Ahsante Mengi kwa kulisema hili. Ngonjera za CCM kwamba Tanzania ni nchi maskini hazikubaliki tena. Tunaona viongozi uchwara wakifanya ufisadi wa hali ya juu na kuwa mabilionea. Tunaona makampuni makubwa toka nchi za magharibi "yakiwekeza" au kutaka kufanya hivyo katika sekta mbali mbali ili wajipatie faida. Hivyo hili la Tanzania ni maskini halikubaliki tena na hatutaki kulisikia. Tunataka kuona utajiri wa Tanzania unawanufaisha Watanzania walio wengi.
Mengi:Tanzania ni tajiri lakini wananchi ni maskini
2008-03-18
Na Joseph Mwendapole
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi, amesema Tanzania sio maskini ila wananchi wake ndio wanakabiliwa na changamoto ya umaskini.
Aliyasema hayo jana ofisini kwake wakati akizungumza na wanafunzi wa Shahada ya Pili kutoka Chuo Kikuu cha PACE kilichoko katika mji wa New York, Marekani.
Wanafunzi hao 15, wanaosomea masuala ya biashara, walimtembelea Bw. Mengi ofisini kwake kupata uzoefu na mbinu mbalimbali za kufanya biashara.
``Tutofautishe umaskini wa watu na wa nchi, watu wakiwa maskini huwezi kusema nchi ni maskini na kwa imani yangu, Tanzania ni nchi tajiri ila wananchi wake ni maskini,`` alisema.
Bw. Mengi aliwataka wanafunzi hao kuyaona matatizo wanayokabiliana nayo kama changamoto na kufikiri namna ya kujikwamua.
Alisema mtu akiyachukulia matatizo kama changamoto, anatafuta mbinu za kukabiliana nayo na hatimaye kuondokana nayo kabisa.
``Ukiona changamoto ukasema ni tatizo litakaa begani kwako siku zote lakini ukilichukulia kama changamoto, utafanikiwa na wengi waliojaribu hivyo wamefanikiwa,`` alisema na kuongeza kuwa yeye binafsi hakuona umaskini kama tatizo bali changamoto aliyojitahidi kukabiliana nayo.
Bw. Mengi pia alielezea siri ya mafanikio yake kuwa ni kumwamini Mungu na aliwashauri kumweka mbele katika kila jambo wanalofanya.
Alisema licha ya kumweka Mungu mbele, wanapaswa pia kujiamini kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa kama wengine waliofanikiwa.
``Kila ukiamka, muombe Mungu na useme ninaweza, nitaweza lazima nitaweza,`` alisema na kuongeza kuwa, mafanikio yake yametokana na kujiamini na kumtanguliza Mungu mbele.
Bw. Mengi ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda na Biashara (CTI), alisema wakati anaanza biashara, hakuwa na mtaji kabisa lakini alijitahidi kukopa na kuanza kutengeneza kalamu nyumbani kwake.
Alisema woga ni adui mkubwa katika biashara na imekuwa ikisababisha watu wengi kushindwa kabla ya kuanza.
Aidha, aliwaasa wanafunzi hao kukumbuka kusaidia jamii watakapopata fedha na kwamba hiyo ndio njia pekee ya kurudisha shukrani kwa Mungu na kwa wananchi.
``Ukifa hutaulizwa mali uliyojilimbikizia bali namna ulivyoitumia kusaidia wenye shida, kwa hiyo mkipata mjitahidi kusaidia wenye shida,`` alisema.
Kwa upande wake, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Bw. Daudi Mwakawogo, alipongeza jitihada za Bw. Mengi katika kupambana na rushwa.
Alisema Bw. Mengi amekuwa akitoa misaada bila ubaguzi wowote na kwamba amekuwa akisaidia waumini wa dini mbalimbali.
Alimwelezea kuwa ni mwanamazingira aliye mstari wa mbele na kwamba mpaka sasa amewezesha kupanda miti milioni 23 hapa nchini.
SOURCE: Nipashe