Walichokuwa wanakosea Amana ni kutowapa mrejesho wa mgonjwa wa Sukari iliyopanda sana mpaka ikaleta compication ya Diabetic Ketoacidosis (DKA). Walitakiwa wawape mrejesho wa namna matibabu yake yanavyokuwa.
Katika complications mbaya na hatari za Kisukari basi hii ndiyo baba lao.
Huwa inatokeaje?
DKA hutokea wakati mwili unapokosa insulini ya kutosha kuruhusu sukari ya kwemye damu kuingia kwenye seli kwa ajili ya nishati. Tunafahamu Insulini ndiyo hufanya kazi ya kusaidia sukari kuhama kutoka kwenye damu na kuingia kwenye seli za mwili.
Hii hali ikitokea, kwa sababu seli za mwili zimekosa sukari kwa ajili ya kuupa mwili nguvu, mwili unaamua sasa kuangalia alternative ya pili ambayo ni Ini (Liver) kuvunjavunja mafuta (Fat) ya kwenye mwili kwa ajili ya kuzipa seli nguvu (Energy).
Sasa hii process huzalisha by-product ambayo ni asidi inayoitwa Ketoni, ambayo sasa inaingia kwenye damu, kisha kutolewa kwa mfumo wa figo. Hii Ketoni ndiyo huleta shida zooote kwenye mwili, maana inaenda kutengeneza asidi kwenye damu kwa sababu inakuwa imezidi sana.
Visababishi vya DKA ni nini:
Cha kwanza lazima mjue kwamba DKA ni Life-Threatening Complication ya Kisukari, na huwapata watu walio na ugonjwa wa Kisukari cha Aina ya 1, lakini pia inaweza kutokea kwa watu walio na Kisukari cha Aina ya 2.
Vichochezi vya kawaida vya DKA ni pamoja na:
1. Maambukizi (Hii ndiyo huwa kisababishi kikubwa cha DKA kwa wenye Kisukari).
2. Kisukari Kinachoanza (Kama Ilivyomtokea Mdogo Wako).
3. Kutokufuata Masharti ya Matibabu.
Matibabu ya DKA huwa Yakoje:
Matibabu ya DKA huwa yana goals kadhaa:
1. Kurekebisha Upungufu wa Maji Mwilini (Dehidration/Hypovolemia).
Kwa sababu mgonjwa wa DKA huwa anakojoa sana, hivyo hupoteza maji ya kutosha, na nadhani mlikuwa mnamuona ndugu yenu akiwa amekauka sana midomo na alikuwa anakunywa sana maji.
Hivyo tiba ya kwanza huwa ni kuwapa madripu kwa fomula maalumu.
Na ili kurudisha maji mwilini huwa inachukua mpaka siku 2 (masaa 48)
2. Kurekebisha Upungufu wa Madini Joto Yaliyopungua hasa Potasiamu.
Moja ya madini sensitive kwenye mwili huwa ni Potasium, na kwa wagonjwa DKA huwa yanashuka sana ambayo inaweza pelekea moyo kusimama ghafla.
Hivyo matibabu ya DKA huwa yanahusisha kumpa mgonjwa haya madini kwa njia ya dripu.
3. Kurekebisha Asidi/Sukari Iliyojaa Kwenye Damu.
Hapa huwa wagonjwa wa DKA wanapewa Insulini kwa fomula maalumu kulingana na uzito wao.
Ndiyo maana ulikuwa unaona wanamchoma insulini, kazi ya insulini inasaidia kuondoa sukari iliyo kwenye damu na kuiingiza kwenye seli za mwili.
Lakini kwa sababu kwenye damu kuna asidi nyingi, huwa hatuishishi sukari ghafla, kwa sababu tunahitaji kuendelea kumpa insulini mgonjwa wa DKA kwa muda mrefu ili isaidie kuondoa asidi kwenye damu. Kwa hiyo sukari yake ikifika 14 huwa tunamtundikia mgonjwa dripu ya sukari ili isishuke zaidi.
Hivyo mkuu matibabu ya mgonjwa wako ni magumu na marefu, yanahitaji uvumilivu wenu.
Wagonjwa wa aina hii wala msishangae sukari kupanda na kushuka, ni kawaida mpaka pale asidi inapoisha kwenye damu ndiyo tunaiacha sukari ishuke mpaka kawaida yake.
NB: Wagonjwa wa Severe DKA huwa wanalazwa ICU. Hiyo ndiyo huwa destination yao maana wanahitaji uangalizi wa karibu sana ikiwemo kupima sukari kila saa.