Mheshimiwa njoo JF upate sababu:
* Asema anajiuliza swali hilo kila siku bila jibu
* Apinga fikra za siasa za ujamaa kuwa tatizo
* Aeleza mikakati ya kuimarisha sekta ya kilimo
*Akiri kuna kipengele katika madini hakimfurahishi
Na Waandishi Wetu (Mwananchi)
RAIS Jakaya Kikwete amesema haelewi ni kwa nini Tanzania bado ni fukara ingawa imejaliwa rasilimali nyingi za asili kuliko nchi nyingi za bara la Afrika.
Rais Kikwete aliyasema hayo Oktoba 4, mwaka huu mjini Paris Ufaransa katika mahojiano na Mhariri wa masuala ya Afrika wa gazeti la Financial Times, William Wallis na Mwandishi wa gazeti hilo,Tom Burgis.
"Hata mimi sielewi. Hili ni swali ambalo hata mimi huwa najiuliza kila siku, ni nini ambacho hatujafanya? Nafikiri tunaongoza barani Afrika katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini."
Alisema hata yeye haelewi ni kipi ambacho bado hakijafanywa ili kuifanya Tanzania kuwa katika nchi zenye maendeleo mazuri katika bara la Afrika.
"Lakini bado tunaendelea kuvutia uwekezaji katika sekta nyingine. Labda ujumbe bado haujafika vilivyo," alijibu Rais Kikwete alipoulizwa kwanini Tanzania bado ni masikini.
Alipoulizwa iwapo tatizo pengine bado ni kutawaliwa na mawazo ya kijamaa, Rais Kikwete alisema:
"Sidhani hilo kama bado ni tatizo. Uwekezaji mara nyingi unatoka sehemu moja kwenda nyingine. Labda wakati wetu utafika katika muda mfupi ujao."
Alipoulizwa juu ya utata wa vivutio vinavyotolewa katika sekta ya madini katika miaka ya nyuma, Rais Kikwete alisema hajui kama kuna utata wowote katika sekta hiyo.
Hata hivyo alikiri kuwa kulikuwa na kipengele kilichowaruhusu wawekezaji katika sekta hiyo kuendelea kudai kuwa wanapata hasara hivyo kila wanachozalisha wawekezaji katika sekta hiyo walitumia kipengele hicho kufidia 'hasara' hiyo.
Alisema kutokana na kipengele hicho wawekezaji walikuwa wakichukua chote walichozalisha bila kulipa kodi kwa madai ya kupata hasara na kwamba wenye mali (wananchi) hawakulindwa, na suala hivi sasa linajadiliwa kwa lengo la kurekebisha.
Alisema makampuni yote ya madini yamekubaliana na suala hilo kwa kuwa wameona kuna hoja ya msingi katika kumlinda mwenye mali inapotokea hasara.
Alipoulizwa iwapo anaridhika na malipo ya dola za kimarekani 200,000 kwa mwaka kama kodi kwa halmashauri migodi ilipo, Rais Kikwete alisema anakubaliana ingawa angependa malipo hayo kuongezwa ili kuwanufaisha zaidi wananchi wa maeneo husika.
Katika mahojiano hayo, Rais Kikwete alisema pamoja na kukua kwa michango ya sekta ya madini na utalii katika uchumi, msisitizo wa serikali ni kuibadilisha sekta ya kilimo ili itoe mchango mkubwa zaidi.
Alisema katika mkakati huo mabadiliko makubwa yatafanyika katika sekta hiyo kwa kuongeza kilimo cha umwagiliaji, kuongeza matumizi ya mbegu bora na utumiaji zaidi wa mbolea.
"Matumizi ya kawaida ya mbolea katika kilimo chetu kwa sasa ni ya chini mno ukilinganisha na nchi nyingine. Kwa mfano, sisi tunatumia kilo nane za mbolea kwa ekari moja ukilinganisha na kilo 577 kwa ekari zinzotumiwa nchini Uholanzi," alisisitiza Rais Kikwete.
Alisema katika mpango wa miaka saba wa kuboresha kilimo, mkazo pia unatiliwa katika kuwatumia wataalam wa kilimo kuwafundisha wakulima mbinu za kisasa za ukulima.
Aidha alisema pia kuwa mpango huo unaangalia masoko kwa ajili ya mazao yatakayozalishwa na wakulima na uimarishwaji wa miundombinu hasa barabara vijijini ili iwe rahisi kwa wakulima kupeleka mazao yao sokoni.
Mbali ya mpango huo kwa wakulima wadogo, Rais Kikwete pia alisema wanaangalia mpango wa kuwavutia wakulima wakubwa katika kilimo cha mazao ya biashara kwa kuweka vivutio vya kifedha.
Alisisitiza kuwa sekta ya utalii bado inaweza kuliingizia taifa fedha zaidi za kigeni kwa kuendeleza ujenzi wa hoteli zaidi katika fukwe na mbuga za wanyama ili kuwavutia watalii zaidi.
Katika mahojiano aliyoyafanya akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete alizungumzia masuala mbalimbali ikiwamo rushwa ndani ya CCM, vyama vya siasa nchini na utegemezi wa wafadhili katika bajeti unavyopungua mwaka hadi mwaka.
Pia alizungumzia kwa kirefu matatizo ya Zimbabwe na uhusiano katika mataifa ya Afrika na China na kuonyesha jinsi nchi hiyo ilivyo rahisi katika utoaji wa misaada ambayo haina masharti magumu kama zilivyo nchi za Magharibi na uwekezaji wa nchi hiyo katika Afrika.
Wakati huo huo, Joyce Mmasi anaripoti kwamba Rais Kikwete amesema ifikapo mwaka 2010 migodi yote ya madini nchini itakuwa inalipa kodi kikamilifu.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akihitimisha ziara yake ya wiki mbili nchini Marekani ambapo alikiri kuwa mikataba ya madini iliyosainiwa zamani ina mapungufu makubwa kutokana na walipa kodi kutolipa kodi ya maana.
Rais Kikwete ambaye aliripotiwa akiyasema hayo kupitia kituo cha Televisheni cha ITV cha jijini Dar es Salaam, alisema kutokana na kuwa mikataba ya zamani ina mapungufu, serikali itahakikisha inabadilisha mikataba mipya ili kuondoa mapungufu ya zamani.
"Wawekezaji wapya hawawezi kupewa mikataba kama ile ya zamani...sasa kama wapya wamepewa asilimia 15, basi hapa hakuna haja ya kuhangaika, huyo atakuwa amekiuka maagizo yangu, huyo mniachie mimi, hiyo ni kazi yangu."
Hata hivyo Rais Kikwete alisema, mipango ya serikali ni kupata asilimia 33 ya faida inayopatikana na akasema, "kama mgodi unapata dola 100, serikali itapata dola 33, hizi ni pesa nyingi na zitasaidia sana" alisema.
Alisema tayari wameanza katika baadhi ya migodi, na kuwa ifikapo 2010, migodi yote tangu ule mdogo mpaka ule mkubwa wa Bulyankulu utakuwa unalipa kodi kikamilifu.
"Tusingebadilisha hiyo mikataba, wenye migodi hiyo wasingelipa kodi mpaka mwisho wa uhai wa migodi hiyo, lakini serikali imeona na kuamua kuipitia upya," alisema.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema lazima tukubali kuwa Watanzania ni wachanga sana katika sekta ya madini na akasema ndio maana serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa haiporwi madini yake.