Tarehe: 15/04/2015 Tanzania ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa miongoni mwa nchi wanachana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni ya kumi na mbili kwa uchumi mkubwa barani Afrika. Kilimo ndiyo uti mgongo wa Taifa kikiajiri takribani nusu wananchi wake wenye uwezo wa kufanyakazi. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 34 ya watanzania wanaishi katika mstari wa umaskini. Nchi imekuwa katika mapinduzi ya kiuchumi tangu mwaka 1985 ambapo Tanzania inaachana na uchumi unaomilikiwa na dola na kuacha uchumi umilikiwe na soko. Tanzania ina ukubwa wa km2 947,303, ikiwa na watu milioni 47.4 kwa mujibu wa takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2014. Taarifa za Wikipedia kuhusu uchumi wa Tanzania zinasema, pato la taifa kwa mwaka 2014 limetajwa kuwa Dola za Kimarekani Bilioni 41.33 huku kipato cha mtu mmoja mmoja ni Dola 1,813 kwa mwaka. Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio kadhaa vya utalii ikiwa na pamoja na mlima mrefu kuliko yote barani Afrika, Mlima Kilimanjaro. Pia ina Ziwa Tanganyika linaloaminika kuwa na urefu kuliko yote barani Afrika. Vilevile Ziwa Victoria na Nyasa yanayoaminika kuwa miongoni mwa maziwa makubwa barani Afrika yanapatikana Tanzania. Kuna mito kadhaa mikubwa, maporomoko ya ardhi, majumba ya makumbusho, mbuga za wanyama, majengo ya kihistoria katika miji ya Bagamoyo, Kilwa, Zanzibar na kwingineko. Haya yote yanaweza kuvutia mamilioni ya watalii toka kona mbalimbali za dunia na kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni. Kwa mfano, mwaka 2012 Tanzania ilipokea watalii 1.043.000 ambao waliingizia taifa Sh bilioni 56. Hivyo, licha ya kuchangia fedha kwenye pato la taifa, kama utatangazwa ipasavyo utalii unaweza kutoa mchango mkubwa katika ukuaji uchumi wa taifa na kutoa fursa nyingi zaidi za ajira kwa vijana. Tanzania pia ina utajiri mkubwa wa madini ya aina mbalimbali yakiwemo yanayopatikana Tanzania pekee yaani madini ya Tanzanaiti. Kadhalika, chuma na makaa ya mawe yamethibitika kuwepo sehemu mbalimbali ya ardhi ya Tanzania. Taifa linaweza pia kunufaika na madini ya Urani katika kutekeleza shughuli zake za maendeleo. Ikiwa inapak ana na nchi zisizo na bahari yaani (Land Locked Countries) kama DRC, Malawi, Zambia, Zimbabwe nk Tanzania inayo nafasi kubwa ya kunufaika kiuchumi kwa kutumia fursa ya kuwa na bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Zanzibar. Nchi hizo hutumia bandari nchini Tanzania kupitishia mizigo yake toka ughaibuni na kadhalika kusafirisha ngambo mazao yanayozalishwa nchini mwao hivyo kutoa nafasi ya nchi kunufaika kiuchumi. Ripoti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ya Novemba 2013, Tanzania ina ekari milioni 44 zinazofaa kwa kilimo. Kati ya hizo, ekari milioni 14 zinazolimwa na wakulima wadogo huku ekari milioni 1.5 zinatumika kwa kilimo cha biashara. Taarifa toka Mpango wa Taifa wa Umwagiliaji yaani (National Irrigation Master Plan) zinasema kuwa jumla ya ekari milioni 29.4 zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Taarifa hiyo inasema hata hivyo, ni ekari 450,392 tu sawa na asilimia 1.53 zinazotumika hivi sasa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini. Licha ya viwanda kuchangia asilimia 22.2 ya pato la taifa viwanda vingi hivi sasa vimekufa na vinavyoendelea kubinafsishwa kwa wageni hugeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia bidhaa huku mashine na mitambo ikiuzwa kwenye chuma chakavu. Hali hii imefanya malighafi za viwanda zinazozalishwa nchini zisafirishwe kwa ajili ya matumizi ya viwanda nje ya nchi hali inayochangia pia uduni wa bei ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi. Takwimu za sensa ya mifugo ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Tanzania ina ngombe 21,400,889. Ngombe 21,125,251 wanafugwa na wakulima wadogowadogo Tanzania Bara huku 155,624 wakifugwa na wafugaji kama hao Zanzibar. Ngombe wengine 120,014 wanafugwa kwenye mashamba makubwa yaliyopo Tanzania Bara. Takwimu za Sensa ya Mifugo za mwaka 2008, Tanzania ina mbuzi 15,085,150 huku idadi ya kondoo ikiwa ni 5,715,549. Mapinduzi makubwa katika matumizi ya mazao ya mifugo kama nyama, ngozi, sufu, kwato na kadhalika yanahitajika nchini ili kutoa fursa ya sekta hii kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na mendeleo ya Taifa. Jambo ambalo hadi sasa watanzania linawatatiza na kuibua dukuduku la kutaka kufahamu Zaidi ni kuwa licha ya fursa zilizopo, zilizotajwa hapa kwa ufupi na nyingine ambazo hatujaweza kuzitaja: KWA NINI TANZANIA BADO NI MASKINI???
Jumatano April 15 saa nne usiku katika kituo cha Channel Ten atakuwepo Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi) David Kafulila na wageni wengine kujadili mada hii kupitia kipindi kipya cha Mada Motto. usikose.
Jumatano April 15 saa nne usiku katika kituo cha Channel Ten atakuwepo Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi) David Kafulila na wageni wengine kujadili mada hii kupitia kipindi kipya cha Mada Motto. usikose.