Wanakijiji: Barrick ilimdanganya Waziri Mkuu
na Chris Mang'era, Tarime
Tanzania Daima
WAKAZI wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa North Mara, uliopo wilayani Tarime, akiwamo Diwani wa Kata ya Kemambo, Agostino Neto Sasi, wameeleza kusikitishwa kwao na uongozi wa mgodi huo, kumpatia Waziri Mkuu, Edward Lowassa, taarifa zisizo sahihi kuwa umejenga shule 13 katika vijiji vinavyouzunguka.
"Tumesikitishwa sana na kitendo cha mgodi wa North Mara kumpatia kiongozi mkubwa wa nchi taarifa za uongo kwamba umejenga shule 13 katika vijiji vinavyouzunguka huku ukijua haujafanya kitu cha aina hiyo," alidai Sasi.
Katika mazungumzo na wanahabari mjini hapa juzi, baadhi ya wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo walidai taarifa yote aliyopatiwa waziri mkuu kuhusu miradi ya kijamii inayotekelezwa na mgodi huo ni ya uongo na hasa kinachowaumiza ni taarifa za madai ya ujenzi wa shule 13.
"Mimi sijawahi kushuhudia kiongozi wa nchi akidanganywa kiasi hicho… niseme tu kwamba karibu taarifa yote iliyotolewa na mgodi wa North Mara kwa waziri mkuu, kuhusu shughuli za maendeleo ya jamiii imejaa uongo.
"… ila kinachoumiza zaidi ni madai kuwa mgodi umejenga shule 13, jamani tutafika kweli kwa kudanganyana kiasi hicho?" alihoji mkazi wa Kijiji cha Kewanja, Gabriel Mwita.
Wanavijiji hao walitaja shule zilizojengwa na mgodi wa North Mara kuwa ni mbili, nazo ni Shule ya Sekondari ya Bwirege ambayo ilijengwa chini ya kiwango, kwa mujibu wa wataalamu na Shule ya Msingi Nyabichune ambayo hata hivyo, kwa sasa inakabiliwa na ukosefu wa nyumba za walimu, hivyo kuwalazimu baadhi ya walimu kuishi kwenye stoo.
Walidai shule nyingine moja ya sekondari na 10 za msingi zilijengwa miaka mingi iliyopita kwa ushirikiano wa wanavijiji husika na serikali, nyingi kati ya hizo zilijengwa kabla ya mgodi huo kubinafsishwa.
Walieleza kwamba mchango uliotolewa na mgodi huo ni kugharimia ukarabati wa baadhi ya majengo ya shule hizo.
Wakizungumzia sh bilioni 42.6 ambazo mgodi wa North Mara ulidai kuzitumia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii katika vijiji hivyo hadi sasa, wananchi hao walisema hawaamini kama kuna kitu cha aina hiyo, kwa kuwa hakuna mwanakijiji aliyeshirikishwa katika matumizi hayo.
Hata hivyo, wanavijiji hao walibainisha fedha zinazotolewa na Kampuni ya Barrick kutekeleza sehemu za baadhi ya miradi ya maendeleo katika vijiji hivyo si msaada kama uongozi wa kampuni hiyo unavyodai, bali ni stahili inayopaswa kutolewa kila unapofanyika uzalishaji na mauzo ya dhahabu kulingana na mkataba uliowekwa kati ya mgodi huo na vijiji vitano ambavyo ni Matongo, Kewanja, Nyangoto, Genkuru na Kerende.
Naye mkazi wa Kijiji cha Kerende, Elia Maginga, alisema uongozi wa mgodi huyo ulijua wazi kuwa taarifa unayompatia Waziri Mkuu ni ya uongo ndio sababu uliamua kumsomea taarifa hiyo ndani ya ofisi ya kituo cha afya cha Nyamongo ambamo haikuwa rahisi kwa mwanakijiji wa kawaida kuingia na kusikiliza.
"Kama taarifa hiyo ingesomwa kwa waziri mkuu katika mkutano wa hadhara, wanavijiji tungeipinga, ili waziri agundue, lakini uongozi wa mgodi ulifahamu hilo ndiyo maana ukatumia ujanja wa kwenda kuisomea ndani ya ofisi ambamo mwanakijiji hakupata nafasi ya kuingia na kusikiliza," alisema Maginga.
Agosti 31, mwaka huu, waziri mkuu, akiwa ziarani mkoani Mara, alipata fursa ya kutembelea kituo cha afya cha Nyamongo, ambapo uongozi wa kampuni hiyo ulimpatia taarifa ya shughuli na miradi mbalimbali ya kijamii iliyotekelezwa na mgodi huo katika vijiji vinavyouzunguka.
Katika taarifa hiyo, uongozi wa kampuni hiyo ulidai miongoni mwa shughuli za kijamii zilizotekelezwa na mgodi huo ujenzi wa shule 13, zikiwamo mbili za sekondari na 11 za msingi.
Mgodi huo unadai kujenga shule za sekondari za Nyamongo na Bwirege, pia shule za msingi Matongo, Nyansangero, Bung'eng'e, Nyabichune, Genkuru, Nyamwaga, Kerende, Nyangoto, Nyamongo, Kenyangi na Nyabigena.
Chanzo: Tanzania Daima