Ni kweli kabisa. Na kwa waliopitia shule pia wanaelewa mwanafunzi anayepata A 9 form IV, na mwanafunzi huyohuyo akashindwa kupata C 3 form VI, ni mwizi wa mitihani. Na hasa kama A 9 zenyewe zilipatikana katika mwaka ambao wengine walifutiwa matokeo kwa wizi wa mitihani.
Nilikuwa katikati ya kazi jimboni nikaambiwa kwamba kuna mwito humu wa Nape na Ridhwan kutaka nieleze elimu yangu. WanaCCM walianza suala hili kwa ari, nguvu na kasi mpya niliposema kwamba nchi imefika hapa ilipo kwa sababu ya udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM.
Nikapuuza, naona sasa limeibuka tena kwa ari, nguvu na kasi zaidi baada ya yaliyojiri bungeni kuhusu hoja binafsi niliyowasilisha bungeni kuhusu maji na mkutano wa hadhara wa tarehe 10 Februari 2013 na masuala ambayo niliipa Serikali wiki mbili kuyatolea majibu ama sivyo nitaongoza maandamano ya wananchi kwenda Wizara ya Maji kutaka uwajibikaji na hatua za haraka.
Kwa mara nyingine tena zinafanyika jitihada za kuhamisha wananchi kwenye mjadala kwa kumshambulia mtoa hoja badala ya hoja, sasa ili turejee kwenye mijadala ya msingi ni muhimu niweke kumbukumbu sawa kuhusu masuala kadhaa kama yalivyoombwa.
Elimu yangu sio siri, nimegombea ubunge mara mbili mwaka 2005 na 2010 na mara zote nimeeleza kuhusu suala hili; Nape na Ridhwan wangetumia tu elimu yao wangetafuta kwenye mitandao na kukuta majibu wanayoyatafuta. Nieleze kwa muktasari tu; nimesoma shule ya msingi Mbuyuni Dar Es Salaam (nilikuwa mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa wa Dar es Salaam).
Nilichaguliwa kwenda Shule ya Sekondari ya Ilboru wakati huo ikiwa ya vipaji maalum, sikwenda; wito ulinituma kwenda Seminarini. Nilisoma Franciscan Seminary Maua (FRASEMA) mpaka kidato cha nne; nilipata daraja la kwanza; nikiwa na alama A katika masomo tisa.
Ningeweza kwenda shule yoyote ya Serikali ya kidato cha tano na sita yenye mchepeo ambapo ningeutaka; lakini niliamua kubaki Dar es Salaam shule ya Tambaza kwa sababu nilitaka kusoma huku nikiendelea na harakati ambazo nilizianza kabla.
Hapa ndio ilikuwa chanzo cha mimi kuingia kwenye kazi ya kuhamasisha mabadiliko kwenye mimbari nje ya utumishi wa madhabahuni. Tukio lililobadili mwelekeo wa maisha yangu, mwaka 1998 nikiwa kidato cha nne; nimesoma na tumeanza mitihani tukatangaziwa kwamba mitahani yote imefutwa baada ya kuvujishwa.Tukarudishwa nyumbani kipindi hicho nikaenda kwenye mafungo kujitafakari kwenye mkoa mmoja nikarejea Dar es Salaam nikakutana na wanaharakati kadhaa wa asasi zisizo za kiserikali; maelezo kuhusu ufisadi yalinifanya nione nina wajibu kwa nchi yangu, nikarejea Seminarini kufanya mitihani nikiwa na fikra tofauti.
Matokeo yakatoka nimefanya vizuri, kwa mifumo yetu mibovu ya wakati huo kwa mara ya pili tena Serikali hii inayoongozwa na CCM haikutambua vipaji na nikapaswa niendelee kujilipia ada mwenyewe kama ilivyokuwa kwa ngazi nyingine za elimu zilizotangulia; hapa nikakata shauri kwamba nitatumia uwezo na uadilifu wote ambao Mwenyezi Mungu amenijalia kuwezesha mabadiliko katika taifa letu.
Nikaamua kuacha kwenda kwenye shule za bweni mikoani na kubaki Dar es salaam nisome Tambaza huku nikiendelea na kazi za harakati; wakati huo nikihamasisha masuala ya ukombozi wa vijana nchini. Pamoja na kusoma kutwa huku nikifanya kazi nilipata daraja la pili katika kidato cha sita.
