Wanadai wenyewe kuna Dunia Tatu. Nchi za dunia ya kwanza ni nchi ambazo zimeendelea, halafu kuna kundi la dunia ya pili ambalo ni nchi zinazoendelea na mwishoni ni nchi za dunia ya tatu, nchi masikini, nchi zenye maendeleo madogo na finyu.
Vipimo hivi hutokana na uwezo wa kirasilimali na kujitegemea kibajeti, kifedha na ubora wa maisha ya watu pamoja na mengineyo kama miundombinu, afya, elimu, ajira na hata mahusiano ya jamii.
Zaidi ni kufahamika kama nchi tajiri zenye kujitosheleza na nchi masikinin ambazo ni tegemezi kabisa na hazina uwezo wa kujitosheleza.
Sasa ni lini basi, Tanzania itakapoondoka kwenye kundi la nchi masikini zilizo na maendeleo kiduchu na hata kwenda daraja la kati la nchi zinazoendelea?
Kama vile katika watu kuna tabaka la juu, la kati na la chini kutokana na mapato na uwezo, je Tanzania kama nchi itaachana lini na Ulalahoi? Je ni jukumu la nani kuitoa Tanzania kutoka Ulalahoi na kuipandisha chati kufikia hata ile hatua ya kuwa Wa-Benzi?
Tanzania ni nchi ya tatu kwa wingi wa dhahabu duniani. Tanzania imerudia kwenye usukano wa nchi inayoongoza kwa kuzalisha katani. Tanzania iko katika nchi kumi zilizo na Uranium ya kutosha. Ongezea madini kama makaa ya mawe, gesi, rubi, almasi, chuma, shaba na hata Tanzanite ambayo ni sisi pekee tunaozalisha.
Tanzania tuna mbuga za wanyama kubwa sana na maarufu duniani. Tanzania kuna mlima mrefu Afrika na inazungukwa na Maziwa makubwa matatu ya dunia hii na ongezea Bahari ya Hindi. Tanzania ina visiwa maarufu vya Zanzibar na Mafia ambako si mazao tuu hata utalii unaweza shamiri.
Tanzania ina ardhi kubwa ya kutosha yenye kuweza kuzalisha mazao ya biashara na kutawala soko la dunia, mazao kama Chai, Kahawa, Tumbaku, Korosho, Pamba na hata mazao ya chakula kama Mahindi, Mpunga, Maharage, matunda, mboga za majani, Mtama, Mihogo, Ngano, Shayiri, Karafuu na mengineyo.
Tanzania tuna samaki wa aina nyingi sana, tuna mifugo mingi ambayo inatufanya tuwe katika nchi tano zenye mifugo mingi Afrika.
Tanzania ina watu takribani Milioni 40 na wanazidi kuongezeka.
Lakini haieleweki pamoja na hazina yote hii na nguvu kazi yote hii ya watu Milioni 40, ambao wamefunikwa na mshikamano na kufungamana kuliko leta Amani na Utulivu wa namna fulani, hadi leo hii tunaendelea kuwa Taifa la Kilalahoi, tukitegemea misaada na mikopo na hata watu kutoka nje waje kuzalisha na kutupa kipato.
Si suala la ni nani Rais au ni chama gani kiko madarakani au ni Siasa gani hata kwa wale wanaodai bado tu nchi changa au ni makosa ya sera, itikadi au mfumo wa kiuchumi ambalo ndi kizingiti cha kuleta maendeleo na kuliendeleza Taifa letu likanawiri na kuachana na umasikini na unyonge unaotufanya tuendelee kuwa Walalahoi.
Si suala la kudai ni mafisadi, wahujumu, wanasiasa, makaburu, wawekezaji, ukoloni, utumwa au lolote lile la kuhalalisha kuwa mpaka leo tunaendelea kuwa Taifa masikini.
matumizi yetu ni makubwa sana, tena ya anasa sana! Ripoti ya wikii hii inasema deni limeongezeka, matumizi yanaongezeka, lakini hatutumii hazina vizuri hata kuitumia katika kujenga msingi imara wa nyumba yetu ili tuweze kuishi hata vizazi 10 bila kuporomoka.
Je twahitaji mme, mke, mtawala hata mshenga wa kutuamsha na kujitambua kuwa Uchumi tumeukalia?
Naibu Waziri wa Fedha Omar Mzee katoa kauli majuzi bungeni akisema tena kwa ukweli mtupu bila kutia vikolombwezo kuwa ni wajibu wa kila mtu kutamani maendeleo na kujiendeleza na si kuisubiri Serikali.
Kauli kama hii iliwahi kutolewa na Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya aliposema kila mtu atabeba Msalaba wake!
Je tumeridhika na Ulalahoi kiasi hicho na kufurahia kuwa Masikini?
Je ni kisingizio gani tulichonacho kwa nafsi zetu moja moja au kwa ujumla wetu kama Taifa kuhalalisha umasikini wetu huu uliokubuhu na kupita kiasi huku kuna wanaoneemeka kupita kiasi kutokana na hazina na rasilimali tulizonazo?
Je ni uzao gani tuusubiri uje kulivusha Taifa letu kutoka kundi hili la nchi masikini na tegemezi na kuwa ni nchi yenye kujitegemea na maendeleo yyake yakawa ni endelevu na kuiendeleza jamii kuelekea kuwa nchi iliyoendela?
Je ni miaka mingapi tunahitaji kuendelea kujifunza na kutamani kufikia tabaka la kati na kuachana na tabaka la kuwa masikini?
Je tunamsubiri Rais au chama gani kishike madaraka ndipo tukate shauri kuachana na unyonge wa mawazo na kujitutumua kila mmoja kibinafsi na kwa ujumla kuijenga nchi yetu na kuvuna na kufurahia rasilimali zetu na hivyo kuondokana na karaha na adha za kuwa masikini?
Ni lini tutaondoka kutoka kwenye kundi la Nchi za Dunia ya Tatu na Masikini na kwenda japo katika kundi la Nchi za Dunia ya Pili zinazoendelea na kupiga hatua mbele?