Kwa mtazamo wangu, Polepole anapoteza muda. Anachokifanya sasa kilipaswa kufanyika tangu mwaka 2000 au angalau 2005. Kwa sasa, hao anaowaita wahuni ndio walioko madarakani, na muda umeshapita.
Kuhusu Magufuli, ukweli ni kwamba alitokana na migongano na usaliti baina ya hao hao wahuni. Tayari wameshajifunza kosa walilolifanya na hawatarudia tena.
Kilicho kibaya zaidi, Polepole anapigania maslahi ya CCM lakini kwa namna fulani anaonyesha chuki ya waziwazi kwa Mama Samia – jambo ambalo linamharibia yeye mwenyewe. Anaposema CCM ifuate utaratibu na katiba iliyojiwekea, ukweli ni kwamba hata viongozi wastaafu kama Jakaya na wengine wa zamani wakimsikia watamcheka. CCM haina utaratibu huo – anayekuwepo madarakani ndiye mwenye uamuzi wa mwisho; ndiye katiba na taratibu zenyewe.
Tukumbuke, Polepole mwenyewe alikuwa sehemu ya uharibifu wa uchaguzi wa 2020 ambapo wagombea wa upinzani walikandamizwa kwa visingizio visivyo na msingi. Sasa leo aje kusema Magufuli alipata kura nyingi kwa heshima kubwa – si kweli. Ukweli ni kwamba CCM ilitumia mbinu za nguvu na yeye alikuwa sehemu ya huo mfumo.
Kwa sasa kinachomtokea ni kwamba Polepole bado hajaamini kuwa Magufuli hayupo na hatarudi tena. Inaonekana kama amepata mshtuko au hata sonona, pengine kwa sababu aliahidiwa mambo makubwa ambayo hayajatimizwa.
Badala ya kueneza taharuki zisizo na msingi, afuate taratibu za chama chake huko ndani. Sisi wananchi wengi hatuna muda na lawama zake dhidi ya CCM au mwenyekiti wake. Watanzania tayari tumeshakubaliana na hali tuliyonayo – liwalo na liwe.
Kwa ufupi, Polepole anapoteza muda wake bure.