Zack Abdul
JF-Expert Member
- Mar 9, 2026
- 1,194
- 911
Mbunge wa Baraza la Wawakilishi na Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu, Simai Mohammed Said, amesema mafanikio ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato yanaonyesha kuwa Tanzania ipo katika mwelekeo sahihi wa kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Fedha Bungeni leo Juni 2, 2026, Simai alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha unaoelekea ukingoni, jambo alilosema linaakisi uimara wa usimamizi wa uchumi wa nchi.
Hata hivyo, alisema bado kuna baadhi ya watu wanaokwamisha juhudi za maendeleo kwa maslahi binafsi, akidai kuwa mmoja wao ni mtu aliyemtaja kwa jina la "Yuda" ndani ya Serikali.
"Kosa la Rais Samia ni lipi? Kumuamini mtu? Kumbe ni Yuda. Yuda huyu amewasaliti ndugu zake mwenyewe, hata familia iliyomlea kisiasa haitaki kumuona. Hata huko nyuma aliwahi kuitwa mzigo, lakini leo mzigo huo tunao ndani ya Serikali," alisema Simai.
Aidha, Simai alidai kuwa mtu huyo amekuwa chanzo cha maumivu kwa watu mbalimbali, akiwemo viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma na wafanyabiashara, huku akisema baadhi ya waliokuwa na mustakabali mzuri wa kisiasa walipoteza nafasi zao kutokana na ushawishi wake na wengine kuingia katika changamoto za kisaikolojia.
"Leo huyo huyo anapita katika nyumba za ibada na maeneo mbalimbali akitafuta huruma ya wananchi. Anajaribu kujijenga kama mwathirika wa mfumo, wakati wengi wanafahamu nafasi yake katika kuathiri maisha na safari za watu wengine," aliongeza.
Kwa upande mwingine, Simai alikosoa kile alichokiita matumizi ya jina la Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa maslahi ya kisiasa, akisema si sahihi kwa mtu yeyote kujinasibisha na urithi wa kisiasa wa kiongozi huyo kwa lengo la kujijengea uhalali mbele ya umma.
"Leo anataka kutuaminisha kuwa Hayati Magufuli alimpenda sana. Kama alimpenda, kwa nini alimuweka mbali? Waliompenda na waliopendwa na Rais Magufuli wanafahamika, na baadhi yao wapo hapa Bungeni hadi leo. Tumwache Hayati Magufuli apumzike kwa amani; alilitumikia taifa kwa kiwango kikubwa. Yuda aache kutafuta huruma za wananchi kwa kutumia majina ya watu waliotangulia mbele za haki," alisema Simai.