Taasisi nilizoanzisha au nilizoongoza katika kipindi hicho na kazi nilizofanya sio siri na zinapaswa kujieleza zenyewe kwa matendo badala ya maneno. Katika kipindi hicho, wakati huo kukiwa hakuna Mfuko wa Elimu wala Bodi ya Mikopo nikashiriki katika ushawishi wa mabadiliko ya kimfumo; nilikwenda Dodoma, tukakutana na wabunge na mawaziri nikawasilisha mada Towards a more functional education in Tanzania, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa Sekondari.
Kati ya wabunge waliosikiliza mada niliyoiwaisilisha wakati huo sasa ni Rais Jakaya Kikwete ( Ridhwan ukiwa nyumbani unaweza kumwuliza maoni yake aliyotoa siku hiyo kuhusu ugharamiaji wa elimu na suala la mauaji ya mwanafunzi wa Iyunga Michael Sikupya). Nilipotoka kwenye mkutano ule Dodoma mwishoni wa miaka ya tisini, nilikata shauri kwamba mwaka 2005 nitagombea Ubunge hii ni baada ya kushudia aina ya wabunge waliokuwepo.
Mwaka 2002 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Es Salaam kusomea Bachelor in Business Administration (BBA) kwenye programu ya jioni; nilifanya hivyo kwa kuamua kwa kuwa nilitaka nisome huku nikiendelea na kazi. Mkuu wa Programu hiyo wakati huo alishangaa sana kwa umri wangu (wakati huo shahada hiyo walikuwa wakisoma wazee watu wazima wafanyakazi) na matokeo yangu (kwa kuwa yaliniruhusu kwenda kuingia kusoma katika mfumo wa kawaida). Nikamweleza akanielewa kwamba sitaki kusoma kama wanachuo wengine wa kawaida, uamuzi wangu huo ulikuwa na gharama kwa kuwatafsiri yake ni kuwa nilipaswa kujisomesha binafsi.
Kwa hiyo mimi ni kati ya wale ambao hatudaiwi na nchi hii kwa maana ya kwamba sijawahi kuchukua ruzuku wala kusomeshwa na Serikali hii inayoongozwa na CCM; nimesoma kwa jasho la wazazi wangu na langu binafsi. Kwa hiyo, nijibu tu kuhusu elimu yangu ya juu kwamba nimesoma miaka mitatu Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (mtu aliyosoma kwa kiwango hicho kwenye baadhi ya vyuo duniani hupewa associate degree).
Mwaka 2004 ikaanza misukosuko mbalimbali, mwaka huo ulikuwa ndio unatungwa muswada wa Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, haya matatizo yanayotokea leo niliyatabiri wakati huo. Niliwasilisha mada kwa wanachuo kwenye ukumbi wa Nkurumah kuchambua udhaifu wa muswada huo na kupata maoni ya wanafunzi kuhusu marekebisho yanayohitajika; wanachuo wakapitisha azimio la kwamba muswada huo upingwe.
Kesho yake nikiwa Morogoro kikazi kukafanyika mgomo hatimaye wanafunzi wakapigwa na kukamatwa.Nakumbuka nilikatiza kazi niliyokuwa nafanya nikarejea kwa kuwa Chuo kiliweka sharti kwamba lazima wanachuo waache mgomo ndio waliokamatwa waachiwe. Wakati huo Serikali ya wanafunzi ilikuwa haisikilizwi, mimi na wengine wachache tukajitolea kuzunguka kampasi na hosteli zote kushawishi wanafunzi kurejea masomoni na wakafanya hivyo.
Serikali ya CCM ikatoa maelekezo kwamba kama tumeweza kuwafanya wanafunzi warudi, hata kama sikushiriki mgomo na sihusiki na masuala ya mikopo kwa kuwa ni mwanafunzi ninayejilipia mwenyewe lazima nisimamishwe; nikiwa mwanafunzi pekee wa BBA niliyesimamishwa wakati huo.
Nikarejea baada ya muda tayari kukiwa na mvutano kati yangu na utawala, mwaka 2005 nikaamua kugombea Ubunge wakati huo nikiwa mwanafunzi; mvutano ukaongezeka zaidi. Na utawala wa Chuo ukawa unapata mashinikizo mengi kutoka kwa Serikali na CCM; wengine wakipendekeza nifukuzwe, wengine nifelishwe na wengine nisiruhusiwe kuingia katika maeneo ya Chuo jioni masomoni kwa kuwa nitakuwa nafanya kampeni.
