inayomjenga mtu mmoja mmoja kujinasua ktk lindi la Umaskini, hivyo ktk jitihada za kujikomboa tunajikuta tunakanyagana hovyo kila mmoja wetu akitaka atoke yeye kwanza utafikiri kaa wa bahari waliowekwa ktk kapu wakisubiri kutiwa ktk sufuria la maji ya moto.
Hivi kweli watumishi wa umma hasa wataalam na mabingwa wetu wanaolipwa mshahara chini ya mil 2 lakini hupewa nyumba, wasilipe maji na umeme, wamepewa fursa ya kufanya biashara nje ya ajira walizoajiriwa wakijenga conflict of interest kiutawala kwa taaluma zao ili kujineemesha bado wana haki ya ki UTU kudai wao malipo zaidi kutokana na ugumu wa maisha japokuwa wanajua fika kwamba Tanzania ni nchi maskini na tumekwama kt umaskini. Viongozi wetu ngazi zote za kijamii tafadhali lihurumieni Taifa letu, wahurumieni waja wenu walipa kodi maana mnawaweka ktk nafasi ngumu sana ya kufikia maamuzi ya kinyama maana tofauti baina ya binadamu na mnyama kifikra ni ndogo sana..