Tanzania na laana ya rasilimali
JAMHURI ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) imetumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kutokana na utajiri wake wa rasilimali, yakiwemo madini aina ya coltan, yenye kutumika kutengenezea simu na kompyuta.
Aina hizo za madini yenye kutumika kutengenezea vifaa vya Kinshasa vya kielekroniki yameguliwa hivi karibuni nchini pia, ni katika Kijiji cha Ngualla, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.
Mafuta, almasi na dhahabu nayo yamegeuka kuwa laana kwa mataifa mbali mbali barani Afrika yakiwemo Nigeria, Sudan ya Kusini, Siera Lion, Somali na Angola.
Baada ya kugunduliwa kwa rasilimali gesi nchini katika miaka ya hivi karibuni, Wataalamu wa uchumi na maendeleo wanajiuliza,
"Jee, gesi na madini kuwa Neema au laana kwa Tanzania na nchi zingine tajiri wa rasilimali barani Afrika!"
Profesa wa Uchumi wa Maendeleo (development economics), katika Shule ya Biashara, Uchumi na Sheria, Chuo Kikuu cha Gothenburg nchini Sweden, Ola Olsson anaiangali neema iliyolishukia Bara la Afrika katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, katika jicho la jinsi rasilimali hizo zitakavyotumika kujenga uchumi endelevu na kujitegemea kwa mataifa hayo, na sio kunufaisha kikundi kidogo cha watawala.
Prof. Olsson alitoa mtazamo wake huo hivi karibuni katika Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Mpango wa Mazingira kwa Maendeleo Endelevu (EFD Policy Day) wakati akitoa mada kuhusu Siasa ya Uchumi ya uendelezaji rasilimali (Political Economy of Natural Resource Exploitation) uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.
Kufanikiwa katika matumizi ya rasilimali yenye tija kwa taifa na wananchi wake, jambo moja la msingi lazima lifanyike, na kwa mujibu wa Profesa huyo wa Uchumi wa Maendeleo, inatakiwa kuwepo kwa uwazi katika mfumo nzima wa uendelezaji rasilimali hizo.
"Transparency is crucial to avoid devastating scenarios. Governments should publish all revenues, whereas firms should publish all payments they make to governments for natural resources. So the people can judge whether revenues are used for sustainable development," anasema Prof. Olsson katika mada yake ya uwazi msingi kwa ukuaji endelevu na uhuru kwa Afrika.
Tafsiri isiyo rasmi, Prof Olsson anasema uwazi ni jambo la msingi kukwepa kutumbukia katika majanga mbali mbali yatokanayo na uchimbaji rasilimali. Serikali lazima zitangaze mapato yote, vile vile makapuni nayo lazima yatangaze malipo yote wanayotoa serikalini kutokana na mapato yatokanayo na rasilimali. Ili watu waweze kuamua iwapo mapato hayo yanatumika kwa maendeleo endelevu.
Kukosekana kwa uwazi katika uendelezaji wa rasilimali, mapato na matumizi yake inaelezwa kuwa msingi wa migogoro inayoibuka na kuendelea kuwepo katika nchi nyingi za Kiafrika zenye rasilimali, yote ikitokana na uchu wa kumiliki mapato yatokanayo na rasilimali hizo kwa manufaa binafsi.
Mapigano yanayotokana na rasilimali hizo ni kwa maslahi binafsi na sio maendeleo ya taifa na watu wake, na hatimaye kuibuka kwa vikundi vya kiharamia, ambavyo hutumia mgongo wa wananchi, kwamba vinapigania maslahi ya wananchi wakati ukweli ni kwamba vinapigania maslahi yao binafsi.
Prof. Olsson anaamini kuwa Tanzania kwa sasa inayo mifumo imara, na kwamba nchi yenye mifumo imara huwa na demokrasia bora na utawala bora.
Nani amiliki rasilimali nchini;
Pamoja na uwepo wa mifumo bora, Profesa huyo wa Uchumi wa Maendeleo anashauri njia iliyo bora katika umiliki wa rasilimali hiyo, na anaitaja ushirika wa pamoja wa Watanzania na makampuni ya nje (joint venture).
Mtaalamu huyo ambaye pia ni mshauri wa Benki ya Dunia anasema ni hatari kuyaachia kuyaachia makampuni am kubwa ya kimataifa pekee kuendeleza sekta hiyo, kutokana na utamaduni wa makampuni duniani wa kuzingatia zaidi utengezaji faida maradufu.