Nikawa katika mtanziko(dilemma) wa kuchagua ama kuendelea na masomo na kujitoa au kupunguza nguvu kwenye kampeni (mbinu nyingi zilitumika wakati huo, sio sehemu ya majibu yangu ya leo) au niendelee na kampeni. Nafsi yangu ikanituma kuamua kuandika barua yakuahirisha masomo, baada ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2005 mazingira yalikuwa yamebadilika sana kuweza kurejea kumalizia mwaka au miezi michache iliyokuwa imebaki.
Mwaka 2006 nikiwa Marekani nilitafakari sana na kufikia uamuzi wa kuendelea na kazi hii ya kusimamia mabadiliko na kujiandaa na uchaguzi wa mwaka 2010. Mwaka 2010 niligombea tena na kushinda wakati huo huo nikiongoza kazi za kitaifa za kampeni makao makuu pamoja na Profesa Baregu na wengine; hakuna mahali popote nilipowadanganya wananchi kuhusu elimu yangu, kama nilivyoeleza hapo juu.
Naamini wananchi wa Jimbo la Ubungo walinichagua kwa uwezo na uadilifu wangu, na walijua pia kwamba nilikuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwa miaka mitatu. Naamini elimu ni kitu muhimu sana kwa kiongozi, lakini wapo wenye elimu kubwa ya vyeti lakini hawajaelimika na wapo wenye elimu ndogo sana ya vyeti lakini wanaelewa mkubwa wa kutimiza majukumu yao ya uongozi.
Tangu mwaka 2012 na 2013, nimekuwa kwenye mtanziko mwingine na viongozi wangu ndani ya chama wanafahamu; niliomba kuachia majukumu mengine yote katika chama ili nibaki na ubunge peke yake niweze kuwatumikia wananchi wakati huo huo niendelee na masomo zaidi ya elimu ya juu katika fani inayoendana na kazi ninayoifanya ya sasa na matarajio yangu ya baadaye.
Hata hivyo, kwa mwelekeo huu wa Serikali na CCM leo nieleze tu kwamba nikifanya hivyo itakuwa faida zaidi kwa watawala tunapoelekea mwaka 2015; hivyo, nimeamua kama nilivyoamua mwaka 2005; kwamba nitarejea masomoni baada ya CCM kuondoka madarakani na Tanzania kupata Serikali mpya itakayoongozwa na CHADEMA. Kwa sasa nitaendelea kujisomea kila siku ninapopata wasaa kwa kuwa elimu haina mwisho.
Wakili Ridhwan katika maandiko yake amefanya rejea ya suala Kihiyo wa CCM Temeke, nashauri arejee kwenye hukumu ya kesi ile na marekebisho ya sheria yaliyofanywa na Serikali yaCCM kuwalinda wabunge wake vihiyo baada ya hukumu.
Mifano hailingani kwa sababu mimi sijatoa maelezo ya uongo popote. Lakini hata kwa wabunge wa CCM wanaotoa maelezo ya uongo wa wapiga kura, marekebisho hayo yamewawekea wigo wa mianya yakutokea mahakamani. Zamani fomu zakuogembea zilikuwa na mahali pa kujaza elimu ya mgombea, sasa kipengele hicho kimeondolewa. Hivyo, suala la kughushi na kutoa taarifa za uongo haliko kama ilivyokuwa awali, isipokuwa kesi inaweza kufunguliwa ya ukiukwaji wa kawaida wataratibu za kampeni kwa kuwashawishi wapiga kura kwa taarifa za uongo (ndani ya ule muda wa kisheria wa kesi kufunguliwa ambao ulishapita).
Halafu ni jukumu la mlalamikaji sio tu kuthibitisha kwamba uongo ulitolewa bali uongo umeathiri vipi matokeo. Ndio maana leo kuna vihiyo wengi tu wa CCM ndani ya Bunge lakini ni vigumu kuwabana kwa mfumo wetu wa sasa. Baada ya majibu hayo marefu, naamini sasa Nape unaweza sasa kurejea kwenye kujibu; Elimu ya Mnyika ina uhusiano gani na CCM kuahidi kwenye ilani yake na kushindwa kutekeleza kwamba ifikapo mwaka 2010 asilimia 90 ya wananchi wa mijini ikiwemo Dar essalaam watakuwa wanapata maji safi na salama? Ridhwan kwa kuwa umeweza kufanya rejea unaweza pia kueleza ni kwanini Rais Kikwete mwaka 2011 aliahidi kuwa tatizo la maji Dar es Salaam litakuwa historia mwezi Februari 2013 lakini mwezi huo umefika na matatizo bado ni makubwa?