Mfumo huo sio mpya, ndio unaotumika na mataifa makubwa dunia pamoja na ule wa dola. Uchuguzi unaonyesha kuwa umiliki wa makampuni kumi makubwa dunia ni ama, umma au serikali (public or state ownership).
Ni kweli gesi kuibadili Tanzania !!
Kugunduliwa kwa gesi nchini kumebadili mitazamo ya watu, hususani viongozi, wengi wakiutazama ugunduzi huo kama dawa pekee ya umasikini uliopo, kwamba gesi iliyogunduliwa itaweza kuibadili nchi ndani ya kipindi kifupi.
Mwananchi mmoja wa mjini Mtwara, akitoa ushuhuda wa vurugu zilizojitokeza baada ya kuanza mchakato wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda jijini Dar es Salaam, aliwalaumu baadhi ya viongozi wa juu nchini akisema waliwaeleza kuwa gesi iliyopatikana kwenye bahari huko Kusini kuibadili Mtwara, itakuwa kama Dubai ndani ya muda mfupi.
Mtazamo huo unaweka matumaini yote kwenye rasilimali hiyo ya gesi, na ni mtazamo ambao unawalemaza wananchi, ambapo hutelekeza shughuli zao za kiuchumi wakiamini kuna utajiri wa gesi, hivyo hawana haja ya kuhangaika tena.
Mkurugenzi Mkuu wa Mpango wa Mazigira kwa Maendeleo Endelevu (Environmental for Development EFD), Prof Gunnar Kohlin anatahadharisha dhidi ya mtazamo huo, akisema gesi pekee haiwezi ibadili Tanzania, bali itafanya vizuri zaidi kwa kutumia vyanzo vingine vya uchumi, akitumia mfano wa nishati ya umeme ambapo anasema bado umeme uzalishwao kutokana na maji, jotoardhi, upepo na jua unao nafasi katika uchumi wa nchi.
Pamoja na tahadhari hiyo dhidi ya utekelezaji wa nyanja zingine za kiuchumi kwa sababu tu ya kupatikana kwa gesi, Prof. Gunnar pia anatahadharisha juu ya kasi katika utafutaji na uchimbaji gesi, akisema ni vema uendelezaji gesi nchini ukafanywa taratibu na kwa awamu.
"It is wise to do it slowly, no need of rush," anasema Prof. Gunnar katika mahojiano yake na Raia Mwema.
Mtazamo wa utegemezi katika rasilimali gesi unachangiwa zaidi na soko la bidhaa hiyo duniani, ambapo nchi za Kiafrika huendelea kuwa wasafirishaji wa malighafi na wapokeaji wa malipo yatolewayo na wanunuzi.
Kutokana na utamaduni huo, ukuaji wa uchumi wa nchi za Kiafrika, Tanzania ikiwemo, hutegemea zaidi bei kwa rasilimali zake katika soko la dunia ambalo ndilo huamua bei ya kununulia. Na hapa ndipo Mtaalamu huyo wa Uchumi na Maendeleo, Olsson anapohoji,
"Nini kitatokea katika uchumi wa nchi hizi pale bei inapoporomoka!"
Ni wazi kwamba, mtazamo huo unaendeleza utegemezi wa nchi za Kiafrika kwa Mataifa yaliyoendelea yenye kuwekeza barani humu.
Mfano hai katika utegemezi wa bei ya soko la Dunia ni Zambia ambayo wakati bei ya shaba ilipokuwa juu uchumi wake ulikuwa imara, lakini ukaporomoka katika kasi ya kutisha baada ya kuporomoka kwa bei ya madini hayo katika soko la Dunia.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Rais, Mazingira, Dr. Binilith Mahenge, Tanzania inaendelea kujifunza kutokana na uzoefu wa nchi zingine ili kupata njia zilizo bora zaidi katika matumizi ya utajiri utokanao na rasilimali hiyo ya gesi.
Hatua ya serikali kutumia uzoefu wa mataifa mengine, ni katika kukabiliana na laana Itokanayo na uwepo wa utajiri wa rasimila, kama ilivyojitokeza katika mataifa yaliyotangulia kuendeleza rasilimali hiyo.
"Tunajifunza kutokana na uzoefu uliopo kwenye nchi zingine, tunafanyia kazi njia za kuepukana na tatizo hili," alisema Dr. Mahenge katika mahojiano na Raia Mwema alipotakiwa kuelezea mtazamo wa serikali katika kukabiliana na tatizo hilo maarufu kama "resource curse."
Chanzo: raiamwema