JJ
1. Shule ya msingi, John Mnyika alikuwa mwanafunzi wa kwanza kwa mkoa wa darisalama. Akachaguliwa kwenda Ilboru lakini akaamua kwenda seminari. (Naachana na hili kwa kuwa ni swala la kiimani)
2. Form 4 akapata A masomo tisa. Katika mwaka ambao matokeo yalikuwa na mushkeli kwa uvujaji wa mitihani. Angeweza kwenda shule yoyote na mchepuo wowote. Akaamua kwenda Tambaza.
3. Form 6 akapata matokeo mazuri tuu (ambayo hayakuwekwa wazi kama matokeo ya form 4)
4. University akaamua kusoma evening classes. (Hakumaliza kwa sababu alizozitaja hapo juu)
Kwa wenye busara, mlolongo wa elimu wa huyu bwana unanuka samaki aliyechina. Mimi binafsi nimesoma Tanga school, wakati wa headmaster Tetti. Wakati sisi tuko O'level pale Tanga school alikuja mwarabu mmoja kujiunga form 5 (PCM) tulikuwa tunamwita "yarabi salama". Yarabi salama yeye wakati akiwa form 5 PCM alikuwa haelewi kwa nini namba ikitoka upande mmoja wa equation na kuvuka alama ya sawasawa na kuhamia upande mwingine mwingine, basi inabidi alama yake ibadilike, kama hasi itakuwa chanya na chanya huwa hasi. Form 5 PCM huyo. Na bwana yarabi salama alikuwa amepata alama A katika hesabu O level. Baadaye ikagundulika kwamba wakati wenzake wanafanya mitihani, yeye alikuwa anazaa mitihani.
Sijui kama msamiati wa kuzaa bado unatumika siku hizi, lakini kuzaa maana yake ni kwamba kuna watu wana networks na mitihani inapotoka na wanapoingia kwenye chumba cha mtihani, hawaji kufanya mtihani ispokuwa wanakuja na "booklet" zao ambazo maswali yanakuwa tayari yameshafanywa. Sasa wakati wenzao wanafanya mtihani wao wanaandika namba yao ya mtihani tuu kisha wanazaa.
a) Sasa, najiuliza. Mnyika amesema kwamba alikuwa wa kwanza mkoa wa darisalama. (Sibishi, lakina Sijui amejuaje)
b) amepata A tisa form IV; lakini hakusema amepata A ngapi form VI. Jee inawezekana ni kwa sababu matokeo yake ya form 6 hayashabihiani na yale ya form 4?
c) A tisa, lakini hakwenda Ilboru. Kwanini mwanafunzi hodari asiwe na hamu na shauku ya kusoma na wanafunzi hodari wengine? Jee inawezekana bwana Mnyika alikuwa anaogopa "to get found out?"
d) Baada ya kupata matokeo mazuri form 6; kwanini asome jioni? Jee alikuwa anaogopa kusoma na wanafunzi hodari?
e) Mpaka leo bado hana degree. [anisamehe kama nimekosea katika hili]. Ni kweli mwanafunzi mwenye uwezo wake wa kitaaluma atakubali kuishia njiani kwa namna aliyoishia yeye?
Sasa kila nikimtafiti huyu bwana Mnyika, samahani, lakini neno kuzaa linapiga kengere zote akilini mwangu. Nadhani huyu bwana ni miongoni mwa wale wenye bahati nzuri ambao huweza kuipata mitihani kabla ya siku ya mtihani.
Nawashaangaa wabongo maana mnapenda kubishana ka kuangalia fulani ana vyeti gani badala ya kuangalia fulani ana nini chenye faida kwa nchi, mbona wapo viongozi wengi tu na wazuri waliowahi kuwa juu ya ulimwengu na hawakuwa na hayo makaratasi ya vyeti mnayojisifu nayo..?
Ni dhahiri kwa elimu aliyonayo anastahiki sana kupongezwa, kwani kazi anayoifanya inamzidi Profesa, tujiulize Maghembe ni Profesa na Mnyika ni form six, lakini nani zaidi kwa kutoa hija zenye mantiki ? Ni dhahiri wengi waliogundua mambo makubwa duniani kama ndege, treni, magari, na mambo mengi hwakuwa na elimu kubwa sana, lakini leo hawa wanaojiita wana elimu wanapata PHD kwa kuzielezea kanuni ambazo kimsing zimeanzishwa na wao, Elimu si degree alizonazo mtu bali ni maarifa aliyonayo nayo mtu ili kuweza kuiendeleza jamii yake, na Mnyika ana maarifa hayo kuliko Mbunge yeyote Bungeni
By Mtanzania Ushauri kwa vijana,
Hii mijadala ya elimu ya Nape na Mnyika ina mafundisho mengi sana kwa vijana kama mnataka kujifunza. Wekeni siasa pembeni na jifunzeni jinsi maisha yanavyobadilika na jinsi ambavyo kushindwa jambo moja sio mwisho wa mafanikio.
Hapa inaonyesha wazi Mnyika alikuwa na uwezo mkubwa sana shuleni na bado ana uwezo mkubwa maana hata hoja zake nyingi zina mshiko. Lakini inakuwaje kwa miaka yote hiyo kashindwa kumalizia hako kadegree ambako kwa uwezo wa Mnyika ni kadogo sana? Sidhani kama muda ndio tatizo pekee, labda hata hakuona umuhimu, kitu ambacho mimi nakielewa maana hata akina BIll Gates, Jobs hawakuona umuhimu wa kubaki vyuoni wakati tayari kichwani walikuwa na uwezo wa kufanya yale waliyotaka kufanya baada ya vyuo.
Tukija kwa Nape ni wazi uwezo wake ulikuwa mdogo, hakuwa na credits za kuingia A-level. Lakini kijana Nape hakulala chini na kuanza kulia au kulalamika, badala yake aliamua kujiendeleza kwa kuunga uunga elimu. Mwisho wa siku amesoma mpaka sasa ana masters yake kwenye Public Administration. Hili ni fundisho hata kwa vijana wote waliofeli mwaka huu, tumieni elimu hiyo ya Nape kama hamasa ya kwamba kama Nape ameweza kwanini na nyie msiweze? Bila kujali umepata sifuri au division four. Elimu ya karne ya 21 bado kijana una nafasi ya kuweza kusoma, kujiendeleza na mpaka hata kuwa profesa ukitaka. Uamuzi ni wako, kuamua kupambana au kuishia kucheka wengine. Ukipata F si unarudia?
Sisi sote tuliosoma zamani tunawajua watu wengi sana ambao form six walipata zero hata ya F zote lakini wengine sasa ni maprofesa, madaktari, wachumi nk. Kama mtu anabisha, awaangalie watu waliokuwa wanasoma PCB miaka ya 80. Utawakuta wengi pamoja na kufeli form six lakini leo wako mbali sana. Walichofanya, walijiendeleza na kufeli form six haikuwa sababu ya kuwakwamisha. Kuna jamaa mmoja juzi juzi akaniambia utani akimsema msomi mmoja maarufu wa sheria TZ kwamba alipata division zero PCB Tabora. Nilishutuka sana, sikuamini. Lakini ukweli ndio huo, kupata four au zero sio mwisho wa elimu.
Binafsi kuna vijana nimewahi kuwasaidia ambao form four walitoka na points kama hizo za Nape. Through kuwashauri na kuwasaidia, leo hii wamemaliza degree zao na wana mafanikio kwenye kazi zao.
Sawa tutumie siasa kuchekana kama kujifurahisha, lakini kwenye mioyo yetu tutambue hili ni somo tosha. Kufeli jambo mara moja sio mwisho wa dunia. Badala yake amka, jipukute na anza safari tena kwa speed hata kubwa kuliko mara ya kwanza.
Wakati wewe unacheka na kupoteza muda, wenzako wanasonga mbele.
Tunachotakiwa kufanya kama jamii inayomzunguka John Mnyika siyo kumzodoa na kumshambulia kwa matusi bali kumpa moyo na nguvu ili arudi shule na kumaliza degree yake ya kwanza.Nina uhakika kama hatafanyiwa hujuma na chuo kikuu John Myika anauwezo mkubwa wa kufaulu.
Ningemsihi sana mdogo wangu Mnyika pamoja na wito alionao wa kujenga Taifa lake bado bila elimu ya darasani inahitajika.Hata jioni aweza kujisomea na akamaliza degree yake.
Viongozi waChadema wanapaswa kumpunguzia kazi kijana wao ili amalize shule yake.Na siyo Mnyika tu vijana wote ambao hawajamaliza shule zao au walimaliza form four wakati ni huu wa kurudi shule na kuendelea na masomo yao.Elimu kwanza siasa baadaye.